Thursday 17 June 2021

 

VIONGOZI WA UAMSHO WAMEACHIWA HURU!?

 Hivi ni Kweli Wapo Huru!? Kama Huna Cha Kuandika Basi Usiandike. 

Ni furaha na nderemo kwa baadhi ya watu, haswa wale wenye kuwaunga mkono viongozi wa Uamsho. Wapo wanaolichukulia suhala la Uamsho kuwa ni la Kiimani zaidi na wapo wanalichukulia suhala hili kuwa ni la Kisisas zaidi na halina uhusiano wowote na imani zao.

Kuachiwa kwao aidha kunatokana na kelele za watetezi na wanaharakati mbalimbali, wakiwemo baadhi ya wabunge hasa kutoka upande wa Zanzibar, vyama vya siasa na wanaharakati wakitaka hatma ya masheikh hao wa Uamsho ijulikane kwa sababu wanasota gerezani kwa muda mrefu bila kujua hatma yao.

Kutolewa kwao gerezani kumekuja siku chache baada ya viongozi mbalimbali wa dini akiwemo Mufti mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir kutaka mamlaka za Tanzania kutenda haki katika kesi dhidi yao.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mashitaka  _(DPP, Sylvester Mwakitalu)_  aliyenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini Tanzania, mashekh wote hao wamefutiwa mashitaka yote na kuachiwa huru na kilichobaki sasa ni taratibu za kutoka gerezani.

Masheikh hao waliokuwa wanashikiliwa gerezani kwa makosa ya ugaidi, walifunguliwa kesi hiyo namba 29 ya mwaka 2014 wakikabiliwa na mashtaka ya kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwawezesha kufanyika vitendo hivyo.

Kila mtu na hoja zake, japokuwa kuna ambao wanalazimisha kuwa ni lazima hoja zao ndio ziwe ndio na ukiwa ukubalini nazo basi wewe si katika wao na Watakupiga Pande.

Tatizo la wanaharakati wengi wa mitandaoni, wamekuwa ni mahodari sana wa kusema na kusema, lakini wengi wao si wenye kuyatekeleza yale wanayo yasema au kuyahubiri. Wengi wao wanaimba kijamaa na kucheza kibepari.

Wanataka kuwepo na demokrasia ya kila mtu wawe na uhuru wa kusema kile wanachohisi ndio sawa kwa yeye kusema, haijalishi kama anafikisha kwa njia ya Busara na Hekima au kwa njia ya Matusi na Kejeri. 

Hao hao ukiwasoma kwenye kuta zao za tovuti baraza na ukiwapinga kwa hoja, watakuzuiya na kuondoa ulicho andika na hutaweza tena kuchangia mada yoyote kupitia wao.

Lengo la mcharazo huu si kujadili kwa nini waliwekwa ndani na sasa wametolewa. Wapo wanaopenda mjadala huu uwepo na wapo wengine washauanza tayari.

Wanatamani wanayoyataka yawe kama wanavyotaka, maswali yamekuwa mengi sana, wapo wanaoona kwanini wametolewa bila kushtakiwa, wapo wanao ona kwanini wametolewa baada ya miaka hisiyo pungua nane, wapo wanao ona kuwa watakosa tena ya kusema. Kila mtu ana mtanzamo wake kulingana na upeo wake, aidha wa kisiasa au kiimani.

Sote tunashukuru kwa wao kutoka, lakini kuna wale wanao ona kutolewa kwao basi kuendane na wao kulipwa fidia la sivyo waishtaki serikali kwa wao kuachiwa bila kushtakiwa.

Wanasahau kuwa makosa walioshtakiwa nayo ni makosa ya uchochezi, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) mwaka 2012 mwezi wa Oktoba, alisema kuwa; Washitakiwa hao Walitoa Matamshi ya Lugha ya Uchochezi Yanayoashiria Uvunjifu wa Amani na Kusababisha Fujo, Maafa Mbali Mbali na Mtafaruku kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mashtaka ambayo yamewekwa kwenye fungu la Ugaidi (SHERIA YA KUZUIA UGAIDI, 2002), makosa ambayo hayana dhamana wala fidia na kwa usalama zaidi wakaamishiwa Tanzania Bara.

Binafsi kwa hapa Tanzania sijawahi kusikia mtu aliyefungwa kimakosa au kushikiriwa na Polisi au Magereza kwa muda mrefu akalipwa fidia.

Msininukuu vibaya, sijasema kuwa wamefungwa kimakosa, bali hao walikuwa wameshikiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania za makosa ya Kufanya Vurugu na Uchochezi.

DPP ALISEMA HANA TENA NIA YA KUENDELEA NA MASHITAKA.

Sote tunapaswa tufahamu kuwa hawa wameachiwa kwa msamaha, 

Amri ya DPP hutolewa kupitia Sheria ya Msamaha wa Rais, hii ni sheria ambayo Rais ndiye anayekubali aidha kuendelea au kutoendelea kuwashikilia nia ya kuwashtaki pale Ushahidi utakapo kamilika.

 Rais wa nchi kupitia DPP uko ndiko maamuzi yanapotolewa na kutekelezwa, kupitia DPP Rais wa nchi ndio mwenye mamlaka ya kutaka na kutotaka.

Hivyo basi tunachotakiwa ni kushukuru kwa viongozi hawa kuachiwa japo kinadharia na ndio ukweli wenyewe walifungwa bila kuhukumiwa, tangia mwaka 2012 walipo kamatwa uko Zanzibar, kipindi cha utawala wa Jakaya Mrisho kikwete na Ali Mohamed Shein.

Na mwaka 2014 wakahamishiwa Tanzania Bara, Mwaka mmoja kabla ya Jakaya Mrisho Kikwete kumaliza muda wake, kipindi ambacho rais wan nchi asingeweza kuwaachia kwa ile sheria Huruma ya Raia kwa Wafungwa maana kulikuwa na joto kali la kisiasa na kesi yao ilikuwa mbichi hivyo vyombo vya Ulinzi na Usalama visingeweza kumshauri Rais awaachie kwa sababu za kiusalama.

Miaka imekwenda si haba, muda umefika na ndipo Rais wa sasa wa Tanzania, Samia Hassan Suluhu akamtaka DPP ajiridhishe kama watu hao ni hatari na DPP akafanya Uchambuzi kwa Wafungwa hao dhidi ya Tishio la Usalama wa nchi kwa kuvishirikisha vyombo vya Ulinzi na Usalama ambao hutazama kitaalamu kama watu hawa ni hatari bado au lah, wakishajiridhisha ndio wanatoa ruhusa kwa DPP kusitisha nia ya kuendelea kuwashikilia (Hii Haijalishi Kama Walitiwa Hatiani au Lah).

Na DPP anapopata taarifa basi analazimika kumtaarifu mkuu wa nchi ili apate ruhusa ya mwisho. Akishapata ruhusa, hapo sasa anawatembelea wahusika (Washtakiwa) uko walipo hifadhiwa na kuongea nao.

Na si kuwa wameachiwa tu bila ya masharti, lahasha, kuachiwa kwao kunaendana na masharti kadhaa, moja wapo ni kutojihusisha na mambo waliyoshitakiwa nayo awali au yaliyowafanya waingie matatani, pia wawe tayari kutodai fidia ya aina yoyote ile na lingine ambalo ni kubwa ni lile la vyombo vya usalama kufuatilia nyendo zao, na si ajabu kwa maisha yao yote au mpaka Rais atakaposema sasa basi,

Na Ikitokea wakavunja moja ya mashariti hayo basi watakuwa wamevunja makubaliano ya kisheria ya masharti ya Kuachiwa (Legal Agreement Terms of Release) hivyo serikali haitasita kuwashughulikia kwa njia inayoona inafaa.

Baada ya makubaliano hayo ndipo sasa ndipo DPP anatoa Maagizo kwa Kamishina Mkuu wa Magereza kuwaachia na ndio kilichofanyika hapo. 


Kuna mengi, yaliyojiri kuna tunayo yajua na yale tusiyo yajua, yaliyoko nyuma ya pazia kwa kuachiwa kwao tunayawacha kama yalivyo, si lazima makaburi yote yafukuliwe.


0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!