Sunday 3 July 2016

JE NI KWELI TUNASIKITIKA AU UNAFIKI WETU TU

Wengi tunasikitika kwa kumalizika kwa Mwezi wa Ramadhani, tunasikitika kwa kuwa ni mwezi uliojaa rehma nyingi na dhawabu tele.

Ukiangalia kwenye tovuti baraza nyingi kama vile Facebook, WhatsApp, Twitter, Instagram na nyinginezo utakutana na maneno mengi yenye kuonyesha Waislamu wengi tunasikitika kwa kumalizika kwa mfungo wa Ramadhani.

Hii ni kuonyesha kwamba wengi wetu tumeweza kuonyesha kuwa tunaweza kuishi kama vile MwenyeziMungu anavyotaka tuishi.

Wengi wetu tumeweza kupumzika kufanya mahasi mengi ambayo siku za kawaida ndio imekuwa ada zetu kuyafanya.

Wengi tumepumzika kunywa pombe, uvutaji wa sigara, maudhurio kwenye madanguro na nyumba za kamali na hata maudhurio ya kwenye mabaa, yamepungua sana. Yote hayo kwa kuwa tupo na tulikuwa kwenye mwezi wa Ramadhani.

Wengi wetu mwezi wa Ramadhani tumekuwa wakarimu sana kwa ndugu, jamaa, marafiki na hata majirani zetu na tumeweza hata kuwakumbuka japo mara moja watoto mayatima, wajane na masikini wasio na uwezo wa kujikimu kimaisha.

Kwa kweli mwezi wa ramadhani umedhihirisha kuwa tunaweza kuishi kulingana na mafundisho ya dini yetu.

Mwezi huu unaisha na ndani ya Mwezi wa Shawwal tu tena ndani ya sikukuu Eid al-fitri  tutavua rasmi lile joho la UchaMungu na kurejea kwenye vazi letu la kila siku.

Vazi lile tunalolipenda sana, vazi la maasi, tutarejea tena kwenye uimbaji wa taarabu na bongo flava, tutarejea tena kwenye uongo, utapeli,unywaji wa pombe na kukesha kwenye mabaa maana ndani ya mwezi wa Ramadhani baa nyingi zimedoda kama si kufungwa kwa muda na hata kwenye nyama choma za kiti moto tutashuhudia zikishamiri upya.

Midomoni tutasema sana kuwa tunasikitika kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani, lakini hali halisi tunafurahia kwa kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani, kwa sababu ile minyororo tuliofungwa kuanzia sasa inafunguliwa na tutarejea tena kwa nguvu zote kwenye maisha yetu tuliyo yazoea, maisha ya wizi wa sadaka za msikiti,na mabalaa mengi ambayo ndio hali halisi ya Uislamu wetu.

Nasema hivyo kwa sababu wengi wetu tumekuwa tukiuogopa mwezi wa Ramadhani badala ya kumuogopa MwenyeziMungu, ndio maana kwenye Mwezi wa Ramadhani tunaweza kuacha maasi na unapomalizika mwezi wa Ramadhani tunarejea kule kwenye maisha yetu halisi.

Sina maana kuwa Waislamu wote wanatabia hii, lakini nadiriki kusema kwamba wengi wetu hayo ndio maisha yetu ya kila siku.

Ni Waislam wachache sana ambao ni mifano katika familia zao au ndugu na jamaa na marafiki zao na hata mtaani kwao ni mfano wa kuigwa, lakini kama atatokea Muislam mwenye tabia hizi, sisi waislam wengine ndio tutamkebei na kumtia midomoni kwa kumshusha hadhi yake na kumuona kuwa si chochote zaidi ya kujitafutia sifa tu.

Basi tufahami kuwa Mwezi wa Ramadhani uja na kuondoka, lakini MwenyeziMungu yupo daima.

Hakika wasio taraji kukutana nasi, na wakaridhia maisha ya dunia na wakatua nayo, na walio ghafilika na Ishara zetu. Hao, makaazi yao ni Motoni kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyachuma. Hakika walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi atawaongoa kwa sababu ya Imani yao. Itakuwa inapita mito kati yao katika Mabustani yenye neema.
SURAT YUNUS [10]: 7-9

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!