Tuesday 29 November 2016

IRELAND 'INAONGOZA DUNIANI KATIKA MAADILI YA KIISLAMU WAKATI ZA NCHI ZA KIISLAMU ZIKIJIVUTA VUTA!

Tafiti zilizofanywa, zimeonyesha kuwa nchi ya Ireland ndio nchi iliyo bora na yenye kufata maadili ya Kiislamu ya fursa na haki, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa Mwaka 2014 ikiwa mbele ya nchi za Denmark, Luxemboug, Sweden, Uingereza, New Zealand na nchi zote za Kiarabu (Kiislamu).

Utafiti huo uliongozwa na Prof. Hussain Askari wa University ya George Washington nchini Marekani ikiwa na kichwa cha habari kisemacho "How Islamic are the Islamic Countries" Kwa Kiswahili kisicho rasmi twaweza kusema "Ni kwa Kiwango kipi Nchi za Kiislamu ni za Kiislamu" kwa maana ya kwamba Je ni Nchi zipi zenye Kufata Uislamu (Islamic Value) katika maisha ya kila siku?

Na utafiti ulionyesha kuwa nchi hizi za Ireland, Denmark, Luxembourg, Sweden, Uingereza na New Zealand na nchi zingine za Kimagharibi zinazotumia kanuni za Kimaisha za Kiislamu zaidi katika maisha yao ya kila siku, ukilinganisha na nchi ambazo zinajiita za Kiislamu.

Utafiti ulionyesha kwamba nchi pekee ambayo ni ya Kiislamu ambayo ndio imeongoza nchi zingine za Kiislamu ni nchi ya Malaysia iliyoshika nafasi ya thelathini na tatu (33) ikafuatiwa na Kuwait nafasi ya arobaini na mbili (42), ikilinganishwa na Marekani nafasi ya 15, Uholanzi nafasi ya 15, Ufaransa nafasi ya 17 na nchi ya Saudi Arabia ikishika nafasi ya 91, Uku Qatar ikikamata nafasi ya 111.

Utafiti huo, uliyochapishwa katika Jarida la Global Economy Journal, unaweza kuwashtua watu wengi na haswa Waislamu na wengi wetu tukijiuliza kulikoni...!?

Tunapaswa kuangalia kwa ukaribu hali halisi ya mambo na jinsi serikali zinavyo waudumia raiya zake.

Wengi wetu na Haswa sisi Waislamu tunafikiria ili nchi hiwe yenye misingi ya Kiislamu basi lazima raiya wake wawe wenye kusoma Qur’an, Kuswali swala tano kwa siku au kufunga mwezi wa Ramadhani na kufata SHARIA. Lakini tunasahau kuwa Uislamu hauishii kwenye mambo hayo tu na kusahau mfumo mzima wa maisha kwa sababu Uislamu ni njia halisi ya Maisha au ndio Mfumo wa Maisha kwa Wanaadamu wote na kwenye mfumo huo kuna mambo mengi sana na si Funga, swala au hijja tu peke yake.

Wengi wetu na haswa nchi tunazo ziona kuwa ni za Kiislamu raiya zake wamekariri Qur’an, Hadith, Sunnah na mambo kadhaa, lakini kwenye utekelezaji ndio tumeangukia kifudifudi. Japokuwa kila leo tunasikiliza hutba mbalimbali na mawaidha kadhaa wa kadhaa, lakini tumeshindwa kuyatekeleza kivitendo yale tunayoyasoma na kuyasikia kila siku na haswa Nchi za Kiislamu, ambazo nyingi ni za Kiarabu zimeshindwa kuyafanyia kazi maneno ya MwenyeziMungu na Mtume (saw) na kuyawacha kabisa na kukumbatia utaratibu waliojibunia wenyewe.

Matokeo yake nchi za Kimagharibi zimeokota ile lulu ambayo nchi za Kiislamu wameitupa na kuifanyiakazi.

Katika kutekeleza utafiti huo, wametumia maadili ya Uislamu katika maeneo kadhaa kiasi cha kuonyesha mafanikio ya kijamii, kiuchumi, utawala bora, haki za binadamu, wanyama na haki za kisiasa, na mahusiano na mafungamano ya kimataifa.
Wakati huo huo nchi nyingi za Kiislamu zimekumbwa na jinamizi la kiutawala, watawala wengi hawakuchaguliwa na nyingine zimeng’ang’ania ufalme na kutumia Dini (Uislamu) kama chombo cha ukandamizaji kwa wananchi wao.

Nchi nyingi za Kiislamu zimekumbwa na majanga ya ulaji wa rushwa, ukandamizaji, dhulma kwa wananchi, kukosekana kwa usawa mbele ya sheria, kukosekana kwa fursa sawa kwa ajili ya maendeleo ya binadamu, ukosefu wa uhuru wa uchaguzi (ikiwemo dini), licha ya utajiri walionao lakini umaskini umekuwa mwingi kwa raiya, serikali zimekuwa zikitumia nguvu kubwa kiutawala, Na mambo mengi ambayo hayakutarajiwa yafanyike kwenye nchi za Kiislamu.

Mfanyabiashara mmoja wa Kichina aliwahi kunukuliwa akisema: ;
"Wafanya biashara wa Kiislamu uja kwangu na kunitaka nifanye udanganyifu kwenye machapisho ya kimataifa kwenye bidhaa zao. Wakati huo huo mimi nikiwakaribisha chakula, wanakataa kwa sababu chakula changu si halali. Hivyo ni halali kwa wao kuuza bidhaa bandia ila kula chakula changu ni Haram?"

Muislamu mwenye asili ya Japan naye alinukuliwa akisema: "Mimi nimesafiri nchi za Kimagharibi na nikauona Uislam Ukitumika katika maisha ya kila siku kwa wasiokuwa Waislamu. Nikasafiri nchi za Mashariki, nikauona Uislam lakini sikumuona Muislamu yoyote. Namshukuru Allah niliujua Uislam kabla sijajua matendo ya Waislamu."

Dini ya Uislamu haipaswi kubakizwa kwenye sala na kufunga tu. Bali Uislamu Ni njia ya maisha na ni jinsi vile sisi tunaishi na kuwatendea wengine.

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) amesema:
Mnamjua nani aliyefilisika? Wakasema (Maswahaba): Aliyefilisika ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na diraham au mali. Mtume (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) akasema: Aliyefilisika katika umma wangu ni yule atakayekuja siku ya Qiyaamah na Swalah zake, Swawm zake na Zakah zake, lakini atakuja akiwa amemtukana huyu, amemtuhumu huyu, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya huyu na amempiga huyu, yatachukuliwa mema yake na kulipwa wale aliowadhulumu. Yatakapomalizika mema yake kabla ya kufidia madhambi aliyowakosea wenzake, zitachukuliwa dhambi za wale aliowakosea kisha atajaliziwa yeye na mwishowe atakuwa ni wa kutupwa motoni.
[At-Tirmidhiy]

Je Waislamu ni yepi katika hayo ambayo tume epukana nayo!?

---

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!