Thursday, 3 March 2016

Nasaha za Kichaa, Mwendawazimu Aliyechanganyikiwa

Siku zote uwa nakaa na kujiuliza, hivi Waislam sisi, tumekumbwa na maradhi gani ya akili, mbona hishma na mapenzi kati ya Waislam hakuna tena, hivi kuwa na uoni tofauti au kuwa katika mtazamo fulani au dhehebu ndio iwe kila siye upande wako si Muislamu?

Nakumbuka kisa kimoja kiliwahi kutokea uko ughaibuni. Kulikuwa na Waislamu wawili ambao wamebahatika kwenda kuishi nchi za nje. Waislam awa ni jamaa na ni ndugu, si katika imani tu, bali ni ndugu haswa.

Tofauti yao kubwa ni mtazamo katika kuyaendea maswala ya imani na aqida. Siku moja walifikishana Polisi na haswa ugomvi wao ulikuwa kuhusu Mu'awiyah (ra) na Imam Ali (ra).

Walianza kama mchezo tu, na mjadala ukandelea mpaka ikawa sasa si majadiliano tena bali ni kashfa, uongo, matusi yasio mfano na kila mmoja kujiona kuwa anajua zaidi ya mwenzake.

Ugomvi ukawa mkubwa na makelele ya kukufurishana, matokeo yake majilani wakaona hawa watu wanaweza kuumiza bure, maana walikuwa awaelewi ni nini haswa wanachogombea.

Matokeo yake wakaitwa Polisi Wakakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi. Afisa wa polisi wa uchunguzi aliyekuwa zamu akasikiliza sababu ya kugombana kwao. Matokeo yake yule polisi akawamuru waletwe Ali na Mu'awiyah hapo kwenye kitengo cha polisi. Kama mashahidi wa Kesi kati ya vijana wale.

Mmoja wa aliyekuwa hapo aliposikia kuwa wanatakiwa kuwaleta Ali na Mu'awiyah akamwambia askari Polisi wa zamu kuwa watu hao walishafariki zamani ni zaidi ya miaka 1300 iliyopita.

Yule Afisa wa Polisi akawashangaa sana vijana wale, kiasi cha kuamuru wapelekwe hospitali ya wagonjwa wa akili!

Binafsi nikawa najiuliza kutokana na kisa kile, hivi tunahitaji hospitali ngapi kuzitibu akili za waliobakia!? Ambao kwa namna moja au nyingine awana tofauti na vijana wale?

Unaweza kushangaa, lakini ni kisa cha kusikitisha na kinaumiza akili, haswa kwa mtu mwenye kuijuwa tarekh ya Kislamu. Kwa sababu tofauti hizi azikuanza leo, na hata hao Maulamaa na hata Maswahaba walitofautiana, lakini haikufikia kiasi ambacho kuitana Makafiri na kukufurishana.

Je Waislam sisi wa kizazi hiki, tunajuwa zaidi ya wale waliotutangulia mbele ya haki? Kiasi cha  kuwatia peponi tuwapendao na kuwatupa motoni tunaotofautiana nao kifikra!?

Hii yote inasababishwa na nini kama si kudumaa au kuto baleghe Kiakili na Kiroho, na ilo ndilo linako pelekea wengi wetu kukosa kuhishimiana katika majadiliano yetu na haswa tunapotumia mitandao ya kijamii.

Kuto kukomaa huku kunaletwa na kuzibemenda akili zetu na kuathili mioyo yetu kiasi cha kutoweza kuona thamani ya majadiliano yetu na kuhishimiana kwetu.

Tunacho angalia ni kuwa nimemshinda fulani, nimekuwa maarufu kwa kumtukana fulani au kwa kuwakufurisha watu fulani au kwa kuwashusha thamani kina fulani.

Nasema hivi, Kwanini Mmeamua kwa makusudi kabisa kuzibemenda akili zenu na hamkubali mtu yoyote mwenye mawazo yanakwenda tofauti na nyinyi, kiasi cha kuwa vipofu wa akili kwa kushindwa kuona au kutambua kuwa binadamu tuna uwezo tofauti katika kuyakabili mambo mbalimbali katika jamii inayotuzunguka.

Wenye akili mnashindwa kuelewa kuwa, sisi WendaWazimu na Vichaa tulio changanyikiwa, ndio watu pekee ambao tunaruhusiwa kuto tumia akili zetu, kwa nyinyi mlio na akili kwa kuto tumia akili zenu ni kutunyang'anya haki yetu ya msingi kwa sababu sisi ni vichaa na zaidi ya hapo tumechanganyikiwa.

Hakika hii ndio hali halisi ya Waislam wengi wa Dot Kom, Kwa kweli kisa hiki kiwe ni funzo kwetu sote na hasa wenye kukufurisha ambao hamna Madhehebu ya Kiislamu iliyosalimika kwao, kwa Maulamaa hawa wa Gugo Dot kom.

Waislam tunapaswa kubadilika, maana Mwenyezi Mungu awezi kubadilisha hali zetu mpaka sisi wenyewe tuchukue hatua za makusudi kabisa na kufanya jitihada za dhati ndipo naye Mwenyezi Mungu atatufungulia milango yake ya Rehma na Uislam utasimama tena.

Siku mtakapokubali kuwasikilia wale mnao waona kuwa ni maasimu wenu, ndipo mtakapo gundua kuwa wale ambao mkiwaona kuwa ni maasimu wenu kumbe ni ndugu, jamaa na marafiki zenu na wanacho kieleza aidha kina manufaa na ukweli ndani yake au tofauti yenu ni ndogo sana na si tofauti ya kuwafanya muwachukie na kuwaona kuwa ni maadui zenu, kiasi cha kuwahukumu kuwa ni watu wa Motoni.

Hakika mmeshafanya makosa na mnaendelea kufanya makosa, mnajitenga na tabia za Kiislam na mnatufundisha sisi wendawazimu mambo mabaya na hata kwa vizazi vyetu na vyenu nyie wenye akili kwa maana ya watoto zetu sote.

Hivi tumefanya jitihada ngapi kuwafikishia Waislam wenzetu ambao kila kukicha wapo kwenye majumba ya ufuska; kama vile mabaa, vilabu vya usiku pamoja na kila kitu ambacho kipo nje ya itikadi na maadili ya Uislamu?

Hakika tunakitenga kizazi na dini yetu. Hawakukosea wale waliosema: "Mtoto Umleavyo Ndivyo Akuavyo."

Na kwa kweli wanatusoma kwa haya tunayo yaandika kwenye mitandao.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!