Thursday, 26 November 2015


Nani Ataniunga Mkono?

Ninakiri kuwa yeye ni mwerevu sana... Ameweza kupelekea tabasamu moyoni mwangu... Ninaweza kupata msaada wake katika kila kitu, lakini pamoja na hayo nataka kumpa talaka.

Unajua kwa nini

Kabla hujaanza kuwaza kuwa kwanini, ngoja nikwambie kwamba jambo hilo sio kama unavyolifikiria... huwenda hujui kwa nini nataka kuachana naye na kwa sababu gani...!
 
Kwa sababu ninayetaka kuachana naye huchukua muda wangu wote na kuifanya akili yangu isishughulike na familia yangu na kunifanya niendelee kukaa naye mpaka usiku wa manane.

Jina lake unalijuwa sana. Ninakiri kuwa naweza kupata msaada wake... Daima yuko ubavuni mwangu muda wote lakini ananizuia kutumia muda kukaa na watu muhimu katika maisha yangu, ananizuia nisikae na familia yangu, ndugu na marafiki zangu.

Kiumbe huyu ni mjanja sana katika kunikamata kiasi kwamba anaweza kunisahaulisha kila kitu... ananihadaa nitumie vitu vyake hata katika maeneo ya ibada, harusini na kwenye misiba, ananisahaulisha mpaka kazi zangu...! Ajabu kubwa ni pale ikitokea nimemsahau kumchukuwa hata nikiwa wapi basi nitarudi mbio mbio kumchukuwa, ilimradi tu niwe naye karibu.

Yaani hajali hata kidogo linapokuja suala la usalama wangu, ananilaghai na kunishawishi niendelee kuutazama uso wake huku nikiendesha gari hata nikiwa kwenye vikao muhimu, nimekuja kushtuka na kuona maisha yangu, maisha ya ndoa yangu na watu wanaonizunguka yakiwa yamechafuka.

Nimekuja kugundua kuwa si mimi tu peke yangu, bali watu wengi wamekumbwa na balaa ili linalo nikabili mimi, wamekuwa hawajali tena na kuona kana kwamba jambo hili ni la kawaida, lakini ni jambo ambalo hatupaswi kupuuza hatari zake...!

Labda nisikuchoshe kwa maelezo mengi kuhusiana na huyo ninayetaka kutengena naye, kiumbe huyu ana majina mengi kulingana na muhusika anaye mmiliki. Lakini kwa ufupi tu na kwa jina lake haswa ni "Hizi simu zinazoitwa Smart Phone" Kwa kweli simu zetu hizi ndio tumezifanya kuwa ndio wana ndoa wetu wapya ndio wake/waume zetu, simu zimekuwa ndio washauri wetu, vibembelezi vyetu, ndio simu zimekuwa kila kitu.

Tuna haja ya kuziweka simu zetu nyuma, sio kuzifanya ziwe katika kiti cha enzi cha vipaumbele vyetu, tukasahau ukaribu wetu na wenza wetu na familia zetu.

Changamoto kubwa kabisa inayotukabili, mimi na wewe ni jinsi gani ya kuzipa talaka simu zetu, na sio simu tu, kwa sababu huyu smart phone anao ndugu zake kina Ipad au kina tablet wakishirikiana na mitandao ya kijamii, kina WhatsApp, Telegram, Facebook, Instagram, Tango n.k.

Tunapaswa turudi katika kufungamana na binadamu wenzetu... Tunapaswa kuweka ahadi kwamba tutatumia muda wetu mwingi bila simu zenu ili tupate fursa ya kurudi kwenye mahusiano na watu wengine.

Tumekuwa hatutembeleani kama zamani eti kisa tunasalimiana kwenye WhatsApp au kwenye Facebook na tuna chat na ndugu zetu na marafiki kwenye mitandao ya kijamii.
Kuanzia leo nakiri mbele yenu kwamba mke wangu na familia yangu na ndugu zangu ni miongoni mwa vipaumbele vyangu "baada ya Allah Mtukufu" na sitaki jambo lolote kuzuia mahusiano yangu nao.
Vilevile nikitaka ushauri wa kidini na kujuwa fatawa zake basi nitatafuta Sheikh au Imamu aliye karibu na kumuuliza kile ninachotaka kukijuwa na si kuuliza kwenye whatsApp au facebook, maana uko kumekuwa kama jalala, kila mwenye lake ulitupa uko kiasi hata kushindwa kujuwa kipi kisafi na kipi kichafu.

Tunapaswa kukiri kuwa sote waume kwa wake, tumezifanya simu zetu kuwa ndio wanandoa wetu kwa njia moja au nyingine na badala ya kuzitumia kwa mambo muhimu tu, basi sote tuyazingatie mambo yafuatayo:

  • Tujifunza kuweka uwiano wa muda tunaoutumia kukaa na simu zetu.
  • Ichukulie simu yako kuwa pambo, sio kipaumbele.
  • Jiwekee mipaka kwenye jambo linalohusiana na simu yako.
  • Jaribu kutumia baadhi ya muda wako bila kuwa na chombo chochote cha kielektroni.

Nimeweka azma ya kuipa talaka simu yangu mwaka huu...!

Ni mimi ndugu yenu,

NASAHA ISLAM

Je, mnaniunga mkono kwa talaka hii au mna maoni tofauti?

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!