Tuesday 23 June 2015


Tutokako kifaa kidogo cha mkononi unachozungumza nacho hivi leo, kiliogopesha mno na aliyenacho basi alikuwa ni mtu wa idara nyeti. Leo hii kimekuwa kifaa maarufu kwa matumizi mbalimbali.

Kifaa hiki kimeenea sana na tena kimekuwa bora mara dufu, na ndio ustaarabu mpya, vizibiti siri vipya na wepesi mpya wa mawasiliano na bado tutaendelea kuunda.

Nauliza Je tunakitumia kwa faida gani iliyo nzuri? 

Binafsi sijui maana hata kwa faida mbaya kwa wengine imetosha, maana hoja ni kuwaumbua wenzio na kuifurahisha nafsi yako. Kwa Allah tungojee hesabu.

Facebook, Twitter, Skype, whatsapp, Youtube na vinginevyo kweli ni daraja fupi za mawasiliano, lakini kwa wasiotumia vyema utu na heshima zao ni daraja dhaifu mno la kukuelekeza kwenye ghadhabu za Allah, kwani unasimanga, unakashifu, unazuwa uongo, unafitinisha na unaiba siri za watu bila idhini zao. 

Vyema kwenye ghafla njema, je kwenye yale yasio pendeza?

Jamani kwanini hata wagonjwa wapo ICU, atokee mtu na umbea wake kwa teknolojia ajidai anakwenda kukagua mgojwa, basi nafasi hiyo ya kipekee ya kusimama na kumuombea dua ndio atammulika na whatsApp huyoo dakika moja mgojwa wa watu kajaa duniani kote ana mipira kohoni, puani na waya za vifuani.

Mmbeya huyu keshakonga roho, kawafurahisha mahasimu wa mgonjwa hata maiti nayo upigwa picha akatangazwa bila ya idhini ya wenyewe.

Njoo kwenye huo mtandao wa Skype, matusi humohumo, wanaonana uso kwa uso, wa Ulaya, Marekani au Arabuni wanasutana kwa mtandao kwa walio Afrika. Kila mmoja anamlaani mwenzie kupitia katika kioo, utadhani jogoo pale aonapo ona jogoo mwingine kwenye kioo, kumbe ni mwenyewe anakiparura kioo, ndio tusi linakurejea.

Tizama mitandao inavyo tuchezea, uko kuchorana na kubadirishana sura na kuvalishwa usivyo vivaa au kuunganishwa na mtu husiye pendana naye, basi usiseme, ufundi wa haya upo kiganjani, tuna umbuana tu.

Nasema, hatutumii nehema vyema, tena na wakati hatuutumii ipasavyo, baadhi yetu hivi sasa hatuwezi kustaamiri dakika tano, tusivute simu zetu, tupigiwe au tusipigiwe, kila mmoja kainamia anapangusa kioo cha simu kama bao la kupigia ramli. 

Anaandika tu akifuta, si mirihi, si shamsi si kamari.

Ebu tukithirishe ibada, Allah tunamsahau, tunatumia vibaya mitandao, je hatujasoma ile ayah ya 148 ya Surat An-Nisaai, inayosema...

"MWENYEZIMUNGU hapendi uovu uenezwe kwa maneno ila kwa mwenye kudhulumiwa. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua"

Basi tuyafanyao Allah anatujuwa, yeye ndiye aliyetuumba, tusijidanganye kwa kuwa ufundi sasa unazidi basi tutakufuru. 

Tunajuwa sasa simu zetu zinafanya kazi hata kwenye pipa la maji.

Nyengine zinafunguka kwa kuzipepesea jicho au kupandisha nyusi, mbali ya hiyo miito ya milio ya mbuzi paka na mingine, inayokera hata msikitini.

Lakini kumbuka wewe na mimi tulikuwa nani kama si tone la maji ya uzazi, tushakuwa wajuwaji kwa kuwakera wengine!?

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!