Monday 15 May 2023

 HIVI KWELI NILIKUFA AU
NILIUWACHA TU UHAI KWA MUDA!?

  •          Naamini Kabisa, Nilikufa Kwa Dakika Kadhaa, Ilikuwa ni Hali ya Kushangaza na Kustaajabisha Mno!
  •       Ni Tukio Lililotokea Zaidi ya Miaka Kadhaa Nyuma, Kabla ya Mabasi ya Mwendokasi...

Siku hiyo ilikuwa kama siku zingine tu zisizo na majina, ile hamu ya katembea kwa miguu na ile taswira ya jiji la Dar, ilisawiri barabara kwenye bongo langu.

Kama kawaida ya mitaa mingi ya Kariakoo, kumejaa watu wa kila aina. Nikapita kwenye mitaa iliyosongamana watu nikishajika huku na kule, nikakumbuka kufuchama Rununu yangu, kwa kuchelea wivi, wasijeichukua bila ruhusa yangu, huku sauti za wabeba mizigo kwenye Rikwama, wakiyosayosa maneno ya kutiana nguvu.

Nikapishana na msukuma rikwama mmoja akanitolea maneno ya kuudhi, sikumjali! Upande mwingine kuna Bodaboda zinafukuzana, nikazikwepa nisipigwe dafrao...!

Huku nikijiwazia, "...hawa waendesha Bodaboda wamekuwa watu wa ajabu sana, ni watu wenye kudhania kuwa wao wana haki ya barabara na hata pembeni ya barabara kuliko mtu mwingine yoyote, na sheria za barabara haziwahusu..."

Ghafla bin vuu..! Nikajikuta napaa hewani, usawa wa futi kadhaa, nikabakia naelea hewani, huku makelele ya watu na kina mama wakiwa kwenye shake kubwa... "Mtumeee...! Kashauwa, Tobaaa yaillahi kijana wa watu..."

Sikumbuki ni nini kilitokea, ila nilicho kiona mpaka leo nikikikumbuka naingiwa na shakawa kubwa yenye kutetemesha mwili wangu na moyo kuingiwa na hofu, kiasi cha kuunyogesha.

Tahamaki nikaona watu kwenye tahanani, huku wametaharuki, wakijikusanya kumzunguka mtu aliyelala pembeni mwa barabara, nikamsikia mdada mmoja akisema, "…Kagongwa na Bodaboda...!"

Kitu cha kwanza kunistaajabisha, ambacho mpaka leo sijui jinsi ya kukielezea wala kuolelezesha, ni ile hali ya utulivu na amani niliyokuwa nayo muda ule. Nilikuwa namuonea huruma kila mtu, kama vile wanapoteza muda wao tu hapa duniani.

Kitu cha pili ambacho kilishtua roho yangu, ni pale nami nilipotaka kujisogeza kuelekea kwenye akhlaki ya ule mkusanyiko... Badala ya kutembea nilikuwa kama mtu anae elea na kujisogeza mzima mzima, sikuwa nakanyaga ardhi, nilihisi wepesi ambao sijawahi kuupata kwenye maisha yangu.

Kuna kitu kilinipelekea nione upande wa machweo ya jua, nikaona viumbe visivyo elezeka, kama vile vinaashiria nisiende huko walipo... Sawia wengine wakiniita nielekee walipo wao, wakiwa upande wa Kaskazini wakiwa na maumbo yenye kupitisha mwanga, mfano wa Jeli...!

Matendo yote hayo yalitokea sanjari...! Nikastaajabia uwezo ule wa kuona pande zote bila kugeukageuka!

Ile hali kwanza haikujisajili kwenye bongo langu, ni mpaka pale nilipojisogeza kwenye lile kusanyiko. Nikapitiliza bila kugusana na mtu yoyote yule, ndipo hapo sasa mshituko mkubwa ulipo nipata.

Nilishuhudia mwili wa mtu ukiwa umelala pembeni karibu na mtaro wa maji, huku mtu mmoja Shaibu mwenye mwili wa ajabu, akijitahidi kushajiishika kutoa huduma ya kwanza, huku akiwazuiya vijana sefule mashakili, wasipenyeze vidole vyao kwenye mifuko ya suruali iliyovaliwa na ule mwili.

Nikamkumbuka yule Shaibu, ni mmoja wa wazee wa mitaa ya kule Gerezani, ni katika jamaa zetu, ananifahamu nami namfahamu, lakini jinsi alivyo kama vile yupo tofauti na watu wengine (Nilikuja Kufahamu Baadae, Kwanini Nilimuona yupo Vile).

Yule Shaibu, alikuwa akinihita kwa jina langu na lababa yangu (Fulani Bin Fulani), huku akishahiri watu wasimamishe gari waupeleke mwili hospitali. "...Simamisheni gari tumpeleke hospitali haraka, huyu bado mzima, mwili ungali moto, si wa ahera huyu..."

Nadhani watu wengine walimuona ni wa kawaida tu, la sivyo, asingesogea mtu karibu yake…!

Nikataka kumwambia kuwa nipo hapa, pembeni lakini sauti haikutoka, maana hata hao watu wengine, wakinipita bila kunikwepa, kama vile mtu anapishana na upepo...!

Ule Mwili Pale Chini, Ulikuwa Ni Mwili Wangu...!

Wakaunyanyua ule mwili na kuupakia kwenye gari la mizigo, Toyota Pickup, ajabu nyingine ni pale nilipo ona ule mwili umeunganishwa na nafsi yangu au sijui niseme ndio roho yenyewe (Wallahi hata sijui ni kitu gani), kimefanana na kama uzi mwembamba hivi wa ajabu, wenye rangi niseme kama nyeupe au rangi ya fedha pamoja na rangi ya Zambarau hivi lakini yenye kupitisha mwanga, kiufupi niseme kama uzi wa kioo wenye kumetameta, wenye kufanana na mwanga au umeme wa radi.

Uzi au kamba ile nyembamba sana ilikuwa imeniunganisha mimi na mwili ule, kupitia kwenye kitovu... Nikajikuta nipo sawia na mwendo wa gari. 

Kupitia barabara ya Msimbazi, kisha barabara ya Uhuru, kuelekea hospitali ya Amana.

Yule Shaibu akaweka mkono wake mmoja kwenye kichwa cha ule mwili kwenye utosi, na mkono mwingine akashika vikidole gumba vya miguu wa kulia na kushoto, kisha akatamka shahada (la 'ilaha 'illa-llahu akitaja na majina mengine ya MwenyeziMungu, Ar-Rahmaan, Ar-Rahiim, Al-Aziiz, As-Samii, Al-Basiir, Al-Wahhaab, Al-Baasit, Al-Ghafuur, Al-Hafiidh, Al-Mujiib, Al-Waduud, Al-Ba’ith, Al-Mu’id, Al-Muhyii, Al-Hayy, An-Nur, Al-Barr, At-Tawwab, Al-‘Afuww, Dhul-Jalaali Wal-Ikraam, Mrejeshe… ).

Akabonyeza kwenye chembemoyo, kwenye mbonyeo ulio baina ya gegedu la mifupa ya mbavu, katikati ya kifua cha mwili ule (mwili wangu), kwa kidole gumba chake, kwa lengo la kusisimua mapavu na moyo wa ule mwili, viweze kurejea kwenye kazi yake...!

Kila alipokuwa akikandamiza kifua cha mwili ule baina ya gegedu na utosi, huku nami nikajikuta naukaribia ule mwili...!

Ni kama vile alikuwa anavuta ule uzi ulioniunganisha mimi na ule mwili...!

Ghafla polepole nikaanza kuhisi kupotelewa na uwezo wa kuona na kusikia, sikusikia chochote, kama vile ninayepoteza fahamu na kuzama kwenye rima, lisilo na mwisho, macho hayakuona kitu... Huku ule uzi ukinivuta na mimi kwa haraka sana kama mtu anayevutwa na nguvu kubwa kelekea ulipo mwili wangu…!

Nilikuja kushituka nipo Hospitali ya Muhimbili, nilikuja kuambiwa kuwa, baada ya ile ajali, wasamalia wema, walinipeleka Hospitali ya Amana, kisha kuhamishiwa hospitali ya Muhimbili.

Uzuri vipimo vilionyesha kuwa sikuathirika sana, kule kupoteza fahamu ni baada ya kujipigiza kichwa kwenye lami.

Kumbe nilipoteza fahamu kwa siku mbili.

Siku ya tatu, baada ya kutoka hospitali, nilimuulizia yule mzee aliyenisadia (Nikamtaja kwa jina), nikaambiwa kuwa, uwenda nimemfananisha tu, maana huyo mzee mbona, alisha fariki siku nyingi sana, ni zaidi ya miaka kumi sasa tangia amefariki...! Kidogo nizimie tena...!

Ndugu zangu, kweli roho zipo, maana zile dakika kadhaa, niliona mengi sana, niliyaona yasioweza kuonekana kwa macho ya kawaida, MwenyeziMungu alifungua pazia la macho yangu ya rohoni, nikaona yasiyo onekana kwa macho ya kawaida.

Kiukweli wala sijui ni kwa jinsi gani naweza kuyahadithia mambo yale yote...!

Nilipotoka hospitali, nilikuja kutafuta kufahamu maana ya yale maneno ya Shaibu yule... Nikayaelewa...!

Wednesday 15 February 2023

TETEMEKO LA ARDHI NCHINI UTURUKI NA SYRIA

Kahramanmaras Lasababisha Watu Zaidi ya Elfu Ishirini na Nane Kufariki Dunia.

Maisha ya Dunia sio Chochote Mbele ya Muumba na Yaweza Kukatika Ghafla Bila ya Kuletewa Taarifa. Tuna Amka Tukilala Tukiwa ni Wenye Kusindikiza Vijana kwa Wazee Kwenye Makazi ya Milele Wakipitia Ndani ya Barzakh.
Zipo njia nyingi za kukatika maisha haya kama vile ajali, maradhi na mauaji.
Hata hivyo, kuna aina nyingine ambayo kwa karne mbili hizi zilizopita, imepamba moto. Ni hii ardhi yetu tunayoringa nayo kushindwa kabisa kuhimili mambo. Hapo tunaona kimbunga, mitetemeko ya ardhi ya kiwango cha juu, joto na baridi kali na balaa kadha wa kadhalika.
Ardhi ya Nchi ya Uturuki na Syria imetikisika, na huu ni mfano mzuri wa kuwazinduana ndugu zengu Waislam. Hakika kuna mengi ya kujifunza kwa sisi Waislam kutokana na matetemeko haya ya ardhi, na haswa matetemeko yaliyotokea tarehe za hivi karibuni, mwezi huu wa February 2023, ni tetemeko lenye ukubwa wa Kiwango cha 7.8 magnitude katika nchi hizo mbili.
Maisha ya watu wasiopungua watu elfu 28 yamepotea ghafla bila ya matarajio.
Na maelfu ya watu wamejeruhiwa na majumba na mali kadhaa zimeharibika. Ile siha na neema aliyowapa Allah imeondoka kwa wepesi kabisa.
Maelfu ya maisha ya watu yamebadilika ghafla ndani ya kipindi kisichozidi nusu saa...!
ALLAHU AKBAR!
Yapo wapi macho ya Waislam kutanabahi kiumbe hichi kinachoitwa ardhi kushindwa kuhimili mambo ya wanaadamu!?
Hali ya huzuni, majonzi na masikitiko imewezwa kupugua kidogo na faraja kupatikana kwa waanga wa tetemeko ilo, pale ubinaadamu na moyo wa kusaidia haraka, ulipojitokeza aidha kupitia serikali zao na serikali za nchi nyingine na mashirika binafsi ya kujitolea.
Hata kwa wale waliokuwa hawana uwezo, nao wanajitolea kusaidia ndugu zao.
Sisi Waislam leo uwezo tunao, badala ya kusaidiana tunaleta jeuri ya neema tuliopewa.
Ni funzo kwa Waislam kuwa Maneno ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) hayaanguki abadan, kuwa siku za mwisho kutakuwa na majanga mengi, vifo vitatokea vingi kwa pamoja na mengineyo:
Uharibifu umedhihiri barani na baharini kwa sababu ya yale iliyofanya mikono ya watu, ili Awaonjeshe (adhabu ya) baadhi ya mambo waliyoyafanya, huenda wakarudi (wakatubia kwa MwenyenziMungu).
Ar-Ruum 30: 41
Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwisha bainisha kuwa maafa yatakuwa ni mengi karibu na Qiyaamah:
“Saa (Qiyaamah) haitosimama hadi elimu ifutwe, wakati kukimbia kwa kasi, mitetemeko kuzidi kwa sana, fitna kutokea na al-Harj kuengezeka.” Akaulizwa, “Ewe Mjumbe wa Allah, nini hiyo al-Harj?” Akasema, “Al-Qatl, al-Qatl (Mauaji, Mauwaji)”.
Imepokewa na Imaam Ahmad
Na kwa vile maneno ya Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) pamoja na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa salam) ni mazima; tujue kuwa mitihani hii ipo, na bila ya shaka kila tuliloahidiwa litatokea, ikiwemo Qiyaamah chenyewe.
Kwa mantiki hiyo; tunatakiwa tustaghfiru na tujiweke tayari na kifo wakati wowote.
Hakuna mwenye mihadi na Malakul-Mawt. Anakuja ule wakati anaopangiwa na Mola wake aje kuzichukua roho zetu. Waturuki na Wasyria wale waliokufa kwa mpigo hakuna hata mmoja aliyejuwa kama siku ile angekufa, ya kwamba angekwenda nchi jirani kwa kukimbia mauti. Laiti ghayb ingejulikana na viumbe, Serikali ya Uturuki na Syria zingekuwa na uwezo wa kuwahamisha watu wake kutoka kwenye eneo la hatari kabla maharibiko hayajatokea.
Hili jambo liwaguse wanaosema: "acha ni-injoi, mie kijana, bado damu inachemka kotekote". Waliokufa katika maafa wamo vijana waliochemkwa na damu mpaka zikatokota kwa afya njema na uzuri.
Na wale walionekana na maumbo madogo, hawakuwa ni vibete au mbilikimo, bali ni watoto wadogo. Hii ni kuonesha kwamba kifo au maafa hayachagui umri.
Hili jambo pia liwaguse wenye uwezo wanaogoma kwenda Hijja, wakisema kuwa mambo bado, ipo siku nitakwenda ilihali uwezo anao.
Nadhani, pengine katika maelfu ya watu wale kuna ambao walikuwa na mawazo kama hayo japo mmoja na hakufanikisha malengo. Na hiyo ni khiyana kwa Allah mtakatifu tunamfanyia, kuwa katupa uwezo na tunautumia kinyume na malengo ya Uislamu.
Liwaguse hili jambo, wale wanaosema watajistiri... tusubiri... tusubiri kwanza...!
Ni vyema nikakomaa hapa, kwani ni mengi tunayojifunza kutokana na mitetemeko hii ya ardhi na maafa mengine ya kiasili.
Mimi moyo wangu umeingiwa na khofu kubwa juu ya mauti na amali zetu, nimeingiwa na imani na watu waliopoteza viungo ambavo sisi tunavyo na badala ya kumshukuru Mola Mlezi wetu, hatuinami (hatusali) mpaka tuanguke (tufariki).
Nimeingiwa na imani kuona vitoto vichanga, wazee na wanawake na wengine wakikosa malazi na sehemu za kijihifadhi.
Nimesikitika kwa kila hali na nikalia ndani ya moyo wangu.
Wa billahit Tawfiyq.

Monday 6 February 2023

 GANDA LA HARAGWE KWENYE JINO

Huku kazini, tulikuwa na mkutano wa kuongelea ufanisi utakaopelekea natija kwenye kazi zetu za Kila siku. Nilikuwa ni mtakadamu kwa siku ile, kwa wanao wasilisha mada...

Kabla sijaingia kwenye chumba Cha mkutano, nikapitia maliwatoni, nikachua na udhu Ili nipate faradhi kabla ya mkutano kuanza. Wakati najiangalia kwenye kioo nikipaka mafuta kupunguza ukavu wa ngozi na baridi, wakati nafanya mkaguo, tahamaki nakenua kinywa, nakutana na twasira ya Ganda la Haragwe limeganda kwenye jino.

Kumbukumbu zangu, zilichelewa kidogo kusajili tukio la mimi kula maharagwe. Ni baada ya sekunde kadhaa, nikakumbuka kuwa nilikula maharagwe na tambi, takriban siku tatu nyuma.

Lile ganda lilinitafakarisha sana, kwanza nashukuru nililiona mapema kabla ya mkutano, maana ningekuwa kituko cha siku kama si wiki nzima, Alhamdulillah tahayuri iliniepuka.

Fikiria mtu unaweza kula chapati na MAHARAGE majira ya asubuhi, ukasindikiza na chai vikombe kadhaa... Ukasukutua kinywa mara tatu...

Mchana ukala ugali na nyama, Ukasindikiza na maji ya matunda, Usiku ukala zako boflo na chai tu...

Kabla ya kwenda kulala, ukapiga mswaki, meno umeyasugua vizuri, bila kusahau ulimi, ukausugua mpaka kwenye koromeo, kisha ukasukutua tena na tena...!

Asubuhi, kabla ya kuwahi kazini unasafisha kinywa kwa kusugua meno vizuri na kusukutua mara tatu, unafika kazini, unacheka na jamaa zako, ghafla tu, wanaona Ganda la Harage kwenye Jino lako la mbele, tena harage lenyewe ni la juzi...!

Kwenye tafakuri yangu, nikagundua mfanano wa sisi viumbe binadamu na Ganda la Harage kuganda kwenye jino.

Na ndivyo binadamu tulivyo, waweza kutendewa wema, ihsani na kila zuri, lakini si sababu ya wewe kutosengenywa, wala si sababu ya wewe kutochukiwa, fanya ufanyalo, utaingia midomoni mwa waja kwa njia hisiyo pendeza kwenye masikio yako.

Ndio, Kuna Viumbe Hapa Duniani, Wapo Kama Ganda la Haragwe...!

Hakika tumefanikiwa katika ili la kutopendana na kuhishimiana, tumefanikiwa kueneza chuki miongoni mwa jamii zetu, si Waislam, si Wakristo, si Wapagani, na huko kwenye siasa za Kisekula ndio kabisa kumeoza, kiasi tumekuwa mbilikimo wa kifikra, tumefanikiwa katika kugawanyika miongoni mwetu na sasa tupo zaidi kimakundi, na wale ambao hawapo kwenye makundi au jumuiya yetu basi huyo si mwenzetu.

Tutamtia midomoni kwa maneno ya uongo na kashfa, mpaka apate shinikizo la moyo na jirani yake mapafu, kama si la figo na maini yake...

Tabia hizi kwa kweli zimemea kwenye nafsi zetu na zimendoa mafungamano ya kirafiki na kindugu na kusababisha majadiliano yetu hukosa busara na hikma kiasi cha kupelekea kwenye utengano na uhasama ambao tunaweza kuuepuka.

Mnisamehe tu, uzee huu, yote haya sababu majuzi nilikula maharagwe, ganda likabakia siku nne kinywani, kweli jitihada haishindi kudura, na takadiri huwezi epuka.

Sunday 8 January 2023


WAZIMU WA MADEREVA WA BODABODA

Hivi Waendesha Pikipiki Maarufu kwa Jina la Bodaboda, Bongo zao ni Zile za Zinjanthropus!?
Safari ya Kutoka Kariakoo Mpaka Sinza, Kwa Siku Moja tu, Nilishuhudia Ajali Saba za Bodaboda. 

Nilipopata likizo yangu ya mwaka, nikafunga safari kwenda Bongo, baada ya kuondoka takriban miaka na miezi kadhaa, kwa kweli nilikuwa na hamu kubwa sana ya kukutana na ndugu, jamaa, marafiki na majirani zangu. Na haswa ukizingania ni miaka imepita na uku hamu yangu kubwa kuona jinsi gani usafiri wa Bodaboda na Bajaj ulivyo shamiri jijini Dar.

Mengi nilisimuliwa kuhusiana na madereva wa Bodaboda na jinsi wanavyoendesha biashara zao, nami nikawa na hamu ya kulinganua na pia kushuhudia kwa macho ni kipi haswa kina ukweli katika hayo masimulizi.

Nakumbuka kuwa Pikipiki zilianza kutumika nchini Ujerumani katika karne ya 19. Ulikuwa usafiri uliokuwa mpya lakini ulirahisisha kuabirisha hasa ukikumbuka watu wa huko wakati huo wengi waliwatumia hayawani kwa ajili ya usafiri.

Huku kwetu enzi ya Mkoloni Muingereza ndio pikipiki zilianza kusambaa sana na kati ya pikipiki zilizopendwa zilikuwa za aina ya BSA kutoka Uingereza, pikipiki hizi zilipata jina kutoka kampuni iliyokuwa inazitengeneza iliyoitwa Birmingham Small Arms Company.

Baada ya Uhuru pikipiki za Honda, Suzuki kutoka Japan na Yamaha, zilipata umaarufu sana, pia kulikuwa na pikipiki aina ya VESPA toka India na BATAVUS za Mdachi nazo zilikuwa maarufu sana hapa nchini.

Umaarufu wa pikipiki ulipelekea serikali kuwapatia Makatibu Tarafa, Mabwana Shamba na watumishi wengi wa serikali pikipiki aina ya Honda 90 na baadae zikaletwa Honda 125. 

Pikipiki hizi zilikuwa ni imara kweli kweli, haswa Honda 90, maana zina uwezo hata wa kufungiwa jembe ulaya (plau) na ukalima kwa kutumia pikipiki.

Miaka yote hiyo waendesha pikipiki walikuwa watu wastaarabu walioheshimika na kuheshimu sheria za barabarani. 

Miaka hii michache zimeingia pikipiki za Kichina, ambazo zimezagaa kwenye biashara inayoitwa Bodaboda.

Waendesha bodaboda wamekuwa watu wa ajabu sana, ni watu wenye kudhani kuwa wao wana haki ya barabara na hata pembeni ya barabara kuliko mtu mwingine yoyote, na kuwa wao sheria za barabara haziwahusu.

Hawa ni watu wanaoamini kuwa ukipiga honi tu inatosha kuyafanya magari, majengo na hata miti kuhama na kuwapisha wao wanapotaka kupita. Kiukweli kwa siku chache nilizokaa likizoni, nilishuhudi mamia ya vijana wakijeruhiwa na wengine kufariki kwa ajaili za kizembe za kila siku za usafiri huu.

Mie naiomba serikali ifanye uchunguzi wa kina kabisa, hivi kwanini watu wakiendesha hizi pikipiki za Kichina akili zao zinahama? Kwanini hizi Pikipiki za Kichina zimewekwa nini mpaka Bongo za waendeshao hizi pikipiki zinakuwa kama za Zinjanthropus!

Mimi na mashaka na sponji inayotumiwa kwenye viti vya Bodaboda, inawezekana ina madini ambayo yakimuingia anae iendesha akili inahama.

Serikali ifanye uchunguzi wa wasiwasi wangu huu. Kwa kuwa sioni sababu kwanini waendeshaji wa zamani walikuwa hawapotezi akili, ila hawa wa Bodaboda akili zao, zinakuwa sio kabisa, hisije kuwa Wachina wana mpango wa kando kutupunguza, ili wahamie Afrika maana... Mmmh!

Wednesday 4 January 2023

MBIOMBIO NIKAJIKUTA NALIKIMBILIA GARI LA KUZOA TAKA

Nilikutana Naye Kwa Kinyozi... Akauliza, Kwa Unyenyekevu Kabisa..!
Basi bhana, Nipo Zangu Varandani, Mida ya Saa Tatu Hivi ya Asubuhi, Ghafala Huko Nje Nikasikia mlio wa Gari ya Kuzoa Takataka. Nikakumbuka Kuwa Nilipaswa Kutoa Pipa la Taka Tangia Jana Usiku... Nikakurupuka kama Swala aliyekoswa koswa na Simba.
Mbiombio nikapitiza uwani, nikakutana na rasharasha za mvua, uku nikijikwaa kizingitini, sikujali sana, nikakamata kishikio cha pipa, nakaliburuza mpaka nje.
Natoka gari lishapita, lipo takribani nyumba ya Tatu toka kwangu.
Sikukata tamaa, nikapiga mbinja, huyo mbiombio nakimbiza gari wanguwangu, kandambili imenichomoka mguuni wala sina habari, kufika ni hoi, nahema kama Mjombakaka aliyekoswa koswa kunyakuliwa na Kipungu.
Nilipo wafikia mmoja wa mzoa taka, akanambia kuwa si gari hili, wao ni wa kampuni nyingine... Nikajikuta nimechoka mara dufu.
Mbio za mita kumi na tano kama si ishirini, zilinifanya niwe hoi taabani, polepole nikajirudia zangu nyumbani, nikaokota ndara yangu iliyonichomoka wakati wa kukimbiza gari la taka, nikajigundua kumbe nimelowana...!
Nikajifuta maji, nikakaa zangu sebuleni, nikajitafakari, nikakumbuka ni siku tatu tu, tangia watu washeherekee mwaka mpya.
Nikakumbuka mengi, yaliopita kwenye maisha yangu, mtu mie niliyekuwa hodari wa mbio, leo hii mita ishirini zimenitoa kamasi...!
Mawazo yakanichukuwa, yakanipeleka siku ya mwaka mpya...
Ilikuwa baada ya kumaliza Faradhi ya salah ya insha, nimekaa na Memsapu wangu, tukiongea na kucheka na huku tukitafakari jinsi Mwaka ulivyopita. Kwa mbali tukasikia sauti za Fashfashi, huku mwanga ukimemetuka. Tukakumbuka kuwa kumbe mwaka umeisha, watu wanashereheka huko nje kwa kumaliza mwaka.
Vijana wangu wakatoka hapo nje, kuangalia fashfashi, zikimemetuka angani. Dakika hazikwisha, nikakatizwa na mlio wa simu ya mkononi. Triiii! Triiii! Triiii...! Kuangali kumbe zilikuwa ni meseji zikiingia mfurulizo. Nikawa najiuliza kuna nini tena mbona meseji nyingi kiasi hiki!?
Nikaamua kuzisoma moja baada ya moja, na meseji zote zikinitakia salamu za mwaka mpya, wenye amani na maisha mema.
Nikajikuta nakumbuka kisa kimoja kilichonipata kabla ya ule mwaliko toka kwa Sahibu yangu, takribani siku sita zilizopita.
Siku hiyo nilipitia kwa Kinyozi kwa dhumuni la kupunguza kidogo nywele na kukata sharubu zangu, maana nazo zilikuwa ndefu, kama Gari Moshi la kuelekea Kigoma.
Baada ya kuchakachua mwendo nikafika kwa Kinyozi, mitaa ya Kariakoo, kumekusanyika vijana kadhaa, wapo wanaosubiri kunyolewa na wapo wenye kupiga ndaro na ndarire za hapa na pale.
Wakati nasubiri zamu yangu, macho yangu yakagongana na mzee mmoja wa makamu hivi, kakonga kiasi chake. Kumtazama vizuri na kuchakata sura yake, nikahisi kumkumbuka.
Ndio Huyu huyu, alikuwa mmoja wa vijana niliosoma nao sekondari, nikamkumbuka kijana mmoja maungo makakamavu, rangi maji ya kunde, nakumbuka nikimtania kwa jina la Andunje. Tulikuwa wote darasa moja ni zaidi ya miongo mitatu sasa imepita!
Ila sasa ndani ya nafsi yangu nilikuwa bado najiuliza, ndio huyu, kijana aliyekuwa akisumbua sana kwenye masomo ya Hisabati pamoja na yale ya sayansi!?
Nikamtazama tena na tena, hakuonyesha kunikumbuka hata kidogo nikataka kumpotezea, lakini upande mmoja wa bongo langu, likanishauri  vingine. Nikatizama kichwa chake, kilichokuwa kimejaa mvi za hapa na pale, uso wake wenye makunyanzi.
Kwa jinsi alivyozeeka, asingeweza kabisa kuwa ni yule kijana niliyesoma naye darasa moja, nikajiliwaza kwa kujisemea moyoni, labda uwenda ni baba yake mdogo au ni watu tu wanarandana!
Zamu yangu ikawadia, nikajisogeza na kukalia kiti cha kinyozi, nikamuelekea jinsi gani nataka... Baada ya kumaliza na kulipa, nikapiga moyo konde na kujipa ujasiri, nikamsogelea na kumuuliza kama aliwahi kusoma shule niliyosomal?
Huku nikimkazia macho nikamuuliza, "Samahani ndungu, wewe ulisoma shule fulani hapa jijini Dasalama!?" Naye akanitazama kwa umakini bila ya kupepesa macho kisha akanijibu "Ndio, nilisoma pale..."
"Ulimaliza mwaka gani?" Nikamuuliza kwa mashaka kidogo!
Akajibu, "Mwaka 1990. Vipi kwani?" Naye akaniuliza!
Nikamakwa, "1990? Ulikuwa kwenye darasa langu!" Nikatamka, na huku mshangao wangu nikiuonyesha wazi kabisa, kwa yeye kutonikumbuka.
Akanitazama kwa muda, kama vile haamini ninachosema... Kisha sasa, Hapo ndipo nilipochoka kabisa, yaani yule babu wa watu akaniuliza, kwa unyenyekevu kabisa, "Samahani, hivi wewe ulikuwa Mwalimu wangu wa somo gani!? Maana mpaka sasa sijakukumbuka bado..."
Nikataka kumjibu kuwa mimi ni Classmate wake, ila kuna kitu kikanizuiya, akili ikafanyakazi kwa haraka sana, nikajisemea kimoyomoyo...
"Mungu wangu! Kumbe Nimechakaa Zaidi Yake, Kiasi cha Yeye Kuhisi Kuwa Miye Nilikuwa Mwalimu Wake... Nikabakia Mdomo Wazi Ukitetema, Huku Kinywani Nikihisi Tewengu, Nadhani Nyongo Ilitema Ghafla!"

Hivi Mwaka Mpya Huwa Tunasheherekea Nini Haswa, Kuzeeka!? 

Saturday 24 December 2022

 WEWE UNGEFANYA NINI

NA UNGEJISIKIAJE!?

Hatoki Mtu Hapa... Mpaka Niupate...!

Sikukuu hii, nilipata mwaliko toka kwa sahibu yangu mmoja, hayati ya ujana wetu tulikuwa wanagenzi katika moja ya shule ya awali, jijini Dar, Gerezani, Kariakoo.

Sahibu yangu huyu imepita miaka mingi hatujaonana, kuonana kwetu ilikuwa kwa nasibu, wiki moja nyuma, nikiwa zangu kwenye harakati za hapa na pale, nikasikia sauti ya mtu anasalimia.

"Kakaa salamaa," akamalizia kwa kuniita jina langu... Kugeuka nakutana na sura ya mtu ninayo ijuwa, ijapo wajihi wake amebadirika, kiribatumbo cha haja, kama kabaila shamba. Lakini sura yake ingali ileile.

Tukasalimiana kwa bashasha, tukakumbushana mengi enzi tukiwa darasani, tukawakumbuka wanagenzi wenzetu waliokuwa watundu, na wale walimu visirani.

Tukaagana kwa yeye kunipa muhaliko, sikukuu hii, niende kwake kumtembelea, ili nami nipate nafasi ya kuiona familia yake, ana mke na watoto watatu.

Siku ikafika, nikachapa lapa, kiguu na njia, nikikatiza mitaa, ni mida ya adhuhuri, baada ya mshuko, jua si kali, ila fukuto la joto, lililotokana na wingu la mvua iliyogoma kunya, lilisababisha kero kidogo kwa wengi wetu tuliokuwa tukitembea kwa miguu, sako kwa bako kuelekea maeneo tofauti.

Baada ya kusubiri kwa dakika kadhaa kituo cha basi, nikapanda moja ya mabasi, maarufu kwa jina la Daladala, abiria ni wengi, siku kama hizi za sikukuu, wengi upendelea kwenda kwenye fukwe za bahari, kuvinjari, nadhani ndio sababu iliyopelekea wingi wa watu kwenye basi na haswa vichugandevu na watoto. Baada ya mwendo wa dakika zisizopungua 25, nikafika safari yangu.

Jamaa yangu ni mtu na familia yake, anaishi na mkewe na watoto zake kadhaa, pamoja na ndugu zake na wafanyakazi wa ndani.

Ma shaa Allah, nyumba yake nzuri, imezungushiwa ukuta mrefu wa futi saba na ushee, mbele kuna geti na kibaraza cha mlinzi. Nyumba imependeza na ina watu kiasi wasiopungua 8 kwa ujumla.

Rafiki yangu ni mtu mwenye uwezo wake kifedha nadhani kutokana na cheo chake serikalini...

Nimefika kwake nikakaribishwa vizuri kwa bashasha, baada ya salamu za hapa na pale, na mazungumzo haya na yale ya enzi tukiwa shule, huku tukijiburudisha kwa sharubati, nikaomba ruhusa niende msalani.

Uzuri wa hizi nyumba, vyoo, Maliwato na Mekoni ni humo humo ndani, wakati nipo msalani nikasikia sauti ya mkewe akilalamika kupotelewa kwa Mkufu Wake wa Dhahabu.

Sikujali sana, nikamaliza haja zangu, baada ya kujisafi, nikatoka zangu na kurudi varandani nilipokuwa nimeketi na mwenyeji wangu, nikawakuta wakazi wa nyumba ile wote wamekusanywa pamoja. Na mara mke wa sahibu yangu anawauliza kwa sauti alio wakusanya, nani kauchukua mkufu wake.

Kila mmoja anakataa, wanasema kuwa hawajui mahala wapi mkufu ulipo, naye bila ajizi akasema kwa ukali tena kwa sauti iliyobeba msisitizo wa herufi kubwa "HUMU NDANI HAKUJAWAHI KUPOTELEWA NA KITU HATA SIKU MOJA, MTANIELEZA LEO MKUFU WANGU HUPO WAPI! Na HATOKI MTU HAPA, MPAKA NIUPATE MKUFU WANGU!"

Nikaona baadhi ya macho yananitazama, ilihali mwenyewe najijua kuwa sina tabia za udokozi wala wivi...!

Nikajikuta nimepigwa na ganzi, mwili ukanisisimka kama mtu aliyeona mzimu wa mtu wa kale.

Nikawatazama na wao wakanitazama, nikamgeukia kumtazama mwenyeweji wangu, akakimbiza macho na kutazama pembeni, kukapita kimya cha sekunde kadhaa...

Nikajiuliza maswali mawazoni, nikakosa majibu, kisha nikakumbuka kuwa dunia ya leo, watu hawakosi majibu, Sasa Basi Kama Ndio Wewe Yamekukuta Haya, Ungefanya Nini?

Monday 5 December 2022

 NILIKWENDA KUNUNUA MWENYEWE DUKANI

Hivi Siku Hizi Bado Kuna Wanao Tafuna Tambuu!?

Nipo Zangu Likizo, Ndani ya Jijila la Dar, Nakatiza Mitaa ya 'Uhindini' Karibu na Palipokuwa na Jumba la Sinema la Cameo, Lengo ni Kuelekea Walipokuwa Wakiishi Wakwe Zangu, Mtaa ya Kisutu.

Nikaikumbuka hii mitaa enzi hizo nikiishi mtaa wa Livingstone, walikuwa wakiuza sana Tambuu, ila ni ayami sasa sijaona 'Wahindi' wala 'Waswahili' wakitafuna Tambuu.

Zamani ukipita hii mitaa unakuta watu wanatafuna tu. Sasa usiombe jamaa awe anatafuna akiwa ghorofani halafu 'aipunguze' mdomoni wakati wewe unapita chini. Utasimulia.

Nikakumbuka kisa kilichonipata, miaka kadhaa nyuma. Nipo zangu nyumbani, mtaa wa Livingstone, Kariakoo. Miaka ile ya 80, bado kinda hata ubwabwa wa shingo bado kunitoka, sina hili wala lile. Hata sijui lile wazo lilikuja vipi, ila mpaka leo naamini kabisa, yaani haki ya Mungu tena, ndani ya mtima wangu kuwa; siku ile nilitembelewa na ibilisi wa Kibaniyani.

Tena atakuwa ni Mgujarati tu afiriti yule ayari, maana si kwa ushawishi ule ulionikamata, kiasi cha kushindwa kufikiria vizuri. Wala sikuwa na uraibu wa kula Tambuu, ila siku ile nilikamatika, nikajikuta nipo kiguu na njia kuelekea maeneo ya Kisutu, Uhindini.

Nikakatiza zangu Mnazi Mmoja, huyoo kiguu na njia, nikapita Mtaa wa Libya, mpaka makutano ya mtaa wa Libya na Zanaki, kisha nikachepuka kidogo kuingia mtaa wa Mtendeni, kisha nikaingia mtaa wa Mlima, kabla ya kukanyaga mtaa niliokusudia, mtaa wa Kisutu, dukani kwa Muhindi, Makaputura.

Ni baba wa Makamu, mnene haswa, kakaa dukani kwake, akipenda kuvaa kaputura akiishikiza kwa anjali, na ndio ikawa rakabu yake, Mzee/Babu Makaputura. 

Duka limesheheni vitu kadhaa wa kadha, vimewekwa bila mpangilio maalum. Harufu ya Agarbatti inachomeka iliyowashwa mbele ya Ganesha na Lakshmiina, ina hanikiza kiasi cha kukera kwenye pua, harufu badala ya kuanisi ikawa inakera kiasi.

Akanitazama, bila ya kutabasamu, anafungua kinywa chake kunisemesha, huku nikishuhudia meno yake, yaliyobadirika rangi na kupata rangi ya Kahawia, iliyochanganyika na Chanikiwiti na mdomo wake uliojaa mate Mekundu kama damu kwa kula tambuu.

Kisha anatema mate mekundu yasiyopendeza, "Nini nataka veve", akaniuliza kwa rafidhi yake ya Kihindi, nami nikajikuta namjibu bila kufikiria, nataka tambuu, akanitazama kisha akaniuliza, "Nani Natuma veve tambuu" Kaka, nikamjibu, "Nambari gani iko nataka" nikamjibu, namba kumi na tatu, "Nambari Kumi na tatu, Taveja yeye" ndio babu, we nipe tu, ataiweza, nikamjibu. "Nataka gapi, bili, tatu inne" Moja tu inatosha.

"Haya subiri kidogo nategeza wewe, ile spesho kabisa, Tikee" uku akitingisha kichwa chake... Nikaitikia Tikee. Kulikuwa na majani ya Tambuu mezani, akachukua jani moja akalipangusa kidogo, kisha akaweka Popoo pamoja na chokaa kidogo juu ya jani la mtambuu, akaongeza na Tumbaku, Kungu Manga kidogo, Jagir gur na vikorokoro vingine wala sivikumbuki tena.

Akachana gazeti na kunifungia, "haya lete shiligi bili", nikampatia, kisha huyoo nikaongoza kurudi zangu, nyumbani. Nikapita mtaa wa Mrima, nikafungua kifurushi changu cha tambuu, nikabugia yote kinywani.

Sikumbuki kutema mate, kila yakijaa kinywani, nayameza kwa ule utamu wa ile sukari guru... Dakika si nyingi, nikaanza kuhisi Andasa ikipanda kidogo kidogo.

Afanaleki! Nikaanza kuhisi ubongo wangu haujatulia, harabu ya ile tambuu, yaani chugachugia, nilitia akili siku hiyo, dunia yote niliona kama inakwenda upande upande, nami nikaifatisha.

Kumbe walio niona siku ile wakastaajabu, wakapatwa na mpagao, mtu mfupi mie kwa jinsi nilivyokuwa nikitembea, kama mtu mwenye milonjo, maana si kwa miondoko ile ya mikogo.

Wakaja kuniuliza, siku ya pili yake, kumbe nilivyokuwa naangaika na andasi kichwani, na mwendo nikabadirisha, nikihisi barabara zimeinamia upande mmoja wa kushoto, nami ili nisidondoke nikajikuta natembea kuinamia upande wa kuume, natembea kama mtu aliyepigwa dafurao na lori la Jay Fong la mwaka 74.

Nilikuwa natembea kama Kaa au Ngadu, yaani nikitembea upande upande, siku hiyo niliongea lugha zote za Kihindi, Kibengali, Kigujarati, Kitelugu, Kiurdu, mpaka Kibanyani nilikijua siku hiyo... Kudadeki.

Hata nyumbani sikumbuki nilifikaje, nilijikuta tu nimepitiliza mpaka uwani, huku nimeshika kibatari nilichokiwasha, tena ni saa kumi jioni, mie naona giza.

Siku hiyo nilitapika mpaka nyongo... Nikanyororeka kama Kinyonga aliyelishwa ugoro... 

Kuanzia siku hiyo nilikoma, sikutia mdomoni si Tambuu wala Kubeli au nduguye Pariki...

Friday 2 December 2022

NILISHIKWA KWA TUHUMA ZA KUSAFIRISHA MADAWA YA KULEVYA.

Nilipo Ruhusiwa tu, Breki ya Kwanza Ilikuwa Maliwatoni...

Nipo Ndani ya Ndege, Aina ya Airbus, Tumehabiri Watu Wengi Sana, Hii ni Moja Kati ya Ndege Kubwa Sana za Abiria, Ndege Inamilikiwa na Shirika la Ndege la Falme za Kiarabu la Imarati (Emirates).

Nikitokea zangu ughaibuni moja kati ya nchi za Ulaya, naelekea zangu Afrika Mashariki kwa likizo fupi.

Nitakaa Dubai kwa siku kama tatu hivi, kisha baada ya hapo nitaunganisha ndege kuelekea kwenye nchi ambayo ndio kuna kitovu changu.

Ndio kwanza nimemaliza kuweka mzigo wangu kwenye Saraka (Dambra) ya kwenye ndege.

Kitu ambacho binafsi sikipendi sana na hii ni kwa sababu ya kimo changu, maana mimi si mrefu wa sifa wala si mfupi wa kuchusha.

Ghafla nikashikwa bega la kushoto, mshiko ule uliandamana na sauti kavu kidogo, ya mwanamke wa Kiafrika, mtu mzima, amekonga kiasi chake, kwa haraka haraka, nikakadiria umri wake, anapata miaka 60 au 65 hivi. Na kwa ile rafudhi yake, nikahisi kuwa anatokea Afrika Magharibi, na kama sikosei atakuwa tu ni Mpopo na kama si Mnaijeria basi ni Mghana.

Akaniomba nimsaidie kuweka begi lake kwenye saraka, yaani sehemu ya juu ya kuhifadhia mizigo.

Lakini ghafla kabla sijainama kuchukua mzigo wa yule bibi, mtu mmoja mrefu kiasi aliyekaa karibu nasi akajitokeza na kumsaidia yule mama mtu mzima.

Kila mtu akakaa kwenye kiti chake, wakati tupo angani, yule bibi akaanzisha mazungumzo. Alikuwa ni mzungumzaji mzuri, mwenye kujua mengi.

Nami kama kawaida yangu, napenda mazungumzo na haswa ninapogundua ninaweza kuelimika kwa namna moja au nyingine.

Tuliongea wakati wote, kiasi cha kuifanya safari ya saa tisa ya kwenda Dubai kuhisi imekuwa fupi sana.

Mara, sauti ya rubani ikasikikia kupitia kipaza sauti akitangaza kwamba tumeingia kwenye anga ya Dubai na muda si mrefu ndege itatua kwenye kiwanja cha ndege cha Dubai.

Ghafla yule bibi ambaye amefanya urafiki nami akanza kulalamika maumivu ya tumbo.

Nami kwa uungwana niliokua nao nikiongozwa na moyo wangu uliojaa huruma kwa yule ajuza, nilibonyeza kitufe cha msaada, na muhudumu wa kwenye ndege akaja kutusikiliza, akataka kujua shida ni nini.

Nikamwambia kuwa jirani yangu hakuwa anajisikia vizuri.

Lakini cha ajabu yule bibi, ghafla alianza kuniita mimi kuwa ni kijana wake (My son, my son...), na uku akiwa amenikamata mkono, hakutaka kuniachia.

Msimamizi akaniambia kuwa hakuna kitu wangeweza kufanya zaidi ya kumpa dawa za kupunguza maumivu na tusubiri hadi tutakapotua.

Yule muhudumu akamtaarifu rubani, naye rubani akatangaza kwamba tumepatwa na dharura ya mgonwa ndani ya ndege na akatushauri sote tutulie na tusiwe na wasiwasi kwani yule mgonjwa atahudumiwa.

Yule bibi alikuwa akilia na kutokwa na jasho kama vile aliyemwagiwa ndoo nzima ya maji.

Nikajaribu kuuachanisha mkono wake na wangu, lakini yule bibi alikataa kuniachia mkono wangu... Kila mtu alidhani kuwa mimi na yule bibi wa Kipopo ni mtu na mwanae.

Ndege ilipokwisha tua na kusimama, yule kijana aliyesaidia kuweka mzigo wa yule bibi kwenye Saraka, aliondoa mzigo wake, kisha akasaidia tena kushusha sanduku la Bibi Mpopo na kuliweka kwenye kiti.

Yule jamaa kabla ya kuondoka alininong’oneza kwa kunishauri nijitenge mbali na huyu bibi na niwaambie wahudumu wa ndani ya ndege kuwa mimi na yule bibi hatukusafiri pamoja.

Wafanyikazi wa kwenye ndege waliniuliza kama tuna uhusiano na bibi yule, niliwaambia kuwa tumekutana kwenye ndege. Sikumjua kabisa kabla...

Wakati naondoka nikamuaga na kumtakia kila la kheri, lakini yule bibi aliniomba nimsaidie kumbebea mkoba wake.

Lakini yule jamaa aliyemsaidia kuuweka mzigo kwenye saraka ya kwenye ndege aliniangalia, tukatazamana machoni, nikamuona akitikisa kichwa kwa msisitizo. Nikamuelewa!

Tukawaachia wahudumu wamsaidie.

Basi mimi na abiria wengine tukatoka ndani ya ndege na kumwacha bibi wa Kipopo anasubiri kiti cha magurudumu.

Nashuru niliweza kujikongoa kutoka kwa yule bibi, baada ya waudumu kufika na kumsaidia mizigo yake na yeye akawekwa kwenye kiti cha matairi.

Tulipokuwa tukingoja mizigo yetu, tukasikia sauti kali ikiamuru "... Stop, Stop! You are Under Arrest...!"

Nageuka kuangalia kumbe anayeambiwa asimame na kuwa amewekwa chini ya ulinzi ni yule bibi wa Kipopo alikuwa akikimbia, akijaribu kuwatoroka Askari na wafanyakazi wa kwenye ndege.

Kumbe walipo mshusha tu, tumbo lilipona ghafla na mara moja na akasimama na kuanza kukimbia uku akimuachia mkoba mmoja wa wafanyakazi wa kwenye ndege, na kukimbia kuelekea nje...!

Kwa bahati nzuri polisi wa uwanja wa ndege walikuwa na kasi kuliko yeye. Walimshika na kumrudisha uku wamemvisha pingu za mikono.

Bibi wa Kipopo bila haya wala soni usoni akaanza kuniita tena... "My son... My son, ooh! How could you do this to me, ooh...!"

Mwanangu ... Mwanangu! Unawezaje kunifanyia hivi...!

Ndio sasa nikaelewa na fahamu kunirudia uzuri, kumbe bibi alikuwa amebeba dawa za kulevya na alikuwa akijaribu kunihusisha na mimi, ili yeye apate upenyo wa kutoroka!

Kwa bahati nzuri, yule bwana ambaye alikuwa amemsaidia kushusha mzigo wake toka kwenye saraka, alijitokeza na kuwaambia polisi wa uwanja wa ndege kuwa mimi na yeye (Bibi wa Kipopo) tumekutana tu kwenye ndege.

Polisi walichukua pasipoti yangu na kumwuliza yule bibi ataje majina yangu kamili ikiwa ni kweli mimi ni mwanae na tulikuwa tukisafiri pamoja.

Kwa neema ya Mungu, sikuwa nimemwambia hata jina langu la kwanza, bibi wa Kipopo akabakia tu anag’aa ng’aa macho! Uku akiendelea tu kusema "...he is my son, ...he is my son, ooh!"

Hata hivyo Polisi wakanitaka nifuatane nao kwenye chumba kidogo ambapo nilihojiwa sana.

"Nilikutana naye wapi? ...Nilipanda wapi...? Huyo bibi alipanda wapi...!?" Na maswali mengine mengi ya kimtego.

Na mizigo yangu yote ilipekuliwa na kuchambuliwa sana, wakachukua alama za vidole vyangu ili wakaangalie kama nilisha wahi kukamatwa...!

Taarifa za kipolisi zilipokuja, alama zangu za vidole hazikupatikana popote, si kwenye mizigo ya yule bibi wala kwenye kazidata za Kipolisi!

Niliruhusiwa kuondoa baada ya takribani saa tatu za mahojiano, maana hata mwenyeji wangu alisha anza kukata tamaa.

Hakuna siku nilijawa na hofu kama hii siku, na haswa kama ujazoea maswala ya kukamatwa na polisi, tena basi nikiwa nchi ngeni, nchi ambayo kesi za dawa za kulevya hukumu yake ni kifungo cha muda mrefu kama si cha maisha, kwa kweli nilichanganyikiwa...

Nilipo ruhusiwa tu, breki ya kwanza ilikuwa ni maliwatoni, uko niliharisha kweli kweli, nadhani ni ule woga na fikra zilizonizonga kuwa sasa ndio basi tena, naiwacha dunia kizembe...!

Tangia siku ile nikajifunza jambo moja, la kutogusa mzigo wa mtu yoyote yule. Labda mzigo uwe wa familia yangu na nimeupakia na kuufunga mwenyewe... 

Zaidi ya hapo hata sijali, tena nimeapa kabisa, Haki ya Mungu tena, sikusaidii, nimekukuta uwanja wa ndege na mizigo yako hata ikiwa unayo mizigo iliyo kuelemea au umekongeka ukakongoroka utaibeba na kuishughulikia wewe mwenyewe.

Sitakupa hata toroli ya kuweka mzigo wako!

Mizigo yako... shida yako... Hiyo ndio sera yangu mpya safarini.

Na kama ni ndani ya ndege na ikiwa huwezi kuifikia sehemu ya kuwekea mizigo, kwenye saraka, na ikatokea kuwa mimi ndiye mtu wa karibu zaidi, nitakachoweza kukusaidia ni kukuambia umwite muhudumu wa kwenye ndege akusaidie...!

Maana Nazi Mbovu Harabu ya Nzima.

Nawatakia Wasafiri, Safari Njema...!

Tuesday 29 November 2022

NILIKESHA NIKIMTAFUTA
Tukio Linalo Fanana na Ukweli!

Alhamdulillah Ndio Neno Nitakalo Lirudisha Kwa Mola Wangu Siku Zote Katika Uhai Wangu Ila Sintoweza Kumsahau Binaadamu Kwa Ukatili Wake...!

Siku ya Jumanne majira ya saa mbili na nusu usiku nikiwa msikitini nikimalizia swala ya isha simu yangu ikiwa katika kimemeshi iliita mara nyingi sana, huwa sina kawaida ya kupaparika ninapokuwa mbele ya Mola wangu...!

Alhamdulillah baada ya swala nilitazama simu nakuona nimekosa miito kadhaa kutoka kwa dereva wa madrassa anae mchukua mtoto wangu na kumrudisha nyumbani siku za masomo... ilikuwa yapata saa tatu hivi usiku...!

Nilishtuka kidogo nakuhisi labda kuna tatizo barabarani nikampigia kwa haraka... Swali la kwanza alilo niuliza... Leo umekuja mwenyewe kumchukua mtoto wako madrassa...!?

Nikiwa katika mshituko nilimwambia siwezi kufanya hivyo bila kutoa taarifa... Basi sheikh tupo hapa karibu saa nzima mwanao hatumuoni, na hivi sasa ni saa tatu usiku...! (Kwa kawaida huwa wanatoka saa Mbili Usiku baada ya Swala ya Isha)

Niliharakisha kwenda nyumbani na kuchukua usafiri kwa haraka na kuelekea madrassa kwake maeneo ya karibu na Vijana Mwananyamala... Kufika nakuta waalimu na walezi wote katika taharuki na kusikitika...!

Nikiwa ni mzazi nilipiga moyo konde na kutaka kujua kulikoni, maelezo yalionyesha kuwa kuna magari binafsi yanayo kuja kuwafuata watoto na yale ya madrassa walio ingia mkataba. Hisia zikaja pengine kwa utoto atakuwa amepanda gari inayokwenda njia tofauti na nyumbani...!

Basi ikawa ni kutafuta namba za simu za wazazi kuwauliza watoto wao kama walikuwa na mwanangu kwenye magari yao na majibu yalirudi yale yale kuwa hapana hatukuwa nae...!

Hapo ilikuwa yapata saa nne na nusu usiku nikiwa katika kuomba dua na kumdhukuru Allah kila wasi wasi unapo itawala nafsi yangu...!

Baada ya hapo tukapata hisia pengine wakati wa kuruhusiwa yeye hakupanda gari yoyote badala yake amefuatana na watoto wanaoishi karibu, wale wanao kwenda kwa kutembea makwao hivyo akapoteza mwelekeo asijue anapo kwenda kwa udogo wake...!

Mimi na mwalimu wake tukaamua kuongozana pamoja na tulitembea mpaka kituo kidogo cha polisi Garden pale Mkwajuni na kuulizia kama wamepata taarifa yoyote ya mtoto aliyepotea jibu lilikuwa hapana. Na askari aliyepo zamu akatuambia kuwa taarifa ya kupotelea kwa mtoto inapaswa itolewe baada saa 24 tangia kupotea.

Subhanallah mtoto mwenyewe ndio kwanza ana miaka minne, nikiwa katika mawazo masaa 24 kwa mtoto wa miaka minne, nikachoka kabisa. Nilicho amua kufanya ni kumwachia nambari zangu za simu askari wa zamu, ili kama kutakuja taarifa yoyote apate kunifahamisha.

Tukarudi madrassa na kuchukua usafiri na kuelekea kituo kingine kidogo cha polisi maeneo ya Mwinjuma ili kuwapa namba zangu kwa taarifa yoyote itakayo patikana.

Baada ya kutoka Mwinjuma, tukaamua kupita njia za ndani ndani huku nikitazama huku na kule, kila mtoto niliemuona, nilihisi anafanana na mwanangu, nasimama kuangalia kama ndie au lah.

Hatimae tukafika sehemu tukakuta mkusanyiko wa watu, nikiwa na ghamu nikawauliza nikiwa sina uhakika wa jibu nitakalopata.

Ajabu wakanambia kuna mtoto katangazwa kapotea yupo msikitni, kwa Makunganya...!

Tukatoka mbio mbio huku nimekunja kanzu yangu, makubazi mkononi kuelekea uko msikitini, uku nikiomba dua za kila aina nilizozikumbuka. Kufika tukafanikiwa kumuona kiongozi wa Msikiti, mtu wa makamu hivi, anafika miaka 50 kwa uchache, huku nikiwa na shauku ya taarifa ya mtoto wangu. Nikamuuliza kuhusiana na huyo mtoto alopotea.

Kiongozi yule akanijibu kuwa ni kweli kuna mtoto wa kike darasani la pili kapotea, umri wake unakadiriwa miaka nane mpaka kumi hivi.

Niliishiwa nguvu nakulazimika kuendelea na safari ya kurudi Mwinjuma...!

Tulipofika kituoni majibu niliyoyapata hapo ni yale yale tu, kuwa tusubiri saa 24 ndio tutoe taarifa rasmi ya kupotelewa na mtoto. Hivyo na hapo kituoni nikaacha namba zangu na kuelekea kituo kingine kidogo cha polisi pale Mtambani.

Baadaa ya kuzunguka vituo kadhaa vidogo vya polisi, vilivyo jirani nikakata shauri kwenda kituo kikubwa cha Oysterbay kutoa taarifa na kujua kama wana habari yoyote ya mtoto alopotea. Baada ya kumaliza maelezo yangu, askari alokuwa zamu akachukua Simu ya Upepo (Radio Call) ili kuwapa taarifa askari waliopo katika doria, kama watapata kumuona mtoto mwenye umri wa miaka minne akitangatanga mitaani wapate kumchukua na kumuifadhi.

Majibishano ya radio ya kituo na walioko doria yakanifahamisha kuwa, kuna operesheni maalum ilikuwa inafanyika usiku ule, na ili tatizo langu lishughulikiwe na askari walioko nje, itabidi kwanza wamalize operation zao kisha ndio watashughulika na tatizo langu.

Kwa kweli nilikuwa nimechanganyikiwa haswa, nikashindwa hata namna ya kufikiri. Ukizingatia kuwa muda umekwenda, kiasi ni saa tisa kasoro usiku.

Ghafla simu yangu ikawa inaita namba ilikuwa ngeni, baada ya kuipokea nikawa naiangalia kama vile kitu cha ajabu. Nataka kuipokea tu, ikakata.

Naangalia vizuri, betri ya simu inakaribia kumalizika, kiasi imebakiza asilimia 10% tu...!

Mara simu ikaita tena, nikaipokea kwa haraka sana na kuelekeza sikioni, kiasi nikajipiga na simu sikioni, na simu kuniponyoka, nikaiokota kwa haraka na kuilekeza sikioni tena, na kuita kwa sauti ya kitetemeshi.

Haloo, baba fulani hapa naongea, nikajitambulisha, sauti ya upande wa pili ikanitaka niende kituo cha Mwinjuma kuna taarifa muhimu inanihusu.

Moyo ukaongeza kasi mara dufu, kiasi cha pumzi kunipaa nikahisi kizunguzungu kwa mbaaali. Nikajikaza kiume nikamfahamisha askari wa pale Oyterbay kuwa nakwenda kituo kidogo pale Mwinjuma.

Baada ya kumwachia nambari zangu za simu, nilitoka mbio nikamsahau hata niliye enda naye pale kituoni, mbio mbio mpaka kituoni, Mwinjuma...!

Nimefika nikihema pumzi juu juu, kama Wibari alokoswakoswa na mbwa wa msasi , Alhamdulillah nilimkuta tayari mkuu wa madrassa na waalimu wengine nao wapo pale, baada ya kungojea kidogo askari wa zamu, aliniita na kuniambia niende upande wa pili. Nikakuta watu kama wa familia moja wanaume wawili na wanawake wawili mmoja kampakata mtoto, kumwangalia vizuri nakumuona mwanangu pembeni...!

Allah Akbar, hakika moyo wangu ulikuwa katika furaha na michirizi ya machozi katika mashavu yangu nikamnyakuwa mwanangu na kumkumbatia kwa furaha, uku namuuliza kwa upole.

Ulikuwa umeenda wapi Arhaan wangu...? Akanijibu kuwa alienda kutembea na rafiki yake...!

Nilitoa shukran zangu nyingi kwa hao wasamaria wema na kisha nikawauliza ni wapi walikompatia mtoto wangu?

Wakanambia wamemkuta sehemu inaitwa Mchangani mbali sana na madrassa kwake na walijaribu kupita nae katika madrassa nyingine kuuliza kama wanamjua walipo kosa ndio wakaamua kumleta kituoni hapo...!

Nikatoa pesa kiasi cha elfu kumi kumi mbili, ili niwape kama ahsante yangu kwao, uku nikiwaambia kuwa japo si hela nyingi, lakini niliomba wazipokee kama shukran na usumbufu walioupata.

Mmoja kati yao akanikatalia kata kata, na kunambia walicho kifanya ni wajibu wao kama wazazi, na tatizo halina mmoja, leo mimi kesho hata wao wanaweza kupata tatizo na wanatarajia wema kutoka kwa yeyote yule.

Uku machozi yakinilenga lenga, nikawashukuru sana watu wale, kisha nilimchukua binti yangu ili kurudi nae nyumbani.

Baada ya kupeana pole na waalimu wake waliohangaika kutembea mtaani usiku ule huku na kule kumtafuta hatimae tumefika nyumbani yapata saa kumi alfajiri, hoi bin taaban.

Baada ya kumuuogesha na kumpa chai tukiwa katika kumuhoji taratibu mimi na mama yake alisema kuwa alikuwa na rafiki yake anaitwa Mwajuma walitoka pamoja ni marika sawa ila huyo anaishi karibu sana na huwa anarudi kwao kwa kutembea tu.

Akaendelea kutufahamisha kuwa walipo fika kwa kina Mwajuma, waliingia ndani ila babake na Mwajuma akamwambia atoke arudi uko Madrassa.

Hebu fikiria ndugu yangu ni wazazi wa aina gani hao... Walioshindwa hata kumuuliza mtoto jina la mzazi au hata nambari za simu!?

Mbaya zaidi walipigiwa simu mwanzo kabisa, tulimpigia mama yake na Mwajuma, akawa hapokei simu, ikawa inaita tu, kisha tukampigia mumewe alipo pokea alisema kuwa hana taarifa yoyote ile kuhusu mtoto wangu.

Hakika binaadamu ni viumbe wa ajabu na katili waso na huruma, binafsi nimesamehe ila sinto sahau somo walilo nipatia usku ule...!

Nikiwa natafakari hali ya usiku ule, nikawa najiwazia tu, vipi kama angelikwenda kwenye barabara kubwa yenye magari mengi na ahadi ikatimia, si wangekuja kujuta au mioyo yao ishaingia kutu, kiasi hawana tena huruma kwa watoto wa wenzao?

Nikaamua tu kumshukuru MwenyeziMungu, mtoto wangu kapatikana salama usalmini...! Nikakatizwa na sauti ya Mwazini ikitukumbusha kuwa muda wa sala ya alfajir umetimu.

Nikanyanyuka zangu taratibu, kuelekea msikitini kutimiza wajibu wangu kwa Mola wangu...!

Alhamdulillah... Ndio neno langu la leo na mpaka kesho kwa Mola wangu...!

Friday 11 November 2022

 BIRIKA BATI, KIKOMBE BATI,
NA HATUKUKOMA.

Hivi wakulaumiwa walikuwa watengenezaji au wanunuaji au watumiaji!?

Yaani hata sielewi, vikombe gani vinaunguza namna ile? Au walikuwa wanatukomesha tukivunja vikombe vya udongo!?

Halafu kikombe cha chai, ila kinapicha ya nyanya. Sikuvipenda, sivipendi, sitavipenda.

Na kwa nini nivipende, uwenda hivi vikombe ndio vimetukomaza midomo tukiwa bado makinda.

Nahisi ndio maana Watanzania tumekuwa watu wa kupiga sana stori... Sasa wewe fikiria chai ya moto, kuiwacha huwezi, hapo sasa ni stori tu, kumbe janja yako unavizia ipowe, hapo ni stori plus umbea na mikingamo.

Basi nikwambie, siku hiyo nikamtembelea binamu yangu wa kike maeneo ya Magomeni, nikitokea zangu maeneo ya Gerezani, Kariakoo, chini nimevalia viatu vyangu vya Kung Fu shuzi, medini Chaina. Shati langu la Juliana, picha ya ndege, kubwa kiasi na chini nimevalia suruali yangu ya kodrai.

Mtu mimi na ufupi huu, ukiniona kwa mbali, utafikiria nguo zatembea zenyewe. Huyoo kiguu na njia, nikakatiza zangu Jangwani, na jua lile la saa tisa alasili. Kufika home kwake, kanikaribisha uwani, nyumba nzima yupo peke yake, wapangaji wapo mitaani, awajarudi bado.

Kanikaribisha kwenye Kigoda, baada ya salamu na kujuliana hali akanikaribisha chai ya mkandaa, akanitilia kwenye kombe la bati, chai imekolea viungo, inawasha kwa karafuu na tangawizi, ikakolezwa na pilipili mtama, chai kama uji wa mgonjwa na mie ujanja ikawa ni kupiga stori za kupoza chai, fu fu fuuu, nyiingi!

Japo tupo uwani, lakini joto la saa tisa, jiji Dar nalo halikuniwacha, utafikiri nimemwagiwa maji, mara akanyanyuka na kuniita niende chumbani kwake...!

"Binamu njoo chumbani nikuonyeshe mambo, ila nakuonya usimwambie mtu..."

Ghafla nikajikuta nameza mate machungu, nahisi nilitaka kutema nyongo, ikaishia kohoni, chai kidogo inipalie, nilajikuta naimeza bila kujua kuwa naunguza kolomeo.

Nami bila ajizi nikajikuta nipo chumbani, hata sijui nimefikaje, maana fahamu zikikuwa zinaingia na kutoka...

Hakuna pa kukaa ila kwenye kitanda, mwenyewe katandika mashuka yake ya kufuma kwa mkono, maua ya rozi (mawaridi), kafanya seti kamili, mapazia ya dirishani na mlangoni. Vingine kafunikia radio yake, kaseti aina ya National na kitambaa kingine kakitandika kwenye meza.

Pembeni ya chumba kuna mtungi wa maji, umefunikwa na sahani ya bati na kata yake imewekwa pembeni kidogo, picha za wanamuziki wa Boney M na ABBA group zilizokatwa kutoka kwenye magazeti ya Sunday News zimebandikwa ukutani, pamoja na picha ya Buraku, kafanana na mwanamke wa Kihindi.

Kwenye meza kuna viboksi viwili vitupu vya sabauni ya Lux na lifebuoy pamoja na kibox cha dawa ya kusugulia meno ya Colgate. Pembeni kidogo, kuna kabati la vyombo lenye wavu, na kabati la nguo lenye kioo.

"Kaa basi hapo we nawe wima wima tu, kama mgambo wa site" sauti yake ikakatiza mawazo yangu yaliokwenda mbali ya hapo, maana mawazo yalikuwa mbingu ya sabaaa nacheka na kufurahi na malaika wa peponi.

Nikakaa kitandani, moyo unakwenda kasi kama wa Mbayuwayu... Akanitazama kisha akanambia, huku kaweka umakini usoni, yaani yupo siriasi kabisa... "binamu hii iwe siri yetu, ukimwambia mtu, mi na wewe basi tena sitakushirikisha kwenye mambo mazuri haya."

Nikahisi masikio ghafla yamenisimama wima kama mbwa wa msasi kaona windo, nikanyoosha na shingo kama Njiwa Manga...

 Nikahitikia kwa kutingisha kichwa, akanambia "Apiya binamu, kuwa hutotoa siri, sema Hakiyamngu..." nikajikuta natamka, kwa kigugumizi, kilicho nikamata, hata kilipotokea sijui...

"Ha-ki ya M-ngu tttena, si-si-mwambii m-mtu mi mi-ye, Waalaahi Nakuapia, mmmh na mchanga huu naramba." Huku nikiinama na kwa kutumia kidole cha shahada, nikapangusa sakafu na kuramba...

Moyo ukaongeza kasi kama garimoshi la Mjerumani kwenye vita kuu ya kwanza ya dunia sanjari na tumbo likapata kusema, gruuuh.

Akanitazama kisha akanambia: "Haya mie nakuamini voo binamu yangu, najuwa we mambo yako ya kizungu, ndio mana nakupendaga..." Akatamka huku anaelekea kabatini kwake na kufungua kabati...

Hamadi, katoa doti tatu za vitenge vya wax na kuvirembea pale nilipo kaa, kitandani. Enzi hizo tukuvihita vitenge vya Burundi.

"Nimeletewa jana na shemejio..." Sauti yake ikaanikiza pale chumbani.

Nikamuuliza, Mmm! Shemeji yupi huyo...!? Yule mjeshi wa Ngerengere!?

Akanijibu: "Uwachi na wewe, wa Ngerengere wapi!? Yule nishamtosa siku nyingi... Huyu humjuhi wewe, mwenyewe anafanyakazi bandarini, hivyo vitenge vya Magamu (Magendo), vilikuwa vinapelekwa Burundi kontena nzima, yeye ndio kavinyakua hivi vitatu, kaniletea nimuuzie."

"Kimoja shilingi 25, ila kwa wewe binamu yangu, nitakuuzia kwa shilingi 22, na wewe ukauze upate faida japo kidogo."

Nikamtazama, kisha nikapiga fundo moja la chai ya moto, yaani hata sikuhisi kuunguzwa, hiyo midomo na koromeo nilikuja kuhisi nimebabuka, usiku wake nisharudi nyumbani.

Ghafla nikajihisi kama biskuti ndani ya chai ya moto au kiowevu, nikawaza mfukoni nina shilingi Moja ya Mwenge na sumni tu ile ya sungura...

Enewi, yalikuwa tu maisha yenye changamoto zake, furaha, uzuni, vicheko vyote vilikamilisha uhalisia wa maisha yetu, hatukuacha kutembeleana, japo bidhaa muhimu zilikuwa adimu... kula kwa kaya...


😉🤭🤣

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!