Sunday 6 March 2016

Tujiangalie na Sisi Wenyewe na Misimamo Yetu

Kila linapokuja swala la kiuongozi haswa kwa nchi kama hii ya Tanzania, kunakuwa na mshawasha wa kujuwa nani na nani watachaguliwa uko serikalini.

Kiongozi akiwa ni Muislam basi Waislam huwa tuna matumaini makubwa kuwa atachaguwa viongozi ambao wanaendana na Iymaan ya Kiislam au kuweka uwiano mzuri kiuongozi na haswa kwenye ofisi za kiserikali na kuzingatia vigezo vya wahusika.

Hayo ni mambo ya kiongozi husika na uchaguwa vile anavyo elekezwa na washauri wake au kwa utashi wake mwenyewe. 

Waislam tunaweza kulalamika pale tunapo ona kuwa uwiano kati ya watendaji wa serikali unachembechembe za udini kwa sababu nchi ya Tanzania inajengwa na Watanzania wenye iymaani kuu mbili, aidha Uislam na Ukristo.

Mara nyingi tumekuwa tukisoma malalamiko mengi sana kutoka upande wetu sisi Waislam, kuwa uwiano wa kiuongozi si mzuri na karibia serikali zote ambazo mtawala mkuu ni Mkristo.

Kweli tuna haki ya kulalamika kwa sababu kwa upande wa Waislam pia kuna watu wenye sifa za kuongoza kama walivyo hao wenye dini nyingine.

Ndani ya Tanzania kuna jumuiya kadhaa za Kiislam na zina malengo yake na uongozi wake, lakini cha ajabu taasisi hizi ni aghrabu sana kuzusikia zikiungana mkono kwenye maswala kadhaa yahusio mustakabari wa Uislam na Waislam wa Tanzania.

Kila taasisi inajifanyia mambo vile wanavyo ona wao, na mara nyingi bila kuzishirikisha taasisi nyingine za Kiislam. Wakati mwingine tunawaona wana harakati wa Kiislam wakitoa matamko kadhaa kwa namna wanavyoona wao tena bila kuwashirikisha Masheikh wengine wenye majina na kukubalika katika jamii ya Waislam nchini Tanzania.

Vilevile kuna baadhi ya makundi ya Kiislam ambayo yenyewe wanaona kuwa kushiriki kwenye kazi za Kiserikali na haswa kwenye uongozi ni HARAMU na ni UKAFIRI na katika madhambi makubwa kwa sababu serikali za kisekula hazitumii SHARIA katika hukmu zake na kuziunga mkono kwa namna yoyote ile ni kwenda kinyume na Uislam.

Hawa wenye kupinga ushiriki wa Waislam kujihusisha na harakati za kisiasa, ufanya harakati zao misikitini, wakipita na kushawishi watu wasipige kura wala kujihusisha na jambo lolote lile linalohusu serikali za kisekula.

Swala la kujiuliza itakuwa vipi pale Waislam wote ambao wapo serikalini watafuata huo ushauri na kujiondoa kwenye nyazifa zao mbalimbali na kurejea mitaani?

Hali hii tu ambayo Waislam ni wachache na tunalalamika kuwa tunaonewa na kunyanyaswa na vyombo vya dola na taasisi zake. Sasa ikitokea kuwa hakuna kiongozi hata mmoja ambaye ni Muislam kwenye taasisi zote za Serikali hali itakuwa vipi, maana si ajabu Waislam tukajikuta ni Wakimbizi kwenye nchi yetu wenyewe.

Kwa upande mwingine kuna Waislam ambao wao wanaona kuwa si vibaya kwa Waislam kupiga kura kwa sababu watakapokuwa Waislam ni wengi kwenye ngazi mbalimbali kwenye serikali, kuna uwezekano wa mambo mengi ya Waislam kunyooka na kuwa mazuri na hata kupatikana kwa unafuu wa kimaisha.

Ukiudhuria mihadhara mingi ukosi kusikia malalamiko kutoka kwa Masheikh na Waadhiri wa Kiislam wakilalamika kuwa Waislam tunanyanyaswa na kuonewa, lakini hapo hapo tunashindwa kujiangalia sisi wenyewe Waislam, tumefanya nini au tunafanya jitihada gani katika kujikwamua katika matatizo haya na hapo hapo kufuata mafundisho ya dini yetu.

Kama hali ni hii ya kila taasisi kujiamulia mambo yake yenyewe, na wakati huo huo kila sheikh kwa kuona kuwa yeye ndio msemaji basi akapanda kwene membari na kulalamika bila ya kuwashirikisha wengine, hatutafika sehemu tukasikika kwa sababu sisi wenye ndani ya Uislam wetu hatuna umoja wala hatupendi kabisa kushirikiana na wengine.

Na ikitokea kushirikiana basi ushirika huo haudumu hata miezi mitatu, tumekuwa kama kundi la Inzi, ukiwaona inzi jinsi walivyo jikusanya kwa wingi na makelele yao, unaweza kuwa na matumaini makubwa. Lakini hasha kitokee kishindo kidogo tu, hata mwanguko wa tawi la mti basi linatutawanyisha na kila mmoja kukimbilia upande wake.

Uko kwenye taasisi za Kiislam, kila leo utasikia kashfa za ulaji wa pesa na kupendelea na wakati mwingine hata kunyoosheana vidole kuwa fulani anahujumu harakati za Waislam. Mambo mengi yanakuwa hayana Baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Wakati mwingine nahisi hii ni kama dalili za adhabu kwetu, maana Waislam tumekuwa hatuna tofauti na hao Wakristo, Wapagani na wale wasio amini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu.

Hizi rehma na riziki ambazo tunazipata mi nahisi ni kwa sababu kuna viumbe vingine ambavyo havina makosa, kama vile wanyama na mimea, kutokana na hao ndio na sisi tunafaidika.

Tujipange, la kama hatutajipanga basi tusilalamike tutakapopangwa na hao wenye kujipanga wakaja kujipanga nasi tukabakia tukilalamika kuwa tumepangwa.

1 comment:

  1. Nukta moja tu. "Tumefanya non au tunafanya jitihada gani katika kujikwamua katika matatizo haya na hapohapo kufuata mafundisho ya dini yetu"

    Matatizo ya kunyanyaswa? Kwani tunataka kupendwa na makafiri, sio katika aqidah yao iliwatupende tuwalinganie wasilimu. Hatahivyo yaonesha hats Mtume saw na maswahabah ra qalinyanyaswa na kutengwa Je waliomba nafasi ya uongozi kwa makafiri wa maka iliwashiriki kuongoza wapunguze manyanyaso na mateso! Hata walipo pewa nafasi ya kushiriki walikataa.

    Kubakikatika dini ni kuhakikisha tunafanya juhudi chanya za maksudi za kiibada kwa kauli na amali kuhakikisha sheria za Alkah zinatawala katika ardhi.

    Hatuoni nchi zenye qaislam 100% katika serikali bado hakuna uislam, mf zanzubar pombe,madawa, ukahaba, nk. Nchi kama saudia nk.

    Hatuoni hata tz nikiongozi gani wakiislam kwakuwa kwake bungeni au ikulu ameleta mabadiliko chanya, kwani hawa qalio mahabusu leo wameswekwa na utawala upi, jaji akiwa nani, ?

    Hatutanabah majibu ya Mtume saw ktk takrima ya uongozi, turejee sababu za kushuka surat kaafirun.

    Uislam hupima mambi kwa halali na haram na sio faida na hasara. Na mafanukio ni kupata radhi za Allah nako nikwa kufuata maamrisho yote na kuacha makatazo yote.

    Hakuna attadaruj/gradualusm ktka uislam.

    Lengo na njia ni ibada lazima viwe hakali.

    ReplyDelete

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!