Thursday, 28 April 2016

WENGI WENYE MADARAKA AFRIKA

NI MANUNDA WALA WATU

Nakumbuka zamani nilikuwa msomaji wa vitabu vya hekaya (Hadithi au ngano) mbalimbali, vitabu ambavyo wengi tulivisoma bila kutafakari undani wake au maana yake kiujumla.

Kuna hii simulizi ambayo naikumbuka mpaka leo na ninaifananisha na maisha halisi ya Mtanzania kwa wakati ule uliopita na wakati huu wa sasa.

Hekaya yenyewe ilikuwa inamuhusu Mtoto wa Sultani Majinun na Paka Nunda Mla Watu. Sultani Majinun alikuwa na watoto saba.
Vilevile Sultani Majinun alikuwa na paka wake mzuri sana ambaye alikuwa anampenda sana. Paka yule mwanzo wake alianza kukamata vifaranga vya kuku. Akaambiwa Sultani, paka anakamata kuku, akawaambia, paka wangu na kuku wangu, basi mwacheni.

Yule paka wa Sultani akaenda akakamata ndama wa ng'ombe. Akaenda akaambiwa Sultani yule, paka amekamata ndama wa ng'ombe, akawaambia, paka wangu na ndama wangu. Wakamwambia, vema, bwana.

Kisa kiliendelea ikafikia mpaka kula watu, Sultani akiambiwa majibu yalikuwa ni yaleyale paka wangu na raiya wangu. Ikafikia yule paka akila kila kitu akionacho cho chote kinachopita katika njia ile, akamata akila.

Ikapelekea Sultani kuwatuma watoto zake kwenda kumuuwa yule Paka maana ameshakuwa Paka Nunda, maana anakula kila kitu hata visivyoliwa.

Lakini watoto zake wote sita ambao Sultani aliwapeleka kumuua yule Nunda mla watu walishindwa na wale wote sita wakaliwa na Nunda yule.

Yule mtoto wa saba, alipoona khabari zile za nduguze walioliwa na paka, akamwambia mama, nami nitakwenda, paka aniue kama alivyoua ndugu zangu. Akamwambia, wee utakwendaje mtoto peke yako? Akamwambia, mimi nitakwenda kwa uchungu wa ndugu zangu.

Akamwambia, vema mwanangu. Akafanyizwa mikate, akapewa na watu wa kumchukulia vyakula. Akapewa na mkuki mkuu mkali kama wembe, na upanga wake. Akamwambia, mama buriani. Akatoka, akaenda zake.

Hata alipokoma viungani akaona jibwa kubwa, akampiga, akamfunga, anamkokota. Akaja anakwimba.
Mama wee, niulaga Nunda mla watu.

Hata akafika Hata karibu na mji. Mama yuko juu, akamwona, akamsikia anakwimba, Akamjibu mamake, akamwambia, Mwanangu, si yeye Nunda mla watu.

Yule mtoto hakukata tamaaa, japokuwa kila akikamata mnyama anaambiwa kuwa siye Nunda mla watu, hata siku moja akawaambia wasaidizi wake, kila mwenye nguo mbili, na avue nguo moja. Wakamwambia, kwa nini, bwana? Akawaambia, huku tu katika mwitu, na mwitu hauna udogo, huenda tukanaswa na miiba au hutaweza kwenda mbio. Na hiyo moja tena shuti tuipige uwinda. Wakamwambia, vema, bwana. Wakapiga uwinda wote. Akawaambia, haya twendeni. Wakaenda kwa magoti hata wakamwona yule nunda pale penye kichaka.

Yule bwana akanena, ndiye nunda huyu... Akawaambia..., tumpige, tumwache? Wakamwambia, bwana, tumpige, tujue kumpata, au tujue tumemkosa. Akawaambia, vema, akawaambia, shikeni bunduki zenu tayari. Akawaambia, bunduki zenu nikiziamru mara moja zilie. Wakamwambia, inshallah, bwana.

Yule mtoto, alipopiga bunduki yake, nazo za watumwa wote zikalia. Yule nunda asiinuke, bunduki zile zalimtosha. Wale wakakimbia, wakapanda juu ya mlima.

Wakarejea siku ya pili na kumkokota yule Nunda mla watu mpaka mjini kwao. Akaenda hata alipokaribia karibu na mji akaimba,
Mama, mama, mama, Nilawa kumakoikoi, nimbe. Mama, mama, mama... Mama wee, niulaga Nunda mla watu...
Mama Mtu akajibu: Mwanangu, ndiyeye Nunda mla watu...!

Hiki ni kisa cha kutungwa hakina ukweli wowote ndani yake, ni riwaya ambayo imeandikwa kwa niya ya kuburudisha na kufundisha kidogo. Lakini tukichambua katika uono wa fasihi na kwa undani tunaweza kuifananisha riwaya hii na maisha ya kisiasa haswa ya Watanzania.

Nunda huyu anaweza kuwa binadamu (Fisadi na Ufisadi) yoyote ambaye aidha kwa njia moja ama nyingine tulimwamini, na kumuheshimu. Binadamu huyu ambaye aidha alipewa madara au alikuja na kutuomba tumchaguwe ili awe ni mtetezi wetu kwenye Nyanja za siasa na maisha kwa ujumla.

Nasi kwa kumuona kuwa ni mwenzetu na ni mwenye kuonesha kuwa ana masikio makubwa ya kutusikia kilio chetu, na ana macho makubwa ya kuona matatizo yetu, mdomo mkubwa wa kuyasemea matatizo yetu.

Lakini tulisahau kuwa Nunda (Fisadi) yule alikua na meno makubwa ya kutafuna mali asili zetu, kutafuna haki zetu, kutafuna kila anachokiona kuwa anaweza kukitafuna na kusahau kuwa kuna waliomchaguwa ili kusaidia kuwaletea maendeleo.
Matokeo yake kila kilicho kizuri si mali ya taifa tena, bali ni mali binafsi za hao tuliowakabidhi madaraka, wanasiasa ambao tuliwapa dhamana ya kulinda maliasili zetu, ili ziweze kutunufaisha sote, matokeo yake kumejengeka matabaka makubwa kati ya wanasiasa na wale wanaoitwa walalahoi.

Lakini kwa bahati nzuri ametokea mtu ambaye amepania kwa hali na mali kumsaka Paka Nunda Mla watu (Mafisadi) ili amuuwe na kumtokomeza kabisa kwenye uso wa Watanzania.

Na jambo ili si rahisi kama watu wanavyo fikiria, kuna wanayama wengi kwa namna moja au nyingine wanaweza kukumbwa na purukushani hii ya kumtafuta Nunda mla watu, wakajikuta aidha wanajeruhiwa au kupoteza uhai wao.

Na hii yote inatokana na hali halisi ya nchi yetu, kwa sababu ufisadi umekuwa mkubwa kiasi cha kuathili Bongo za Watanzania wengi, ambao ufisadi sasa ni jambo la kawaida na akitokea mtu ambaye si fisadi uonekana wa ajabu sana.

Watanzania awa wanaweza hata kumtengenezea uongo ili naye aonekane kuwa hana tofauti na mafisadi wengine, na hii inatokana na watu wachache ambao kwa namna moja au nyingine wanafaidia na ufisadi huu au tu wanaona raha kwa kuwa fisadi yule ni mtu kutoka kabila lake au dini yake au chama chake.

Vilevile wanaweza kutokea wachache wakaitumia hii nafasi kujinufaisha au kutaka kuwakomoa wale wachache ambao wameonyesha tangia uko nyuma kuwa si mafisadi, kiasi ilipelekea mafisadi uchwala kukosa kufisadi na wakajenga chuki kiasi ya kuwafanya wasione mazuri ya viongozi wachache walioko madarakani.

Hapa ndipo kunakohitajika umakini wa hali ya juu, ili kusitokee kuchongeana kusiko na sababu za msingi. Viongozi wasichongeane kwa sababu tu za Kisiasa, Ukanda, Ukabila au hata kwa imani zao za kidini. Tunatarajia viongozi au hao waliopewa majukumu ya kuchunguza utendaji wa viongozi wanakuwa wenye kutenda haki, maana bila hivyo kutapelekea wengi kukosa tena imani na serikali na kuona kuwa kinachofanyika ni udikteta na si uongozi uliotarajiwa.

Na kwa upande wapili, Watanzania tunapaswa kumsaidia mtu ambaye ameonyesha ushupavu wa kumsaka Nunda mla watu, je hatuoni kuwa tunawajibika kwa asiliamia zote kumuunga mkono na kujitolea kwa hali na mali kwenye vita hii ya kumsaka Nunda mla watu ili tujikwamue kwenye makucha na midomo ya wenye uchu wa uchumi wa nchi yetu ambao kwa wameshaota mizizi kiasi cha kutisha?

Tutakapo weza kusimama bega kwa bega na Uongozi huu, uwenda hali ya nchi ikaboreka na kuwa afadhali japokuwa si kwamba sote tutakuwa matajiri au wenye uwezo kama hao walio na uwezo kifedha, na wala si unafuu wa kisaikolojia tu, kwa kuona kuna watu wanawajibishwa kulingana na utendaji wao kuwa si wa kuridhisha.

Tunacho tarajia ni kuona kuwa uduma za kijamii kama vile Hospitali, Usafiri, Elimu na hata upatikanaji wa uduma za maji safi na umeme bila kusahau chakula, mavazi na malazi, nakadharika vinapatikana na vikiwa katika hali bora na kila mwanachi awe na uwezo wa kuvipata na kunufaika navyo.

Hatutaki kufarijiwa kisaikolojia, kwa kuona tu baadhi ya wafanyabiashara au kwa baadhi ya wahusika wa uduma za kijamii wakiwajibishwa tu, bali tunataka hata ile mikataba tata ambayo wengi wetu hatuijui zaidi ya kuiskia au kusoma dondoo zake kwenye vyombo vya habari ikishughulikiwa kikamilifu na tukapata rejea zake.

1 comment:

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!