Tuesday, 12 April 2016

Ukipenda usipende rafiki zako wamekuweka katika kundi fulani, unaweza kuwa na mtu ambaye rafiki zako wanakukumbuka kila mara kwa kukutakia mema, au unaweza kuwa aina ya rafiki ambaye rafiki zako wakikuona tu wanaanza kukutukana na kukulaani.

Sasa wewe unajijua rafiki zako wamekuweka kundi gani?

Inawezekana wewe ni aina ya rafiki ambaye unakumbukwa tu kama kukiwa na mnuso au watu wanataka kutoka out, hasa kama una pesa au gari, lakini kama hakuna ishu hakuna anayekutafuta.

Au wewe ni aina ya rafiki ambaye watu wakiishiwa ndio wanakukumbuka? Maana unauwezo wa kumkopesha mtu hata akipiga simu saa nane za usiku, bila matatizo unamtumia hela tu, halafu uzuri wake wewe huwa hudai kiviiile. Halafu kizuri zaidi siku za sikukuu unawakaribisha wote unaowadai kwa bonge ya mnuso, tena kiroho safi.

Au wewe ni yule rafiki ambaye akiombwa mchango, hata ile michango ya kiajabu ya kisiku hizi inayosema mchango si chini ya laki we unatuma tu, halafu kwenda shughuli huendi? Au wewe ndio wale marafiki ambao kamwe hawachangii mchango wowote, hata kama unamsaidia?

Au wewe ndie aina ya rafiki ambaye ukisikia mwenzio anashida lazima uhangaike kumsaidia, hata kama ukisikia yuko gerezani Uchina utaenda tu kujaribu kumtoa? Yaani aina ya wale tunaowaita marafiki wa ukweli? 

Tatizo ni kuwa marafiki wa dizaini hii wako wachache sana. Au wewe ndio wale marafiki ambao hawana doa, wana kazi nzuri, nyumba nzuri, wanavaa vizuri, wana stori nzuri, wana roho nzuri, yaani mpaka wenzio wanataka kuwa karibu na wewe kila mara? 
Au wewe ndiye yule rafiki ambae wenzako wanakufanya kichwa cha habari kila wakikutana? Kazi yao kukuongelea wewe tu na vituko vyako, ukitokeza tu wanaanza kukuchekea na kukukaribisha, ukigeuka tu stori ni kuhusu wewe, ulivyofumaniwa huku, ulivyoiba kule, ulivyofukuzwa kazi mwaka juzi, yaani wewe ndie chachu ya mazungumzo?

Au wewe ndie yule rafiki anaedai anamjua kila mtu? Ukiulizwa kuhusu Ikulu, kuna mtu unamjua, TRA kuna mtu unajua, msikitini kuna mtu unamjua, kanisani kuna mtu unamjua, Bongomuvi kuna mtu unamjua, Bongoflava kuna mtu unamjua na wote hao unadai unawajua kiundani, au wajomba zako au unawadai?

Au wewe ndie aina ya rafiki ambae unajua mambo yote kuhusu rafiki zako? Majina ya wake zao, waume zao tarehe zao za bethdei, maduka wanayonunua nguo, pafyumu wanazotumia, hata dawa walizokunywa walipougua mara ya mwisho?

Au wewe ndie aina ya rafiki watu wenzio wakikuona mapema wanakukwepa maana huna siri kila unalosikia na kuona haraka sana unalisambaza? Na kwa siku hizi za mitandao ya kijamii watu wanakukwepa kama ukoma.

Au wewe ni aina ya rafiki ambaye ukimuona rafiki yako yoyote lazima umpige mzinga, hata kama umeshinda mamilioni ya Zembwela jana yake tu? Maana kuna wengine hawaombi kwa kuwa wanashida laa wanaomba kwa kuwa wamezoea kuomba, hata kama mfukoni ana alfu kumi akikuona mkononi una shilingi mia mbili, ataomba mgawane.

Haya wewe ni rafiki aina gani?

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!