Wednesday 16 December 2015

KUMKARIBISHA MTUME (s.a.w) MAJUMBANI MWETU?

Kama Mtume Muhammad (s.a.w) akibisha hodi mlango wa nyumba yako kutaka kukutembelea, utapenda asione kitu gani?

Bila shaka swali hili ni muhimu sana.
Utakuwa na hali ya kubabaika na kusema, “Sitaki aone hiki na kile”.

Utakuwa na wasiwasi kuwa asione vitu fulani, na kwamba akiviona hatafurahi.

Hali na hisia kama hizi zilikuwepo wakati wa zama za Mtukufu Mtume mwenyewe. Kwa mfano, mke wa Mtume (s.a.w), bibi Aisha (r.a) au binti yake, Fatma (r.a), walikuwa wakiondosha firashi au mapazia yaliyopambwa sana kabla hajawasili, kwa sababu walikuwa na wasiwasi kwamba asingeyapenda.

Maswahaba, nao pia, walihakikisha wanaepuka kumfazaisha Mtukufu Mtume (s.a.w). Wanapohisi kuwa kitu fulani hajakipenda, walikuwa kihuzunika sana.

Ni kwa sababu hiyo kwamba kanuni ya “kutomfazaisha Mtume” inajitokeza sana katika uhusiano baina ya Mtume na Waislamu.

Kuenenda katika namna ambayo itamhuzunisha na kumfazaisha Mtume ni sawa na kufanya mambo ambayo hayataridhiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hatuna budi kuwa na adabu kana kwamba muda wote tupo na Mtume wetu na kwamba tunaishi naye katika zama alizoishi.

Hivyo tunatakiwa kuwa na fikra hii: Tutajisikiaje atakapoyaona matendo yetu Siku ya Kiyama pindi vitabu vya maisha yetu vitakapofunuliwa mbele yake na mbele ya kila mtu?

Mwenyezi Mungu tayari ni shahidi anayetushuhudia na kutuona kwa kila tunachokifanya, kwa sababu “yuko pamoja nasi popote tutakapokuwa.”

Kama ambavyo itakuwa wendawazimu kufanya kitu kibaya wakati Mwenyezi Mungu anashuhudia unachokifanya, fikiria ni kwa kiasi gani Mtume atahuzunika na kufazaika utakapofanya kitu asichokipenda wakati anapigania kuuombea shafaa Umma wake!

Hivyo basi, kuyajua mambo yatakayo mhuzunisha na yatakayomfazaisha Mtume (s.a.w) ni jambo muhimu mno.

Kwa mfano, mara kadhaa Mtume alisema kuwa: “Wale wanaofanya haya na yale si katika sisi.”

Wakati mwingine akisema mtu huyo: “Asiukaribie msikiti wetu.”

Mara nyingine rangi ya uso wake mtukufu ilikuwa ikibadilika anapoona watu wakifanya matendo hayo. Na wakati mwingine sauti yake ilikuwa ikibadilika.

Utajisikiaje utakapokuwa miongoni mwa wale aliowaelezea kuwa “si katika sisi”?
Utajisikiaje kuwa miongoni mwa wale ambao Mtume (s.a.w) alisema kuwa “wasiukaribie msikiti wetu”?

Ka’b bin Malik alikuwa miongoni mwa Maswahaba ambao Mtume (s.a.w) alikataa kuongea nao; na mbaya zaidi akawausia Maswahaba wengine wafanye hivyo hivyo. Ka’b bin Malik anatuelezea jinsi alivyokuwa na shauku ya kutazamwa na Mtukufu Mtume (s.a.w) na kuliona tabasamu lake. Qur’an Tukufu yenyewe inasimulia jinsi ardhi ilivyoonekana kuwa finyu kwao kutokana na tukio hilo.

Swahaba huyo aliyekaripiwa kwa kuambiwa mara kwa mara: “Uliufungua moyo wake na kuutazama?” alilalama akisema: “Natamani kama ningekuwa nimesilimu siku hiyo tu nisiyasikie maneno hayo kutoka kwa Mtume.”

Mara nyingine Mtume (s.a.w) hujiweka mbali, lakini hatuwezi kujua kikamilifu ni kwa kiasi gani tunapomfadhaisha huzipasua nyoyo zetu.
Katika uhusiano wetu mbalimbali, kujitenga au kutozungumza na mtu husababisha maumivu ndani ya nyoyo zetu.

Alichofanya Ka’b bin Malik kikamfadhaisha Mtume (s.a.w) ni kutoshiriki katika Vita vya Tabuk bila udhuru wowote, hata baada ya kutakiwa kushiriki. Hiki kilikuwa kipindi kigumu sana kwa Waislamu wote, kipindi chenye tabu na joto kali; katika kipindi hicho suala la mavuno lisingefanywa kuwa udhuru. Mtume wa Mwenyezi Mungu alifadhaishwa; aliumizwa na alionesha fadhaa yake kwa Ka’b na watu wengine wawili ambao hawakushiriki katika vita kwa namna ambayo ilibaki kuwa mfano kwa wengine wote.

Radiamali ya Mtume (s.a.w) alipouliza: “Uliufunua moyo wake ukautazama?” huku rangi ya uso wake ikiwa imebadilika, ilielekezwa kwa mujahid aliyekuwa ameua mtu ambaye alikuwa ametamka kalmia tawhid wakati wa vita. Mujahidi huyo alitoa hoja kwamba mtu aliyemuua alikuwa ametamka shahada kwa sababu ya kuogopa kifo. Lakini jihad haikuanzishwa ili kuua watu bure. Jihad haikuanzishwa kwa lengo la kuua watu hovyo na kwa ajili ya kutuliza hasira na chuki. Swahaba huyu alitambua jinsi Mtume alivyokuwa amefadhaishwa na kitendo chake hicho na moyo wake ukaingia katika hali ya majuto.

Angalia mfano mwingine wa unyonge uliomkumba Abu Dharr:
Siku moja Abu Dharr alimuita Bilal kuwa ni “mtoto wa mwanamke mweusi.” Tukio hili lilipomfikia Mtukufu Mtume (s.a.w) alichokizwa sana na kitendo hicho cha Abu Dharr na kusema: “hii ni tabia ya kijahiliya.” Kuambiwa kuwa ana “tabia ya kijahiliya” ilikuwa ni shutuma nzito sana.
Waislamu walikuwa wameshatoka katika “Zama za Ujahiliya” na walikuwa wamepata nuru ya “Uislamu.” Abu Dharr alihuzunika sana na kukiweka kichwa chake mchangani huku akisema:

“Sitakiinua kichwa change mpaka Bilal atakapokuja na kunikanyaga kichwani kwa miguu yake.”

Kizazi hiki kilikuwa kikiomba aina hii ya msamaha pindi Mtume anapofadhaika.

Mtukufu Mtume (s.a.w) alihuzunika na kufadhaika sana pindi makabila mawili ya Madina, Aws na Khazraj, yalipozozana na kutaka kupigana hata baada ya kuingia katika Uislamu. Pindi mabishano baina ya makabila hayo yalipokuwa makubwa kuzidi udugu wa Kiislamu aliokuwa akiujenga, alifadhaishwa mno.

Alipoona ngano inayouzwa haikuwa na sifa zinazolenga, alisema: “Mwenye kutuhadaa si katika sisi.”

Siku moja Mtume (s.a.w) aliona kipande cha Taurati mikononi mwa Umar, rangi ya uso wake ikabadilika.

Umar alikuwa akishughulika na maandiko yaliyopotoshwa ilihali Qur’an ya Mwenyezi Mungu ilikuwa ikiendelea kuteremshwa. Mtume alikereka kwa kitendo hicho na mara moja Maswahaba waliokuwa hapo wakabaini hilo. Abdullah ibn Zaid akamgeukia Umar na kusema:

Mwenyezi Mungu ameipiga miguu yako? Huoni kuwa uso wa Mtume wa Mwenyezi Mungu umebadilika na huoni alivyokereka?

Hapo hapo Umar akasema:
“Tumeshuhudia kuwa Allah ni Mola wetu, Uislamu ni dini yetu, Muhammad ni mtume wetu, Qur’an ni muongozo wetu na tumeridhika navyo.” Hii ilikuwa kama kujadidi imani yake.

Mtume (s.a.w) alifadhaishwa alipoona watu wakizidisha kiwango katika matendo ya ibada, wakafanya zaidi ya alivyofanya, na hivyo kuishusha hadhi ibada ya Mtume (s.a.w). Akasema:
“Angalia! Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa mimi ni mwenye kumcha zaidi Mwenyezi Mungu na kumuabudu kuliko mtu yeyote.”

Hapa tunaweza kutarajia kipi kitakachosemwa na Mtume (s.a.w). Baada ya kuelezea kwa kiasi gani hufanya ibada na kuyaelezea maisha yake, anahitimisha kwa kusema:
“Mwenye kwenda kinyume na sunnah yangu hayupo pamoja nami.”

Hivyo, mtu anayetumia siku nzima – usiku na mchana- akifanya ibada tu anaweza asiwe “pamoja naye”. Kuwa “pamoja naye” huwezekana tu kwa kuishi kwa mujibu wa “sunnah yake”; kwa maneno mengine, kuishi kama alivyoishi.

Wakati wa Hudaybiya, Maswahaba walipoonesha ubaridi kuhusu vipengele vya mkataba wa amani na Abu Jandel aliporejeshwa kwa washirikina akiwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, Mtume (s.a.w) alikereka mno.

Katika vita vya Hunayn, uvumi ulipoenea kwamba “Muhammad amekufa”, Waislamu wakataharuki na kuanza kusambaratika, Mtume aliachwa akiwa peke yake katikati ya panga za maadui…

Yatupasa kukumbuka alipokuwa akiita:
“Enyi Ansar! Enyi Muhajriina! Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Njooni; mimi ni mja na mjumbe wa Mwenyezi Mungu!”

Swali lifuatalo ni muhimu sana:
“Kuna tofauti gani kati ya utambuzi wa kuepuka matendo yanayomfadhaisha Mtume kwa wale waliokuwa wakiishi katika zama za furaha na utambuzi wa wale wasioishi katika zama hizo?”

Mara kwa mara alikuwa akienda katika nyumba za Waislamu kama mgeni na daima nyumba zao zilikuwa tayari kumpokea Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu.
Sasa Tuziangalie zilivyo:

  • Nyumba zetu…
  • Nyoyo zetu…
  • Barabara zetu…


Bila shaka angetuona leo angesema haya:
“Kipi kimewakuta mkatawanyika? Nyoyo zenu zimegawanyika… Ulimwengu wenu umejawa giza… Idadi yenu ni kubwa lakini nyoyo zenu zina woga na wasiwasi. Mnasoma Qur’an lakini haipiti katika makoo yenu. Ni ibada zipi mnazofanya zinazostahiki kupokelewa?

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!