Monday 18 May 2015


Wakati mwingine uandishi ni uwakilishi wa kweli wa mawazo ya mtu yakiwakilisha jamii ya watu wa aina fulani, aidha kitabaka, kijinsia au hata kiimani.

Upeo wa maisha ya wanadamu huangazwa kwa nuru ya mapenzi. Mapenzi yana taathira kubwa na ya kudumu na yana nguvu kubwa katika maendeleo ya kimaada na kiroho ya mwandamu. Nguvu hizo huanzia kwenye mkondo wa maumbile ndani ya dhamiri ya mtu na ya maana na kumalizikia katika hazina kubwa isiyo na kikomo.

Unapoandika jambo lolote lile kwenye haya majukwaa ya wazi, yakiwemo magazeti au mabaraza ya kwenye mitandao au kwenye simu na mengineyo, wasomaji wako watakuwa wanaiangalia ile jamii unayo iwakilisha kwa jicho la mashaka au bashasha na kuzua maswali mengi vichwani mwao.

Jamii zetu zina matatizo mengi yanayoikabili, matatizo ambayo kila kukicha yanaongezeka na kukosa utatuzi yakinifu. Maadili machafu ni machafu kama vile mwili mchafu usababisha harufu mbaya na kuwakera walio jilani nawe, hivyo hivyo tabia mbaya ukera na kuathiri jamii inayo kuzunguka.

Katika ulimwengu huu uliojaa taharuki na vioja, binadamu huwa daima katika harakati na pirikapirika akiogelea katika mawimbi ya matatizo na masaibu.

Maisha yake hufuatana na mashaka na matatizo, isipokuwa tu awe anachuma maua adimu katika bustani la maisha au awe anapata matumaini na matarajio yake moja baada ya moja. Madhali uzi wa uhai wa mtu haukukatwa kwa mkasi wa mauti, basi kila siku huwa na matumaini, huhangaika na hutafuta mafanikio. Taa ya matumaini ndiyo inayomwangaza mwenye matumaini, na matumaini hayohayo ndiyo yanayomgeuzia maisha yake machungu kuwa matamu.

Huenda mara nyingine mojawapo kati ya silika za kimwili kama vile uroho au ubarakala ikaasi na kuwa ni chanzo cha masumbuko ya mtu. Uhasidi ni mojawapo kati ya matunda ya silika za kimwili kitamaa, ambao hujidhihirisha kwa kutamani vibaya, kuitia pingu dhamiri njema na tambuzi, na kumzuia mtu kuyapata matarajio halisi ya maisha yake. Mwenye kijicho hawezi kumtazama mwenzake akistarehe au akifanikiwa; moyo wake humchoma na husononeka kila anapowaona wenzake wananeemeka.

Roho zetu ni kama jangwa lisilo na ngome wala ukuta ambapo wezi wa furaha na mafanikio huweza kuingia kwa urahisi. Upepo mdogo kabisa huzitia wahaka na wasiwasi nyoyo zetu. Maadui wengi wa tamaa na hawaa huingia majumbani mwetu na kila mmoja hutuamrisha na hutusugua roho zetu.
Kila mjinga hujua kwamba anapoumwa sana na kichwa inambidi aende kwa daktari kutibiwa, lakini yule mwenye kuugua uhasidi inambidi ateketee moyoni mwake!

Kuna masuwala ambayo yameanza kujikita sana kwenye mabaraza ya mitandaoni, masuwala ambayo athari yake kama hatuta tatua sasa basi itakuwa majuto makubwa sana siku za mbeleni. Masuwala haya ni yale ya kiitikadi za Kimadhehebu. Haya ni masuwala ambayo yemesababisha upofu wa akili na nafsi, kiasi ya kwamba hatuoni wala hatusikii lolote lile lililo nje ya itikadi zetu za Kimadhehebu. Haya masuwala ambayo moto wake kama hatutoangalia basi utateketeza Uislam na Umoja wetu na kutujengea uadui wa kweli uko mitaani.

Waislam na Jamii zilizojikita mitandaoni hivi leo, inalichukuliya suala hilo la Ubaguzi wa na Kimadhehebu, kuwa ni muhimu sana kwenye bongo zao, kiasi ya kwamba kutoa uzito wa tani kadhaa za chuki ma machafuko yenye kuathiri nafsi na bongo za wasomaji. Lakini kiuhalisia na hasa wale ambao wapo ugenini haswa nchi za ulaya na Amerika. Wamekuwa wanashikana na kushirikiana kwa misingi ya maeneo walikotoka, yaani Utaifa. Hadi imefikia shughuli mbalimbali

kuendeshwa kwa misingi hiyo pamoja na shughuli hata za dini ambazo mtu si wa imani ile uudhuria na kushiriki kikamilifu kabisa.

Ni muhimu sana kwa wale wenye kuleta umadhehebu washiriki katika kuimarisha hali ya Uislam! Ni jambo la kusikitisha sana kuona baadhi ya Masheikh na Wasomi wa Kiislam wamelinyamazia jambo hilo na hali wanaliona mbele ya macho yao na kusikia likizungumziwa na zaidi ni kuwa kuna hata kati yao wenye kushiriki katika kuihamasisha na kuikuza hali hiyo.

Kwa hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu, kuyapiga vita kwa nguvu zote kila ambapo tutaona mambo haya yanajitokeza. Na khasa kwa wale viongozi na wasomi wa kidini, na wasimamizi wa haya majukwaa baraza, wahakikishe mambo haya hayapewi nafasi kwani Ushabiki wa Kimadhehebu ni adui yetu na Uislam wetu, na sio wao kuwa wa mbele kuyashabikia au kuyanyamazia.

Basi namalizia kwa kusema kwamba, Mapenzi kwenye Uislam na Nasaha njema ni sababu muhimu kabisa ya kumvuta mtu. Mtu mzuri kwa tabia na amali ni kama taa inayong'aa yenye kuongoza fikra na maendeleo ya jamii. Usafi wake wa moyo una taathira kubwa katika muundo wa maadili ya watu.

Qur'an Surat Al I'Mran [3] 103
Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka.”

Basi na tujirekebishe japokuwa hatupendi.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!