Tuesday 11 July 2017

TOFAUTI ZA KUWASILISHA HOJA.
Matusi, Kashfa, Dharau, Kejeli & Kebehi.
Hivyo vyote Havijibu Hoja.

Watu wengi upenda kujiingiza kwenye mijadala mbalimbali ya kijamii, iwe ya kisiasa, kiuchumi, michezo na kadharika. Lakini si wote wanaochangia hoja ni mahiri na waelewa wa kile wanacho kichangia. Na hii ndio inapelekea baadhi ya wachangiaji wasio mahiri na uelewa kujiingiza kwenye kuchangia vitu ambavyo vipo juu ya upeo wao wa kifikra.

Watu hao wanajikuta wanalazimisha hoja na hata kutumia maneno ya kejeri, kashfa na hata matusi, wakidhani kuwa kwa kufanya hivyo ndio watakuwa wamechangia mada au kutatua tatizo lililopo kipindi hicho.

Mara nyingi tumewashuhudia wanasiasa au wafuasi wa vyama mbalimbali aidha kwenye mikutano ya hadhara au kwenye mitandao ya kijamii (tovuti baraza), wakivurumisha matusi na maneno ya kejeri wanapo wasilisha au kujadili mada husika.

Ukosefu huo wa hoja zenye mashiko na utumiaji wa matusi kwenye kuwasilisha hoja, kwa watu wa namna hii, nawaona ni sawa na mtu ambae ajabalehe kiakili, japo anaweza kuwa na mwili mkubwa na kichwani akabeba mvi au mzuri wa umbo, vyote hivyo haviwezi kumpa sifa kama hatoweza kuwasilisha hoja kwa vigezo vya mtu aliyekomaa na kubalehe kiakili na kiuzoefu, kwenye jambo au mada anayoijadili.

Ukosefu huo wa baleghe ya kiakili ni janga kubwa sana, si kwa vijana tu, hata kwa watu wa makamo, ambao kwa namna moja au nyingine tunategemea kusikia busara zikitoka kwenye vinywa vyao!

Kwa Kukosa baleghe ya Kiakili, ndiko kunako pelekea wengi kukosa busara na kupelekea upungufu na ukosefu wa adabu katika majadiliano. Watu wa namna hii kwa makusudi wameamua kuzibemenda akili zao kiasi cha kutoweza kuona thamani ya majadiliano au uchangiaji wa mada husika, kiasi hoja zao zikapwelea kwenye lindi la choo cha shimo kilicho jaa uchafu.

Mtu anapotaka kuchangia hoja au kutoa hoja zake, hana budi kwanza kufiria kile anachotaka kuchangia, je kitaleta athali gani katika jamii, je jamii itafaidika na atakacho kisema au itavurugika!

Hapo sasa ndipo mtu anapopaswa kujua maana ya neno HOJA. Hoja ni maelezo yenye msingi na vigezo vinvyothibitisha ukweli au uthabiti wa jambo aghrabu kupinga maelezo ya awali au kuthibitisha uhalali wa jambo husika kupitia maoni au mapendekezo anayoyatoa mtu kutokna na jambo husika. Iwe kwenye mihadhara ya dini, siasa, uchumi au hata michezo.

Wengi wetu tumekuwa watu wa kupenda sana siasa, ila wengi hatujui nini siasa, japokuwa neno siasa limekuwa si neno geni, kwa maana ni neno la kawaida sana midomoni masikioni mwetu, lakini ukimuuliza mtu nini maana ya neno siasa, si bure ukamkuta amekwama hasijue jinsi ya kulielezea.

Basi tunapaswa kujua maana ya neno hili SIASA, ambalo maana yake ni mfumo wa kiitikadi unaotumiwa na kikundi cha watu au jamii fulani kuendesha mambo yao pamoja na jamii hiyo kiitikadi, na lengo haswa ni kuboresha hadhi ya mtu/watu na jamii kwa ujumla.

Sasa basi kama siasa lengo lake haswa ni kuboresha hadhi ya mtu/watu na jamii kwa ujumla. Haya Matusi, Kejeri na Kashfa zisizo za kweli zinatokea wapi? Je Matusi na Kejeri hizo ndizo zitanufaisha na kuboresha mustakabari wa jamii yetu!?

Unaweza kukutana na mtu akatetea matusi kwenye uchangiaji wa hoja zake, kwa kusema, "...Ooh mbona hata ulaya na Amerika watu wanatukana na hakuna tatizo!"

Mtu wa namna hii namuweka kwenye kundi la watu waliofirisika kiakili na atakuwa ameibemenda akli yake. Kwa sababu mtu mwenye kutetea hoja za matusi ni mtu hasojua mila wala kujua utamaduni wetu Waafrika. 

Pili si kila kinachofanyika Marekani au nchi za Yuropa basi nasi tukiige na kukikumbatia, Waafrika tuna mila na tamaduni zetu na mojawapo ni kutotumia matusi katika mijadala au kwenye majadiliano yetu.

Hizo nchi za Amereka na Yuropa wamesha poteza mwelekeo katika maadili ya kijamii.

Na siku zote ukiona mtu anatumia matusi kwenye mjadala basi ujuwe kuwa kaishiwa hoja...

Matusi ni utovu wa nidhamu na ni dalili ya kutoweza kutetea hoja husika, matokeo yake ndio mtu anatukana kwa sababu hana hikma wala busara ya kimazungumzo.

Sababu kubwa ni kwamba wengi wao hawana tena ule uzalendo wa kutetea nchi na wananchi, wengi hivi sasa wanajali maslahi ya muda mfupi na faida za papo kwa papo. Hali hii imetokana na watu kukata tamaa ya maisha na kuamua kubangaiza bangaiza tu ili siku ipite na yeye au wao wapate mradi wao/wake wa siku ile.

Ndio watu kama hawa mimi siwaiti wabangaizaji tu, bali kama si Wachawi basi ni Mandondocha au Misukule ya kisiasa, ambao hawajui wanacho kitetea, wala wanacho kipinga, yaani wapo wapo tu, hawana tofauti na hao misukule na mandondocha ya kichawi.

Mradi wao wamepata mlo wao wa mashudu/pumba za mahindi, basi hawana fikra endelevu tena zaidi ya Matusi, kashfa na kejeri.

Binadamu uliye kamilika lazima uwe na tofauti kubwa sana na msukule au ndondocha, tena kwa viwango vikubwa sana. kila mtu ana fursa nzuri ya kuyaelekeza kwa busara mawazo yake katika maisha. Lakini basi hakuna kitu kilicho muhimu kwa mtu na kwa wakati huohuo kikawa kigumu zaidi kama kuidhibiti hisia na matamanio ya nafsi yake.

Basi tunashauriwa kwamba yale tunayo yataka kuwa yasizidi kupita kiasi na kuondoa busara zetu, kiasi ya kwamba tukawacha kushirikisha akili zetu katika kuyaendea yale tunayo yataka yawe.

Na hali hii tukiiachia kuendela basi huwa ni muhali kupatikana mafanikio ya maisha kwa sababu kama hakuna nidhamu katika majadiliano basi hakuta kuwa na muwafaka, na siku zote tutakuwa kama kuku wa kienyeji kwenye banda, kwa maana hakuna masikilizano...!

Masikilizano na ushirikiano na watu wengine, ndio msingi muhimu wa maisha ya katika jamii yoyote ile. Sharti la kwanza kabisa la kuwepo upendano na masikilizano ni kuheshimu hisia na haki za watu unaofanya nao majadiliano. Jambo hili ndilo linaloimarisha na kudumisha uhusiano kati ya kila mtu.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!