Thursday, 10 December 2015

"Uislamu ni usafi, basi jisafisheni, kwa hakika hatoingia mtu peponi ila yule msafi".

Watu wengi siku ya tarehe 9 Desemba waliwajibika katika swal zima la kuunga mkono kauli ya rais na kufanya usafi wa maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Wengi wetu tulijikuta tukiunga mkono swala ilo aidha kwa kuwa tu ni wapenzi wa siasa na wanachama wa chama tawala au ni ushabiki au kwa kuwa ni Watanzania na tunaona kuwa ni wajibu wetu na ni swala nzuri kulitekeleza kwa sababu ni jambo ambalo litaweka mazingira yanayo tuzunguka kuwa ya kuvutia zaidi.

Binafsi sioni tatizo kweye utekelezaji wa jambo ilo na usafi huu husiwe wa mwaka mara moja tu, bali huu uwe ndio utamaduni wetu daima dawamu.

Uislamu umehimiza usafi kwa kila binadamu kwa kila upande aidha usafi wa mwili (kiwiliwili), Mavazi yake (nguo) na hata majiani tunapopita ili ajilinde na uchafu unaosababisha maradhi na abakie salama katika siha njema.

Tabia ya baadhi ya watu kutupa taka njiani, au wale walioko ndani ya magari kutupa vikopo vya soda, juisi na kadhalika, ni katika mambo yasiyotakikana kwa Muislamu na asiye Muislamu.

Usafi na kujitoharisha ni jambo linalopendeza na MwenyeziMungu anapenda wanaojiweka katika hali hii ya usafi kama tunavyosoma kutoka Surat Baqara [2]: 222

"...Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha."

Binafsi naliangalia swala ili kwa muono mwingine kabisa, kweli tunaweza kuwa na mazingira masafi na yenye kuvutia sana kiasi mtu akaona raha kuyatazama maeneo yetu na mazngira yake, lakini kama nchi na wananchi ndani ya nafsi zao wakakosa usafi wa nafsi, usafi huu wa mazingira hautasaidia chochote kwenye maisha ya Mtanzania.

Hata hivyo neno "Usafi" lina maana pana kiasi, hii ni kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu umeugawa usafi katika maana mbili, kwanza usafi wa nje na pili usafi wa ndani (usafi wa moyo).

Kitu kikubwa kinachopaswa si tu kusafisha mazingira tunayoishi, bali pia tunapaswa kuzisafisha nafsi zetu kila leo, ili zipate kuwa na subra na kuwa mbali na uchafu wenye kuchafua nafsi zetu, kama vile Kumshirikisha MwenyeziMungu, Uongo, Utapeli, Wizi, Uzinifu, ulaji wa Riba na Rushwa, kukataa na kuupiga vita Ufisadi na dhurma za aina zote na yale yote yasio pendeza machoni mwa jamii na Muumba wetu.

Usafi wa nafsi ndio unatokana na itikadi safi na sahihi. Itikadi ya kuamini MwenyeziMungu mmoja asiye mfano, asiye na mwana wala baba. Matunda ya usafi huu huonekana kwa tabia njema zinazoupamba utu. Uaminifu, ukweli, kujiheshimu, kutojivuna, kutokuwaringia watu, kuwasaidia wenye shida, kuwatendea wema watu wengine, kuwafikiria watu wengine vizuri na tabia nyingine zote nzuri ni matokeo ya usafi huu wa ndani.

Usafi wa aina hii tu ndio utakaoiweka dunia katika hali ya usalama na amani. Aidha, kukosekana kwake ndiko kuliko itumbukiza dunia katika machafuko na misukosuko isiyokwisha ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, mauaji ya kinyama na dhulma kama yale tunayoyashuhudia hivi leo kwenye nchi mbalimbali duniani.

Usafi ni alama ya kweli ya imani. Kwa hivyo, Muislam hana budi kuusafisha moyo wake, kiwiliwili chake, chakula chake, kinywaji chake na kila kitu chake. Vile vile kuwaimiza watu wengine kuyafanya matendo mema.

“Hakika, Sisi ni watu tulioletwa na Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuwatoa watu kwenye ibada ya waja kuwatia kwenye ibada ya MwenyeziMungu peke yake na kutoka kwenye dhiki ya dunia kuwatia kwenye wasaa na nafasi yake, na kutoka kwenye jeuri za dini kuwatia katika uadilifu wa Uislamu.”

Kwa ufupi tunaweza kusema kuwa Usafi maana yake ni kusudio la mja katika kauli na matendo yake, yawe ya dhahiri au ya siri ni kwa ajili ya kutaka radhi za MwenyeziMungu na si kwa kumuogopa kiumbe mwenzake.

Kama vile tunavyosoma kwenye Qur'an Tukufu, surat Al-Bayyinah [98] aya ya 5:

"Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Sala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia kwenye hadith iliyopokewa na Abu Dharr(ra) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Nilionyeshwa ‘amali za Ummah wangu, nzuri na mbaya. Nikapata katika ‘amali zao nzuri ni udhia unaoondoshwa njiani. Na nikapata katika ‘amali zao mbaya kohozi linaloachwa Msikitini pasi na kuzikwa (kufukiwa). Muslim.

Nimalizie kwa kusema kuwa Muislam Safi anapaswa kuwa na Ikhlaswi yaani kumtakasia nia katika kumuabudu Allah (Subhaanahu wa Ta’ala), kukhofu shirki na kupinga machafu ndio msingi mkuu wa kuimarika Uislamu.

Yanapokosekana haya ndio huzama mizizi ya Uislamu na kutositawi matawi yake. Hii ndiyo Ikhlaswi aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakaishughulikia Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) katika kuithibitisha na kuimakinisha. Kinyume chake ni kufanya Shirki.

Hayo ndio malengo yetu ya kuufuata Uislamu, sio sisi Waislamu kuwa ni wenye kumshirikisha Mola wetu kushiriki kwenye kila maovu na machafu mengine yanayo mchukiza MwenyeziMungu, kiasi mashaka ya ulimwengu huu na kushughulika mno na kuchuma mali bila ya kubagua halali wala haramu.

Uislamu ndio njia yetu iliyo nadhifu inayokubalika na nyoyo zetu, tuwe na Ikhlaasw madhubuti ili tupate kuondokana na dhulma tunayotendewa Waislamu.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!