Thursday 26 November 2015


Mama mmoja muuza samaki kutoka nchini Uganda amekuwa wakiweka akiba kwa kipindi cha miaka 10 - kutokana na biashara yake hiyo - ili aweze kwenda kutekeleza ibada ya Hijja mjini Makkah.

"Nina shauku kubwa kufika Makkah, kulishuhudia kaburi la Mtume Muhammad (s.a.w), Mlima Arafat na kunywa maji ya Zamzam,” amesema Bi. Kasifah Nankumba mwenye umri wa miaka 58 wakati akizungumza na shirika la habari la Uturuki, Anadolu. "Masheikh wametupatia muongozo kuhusu safari hii. Nina shauku kubwa. Ninahofu kuwa naweza kuzimia.”

Kwa muongo mmoja sasa, Bi. Kasifah amekuwa akiweka akiba kidogo kidogo kutokana na biashara yake halali ya kuuza samaki ambayo amekuwa akiifanya kwa miaka 28 katika soko la Kalerwe jirani na mji wa Kampala.

Mama Kasifah anakumbuka mwaka 2006, alipokuwa amekaa, ghafla alijsikia kuwa anawajibika kutekeleza ibada ya hijja.

"Lakini sikuwa na pesa yoyote, hivyo wazo hilo nililiweka pembeni,” anasema.

Hata hivyo, baadaye alipata fursa ya kukutana na mtu anayejulikana kwa kusaidia safari za Mahujaji kwenda Makkah.

Mtu huyo ajulikanaye kama Haji Musa, alimtambulisha kwa meneja wa shirika la Mityana Hijja and Umrah Tour Agency, ambaye alimshauri aanze kuweka akiba.

Kutokana na akiba yake, walianza kumnunulia dola na kumkabidhi risiti.
Kuanzia mwaka 2007 mpaka 2009, aliweza kuweka akiba ya kiasi kidogo cha dola 4 mpaka 5 kwa mwaka".
Mwaka 2009, alisikia kwamba kuna mtu anayesaidia ufadhili kwa mahujaji na hivyo akaanza kumtafuta. Siku mbili baadaye alifika nyumbani kwa Hajji Kajumbi.

"Nilimwelezea suala langu, lakini kwa bahati mbaya hakuweza kunisaidia”, anasema.
Alimuonesha risiti za dola alizoweza kuweka akiba kwa miaka mitatu.

"Aliniombea dua na kisha akanitaka niongeze uwezo wa kuweka akiba, huku akiniambia niwe nawasilisha kati ya dola 100 na 200 kwa shirika lile la hijja," anasema.

Kuanzia wakati huo alianza kuwasilisha akiba yake kila baada ya miezi minne au mitano.
Mnamo Juni 15, 2015, alipokea simu kutoka kwa meneja wa ofisi ya Hijja akamwambia: "Hajjati Kasifah, pesa uliyoweka akiba sasa inatosha kwa safari ya Hijja.”

"Nilikuwa sokoni, aliniita mara nne lakini nilishindwa kuongea.”
Sasa akiwa mwenye furaha alihudhuria Masjid Wandegeya, ambapo alikuwa akipata mafunzo na maelekezo juu ya safari, akasema: "In sha Allah, nikirudi kutoka Makka, nitakaa nyumbani na kuendelea kufanya ibada; sitarudi kukaa chini na kuuza samaki.”

Wakati raia 750 wa Uganda wamekwenda Makkah mwaka huu, idadi hii imepungua sana tofauti na miaka iliyopita.

Kwa mujibu wa Sheikh Ali Juma Shiwuyo wa idara ya Hijja na Umrah ya Baraza Kuu la Waislamu wa Uganda, katika miaka ya 1960 na 1970, maelfu ya Waganda walikuwa wakienda hijja kila mwaka.

"Marehemu Rais Idi Amin Dada alikuwa akiunga mkono; alikuwa akituma watu kati ya 6,000 na 10,000 kwenda kufanya ibada ya hijja kila mwaka,” anasema.

Awali Saudi Arabia iliweka nafasi 1,200 kwa mahujaji wa Uganda, lakini Shiwuyo anasema kuwa idadi hii haijaongezwa kuendana na ongezeko la idadi ya raia wa nchi hiyo.

Uganda ilipanga kutuma raia wake 750 – wakiwemo wanwake 415 – kwenye ibada ya hijja ya mwaka huu mjini Makkah.

"Mwaka 2014, tulikuwa na mahujaji 957 tu [kutoka Uganda] kutokana na kupanda kwa thamani ya dola,” anasema. “Mwaka jana mahujaji walikuwa wakilipa dola 2,178; sasa gharama imekuwa dola 4,150."

Ukosefu wa shirika la ndege la taifa nchini Uganda imekuwa changamoto nyingine.
"Wakati wa Amin, tulikuwa na shirika la ndege la taifa, na alihakikisha kuna ndege kwa ajili ya mahujaji,” anasema Shiwuyo.

"Lakini kwa sasa tunalazimika kuongea na mashirika ya ndege ya kigeni, na hili linafanya gharama kuwa kubwa,” anasema.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!