Thursday, 4 February 2016

VISA NA MIKASA MITAANI:

Kila mtu anapenda watoto wachanga. Hata jitu ambalo huwa mara nyingi halicheki na mtu liko siriaz wakati wote likikutana na katoto kachanga utakuta linaanza kutabasamu, tena likibeba katoto kachanga utaona nalo linageuka kuwa litoto. Utaona linaanza kuongea na mtoto mchanga lugha za ajabu kabisa utadhani wanaelewana, utasikia, ‘Shum Babu, toto shum babu aijigijigijigi, awawawawa, abububujijiji’ na maneno mengine yasiyoeleweka eti ndio mtoto atacheka. Kama mtoto atalishika ndevu basi hapo halitoki, nalo linarudia utotoni.

Lakini leo ntaongelea zaidi upande wa wababa. Wababa wenzangu, napenda nichukue nafasi hii kuwataarifu kuwa kucheza na watoto wachanga kuna masharti yake, ndio maana leo nimeona nikumbushe hili maana kwa kuvunja masharti haya kumeshasababisha majanga makubwa .

Najua wabishi wameshakaa mkao wa kubisha, lazima saa hizi wanasema kimoyomoyo,’ Hakuna kitu kama hicho hakuna masharti wala nini’. Mi nasema sawa hebu nisikilizeni kwanza.

Ndugu zangu sharti la kwanza usicheze na mtoto ambaye ndo kwanza katoka kunyonya. Kama umevaa kanzu yako kali, kabla hujaanza kucheza na mtoto mchanga, hakikisha kuwa imeshapita zaidi ya nusu saa toka alipomaliza kunyonya. Watoto hawa wajanja sana, wakijua kuwa kanzu yako bei mbaya basi watakutaim na kutumia nafasi hiyo kukucheulia maziwa na kama hukujiangalia vizuri unaweza ukaingia kwenye mkutano wa Kimataifa kumbe mgongoni una michirizi ya maziwa ya mgando.

Sharti la pili linahusu wale ambao hupenda kucheza na watoto kwa kuwanyanyua juu ya vichwa yao, kabla hujaanza kamchezo hako, hakikisha mtoto kavaa nepi. Katoto kakijua una kamchezo hako, katajifanya kanacheka sana na kufurahi kila ukikanyanyua juu, kumbe huo mtego, iko siku ukikanyanyua juu kama hakana nepi katakutaimu na kukukuharishia kichwani, chunga sana, maana inawezekana wakati huo mdomo wako uko wazi.

Hutu tutoto twa siku hizi twa Dot com, tunaanzaga ukorofi tumboni. Kuna wataalamu wanadai eti kwa kuwa vitanda vya siku hizi vipana sana, sita kwa sita, hivyo wakati wa kutengeneza watoto, ule uhuru wa kubingilika huku na kule kuna sababisha vitoto vyenye akili za ajabu, tofauti na zamani kitanda ni cha upana wa futi mbili na nusu kwa urefu futi nne, hivyo shughuli ilikuwa na dispilini na watoto nao walizaliwa wakiwa na displin. Hayo maneno ya watafiti si yangu msiniue bure, mjumbe hauwawi.

Sharti jingine ni mavazi, hakikisha unavaa mavazi stahili wakati unaanza kucheza na kitoto kichanga. Najua mkeo akipata mtoto, mbaba unapenda kuzurura na kitoto chako toka mtaa hadi mtaa ili watu wajue we ni dume la mbegu, au ukitoka kazini unashinda nacho mkononi, kuna raha yake sana. Tena kwa kweli huo ndio muda pekee wakufaidi mtoto, mitoto mingine ikikuwa inakuwa ya ajabu mpaka unajiuliza hivi hili toto langu kweli?

Sasa kuna ndugu zangu wakiamka, hasa Jumapili huvaa kanga tu na kuanza kuzurura na kitoto begani, sasa hili si vazi mwafaka ikiwa utataka kuzurura na kichanga chako, kuna matatizo mengi yanaweza kukukuta. Bado tunahadithiana mtaani mkasa wa jamaa ambae alikuwa anakirusharusha juu kichanga chake kwa furaha mbele ya nyumba yake, mama mkwe wake akiwa jirani hapo anaota jua, sasa kuna wakati alipokirusha juu taulo alilokuwa amevaa likafunguka, mtoto yuko hewani jamaa akawa na kitendawili adake mtoto au adake taulo?

Kuna hii ishu siku hizi ya wababa kuvalia suruali na kaptura katikati ya makalio. Niseme tu wazi hili pia si vazi muafaka ikiwa uko na mtoto mchanga, kwanza ilikukwepa mkasa kama uliomtokea jamaa hapo juu, lakini pia vazi hili baya zaidi kama mtoto ulie nae ndio kwanza anajifunza kutembea.

Juzi kati nimeshuhudia kwa macho yangu rafiki yangu fulani kule Kimara Baruti akijikuta katika wakati mgumu, baada ya mtoto wake ambaye anajitahidi kujifunza kutembea, alipong’ang’ania suruali ya baba yake ajishikilie ili asimame, sasa baba mtu kavaa suruali hii staili ya nusu mlingoti si ikaachia na kushuka chini, jamaa kamkaripia mtoto na kujitahidi kupandisha suruwali lakini tayari wote tuligundua kuwa bukta ya ndani ilikuwa na matundu mawili ambayo yalionyesha kila dalili kuwa yalisababishwa na panya.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!