Monday 19 September 2016

HAKUNA WA KUKIZUIYA

Kwa hakika wewe utakufa, na wao watakufa. Kisha bila ya shaka mtagombana Siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu Mlezi.
Qur'an SURAT AZZUMAR [39]: 30-31

Hakika wewe, Muhammad, na wao wote mtakufa. Kisha baada ya kufa kwenu mtafufuliwa mbele ya Mwenyezi Mungu mkishitakiana nyinyi kwa nyinyi. 

Katika maisha yote Mwanadamu hapa ulimwengu, Wanaadamu wameuelewa ulimwengu wao katika nyanja mbalimbali za kisayansi. Tafiti mbalimbali zimefanyika ili kuweza kuelewa Ulimwengu na dunia yao.

Moja ya tafiti hizo ni kuhusiana na Umauti au kifo, yaani pale binadamu anapokosa uhai, ukiachana na sababu sababishi, yaani kama vile maradhi na ajali ni kitu gani haswa kinacho sababisha binadamu huyu kupoteza uhai wake.

Kutokana na kushindwa kwa njia zao mbali mbali za uchunguzi, ndio baadhi yao wamekuwa na fikra potofu kuwa uhai huu tulio nao ni kani tu na baada ya nguvu zake kwisha basi binadamu upoteza maisha yake na baada ya hapo hakuna tena kinacho endelea, yaani hakuna kitu kinachoitwa maisha baada ya kifo.

Imani hii ndio iliyozaa falsafa za kishirikina na za kilahidi za Ugiriki na dini za Sumeria za Misri ya kale.

Miongoni mwa vitu vyenye nguvu ambavyo Mwenyezi Mungu amevibainisha katika Qur’an ni umauti au kifo na ndio mwisho wa Binadamu hapa duniani.

Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, aliye juu ya waja wake. Na hukupelekeeni waangalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu humfisha, nao hawafanyi taksiri.
Qur'an Surat Al - An-A'am [6]:61

Sasa Nini neno Kifo au Mauti na kwa nini tunakufa au Inakuaje tunafariki?

Neno Kifo ni hali ya kukosa uhai wa kimaisha ya mtu au kiumbe aliyekuwa hai. Wataalamu wanatuambia kuwa kifo ni hali ya ukosefu wa utendaji kazi wa kibiolojia mwilini mwa kiumbe hai au kusimama kwa michakato muhimu katika seli au tishu za kiumbe hai. Hali hii usababishwa aidha na uzee(senescence), Magonjwa, kujiua au kuuliwa, uksefu wa chakula kama vile njaa, upungufu wa maji mwilini, majeraha yaliotokana na ajali n.k

Katika chunguzi za Kisayansi Wanasayansi wanatufahamisha kuwa 'Gene' aina ya (MYC au c-Myc), kuwa ndiyo yenye dhamana ya kushughulikia ukuwaji wa mwili wa binadamu na ndio hiyo hiyo yenye kusimamisha ukuwaji wa mwili wa binadamu. Hii Gene inapofikiwa tamati yake, usimamisha mfumo nzima wa cells za mwili, na kusababisha celi hizo kufa kidogo kidogo.

Kama vile binadamu alivyoumbiwa uhai vilevile ameumbiwa udhaifu kiasi cha kupatwa au kushambuliwa na maradhi mbalimbali,  kuanzia maradhi ya Kisukari, Saratani, presha na maradhi ya moyo, na mengineyo mengi.

Hali hii ya maradhi ni moja katika dalili za kuanza kujitaarisha na ile safari ilotajwa katika Surat Assajdah ayah 11.

Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliye wakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi.
Surat Assajdah [32]: 11

Kumbe kifo au umauti anao upata binadamu si mwisho wa uhai wake, bali ndio mwanzo wa uhai mwingine usiokoma, hali hii ambayo kila binadamu atakumbana nayo ndio ile hali ya sakaratil-Mauti.

Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha.
Qur'an Surat Al-Mulk [67]: 02

Japokuwa tunaambaiwa kuwa hali hii ya umauti ni kujaribiwa tu kwetu sisi, lakini ni katika hali ambayo ni ngumu sana kwa binadamu kukabiliana nao.

"Mtume (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) alipokuwa amelala katika tandiko la Mauti, ndani ya sakaratil mauti, alikuwa akijipangusa uso wake kwa maji ya baridi huku akiomba kwa Mola wake; "Ewe Mola nipunguzie maumivu ya kutokwa na roho".

Ikiwa Mtume wa MwenyenziMungu aliomba hivyo, kuna hali gani baina yetu sisi!?


Hali hii ya maumivu ya kutokwa na roho, ni hali ambayo binadamu itamkuta na kukabiliana nayo, hakuna mtu ambaye anaweza kujuwa maumivu ya kutokwa na roho zaidi ya muhusika mwenyewe.

Tuangalie madaktari na mabingwa wa utabibu wanasema nini kuhusu wagonjwa walioko kwenye sakaratil Mauti:

'Mgonjwa anaefariki kwa Matatizo ya hali uhalibifu wa viungo vya ndani ya mwili (organs), ambavyo vimepatwa na maambukizi, upelekea hali mbaya sana ya hatari ya shinikizo la damu na upungufu katika metaboli ya seli. Kunako sababishwa na uwepo wa bakteria wanao sababisha kutengeneza usaha au sumu katika damu au tishu za mgonjwa husika (sepsis). 

Mgonjwa huyu upata kitu kinachoitwa kwa kitaalam Septic shock na uhangaika na kufanya vishindo vingi sana, kwani wakati huo hutokezea mambo kadhaa, kama vile. 

Kuwa na homa kali, ikifuatiwa na mapigo ya moyo yanapiga kwa haraka sana, halafu matatizo ya pumzi yanaongezeka na hupata tabu kuzivuta, na tabu kubwa inamkabili, na ikipimwa damu yake itakutwa na upungufu wa hewa ya Oksije (Oxygenation).

Madakatari wakisha ona hali hiyo uchukuwa hatua kadhaa ili kumsaidia mgonjwa huyo.

Kwanza watamwekea mipira ya kumsaidia kuvuta pumzi ili aweze kuhema vizuri, lakini hata hivyo haisaidii chochote, na ikiwa hajapigwa sindano za kumlevya ili kumpunguzia maumivu basi utaona yeye mwenyewe ananza kupoteza fahamu, na hapo tena madaktari wanaweza kumpiga picha za 'CT scans' na 'ultrasounds', na kumfanyia kila aina ya uchunguzi wa damu yake ili kuchunguza sababu zozote za maambukizi kwenye damu yake.

Lakini kufikia hapo hawawezi tena kugundua chochote, hata watakapoitwa mabingwa wa fani mbali mbali za kiutabibu wa mwanaadamu, na wote hukusanyika hapo ili kuchangia maarifa yasiyokuwa na uhakika, na mgonjwa huwa anasafirishwa baina ya 'Intensive care' na 'X-ray department' ili kupata kuona kama kuna jambo limejitokeza, na ikipatikana dalili ya matumaini kidogo tu, labda homa imeshuka, basi kama yule mgonjwa anafahamu basi hupewa habari hiyo lakini zikipatikana habari mbaya, basi hizo huzuiliwa baina ya Madaktari.

Viungo kimoja baada ya kimoja kama vile Ini, uanza kupungua uwezo wake wa kufanyakazi, na katika hali hiyo Madaktari huanza kutizamana, na mgonjwa yuko kwenye maumivu makali mno, na matibabu yanaendelea ili kumnusuru mgonjwa na kifo, lakini sehemu muhimu za mwiili 'major organs' zote zinashaanza kusita kutenda kazi zake, na kama kuna matumaini labda ya ushindi japokua kidogo, lakini wakati mambo yote haya yanaendelea kuna kitu kinatokea bila ya kutarajiwa japokua jitihada yote inafanyika lakini Mabingwa wote walokusanyika huanza kwa huzuni kujitenga na yule Mgonjwa kwa kujua sasa Mauti yanakarubia. 

Ikiwa mgonjwa ana bahati kubwa, na machungu yakiwa makubwa sana basi hupoteza fahamu (huenda katika Coma) akawa hajui chochote kinachoendelea.

Familia yake inatoka katika ile hali waliyokuwa nayo ya wasi wasi, na kuingia katika hali ya ukataji wa tamaa au kuvunjika moyo, halafu huingia kwenye kukata matumaini kabisa.

Hapo tena wengine wanaanza kupanga mazishi. Hata Madaktari na Manasi tena hapo wanaanza kujiuliza wenyewe kwa nini wanadeleza kumpatisha tabu kiumbe yule, na wengine huendelea labda kwa matumaini huenda watashinda, lakini mwisho huwachia mkono, na hapo tena utaona hata wale Madaktari mabingwa machozi yanawamiminika, wanageuza uso ili Madaktari
wadogo wasiwaone. 

Hapo ndio Qurani inapouliza Surat Al-Waaqia'h [56]: 83-87

Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo, Na nyinyi wakati huo mnatazama! Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi. Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu, Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
Surat Al-Waaqia'h [56]: 83-87

Naam, Maprofesa ndio wamekusanyika, ugonjwa unajulikana basi mzuieni asitoke hiyo Roho, huku kidogo kidogo Malaika wanaendelea kuitoa Roho ya mwanaadamu na hakuna yoyote atoweza kuzuia. Hiyo ndio hali ya sakaratil Mauti.

Basi ujue ikiwa utakua mja mwema hali gani inakua wakati wa sakaratil mauti? Inakuwa hivi usije ukakata tamaa kabisa ukaona ndio umekwisha, laa ikiwa umefungamana na mambo mema ahadi gani unapewa?

"Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa."
Surat Fuss'ilat (H'a Mim Sajdah) [41]: 30

Hiyo ndio hali ya mwanaadamu kwa uchache, na ndivyo atavyokumbana na siku yake ya Mauti na wala haina kuepukika na wala haijulikani.

Tunapeana habari kama hizi ili hiwe zinduko kwetu sisi sote, kama umezama kwenye mambo na umesahau akhera basi ukumbuke haraka sana kwamba (As-Saffar-Tawila) Safari ni ndefu, ipo inatukusubiri.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!