Tuesday 12 May 2020

Kwani Jukumu La Kulea Yatima ni la Nani!?

Mara nyingi, uona matangazo ya kuchangia vituo vya kulelea Mayatima, na haswa kinapofika kipindi cha mwenzi wa mtukufu wa mfungo wa Ramadhani.

• Swali ambalo tunapaswa kujiuliza, hili jukumu la kuwalea Mayatima ni la nani?
• Je ni jukumu la ndugu na jamaa katika familia au vituo vya wajasiliamali?

Binafsi sipingi huu utaratibu (wa bora nusu shari) wa kuwakusanya kwenye vituo, lakini  Waislamu tunapaswa kuamka na kuzipa baraka nyumba zetu kwa kuwalea Mayatima kwenye majumba yetu.

Kwa kuanzia tuangalie suala zima la malezi katika jamii, suala la malezi ni jambo la wajibu katika Uislam, kwani mtu (mtoto) akosapo malezi ya sawa bila ya shaka atakengeuka na atapotea. Kwa maana hiyo ndiyo Uislam ukawapa familia (ndugu na jamaa) wajibu wa kumhifadhi na kumlinda mtoto ili asipotee.

Katika Uislamu, haki ya kwanza kabisa, inamwendea Mama mzazi, bibi na babu wa pande zote mbili madada na makaka, kisha mama wadogo, kisha wapwa, kisha mabint wa kaka, kisha mashangazi, na kufuatia ndugu wengine kama ilivyo kwenye utaratibu wa mirathi.

Katika Suala la kulea yatima tutambue kuwa hili ni jukumu zaidi kwani kulea yatima kuna fadhila nyingi na ujira wake ni mkubwa mno. Na kutomlea vizuri pia kuna hatari yake.

Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametaja fadhila za Yatima mara nyingi sana katika Qur'an:
Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika nao basi ni ndugu zenu; na Allah Anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na Allah Angelipenda Angelikutieni katika udhia. Hakika Allah ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Surat Al-Baqarah: 2:220

Vilevile kwenye ayah nyingine, tunafahamishwa hivi:
Wanakuuliza watoe nini? Sema: Kheri mnayoitoa ni kwa ajili ya wazazi na jamaa na mayatima na masikini na wasafiri. Na kheri yoyote mnayoifanya Allah Anaijua.
Surat Al-Baqarah 2:215

Na khaswa mlezi wa yatima ni ndugu au jamaa wa damu Allah Amesisitiza:
Hakuweza kuvikwea vikwazo vya milimani (njia nzito ya kukufikisha peponi)?
Na nini kitakujuvya ni nini njia ya vikwazo vya milimani (njia ya kukufikisha peponi)?
(Kuvikwea vikwazo vya mlima huo ni) Kumkomboa mtumwa
Au kumlisha siku ya njaa.
Yatima aliye jamaa.
Surat Al-Balad: 11-14

Vile vile kasema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
Mimi na mwenye kumlea Yatima kama hivi. (Akaashiria kidole cha shahada na cha katikatikati pamoja na akaviachanisha baina yake.
Al-Bukhariy.

Kasema tena Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
Mwenye kuweka mkono wake kwenye kichwa cha Yatima kwa upole, Allah Humuandikia jema kwa kila unywele aliougusa kwa mkono wake
Imaam Ahmad.

Vilevile na katika kuwafanyia maovu Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametuonya:
Basi yatima usimwonee
Surat Adh-Dhwuhaa: 9

Amesema Allah Aliyetukuka:
Hakika wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni.
Surah An-Nisa 10

Na Amesema Aliyetukuka:
Wala msiyakaribie mali ya yatima ila kwa njia ya wema kabisa
Surah Al-An'am: 152

Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima.
Surat Al-Fajr: 17

Binafsi naweza kusema Waislamu sisi wa Sasa tumeuacha Uislamu na tumeutupilia mbali, tumeugeuza kama nguzo za mitumba sagula sagula, tunachagua kile ambacho tunaona ndicho tunachokitaka na kuacha kile tunacho kiona ni marapurapu.

Matokeo yake ndio hayo ya kuwasahu watoto Mayatima mpaka wanalelewa kwenye vituo, wakati hao watoto haki yao haswa ni kulelewa kwenye familia na si kwenye vituo kama hivi na hikma yake kwa watoto kulelewa kwenye familia, ili wakue wawe na mapenzi ya kifamilia uko watalelewa kama watoto wengine wenye wazazi na si kama walelewavyo kwenye vituo.

Huyu mtoto yatima aliyefiwa na baba yake au akafiwa na wazazi wake wote wawili, akishakuwa kijana anayejitambua na akafahamu ndugu na jamaa zake walimtelekeza na kumweka kwenye vituo vya kulelea mayatima, matokeo yake hatokuwa na mapenzi ya dhati na jamii na hata ya familia yake.

Ni ajabu sana na ni jambo lisilokubalika hata kidogo, mtoto anafiwa na baba yake kisha ndugu wa karibu wamtelekeze kwenye vituo vya kulelea watoto.

Huu ni udhaifu mkubwa sana wa imani. Tubadirike.

Allah atulinde na mitihani kama hii ya kuwadharau Mayatima wanaotuhusu wa ndugu wa karibu na kukimbilia kuwapeleka kwenye vituo maalum wakalelewe uko. Aamiyn

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!