Monday, 2 November 2015


Katika pitapita zangu uko mitandaoni, nikakutana na makala moja iliyokuwa ikizungumzia nchi ya Urusi nchi ambayo muda mwingi ni wakati wa baridi, kipindi cha baridi ni miezi tisa na miezi ya joto ni miezi mitatu tu katika mwaka mzima.

Ni nchi ambayo ilikuwa ikifuata siasa za kikomunist ambazo ni siasa za matabaka kati ya watawala na watawaliwa. Siasa za kudhibitiana kwamba usifikiri wala usifanye kama utakavyo, bali ufikiri na kufanya kama ambavyo serikali inavyotaka; ili kutimiza lengo lake la kuwadhibiti raia wa Urusi na kufanya yale waliokuwa wamekusudia serikali ikitumia kitengo chake cha usalama wa taifa wa nchi hiyo (KGB) iliweza kuweka mikakati ya kuwadhibiti wananchi kwa kuwafanya wawe walevi muda wote, na washindwe kufuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yanaendelea katika nchi yao.

Serikali ilijenga viwanda vingi vya kutengeneza pombe kali ya vodka na kujenga vibanda kila mita mia moja vya kununulia vodka hizo kwa kutumbukiza senti tano na kupata glasi moja ya vodka! Kulingana hulka hii kila mtu akawa mlevi na mwisho Urusi ikabakia kuwa taifa la walevi na huku wakomunist wakiendelea kulifisadi taifa hilo.

Wakati nikitafakari hali ya Urusi kipindi cha ukomunist, nikaifananisha hali ile na hali ya Waislam wa zama hizi tulizonazo hivi sasa. Tofauti ni kuwa Waislam siyo walevi wa vodka kama vile wenzetu wa kule Urusi. Lakini pamoja na kwamba sisi siyo walevi wa vodka ila sisi tumeingia katika ulevi mwingine wa kushabikia Umadhehebu! Ushabiki wa kimadhehebu umekuwa kama ugonjwa wa kuambukiza ambao umesambaa kwa kila Muislam haijalishi anaishi mjini au kijijini; ushabiki wa kimadhehebu umekuwa ugonjwa ambao umesambaa mpaka kwenye damu zetu.

Afadhali basi ushabiki wa Kimadhehebu tungelikuwa tunashabikia maendeleo ya Uislam na Waislam husika ili kukuza elimu zenye kuweza kuwakwamua Waislam Kielimu, kiuchumi na kimawazo na kujitambua, lah hasha, ushabiki umejikita kwenye Maswala ya hitima, maulidi kujuwa kama Qur'an ni kiumbe au si kiumbe, Qunuti au tusiqunuti, haya ni mambo yenye ikhtilafu baina ya wanazuoni wetu. Baadhi ya wanazuoni wanasema haifai kusoma hitima na maulidi, lakini pia wapo wanazuoni wanaotetea mambo hayo. Wapo wanaosema kuwa Qur'an ni kiumbe kwa hoja zao na wapo wanaopinga kwa hoja zao. Na wote wanatoa hoja na dalili nzito nzito kutoka katika Qur’an na Sunna ya Mtume (s.a.w.).

Waislamu yahitaji kuzinduka. Tuziache ikhtilafu zetu ndogo ndogo kuwa ndiyo sababu ya kutugawa na kudhoofisha umoja wetu. Kama kulikuwa na wakati ambao Waislamu walihitaji umoja na mshikamano basi huu ndio wakati wenyewe.

Haikutosha utengano wa kimadhehebu, Waislam sisi tukaamua kujiunga kwenye vyama vya kisiasa, tukawa waumini wazuri kwenye itikadi za kisiasa kiasi ya kwamba Waislam tukajikuta hata kusalimiana na kuzikana inakuwa shida.

Siasa zimekuwa ndio kama dini, watu hawali, hawanywi bila siasa, kila mahala siasa ndio mazungumzo. Imefika mahala watu wanakufurishana sababu ya siasa. Hakika hatujitambui wala hatujui tena nini wajibu wetu kwenye hii dunia. 

Uislamu ni dini iliyojengea katika misingi ya umoja. Ndiyo maana tukaona hata ibada zake zimelenga zaidi katika kuleta umoja baina ya Waislamu. Kwa mfano, mtu anaweza kusali sala ya faradhi peke yake; lakini sala ya jamaa Msikitini ina daraja 27 juu ya sala ya mtu peke yake. Kuna saumu nyingi za sunna, lakini saumu yenye fadhila kubwa ni ile ya faradhi ya funga ya Ramadhani, ambayo Waislamu wote duniani huifanya pamoja. Tukija katika ibada ya Hijja tutaona kuwa kuna Umra, ambayo ni Hijja ndogo mtu anaweza kuitekeleza peke yake, wakati wo wote; lakini Hijja yenyewe ambayo ndiyo yenye malipo makubwa mbele ya Allah (s.w.) lazima itekelezwe na watu wote, kwa pamoja na kwamuda maalum. Tutaona lengo kubwa la ibada kufanywa hivyo ni kwa ajili ya kuwafanya Waislamu wawe na umoja.

Qur’an na Sunna zimesisitiza sana juu ya umoja na kutahadharisha juu ya utengano. Wahenga walisema: "Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu".

Lakini inaonekana sisi Waislamu hatuna habari na hayo kabisa. Tuko tayari tutengane na tuwe dhaifu kwa ajili tu ya kuendekeza ikhtilafu zetu.

Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.
Qur'an An-Nisaa 4: 59

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!