Saturday 7 April 2018

 KUMBUKUMBU YA SHEIKH ABEID AMANI KARUME
4 Agosti, 1905 - April 7 1972.

Sheikh Abeid Karume alizaliwa tarehe 4 Agosti, 1905 katika Kijiji cha Pongwe eneo la Mwera Kisiwani Unguja.

Ni mtoto wa kwanza kati ya watoto watano wakiwemo wanaume watatu na wanawake wawili. Wote hao ni marehemu.

Ni mtoto wa mkulima, mwenye asili ya kutoka Nyasaland (sasa Malawi) kwa upande wa baba ake bwana Amani Karume na mama Bi Amina binti Kadudu, Mnyarwanda kutoka nchini Rwanda. Wazazi hao walikutana Unguja katika harakati za biashara na hatimaye kufunga ndoa na kujaaliwa kupata watoto hao watano.

Abeid alikuwa mtoto mtiifu na mnyenyekevu kwa wazazi na mpenzi kwa watoto wenziwe na wakubwa pale kijijini. Huruma ilikuwa moyoni mwake, misaada mikononi mwake na umakini kwenye sura yake.

Huyo ndiyo Abeid Amani Karume.

Alipofikisha umri wa miaka minane (8) alipatwa na msiba wa kufiwa na baba mzazi, Amani Karume. Mzee Amani alikuwa ni muhimili wa Abeid kati ya mihimili yake miwili katika malezi yake; baba na mama.

Muhimili huu ulipunguza nguvu ya malezi yake na kuegemea katika muhimili mmoja tu wa mama mzazi. Dalili za kukosa baadhi ya haki zake za msingi za utotoni zilianza kujichomoza akiwa na umri huo wa miaka 8.

Haki mojawapo ya msingi ya kupata elimu shuleni iliyumba ingawaje Abeid alianza shule ya msingi Mwera akiwa na miaka minane, haikufua dafu. Mama yake alimpeleka mjini Unguja kwa mjomba wake akaendeleze kisomo chake, nako kulimtupa nje ya shule.

Mtoto Abeid Amani Karume hakupata masomo shuleni zaidi ya miaka mitatu, lakini alipata masomo ya ulimwengu zaidi ya miaka ishirini na hivyo kumtia katika kundi la wasomi wa ulimwengu na kufanya vyema masomo ya Maarifa, Historia, Jiografia, Siasa na Haki.

Masomo hayo ya ulimwengu ukweli ndiyo yaliyompa fahamu, ujasiri na maarifa ya kusema na kutenda jambo ambalo kwake na kwa wenzake ni jibu tosha na sahihi katika kuendesha maisha hapa duniani.

Alitambua hasara ya kuwa maskini na faida ya kuwa tajiri, ubaya wa kuwa mtumwa na uzuri wa kuwa muungwana. Hakusita kujua ujinga wa kukosa elimu na uelevu wa kuwa na taaluma. Wala hakusahau madhila ya dhuluma na ukwasi wa haki kwa mtu yeyote.

Utambuzi huo ulimtia katika biashara na uchuuzi mdogo wa bidhaa mjini Unguja na mwisho kuzama katika kazi ya ubaharia ndani ya meli ya Golden Crown mwaka 1920 na kuendelea kuwa baharia katika meli mbalimbali hadi Septemba 23, 1941 alipoacha kazi ya ubaharia.

Abeid Karume alijiunga na vijana wenzake si katika mambo ya biashara, uchuuzi na ujana tu bali alithubutu kuunda vyama vya michezo, siasa na umoja wa kutetea haki za wafanyakazi na wakulima wa Unguja na Pemba.

Kuanzisha klabu ya michezo African Sports, mwaka 1931 na baadaye kubadili taratibu za michezo kuwa za siasa chini ya The African Association mwaka 1934 na hatimaye kuunganisha chama hiki na Shirazi Association mnamo Februari 5, 1957, si jambo la masihara.

Chama Cha Afro-Shirazi chini ya uongozi wa Sheikh Abeid Amani Karume kilipambana na utawala wa kisultani kupinga uonevu, dhulma, unyonyaji na kudai haki na uhuru wa Mwafrika ndani ya nchi yake.

Mapambano haya hayakuwa mepesi kwa ASP, kwa sababu utawala wa sultani ulitumia hila, njama na dhuluma katika chaguzi mbalimbali na vyama vya siasa vilivyodhaminiwa na kusimamiwa na sultani.

Sultani wa Unguja na Pemba, Abdulla Jamshid na vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP), Muslim Association na Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP) walifanya hiana katika chaguzi kuu tatu, ASP kushindwa.

Uhodari na ushujaa wa Sheikh Abeid Karume katika kushawishi, kuhamasisha, kuanzisha na kuendeleza vyama vya michezo, siasa na vyama vya wafanyakazi na kupinga neno “African” lisiwepo, kulitingisha utawala wa sultani.

Kushindwa kwa ASP kwa hila za sultani na Mwingereza kulifanya Zanzibar kupata uhuru Desemba 10, 1963 chini ya vyama vya ZPPP na ZNP vikaungana na kuunda serikali iliyoongozwa na Waziri Mkuu, Sheikh Mohamed Shamte. Uhuru huo uliwakera mno wanachama wa ASP.

ASP ikishirikiana na Umma Party iliyoongozwa na Abdulrahman Babu, waliunda kamati ya mapinduzi iliyoongoza na kufanikisha mapinduzi ya Januari 12, 1964.


Baada ya mapinduzi, ASP na Serikali yake, vikiongozwa na Sheikh Abeid Amani Karume viliweka mapinduzi katika uchumi, elimu, 
kilimo na afya na kuweka hali za wananchi sawa. Ujenzi wa majengo bora na ya kisasa ulipata kasi ya maendeleo.

Usafiri na usafirishaji wa angani, ardhini na majini uliimarishwa na huduma za afya, maji na elimu zilipewa kipaumbele. Michezo, 
utamaduni na habari zilifunguliwa milango kwa wananchi na wageni kama watalii.

Dhamira ya kujenga uchumi na umoja wa Mwafrika, Zanzibar iliungana na Tanganyika na kuunda muungano wa Tanzania, Aprili 26, 

1964 maendeleo na mafanikio yote haya yamepatikana chini ya uongozi wa Sheikh Abeid Karume.

Ndoto na dhamira yake ya kuleta maendeleo zaidi katika visiwa vya Zanzibar ilikatishwa hafla siku yaApril 7 1972. SheikhAbeid Amani Karume aliuwawa na wapinga mapinduzi na maendeleo mema ya visiwa vya Unguja na Pemba walitumia mtutu wa bunduki kutoa uhai wa kiongozi huyu shupavu na mtetezi wa wanyonge, mjini Unguja.

Ni siku ya huzuni kwa Watanzania tunapokumbuka tukio la kikatili la kuuawa kwa mwanamapinduzi, mkombozi na mpigania haki ya Mwafrika na mpenda amani duniani. Akiwa ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Chama Cha Afro-Shirazi (ASP) Kisiwandui akicheza bao na viongozi wenzake, ghafla alishambuliwa kwa risasi na muuaji aliyedhamiria kufanya uovu huo.

Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliuawa kikatili.

Mchango wa mwanamapinduzi huyu daima hautasaulika katika Historia ya visiwa hivi vya Unguja na Pemba.

Tutaendelea kumuenzi, kutunza kumbukumbu zake na mambo mema aliyotuachia pamoja na kuendeleza harakati zake katika kujenga umoja, ushirikiano na uongozi kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!