Saturday 24 October 2015


Nimeamka ghafla kutoka usingizini ambako nilikuwa nimeota ndoto ambayo sijui niite ya kutisha au ndoto ya majinamizi au yenye kunipa ujumbe wa aina fulani. Ndoto hii kwa kweli imesababisha niwe na mawazo mengi yakipishana uku na kule kwenye ubongo wangu, kama vile nipo mitaa ya Kariakoo.

Na haswa ukizingatia yamebaki masaa kadhaa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hii, uchaguzi ambao utaamua nani atakuwa mtawala wa nchi ya Bongoland.

Sielewi kwa nini nimeota ndoto ile, labda kwa kuwa nimekuwa msomaji wa mabandiko mengi yanayo uhusiana na huu uchaguzi. Kiasi ya kuweka athali mchanganyiko kwenye akili yangu.

Ukiondoa wanasiasa wenye kupiga kampeni zao ili wachaguliwe, upande wa pili kuna wale ambao kampeni zao wamezielekeza kwenye imani zao za dini.

Hawa wamegawanyika pande mbili kuu, kundi la kwanza ni la Waislam na kundi la pili ni la Wakristo. Makundi haya kwa ujumla wao ndio wanachukuwa idadi kubwa wa raiya ambao wanaoweza kutuchagulia Rais na chama kitakacho kuja kutawala baada ya uchaguzi kwisha.

Pande hizo kuu mbili nazo zimegawanyika. Kwa upande wa wakristo kila kundi linataka rais atoke kwenye dhehebu lao, japokuwa kampeni zao si za wazi sana, kwa sababu zinafanyika kwenye majengo yao ya ibada. (Hao tuwaache kwanza).

Nizungumzie tu upande wa Waislam na kampeni zao kuelekea uchaguzi huu wa mwaka 2015. Upande huu wa Waislam kuna makundi mawili ambayo yanarumbana na haswa kupitia mitandaoni na wachache wakizifikisha fikra zao kwenye misikiti na majukwaa yasio rasmi.

Kuna kundi ambalo hivi sasa linalopinga upigaji wa kura kwa sababu ambazo wanaziona wao kuwa ni sawa ili kundi miaka kumi (10) iliyopita halikuwa na nguvu na hata misimamo yao haikujulikana sana, labda kwakuwa tu hawakuwa wakitumia mitandao ya kijamii kama ilivyo sasa.

Hawa wanachosema ni kuwa kwa Muislam kupiga kura kumchaguwa kiongozi atakaye kwenda kusimamia katiba ambayo haitokani na Qur'an ni Ukafiri na atakayepiga kura basi anasimamisha ukafiri.

Kuna ambao wanaunga mkono upigaji wa kura kwa kutoa hoja zao mbali mbali na wakizingatia kuwa nchi hii si ya hao makafiri peke yao, ni nchi yenye Waislam na Wakristo na wachache wasio na dini rasmi. Kukaa pembeni na kuwacha kuchagua kile ambacho kinaonekana kinaweza kuleta uafadhali kwenye mustakabari mzima wa Waislam na Uislam ni jambo bora na lenye manufaa kwa Waislam na Uislam wao.

Jambo ambalo limekuwa likinisumbua akilini na kunishtua kwa kiasi fulani ni pale wazo la kutopiga kura kwa mfano likikubaliwa na Waislam wote, wenye kujitambua na wale wasiojitambua (kumbuka kuwa nchi ya Bongo Waislam ni wengi kuliko wale wa upande wapili). Wakagomea kupiga kura na wale Waislam wote walioko serikalini nao wakaachia vyeo na nyazifa zao na wakaacha kuwatumikia wananchi kupitia serikali kwa maana walioko uko wizarani na maeneo mengine kama vile Jeshini, Polisi, Magereza Uhamiaji na taasisi zote za serikali, kwa sababu hao wote wanasimamia katiba hii tulionayo ambao inatambuliwa ndio mwongozo wan chi ya Bongoland.

Taswira iliyonijia ni kuona nchi tukiwakabidhi rasmi Wakristo waendeshe vile wanavyotaka kwa sababu hakuna Muislam yoyote yule ambaye anaweza kusema kuwa ilo ni kinyume japo kwa kile kidogo tunachoweza kukitetea.

Binafsi nasema kuwa kama kweli mnataka watu wasipige kura kwa kuwa tu mna misimamo yenu ambayo mpaka sasa hamja elezea baada ya Waislam kutopiga kura na wale walioko uko serikalini wakatoka, kitakacho fuata ni nini, au tutasema nchi hii ni ya kikafiri na hatupaswi kuishi kwenye nchi ya kikafiri, je mnataka tuwe wakimbizi katika nchi tuliozaliwa nchi ambao baba zetu walipoteza mali zao na maisha yao,katika kutafuta uhuru!?
Kama wewe na mimi ni Waislam wenye uchungu na Uislam wetu, tujiulize kwanza, tumeufanyia nini Uislam kiasi cha Waislam na wasio Waislam wakaona faida ya Uislam kiasi wakatamani kuwa Waislam!?

Tafakari, kisha vuta fikra na kutathmini ni vipi hali ya Waislam itakavyokuwa pale mawazo yenu yakifanyiwa kazi, kwa sababu katika Uislam hakuna maamuzi ya bora liende au tutajuwa uko mbele, Tumpate aliye na afadhali kisha, kisha tujipange na kujipanga uko si kwa muda wa miaka mitano au kumi. Kujipanga ni kuwa na mashule kuanzia za chekechea, mpaka vyuo vikuu, uku tukihakikisha kila anayemaliza uko basi anajitambua.

Tukiweza kuwa na watu wakutosha kwenye Nyanja nyingi za kiserikali, wabunge wa kuweza kupinga na kupitisha kile ambacho kitaweza kuleta unafuu kama si kuondoa kabisa kero zetu, hapo ndipo tulete hizo kampeni zetu, na si kwa kuhamasisha tusipige kura, lah, kuhamasisha tuwe na kile ambacho tunakiona kuwa ni bora kwa kila Raiya wan chi hii.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!