Friday 2 September 2022

 
NJUGUMAWE

KWA KIINGLISHI ZINAITWAJE!?

Nakumbuka Mara ya Mwisho Kuzitia Kinywani Ilikuwa ni Zaidi ya Miongo Mitatu na Nusu Iliyopita Tukiwa Mandarini.

Porojo na Ndarire bila Ndaro za Fikra Nasaha

Njugumawe zile zilivuta tamaa na Ghamu, iliyoletwa na njaa pamoja na Raghba tulizokuwa nazo kutwa nzima, zilikuwa zimeungwa kwa tui la nazi ya Mdondoo, zikaongezewa ladha ya Iliki kidogo na kwa sukari ya Kurashia.

 

Tukiwa kwenye Marago, huku tumekaa juu ya jamvi lililoshonwa kwa Mafunjo, tukikingwa jua na Shamiana. Sariri zikiwa zimening'inizwa huku na kule. Angani mwonzi wa jua ulikuwa umefichwa na Moshi wa Mafunde funde.

 

Kweli Nikaginizika kuwa "Mzungu wa kula hafundishwi mwana," maana chakula kile jinsi kilivyokuwa kitamu, kiasi cha kuwavutia Sisimizi, wakija kwa Mdorongo, wakiokoteza vilivyo dondoka ardhini.

 

Pembeni juu kidogo, kuna Shubaka kubwa, kumewekwa Runinga ikionyesha kipindi cha ngoma za asili, na wacheza ngoma ya Mdurenge wakicheza kwa namna ya Mdomwa.

 

Mandharinyuma, ilikuwa ni ya milima na mabonde kwa mbele ilikuwa uwanda mpana wa Nyika bulibuli. Juu angani, Vijumbamsale, Vinega na ndege wengine wakiruka kwa amani.

Nyuki, Bunzi, vipepeo na wadudu wengine wakiruka kujitafutia riziki huku na kule, wengine wakimkimbia Chekeamwezi, kiasi cha kuifanya mioyo yetu kuwa na Buraha na furaha.

Upepo mwanana Pepezi ukipiga nyuso zetu, ukituburudisha, na kufanya Chamchela ndogo ndogo za hapa na pale.

Nyani Wakiriarilika huku na kule, wakituonyesha Ngoko zao. Juu ya miti kulikuwa na Kindi wakikimbizana na Goromwe na kwa mbali tukiwaona Ngosi, Dondoro, Funo, Pundamwitu na Hayawani wengine wakila nyasi mbugani na wengine wakinywa maji bwawani, wakiwemo pamoja na Kongoti.

Upande wa pili wa Jimbu, tukiwaona Twiga kwa madaha, wakikimbizana, tukinogeshwa sana na Milonjo yao, kiasi cha kuwaduwaza baadhi yetu, ilikuwa mandhari yenye kupendeza na kuvutia, ikituonyesha utukufu wa Muumba, katika uumbaji wake.

Pembeni yangu kulikuwa na Konzo pamoja na kisu cha Msasi. Ndani ya Shamiana kwa juu, kulikuwa na Visusu kadhaa, vilivyotawanywa huku na kule.

Tukiwa tumehamanikishwa na mlo, Ghafula mvua ikaanza kunyesha, na kupelekea majani ya Mnyegea ulioko karibu, kudondosha matone makubwa ya maji, kiasi cha kutengeza Mvo na huku Riha ya vumbi la udongo ikahinikiza eneo zima.

 

Sauti ya Mungurumo mkubwa wa Radi ikasikika angani na kuifanya mioyo yetu kushituka, huku ikitanguliwa na mng'aro mkali wa umeme...

Nikanyanyua Rununu yangu na kuangalia muda, ilikuwa ni saa kumi na moja unusu za jioni, nikakumbuka jambo lililonifanya nitabasamu, nikajiuliza tena…

 

HIVI HIZI NJUGUMAWE, ZINAITWAJE KWA KIINGEREZA!?

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!