Tuesday 20 October 2015

Uchaguzi Mkuu hapa nchini umekwishafika. Utafanyika tarehe 25th Oktoba 2015.

Dini yetu tukufu ya Uislamu inatufundisha kuchukua tahadhari katika maisha yetu yote. Inatupasa kuchukua tahadhari kila tuonapo jambo linaloweza kuleta hatari au kutishia usalama.

Ni kutokana na hali hiyo tumeona ni vyema kutoa taadhari hii kwa ndugu wote kwa ujumla wapate kuzingatia na kuchukua hatua za kujihadhari na mambo yafuatayo wakati wa uchaguzi huu.

Tunatoa maelezo haya baada ya kuzingatia hali ilivyo na kuona kuwa upo uwezekano wa kutokea vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani. Hayo yakijiri, yataambatana na jitihada za vyombo vya dola kuyadhibiti. Madhara yanaweza kutokea kutokana na vurugu zenyewe na hata kutokana na jitihada za vyombo vya ulinzi kudhibiti vurugu hizo.

Tahadhari zifuatazo zaweza kuiepusha wewe na watu wako kutokana na madhara na shida wakati huo.
Tunatoa mwongozo huu hali ya kuwa ni wenye kumuomba Allah Atuhifadhi na Atulinde kutokana na kila aina ya mabalaa na majanga.
Kwa kufuata misingi ya Dini yetu tunamuomba kila muislam kuchukua tahadhari na kushikamana na muongozo huu kwa lengo la kujiongezea usalama.

KWA NINI TAHADHARI:

I. Uzoefu unaonyesha kuwa vurugu zinaweza kuzuka siku ya upigaji kura, au katika siku za kuhesabu kura, au wakati wa kutangaza matokeo katika vituo, na mara baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais. Vitisho vya matumizi ya nguvu za umma vinaashiria kuwa huenda vurugu zikadumu kwa muda mrefu na kusambaa sehemu nyingi.

II. Kuna uwezekano wa kukatika kwa umeme na kuwepo upungufu wa petroli, dizeli, gesi, mafuta ya taa na maji.

III. Kuna uwezekano wa mifumo ya mawasiliano ya simu kutokuwepo, kwa maana ya kwamba watu wanaweza wasiwe na mawasiliano kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS), simu, e-mail n.k. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kuwa mitandao ya kijamii ya Mawasiliano haitafanya kazi siku ya uchaguzi na siku kadhaa baada ya hapo.

USHAURI WA KUFUATA:

1. Jitahidi usipate mshituko kama patatokea vurugu katika eneo la karibu unapoishi. Kuwa mtulivu na tafuta ufumbuzi wa tatizo lako kwa njia nzuri.

2. Hakikisha wewe na familia yako mpo nyumbani baada ya kupiga kura, wakati kura zinahesabiwa na matokeo yanatangazwa. Matokeo uchaguzi wa rais yanatarajiwa kuanza kutangazwa kuanzia tarehe 28th October 2015. Msitembee atembee nje bila sababu ya lazima.

3. Jiepushe na kuwapeleka watoto shuleni kuanzia tarehe 26 Oktoba 2015.


4. Familia zetu zisitoke nje siku ya tarehe 28th Oktoba 2015 bila sababu ya lazima sana mpaka hali itakapothibitika kuwa shwari.

5. Hakikisha milango na komeo zote za milango katika maeneo ya kuingia katika nyumba yako ziko katika hali ya usalama na umadhubuti. Kama kuna haja ya kufanya marekebisho na maboresho ili kuiongezea nguvu basi fanya hivyo kabla ya siku za hatari.

6. N.unua umeme wa luku za kutosha toka tarehe 24th Oktoba 2015 mpaka tarehe 15th Nov. 2015. Ikiwezekana weka wa mpaka mwisho wa Novemba.


7. Hakikisha simu zako zina muda wa maongezi wa kutosha na una vocha za kutosha nyumbani kwa mawasiliano ya wiki mbili hata zaidi.

8. Jitahidi uwe na chakula cha kutosha nyumbani kuanzia tarehe 24th Oktoba 2015 mpaka tarehe 15th Novemba 2015 au hata zaidi. Mfano wa vyakula: mchele wa kutosha, Maharage, unga wa ngano na sembe, mafuta ya kupikia, viazi, vitunguu, nyanya za kopo za bakhresa, nazi za bakhresa – hivi ni baadhi tu ya vyakula; pia usisahau maji ya kunywa, mkaa au gesi kama unatumia gesi.

9. Pia tunashauri uhifadhi maji ya akiba kama una matangi yaanze maji kama huna jaza ndoo zote na vyombo vya kuhifadhia maji. Pia vyema uwe na tochi na betri za kutosha, taa za solar (mwanga wa jua) n.k. Mwanga ni muhimu wakati wa dharura.

10. Hakikisha kwa wale wote wanaotumia dawa kila siku kama za kisukari, presha, pumu n.k wana dawa za kutosha kwa mwezi mzima wa Oktoba na Novemba. Dawa nyingine ambazo zinatumika kila siku kwa dharura kama Panadol, dawa za vidonda, bendeji na plasta vizuri uwe nazo pia. Viwembe vipya na mikasi midogo pia uwe navyo.

11. Mjihadhari na kukaa na kuzungumza katika makundi ya watu zaidi ya watatu mahali popote pale na hasa nyakati za usiku. Kwaweza kuwa na misako na kamatakamata.

12. Jiepusheni na kuzungumza mambo ya siasa hadharani na kutuma ujumbe wa sms,  whatsApp, e-mail nk kuhusiana na matukio ya kisiasa. Meseji zote zinaweza kufuatiliwa na ukakamatwa. Usitume matokeo ya uchaguzi hata kama ni kweli kabla hayajatangazwa na msimamizi wa uchaguzi, ni kosa la jinai na adhabu ni kubwa. Utaharibu maisha yako.

13. Jiepushe na kufanya midahalo na majadiliano ya kisiasa mitaani na kuonyesha ukereketwa wako na chama chochote cha siasa.

14. Vijana wote wanatahadharishwa na mikusanyiko na mishughuliko yoyote ya nje hasa ya usiku katika mwisho wa mwezi wa Oktoba na mwanzo wa Novemba.

15. Jiepushe na malumbano ya aina yoyote yale na askari na polisi wakiwemo wa usalama barabarani (traffic), askari wa kawaida au wana Usalama wengine.

16. Hakikisha una kitambulisho, (kadi ya kupiga kura, kadi ya uraia, leseni ya udereva au aina nyingine ya Utambulisho), muda wote ambao upo nje ya nyumba yako katika mwezi wa Oktoba na Novemba. Wahimize watu wako kufanya hivyo pia.

17. Wasiokuwa raia wa Tanzania muda wote watembee na vibali (Permit) au hati ya kusafiria (Passport). 

18. Siku ya kupiga kura, baada ya kupiga kura, vizuri sana urudi nyumbani, jitahidi kuwa mbali na vituo vya kupiga kura. Wahimize watu wako kufanya hivyo pia.

19. Jiepushe kabisa na kuharibu mabango au vipeperushi vya kampeni vya  wagombea.  Ni kosa la jinai na unaweza kufungwa. Lakini pia mashabiki wenye hasira wanaweza kukudhuru.

20. Kwa wale wote wenye watoto wao wadogo wahakikishe mahitaji ya watoto wao hasa chakula chao maalumu kama maziwa, dawa zao, nepi nk, zipo za kutosha.

21.  Tuwe na nyumba nyingine (ndugu, jamaa n.k) ya kwenda kama maeneo tunayoishi tunahisi hayapo salama kwa kuwepo wingi wa askari, vurugu n.k.

22. Tafuta na hifadhi namba za huduma za dharura kama namba ya polisi ya kituo cha karibu, namba ya zimamoto, namba ya Tanesco, na ya gari la wagonjwa mahututi, pamoja na namba za ndugu na jamaa. Hifadhi kichwani, katika simu lakini pia ziandike katika kitabu na uwe nacho karibu saa zote.

23. Andaa orodha ya ndugu na jamaa na wekeni mtandao wa ndugu na jamaa na kujulikana hali na kupashana habari juu ya hali ya usalama na mfanye taratibu za kusaidiana katika hatari na madhara.

24. Weka pia akiba ya pesa taslim kwa matumizi ya kila siku na kwa matumizi ya dharura ikiwemo nauli kwa ajili ya safari za ghafla ikilazimika kufanya hivyo. Weka pesa katika simu yako pia. Lakini kumbuka kuwa yawezekana mitandao ya simu isifanye kazi ipasavyo.

25. Wenye magari wayaweke tayari kwa safari ndefu. Service, matengenezo na mafuta ya kutosha.

26. La mwisho, gumu lakini muhimu sana. Ikitokea nyumba yenu kuvamiwa na makundi ya vurugu chukua hatua zifuatazo:

A. Zima umeme main switch.

B. Zima taa zote ndani na nje zikiwemo kandili, taa za betri na za chaki.

C. Piga simu polisi haraka kisha kwa ndugu na jamaa ili kuomba msaada.

D. Ikiwa upo uwezekano, ondokeni haraka kwa kificho bila kuonekana. Ikifanikiwa kutoroka kimbieni mbali na kujificha na mkiiweza mwondoke kabisa eneo hilo.

E. Ikishindikana kutoroka, msibweteke. Ni wakati wa mapambano, lindeni usalama wenu kwa nguvu na maarifa. Fungeni milango, sukumieni vitu vizito kama meza, kabati, kitanda, nk, kuiimarisha isifunguke. Tumieni silaha mlizonazo kujilinda ikiwa ni pamoja na mapanga, visu, michi au mitwangio, chumvi, pilipili, nk.
Pambaneni kuzuia wavamizi wasiingie ndani - kumbuka ni rahisi kumzuia adui mlangoni kuliko kupambana naye akishaingia ndani.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!