Thursday 15 September 2016

 NA MAFUNZO TUNAYOPATA

Maisha ya dunia sio chochote mbele ya Muumba na yaweza kukatika ghafla bila ya kuletewa taarifa. Tuna amka tukilala tukiwa ni wenye kusindikiza vijana kwa wazee kwenye malazi ya milele ndani ya Barzakh. 

Zipo njia nyingi za kukatika maisha haya kama vile ajali, maradhi na mauaji. Hata hivyo, kuna aina nyingine ambayo kwa karne mbili hizi zilizopita, imepamba moto. Ni hii ardhi yetu tunayoringa nayo kushindwa kabisa kuhimili madhambi yetu yaliyopindukia mipaka. Hapo tunaona kimbunga, mitetemeko, kiwango cha juu cha joto au baridi kali na kadhalika.

Ardhi ya Mkoani Bukoba, nchini Tanzania ni mfano mzuri wa kuwazindua ndugu zetu wa Kiislam. Hakika kuna mengi ya kujifunza kwa Waislam kutokana na tetemeko lililotokea tarehe Tarehe 10 Septemba 2016, tetemeko lenye ukubwa wa magnitude 5.7 huko Nsunga, mkoani Kagera. Maisha ya watu wasiopungua kumi (10) yalipotea ghafla bila ya matarajio. 

Na watu wasiopungua mia (100) walijeruhiwa na majumba na mali kadhaa zimeharibika. Ile siha na neema aliyowapa Allah iliondoka kwa wepesi kabisa. Mamia ya maisha ya watu yamebadilika ghafla ndani ya kipindi kisichozidi nusu saa... ALLAHU AKBAR! 
Yapo wapi macho ya Waislam kutanabahi kiumbe hichi kinachoitwa ardhi kushindwa kuhimili madhambi ya wanaadamu?!

Hali ya udhuni na masikitiko imewezwa kupugua kidogo na faraja kupatikana kwa waanga wa tetemeko ilo, pale ubinaadamu na moyo wa kusaidia haraka, ulipojitokeza aidha kupitia serikali au vyama na watu binafsi, hata kwa wale waliokuwa hawana uwezo, nao wamejitolea kusaidia. Sisi Waislam leo uwezo tunao, badala ya kusaidiana tunaleta jeuri ya neema tuliopewa.

Ni funzo kwa Waislam kuwa Maneno ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) hayaanguki abadan, kuwa siku za mwisho kutakuwa na majanga mengi, vifo vitatokea vingi kwa pamoja na mengineyo:

Uharibifu umedhihiri barani na baharini kwa sababu ya yale iliyofanya mikono ya watu, ili Awaonjeshe (adhabu ya) baadhi ya mambo waliyoyafanya, huenda wakarudi (wakatubia kwa MwenyenziMungu).
Ar-Ruum 30: 41

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwisha bainisha kuwa maafa yatakuwa ni mengi karibu na Qiyaamah:

“Saa (Qiyaamah) haitosimama hadi elimu ifutwe, wakati kukimbia kwa kasi, mitetemeko kuzidi kwa sana, fitna kutokea na al-Harj kuengezeka.” Akaulizwa, “Ewe Mjumbe wa Allah, nini hiyo al-Harj?” Akasema, “Al-Qatl, al-Qatl (Mauaji, Mauwaji)”.
Imepokewa na Imaam Ahmad

Na kwa vile maneno ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) pamoja na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) ni mazima; tujue kuwa mitihani hii ipo, na bila ya shaka kila tuliloahidiwa litatokea, ikiwemo Qiyaamah chenyewe. Kwa mantiki hiyo; tunatakiwa tustaghfiru na tujiweke tayari na kifo wakati wowote.

Hakuna mwenye mihadi (appointment) na Malakul-Mawt. Anakuja ule wakati anaopangiwa na Mola wake aje kuzichukua roho zetu. Wahaiti wale waliokufa kwa mpigo hakuna hata mmoja aliyejuwa kama siku ile angekufa, ya kwamba angekwenda nchi jirani kwa kukimbia mauti. Laiti ghayb ingejulikana na viumbe, Serikali ya Haiti ingekuwa na uwezo wa kuwahamisha watu wake kutoka kwenye eneo la epicenter kabla maharibiko hayajatokea.

Hili jambo liwaguse wanaosema: "acha ni-enjoy, mie kijana, bado damu inachemka kotekote". Waliokufa katika maafa uwenda walikuwemo vijana waliochemkwa na damu mpaka zikatokota kwa afya njema na uzuri. Na wale walionekana na maumbo madogo, hawakuwa ni mbilikimo (watu wafupi), bali ni watoto wadogo kuonesha kwamba kifo au maafa hayachagui umri.

Hili jambo pia liwaguse wenye uwezo wanaogoma kuhiji, wakisema kuwa watakwenda baadae. Nadhani, pengine katika mamilioni ya watu wale kuna ambao walikuwa na mawazo kama hayo japo mmoja na hakufanikisha malengo. Na hiyo ni khiyana kwa Allah mtakatifu tunamfanyia, kuwa Katupa uwezo na tunautumia kinyume na malengo ya Dini. Liwaguse hili jambo, wale wanaosema watajistiri... tusubiri... tusubiri kwanza...

Ni vyema nikakomaa hapa, kwani ni mengi tunayojifunza kutokana na mitetemeko hii ya ardhi. Mimi moyo wangu umeingiwa na khofu kubwa juu ya mauti na amali zetu, nimeingiwa na imani na watu waliopoteza viungo ambavo sisi tunavyo na badala ya kumshukuru Mola Mlezi wetu, hatuinami (hatusali) mpaka tuanguke (tufariki).

Nimeingiwa na imani kuona vitoto vichanga, wazee na wanawake na wengine wakikosa malazi na sehemu za kijihifadhi. Nimesikitika kwa kila hali na nikalia ndani ya moyo wangu.

Wa billahit Tawfiyq.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!