Saturday, 11 August 2018


TAADHARINI NA HAYA MATUMIZI YA MADAWA.

Siku hizi kumekuwa na ongezeko kubwa sana la wataalam (?) walio ingilia fani za utabibu. 
Wengi wetu tunasikia au kusoma matangazo mbalimbali ya aidha waganga wa Kienyeji au awa wengine wanaodai kutibia kwa madawa ya KISUNNAH.

Hapa nitawazungumzia awa wa mitishamba iliyobadirishwa jina kwa kuitwa DAWA ZA KISUNNAH wakiwa na maana kuwa Mtume (saw) aidha alitumia au aliagiza tujiponyeshe kutokana na kitu fulani au zilitumika na yeye akazinyamazia kwa maana kuwa zinafaa.

Nakumbuka zamani ila si sana, tukiwaona Wazigua/wasambaa na Wamasai sana ndio wakiuza dawa za kienyeji, upande wa pili kulikuwa na madawa ya Kiarabu. Kwa pale Dar kulikuwa na duka moja maarufu sana kona ya mtaa wa Sikukuu na Uhuru likiitwa duka la Totti na kulikuwa na mengine maeneo ya Kariakoo, pia kulikuwa na mtu maarufu akiitwa Salehe Madawa.

Baadae sana kuanzia mwaka 2000 kati kukazuka watu wachache haswa nje ya misikiti, wakiuzauza Habatsouda, Asali na vichupa vya uturi na ungaunga wa madawa ya mizizi. Dawa hizi zikaja kupata umaarufu wa ghafla na wengi wakajiingiza kwenye uuzaji wa hayo madawa na kuyapachika jina la Madawa ya Kisunnah.

Binafsi si kwamba nakataa kuwa hakuna uponywaji kwa kutumia dawa za miti shamba (Herbal Medicines) nakubali sana, ila kama ilivyo kwa madawa ya hospitalini ambayo watoaji wake wamesomea hiyo taaluma, na hata uku kwenye tiba mbadala, nako pia kunatakiwa kuwepo na wataalamu ambao wamesomea hizo tiba na si kusomea tu kwa wiki moja au mwezi mmoja, lah hasha, ni kusomea kwa miaka kadhaa ili mtu kweli awe mahiri kwenye kutoa hizi tiba.

Waganga wetu awa ukiongea nao, utawasikia wakijilinda kwa maneno mazuri sana, kama vile bi'idhnillah utapona tu. Wengi kwa kusikia neno ili wamekuwa wakiingia na imani kuwa MwenyeziMungu ndio anayeponya na hizi dawa ni sababu tu ya kupelekea uponywaji huo.

Watu wengi wamajikuta wakiingia mkenge na kuwaamini waganga njaa awa kwa kuwaamini na kununua dawa zao ambazo ni aghlabu sana kuponyesha watu. Tena si ajabu ukawasikia hata Wamasai nao wakitangaza dawa zao na kukwambia kuwa za kwao ni zaidi ya zile za Kisunnah, maana nao washaona kuwa kuna ushindani, nao imebidi wabuni slogan mpya kuwa za kwao ni zaidi ya sunnah.

Ni kweli kabisa, sote tunategemea uponywaji kutoka kwa MwenyeziMungu, na hizo dawa ni sababu tu, lakini hata hivyo hatupaswi kujilia dawa ovyo ovyo au tukamwamini kila muuza dawa kuwa ana dawa mujarabu eti tu kwa kuwa mponyaji ni MwenyeziMungu na hizo dawa ni sababu tu, na ndio maana uwezi kukuta mgonjwa wa Malaria akapewa Asprin au panadol tu, kwa kuamaini kuwa bi'idhnillah atapona, la hasha, atapewa dawa husika iliyofanyiwa majaribio na kuhakikishiwa kuwa ndio yenye kuuwa vijidudu (parasites) vya Maralia kisha hapo ndio neno bi'idhnillah linaweza kutumika.

Lakini sivyo kwa matabibu wetu awa, ambao ukiwadadisi sana utawasikia wakisema mbona hata hizo dawa za mahospitalini pia wakati mwingine watu awaponi na wanakufa au kudhurika na hayo madawa!?

Ni kweli na ndio maana dawa za hospitalini zote zimewekwa taadhari na maelezo ya kina kuwa ukiwa na hali fulani au ukiwa unatumia kitu fulani usitumie hizo dawa na pia wanaelezea athari zake kiafya kabla ujaanza kuzitumia na si kujitungia tungia tu masharti.

Mnifahamu hapa, sina lengo la kuwakataza watu wasitumie hizo dawa zilibatizwa jina la Dawa za Kisunnah, lah hasha, lengo langu haswa watu wanapaswa kuwa makini na waangalifu sana, na ikiwezekana serikali hiingilie kati swala hili ili kuepusha madhara zaidi kwa watumiaji wake.

Ndio tumeambiwa kuwa kila ugonjwa una dawa yake, lakini si wote wajitangazao wanajuwa hizo dawa ziwe za kienyeji, miti shamba au hizi za kienyeji zilizopandishwa daraja na kuitwa za Kisunnah.

Dawa zote aidha ziwe za Hospitalini. Waganga wa Kienyeji au za Kisunnah, zinapaswa kuwa salama na kutolewa na watu ambao ni wataalam wa hizo dawa na si kila mwenzangu na mie kujitia uganga wa kutaka kuchezea miili ya watu.

Swali la Kujiuliza, unapohitaji dawa za miti shamba, kuna vipimo vyovyote vya kiafya ambavyo ufanyika kabla ya kupewa dawa husika?
Je wanajuwaje kuwa kipimo hiki au kile ndio sahihi kulingana na ugonjwa wako, je wanajuwa historia yako kiafya?

Magonjwa mengine ni dalili ya kusumbuliwa na mamtatizo mengine yaliyojificha, mfano mwanamume anaweza kulalamika kuwa ana upungufu wa nguvu za kiume, kumbe tatizo lake linatokana na Magonjwa mengine kama vile kisukari au saratani au Msongo wa mawazo au amekuwa ni mtumiaji wa muda mrefu wa aina fulani ya dawa kwa mfano dawa za kudhibiti msukumo wa damu (BP), vilevile yawezekana ni aliokuwa nao yaani ni mwenye Umri mkubwa au ni ukosefu wa usingizi wa kutosha na wakati mwingine ni Matatizo ya kihomoni tu.
Sasa haiwezekani mtu alalamike kuwa ana tatizo kisha apewe dawa bila kujuwa sababu ya ilo tatizo lake na icho ndicho kinacho fanyika uko mitaani.

Naandika hivi kwa sababu athari za matumizi ya haya madawa ya kienyeji na haswa hzi dawa za kuongeza nguvu za kiume zimekithiri sana siku hizi, mtu ili aonekane kuwa mahiri basi lazima akubali kuwa ana uwezo wa kutoa dawa za kuongeza uwezo wa jimai (Nguvu za Kiume) na mbaya zaidi hakuna ugonjwa unao mshinda.

Wapo watu wanalia baada ya kutumia dawa mbali mbali, kiasi wamejikuta kuwa yale walioyategemea yamekuwa ni kinyume chake kabisa.

Wengine wanalalamika kuwa zamani gari zao ilikuwa ukiziwasha (Kupiga start) ni kisi cha mara mbili tatu gari inawaka, japo kwa kusua sua lakini kiasi inatembea, lakini siku hizi tangia watumie hizo dawa, gari zao shurti kwa kusukumwa tena karibu na nusu ya safari, kiasi hata gari ikiwaka hata huyo abiria anapoteza hamu yote ya safari... Na Dereva nae hata nusu safari hafiki, kiasi robo safari tu, sekunde therathini nyingi, gari lishazima kabisa, hapo tena mpala kesho kama si wiki kuwaka tena.

Kuna kesi nyingi sasa za wanawake kukimbia waume zao au waume kukimbia wake zao, sababu ya wanaume kutoweza kuwaridhisha wake zao.

Taadhari tu, si kila muuzaji bidhaa anauza bidhaa itakayokidhi haja zako, jaribuni kuwa makini sana kwenye swala la afya zetu, tukiwa na matatizo ni bora kuonana na madaktari waliobobea kwenye hizo tiba na si kujitafutia shoti kati.

Kwa wale watakaopenda kujuwa dawa alizotumia Mtume (saw) basi wanaweza kukitafuta kitabu kinachoitwa:
Healing With The Medicine Of The Prophet, mwandishi wake ni Imam Ibn Qayyim Al-Jauziyah.

Binafsi ninacho nilizawadiwa na Swahiba wangu, siku nilipokutana nae Alhamdulillah ni kitabu kizuri sana kuwa nacho. 

Pia kinapatikana online kwa wale watakaopenda kukipakuwa...

 Healing With The Medicine Of The Prophet

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!