Monday, 18 January 2016

VISA NA MIKASA MITAANI

Nakumbuka zamani, uku mitaani kwetu ambako mnapaita uswahilini au kwa lugha ya kisikuhizi Uswazi, kulikuwa na tabia moja linapokuja swala la harusi au hata unyago.

Wengi walipendelea kuita vikundi vya ngoma na haswa ngoma ya Mdungiko... Ngoma hii ilikuwa ikipigwa na kina baba na wachezaji wengi walikuwa ni kina mama na watoto wadogo.

Siku hizi ngoma hii haipo tena labda kupatikanaji wake ni wa nadra sana. Sasa hivi kuna vikundi vingine kama vile Baikoko navinginevyo.

Ndio utakuta wengine nahisi ndio wamekuwa wapiga debe wa madala dala vituoni na wengine nahisi kama wamejiliwa kuwa mgambo wa manispaa.

Wapigaji wa ile ngoma ya mdundiko enzi zile walikuwa kama mateja kwa kuzoea kwao kupigapiga zile ngoma, kiasi ambacho nahisi wakikosa kupiga basi hamu yao umalizikia kwa watu wengine na haswa wake zao.

Kuna wanaume ambao mpaka leo wanadhani, kwa akili zao fupi kuwa kupiga wake zao ndio kuonyesha kuwa wao ndio wanaume wa ukweli. Juzi kati hapa kwetu jamaa mmoja mwenye akili fupi kama hizo, ambaye daima haoni tabu kumshushia mkewe kipondo kama vile anapiga ngoma ya mdundiko au Mganda, yalimkuta makubwa maana siku hizi anatembea huku anachechemea.

Watu wote tulikuwa vyumbani mwetu. Kama mnavyojua hizi nyumba za kupanga zisizo na dari unasikia kila mtu anafanya nini, kila chumba kimefungua redio au TV ya stesheni tofauti, wengine unasikia wakikoroma wengine wakicheka ndio mambo yetu tena, ghafla tukaanza kusikia vikombe na sahani zikivunjwa, kelele za mabishano makali yakaanza, tukajua jamaa yetu kishalianzisha kwa mkewe kama kawaida. Kisa haswa kilikuwa jamaa katafuta chupi yake haioni.

Taabu ikaanza jamaa kama kawa akaanza kumshushia kipondo mkewe puu... puu... pu, mama wa watu akaanza kulia kwa uchungu. Tukaenda kuamulia tukakuta wamejifungia ndani, ikawa tunajaribu kumsihi jamaa toka kwenye korido. Kila tulipogonga kumsihi jamaa afungue mlango, alitujibu ‘Hayawahusu tokeni’ Tukabaki kusikia tu kilichokuwa kikiendelea kule ndani.

MUME: Shenzi wewe (puu), huna akili (puu, puu, puu) chupi yangu iko wapi, umeshahonga kwa mambwana zako, (puu). Ni wazi mwanamke alikuwa anashindiliwa ngumi nzito.

MKE: Uuuuuuuuuuuuhwiii... Mume wangu unaniua bure sijui mwenyewe umeweka wapi!

MUME: Kufa(puu), kufa shenzi we (puu, pu), Wanakufa panya itakuwa wewe...!

MKE: Baba nisamehe kumbukua mimi mjamzito, muogope Mungu Mume wangu!

MUME: Kwanza mimba siyo yangu (puu), Malaya mkubwa (puu).

Ghafla kukatokea kimyaaaaaaa, mke halii wala mume haongei na ngumi zimesimama. Tukajua jamaa kauwa mkewe...! Dakika chache baadae tukasikia sauti nyembamba ya ukali...!

MUME: We Malaya ntakuua, nasema ntakuua... (kimya).

MUME: Nakwambia niache...! (kimya).

MUME: Aise ntakufanya kitu kibaya sana niachie nakwambia! (kimya).

MUME: (Kwa upole, uku sauti ikitoka kama mgonjwa wa pumu) Unajua unaniumiza mwenzio...!

MKE: (kimya).

MUME: Aise niache bwana...!

MKE: (kimya).

MUME: Nyamtondo mke wangu Please niache, naomba uniache... Unajua utaniua kizazi mke wangu... niachie nakuomba. Mama mpenzi naomba niachie... Oooh! Mmmh! iiiiih... Uuuuh!

Huku nje tukashangaa vipi leo mtemi anabembeleza? Kuna nini?

MUME: Ndugu zangu nisaidieni mke wangu ananiua ukuuu, uwiii ananiua ameshika nanihiiiuuuu... Jamani nisaidieni...EeeeH Mmmh! iiiiih... Uuuuh!

Kwa kuwa mlango ulikuwa umefungwa ilituchukua muda kuuvunja, wakati huo jamaa tumemkuta hoi kijasho kikimtoka uku machozi, yaliyochanganyika na makamasi mepesi vinamtoka kwa pamoja, mke katulia kimya, ameminya sehemu nyeti. Yaani majeshi yamekamata ikulu na nchi imesalimu amri...!

Jamaa yetu kawa mpole kuliko mdoli wa kuchezea...! Ana wiki ya pili sasa anatembea kama wale pengwini au bata mzee!

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!