Sunday, 4 September 2016

Tumehamia kwenye Mitandao ya Kijamii.

Misikiti leo hii imekumbwa na matatizo mengi sana ambayo sio tu yanaurudisha nyuma Uislamu, pia kuupa picha isiyo yake. Misikiti mingi mijini na vijijini imekuwa ndio mahala pa kuchochea migogoro na tofauti ya madhehebu, Misikiti kuongozwa na watu wasio na elimu pana na hivyo kushindwa kuiathiri jamii.

Uchafu katika Misikiti yetu, kuanzia ujenzi holela, uchakavu wa majengo, maliwatoni na sehemu za kuchukulia udhu zinaleta picha mbaya ya Uislamu wakati Uislamu unasisitiza usafi.

Leo hii, Maimamu na Makhatibu wetu kwa kukosa elimu zote kwa upana wake wameshindwa kuiathiri jamii, hawa ndio waliotakiwa kufanya kazi ya kuwa viongozi wa jamii.

Msikiti unashindwa kuwa hata na wahasibu wa kudhibiti mapato na matumizi ya Msikiti wakati kila kukicha michango inatolewa!

Misikiti imekuwa haina vitengo vya ushauri nasaha, kama vile Ushauri wa mambo ya Ndoa, Ushauri wa mambo ya Kijamii na Watoto, Ushauri wa Kibiashara na kadhalika. Matokeoa yake mtu akiwa na tatizo na mpangaji wake au Mume na Mke wakikorofishana, ukimbilia aidha serikali za mitaa au kwa mjumbe wa Nyumba Kumi.

Hata watoto wetu imewalazimu kuiga mambo kwenye TV na Video Game kwa sababu Misikiti imeshindwa kuwaandalia madarasa ya chekechea za Kisasa, sehemu ambayo wangeweza kujifunza tabia njema za Kiislam.

Misikiti imekimbiwa na vijana wetu wanaoathirika na Umagharibi kwa sababu Misikiti imeshindwa kuwahudumia. Kama Misikiti ingekuwa na maktaba zenye vitabu na magazeti kutoka kila fani, vijana hawa wasingepata fursa ya kwenda kuharibiwa "British Council au American Library".

Misikiti si sehemu ya kuswalia tu, kama ilivyozoeleka na wengi msikiti ni kituo (centre) hivyo tunaposema mathalani "Masjid Nuur" tuna maanisha kituo chenye mambo mengi sana. 

Msikiti hisiwe ni sehemu ya kuswalia tu peke yake, bali Msikiti unapaswa kuwa kituo cha elimu au taasisi ya kielemu kwa maana ya education centre, zahanati (kama sio hospitali kamili), kumbi za sherehe za Kiislamu, hosteli kwa wanafunzi na wasafiri au wageni, baraza la Shuura au bunge, Information centre kwa ufupi ni kituo (centre) cha mambo ya kijamii na mengineyo na ni kielelezo cha usawa baina ya wanajamii.

Lakini leo hii, tumehamisha mijadala yetu kwenye mitandao ya kijamii, na tunayo yajadiri uko si kuimarisha mustakabari wa jamii ya kiislam, lahasha, bali ni yaleyale tu ya kukufurishana. Kwa nini nyinyi mnatingisha vidole, kwa nini hamsomi maulidi, kwa nini nyingi hamfungi mikono, nyinyi mbona ndevu zetu ndefu kuliko sisi kwa nini nyinyi vile nyinyi hivi.

Misikiti yetu inapaswa iwe ya kisasa iwe na mikakati ya kujiendesha kifedha badala ya kusubiri tu michango ya waumini, hivyo kwa Misikiti inayojengwa au itakayojengwa basi wahusika wanapaswa kubuni mipango na mikakati itakayowezesha Misikiti kujiendesha, haiyumkiniki kwa Misikiti yenye wasaa wa nafasi kushindwa kuwa na vitega uchumi kama maduka, maofisi n.k.

Ni jambo la aibu kwa Misikiti kukosa vitu vidogo vidogo kama simu au Internet au Tovuti ya msikiti, ili kuwe na urahisi wa mawasiliano na waumini wake.

Hakika wanao amirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na wakashika Sala, na wakatoa Zaka, na wala hawamchi ila Mwenyezi Mungu. Basi huenda hao wakawa katika waongofu.
AT-TAWBA: 18

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!