Sunday 1 November 2015


Assalamu Alaiykum wa rRahmatullah wa Barakatuh

Asubuhi ya leo, baada ya swala ya Alfajir nilishtushwa na mlio wa simu kutoka kwa moja ya ma-group ya WhatsApp katika group nyingi ninazo shiriki.

Baada ya kupitia jumbe moja baada ya moja, likanijia wazo ambalo nilikuwa nalo kabla, jumbe hizi za asubuhi zimekuwa kama kichocheo kwenye akili yangu na kunifanya nikumbuke kile ambacho nilikuwa nikikifirika kwa muda kidogo.

Binafsi nikiwa kama mwanaharakati katika kufikisha daawah, haswa kwa wale ambao wamekumbatia iymaan zingine na hata wale ambao iymaan ya kuwepo Muumba kwao wameipa mgongo, tumekuwa tukijitahidi sana kuwaita wasio Waislam, warejee kwenye dini ya kweli, dini ya kimaumbile ya mwanadamu.

Alhamdulillah, wengi wetu tumeshuhudia kama si misikitini basi kwenye mihadhara mbalimbali, ndugu zetu katika Adam, wakirejea kwenye haki. Na mara nyingi tukisikia mwangi wa Takbiiir, kisha tukaitikia Allahu Akbar, kwa furaha na bashasha kubwa sana, kwa kumkaribisha au kuwakaribisha ndugu zetu katika haki.

Tumeshuhudia na hata kuwapa mikono na tukiwakumbatia kwa furaha na bashasha kubwa. Kwa kweli ni jambo lenye faraja kubwa sana kushuhudia yale ambayo umeyafanyia kazi kwa njia moja ama nyingine na kisha MwenyeziMungu akatia hidaya na kuwalainisha nyoyo wale ambao aidha ulijadiliana nao kwa amani na upendo au walijadiliaa na ndugu zetu kisha wakachukuwa maamuzi ya busara, kurejea katika haki. Kwa kweli ni furaha kubwa sana.

Swali la kujiuliza kwa kila Muislam, je furaha na bashasha hizo zote, uwa tunaziendeleza au tunaishia kuwakumbatia na kupiga nao picha kisha tukazituma kwa Facebook au WhatsApp au kwa Instagram tu, ili kupata "Like" kisha baada ya hapo, ndio Maasalaam. Hatuwajali tena.

Kuna makala nimewai kuisoma mahala kuwa karibia asilimia 60% - 75% ya Wanao silimu basi urejea kwenye iymaan zao za awali. Yawezekana kuwa mwandishi amezidisha au kuweka chumvi kwenye makala yake. Kuna makala nyingine wanasema ni asilimia 25% tu ndio urejea au wanakuwa ni Waislam jina. Jambo la kulizingatia hapo kuwa ni kweli wapo ambao wanasilimu na baada ya muda aidha wanarejea kuwa si Waislam tena au wanakuwa ni Waislam jina tu, kama vile baadhi yetu ambao tumezaliwa Waislam lakini uwa tunasubiri mpaka Mwezi wa Ramadhani ndio tunakuwa Waislam kwa mavazi, kwa funga na sala hazitupiti, Baada ya hapo kanzu na kofia na Uislam wetu tunaufungia kabatini, mpaka mwakani.

Tukatae au tukubali, kuwe na idadi kubwa au idadi iwe ndogo ya wanao ritadi, sisi Waislam tunawajibika kwa namna moja au nyingine. Nasema hivyo kwa uzoefu nilio nao. Naweza kuuliza swali moja dogo, ni wangapi katika sisi ambao tumeweza kwa makusudi kabisa kuambatana nao au kuwa karibu na ndugu zetu wanaorejea katika haki (kusilimu)?

Ni wangapi katika sisi ambao tumeweza kuwakaribisha ndugu zetu awa majumbani mwetu au kufanya nao urafiki, ili wapate kujifunza kwetu dini ya Kiislam.
Ni wangapi ambao tumejitolea kwa hali zetu na ujuzi wetu na uzoefu wetu, kuwafundisha Uislam ndugu zetu hao? Je baada ya wao kuslimu na kuambulia kukumbatiwa na kupewa mikono na kupigwa picha za kwenye facebook na WhatsApp ndio basi tena, hatuwatafuti na kujuwa wanaendelea vipi katika swala zima la wao kujifunza ili wawe mfano mzuri katika dini na jamii kwa ujumla, Je ndio Mtume (saw) alivyo fanya!?

Naomba nieleweke, sina maana kuwa tuwatafute na kuwapa mapesa, lakini yatupasa kuelewa kuwa ndugu zetu awa, wameacha mengi uko watokako, wakakumbatia Uislam aidha baada ya sisi kujadiliana nao kisha wakatosheka au wao wenyewe tu kwa jitihada zao wakaamua kusilimu.

Kuna mambo mengi tu ambayo upelekea baadhi ya watu kuamua kurejea katika iymaan zao za zamani, aidha kwa kukosa ushirikiano walioutegemea, au kwa kuona kuwa maneno tuyasemayo majukwaani ni tofauti na matendo yetu, au kwa kukosa tu watu wa kuwa karibu nao ili kujifunza zaidi na kuujuwa Uislam vile utakiwavyo.

Wengi wetu tukisha ona tu, mtu kasilimu basi jambo la kwanza haraka haraka, tunataka wabadili majina, kama ni mwanamume atavutwa kando na kuuliza kama ameshakatwa ile nanii yake, hapo hapo tunataka waanze kufunga sunnah siku za Jumatatu na Alhamisi au kumwambia iki na kile na kama ni Mwanamke, tutataka kujuwa kama kaolewa ili tuwape nusra, kiasi wengine tunawachanganya. Sikatai kuwa Muislam anapaswa kuwa vile inavyotakiwa awe, lakini tunapaswa tuwe na subra, tuwaelekeze kwa utaratibu na tuwe karibu nao sana, ili wajifunze kwa utaratibu maalum (kama Upo).

Tuwakaribishe tuwe nao karibu, kwa sababu kwa kuwa nao karibu ndio kutafungua mioyo yao nao watafunguka zaidi, na hata kama ndani ya nafsi zao kuna shaka katika kuyaendea baadhi ya mambo, watatufahamisha nasi tunaweza kuwatafutia ufumbuzi wa maswali yao yanayowasumbua. Kwa sababu binadamu ameumbwa akipata msongo wa mawazo na akakosa majibu mwafaka kwa kwa yale yanayomsumbua anaweza kutafuta ufumbuzi wowote anao ona kuwa unafaa kwa wakti ule. Wakati mwingine anaweza kufanya maamuzi mazuri ya busara au akaamua kuchukuwa maamuzi ambayo si mazuri. Matokeo yake aidha akawa si Muislam wa vitendo akabakia kuwa Muislam jina tu au akaamua kurejea aliko toka.

Haya pia yaweza kutumika kwa kina siye ambao ni Waislam Wallahi wa mwezi wa Ramadhani tu. Waislam tukirejesha upendo miongoni mwetu, tukawa kitu kimoja, basi tutaona mabadiriko mengi sana katika jamii zetu. Lakini tukiwa kila mtu anajikumbatia mwenyewe na familia yake, basi tusitarajie nehma yoyote kutoka kwa MwenyeziMungu na tutaendelea kulaumu na kulaumu, ilihali maadui zetu ni nafsi zetu wenyewe kwa kukosa kuifanyia kazi ile ayah kwenye Qur'an isemayo:

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo.  Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka. Na uwe kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri na unao amrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio walio fanikiwa.
Qur'an Surat AL I'MRAN [3]: 103 - 104

Basi ndugu zanguni katika Iymaan, tuwe miongoni katika hao waliofanikiwa kwa sababu ahadi ya MwenyeziMungu ni ya kweli.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!