Wednesday 17 February 2016



Wabongo bwana hahahahahahaha Wabongo kiboko. Kwa wale ambao wamaishi ughaibuni na hawajawahi kuja Bongo kwa muda mrefu sana, nawataarifu kuwa mnapohangaika kutafuta viza za kuwaruhusu kuja Bongo, mjitayarishe kabisa kuwa  Wabongo ni binadamu wa aina nyingine kabisa hapa duniani yaani ni spishi closi bridi na wale watokao sayari za mbali sana.

Kwanza vimbe awa wa Bongoland, wana sifa kubwa mbili, kwanza wanapenda sana kudanganywa na pili asilimia kubwa ni waongo wa kutupwa, siyo kwamba walizaliwa hivyo, hapana lakini wanalelewa na kutengenezwa kuwa hivyo. Mbongo wa kawaida analelewa na kukuzwa katika malezi ya kujua na kuamini kuwa kusema au kuamini ukweli basi ujue imekula kwako.

Mbongo wa wastani huanza kufundishwa mapema na wazazi na walezi wake kuwa kusema ukweli ni hasara kubwa. Wakati Mbongo bado mtoto mdogo, katika chezacheza yake bahati mbaya akaangusha kikombe au sahani ikavunjika, mama yake lazima atapiga kelele, "Nani huyo kavunja kikombe?", kwa kuwa watoto bado malaika basi kwa mara ya kwanza lazima aliyevunja atasema , "Mimi mama". Hapo atashushiwa kipigo kilichoambatana na matusi, 'Mjinga mkubwa wewe, nyauba unusu, unanimalizia vyombo vyangu, baba'ko mwenyewe mlevi hajanunua chochote humu ndani, mbuzi kasoro mkia wee'.

Akirudia tena kosa kama hilo akisema ukweli anakula kipigo,  kwa hiyo siku nyingine akivunja kikombe, swali likija "Nani huyo kavunja kikombe?" Mtoto wa Mbongo aidha atanyamaza au atasema "Kuna panya mkubwa kapita kaangusha".

Basi panya atatukanwa lakini ndiyo hivyo tena adhabu hakuna. Somo zuri tu linakuja, akiwa bado kinda Mbongo anaelewa kuwa kusema ukweli ni hasara.

Mbongo akianza shule anagundua kuwa mila ni ileile, ukikosa ni kosa kukubali kosa maana hiyo ni njia ya uhakika ya kula viboko toka kwa waalimu, au hata kufukuzwa shule, kimsingi hapa anazidi kufuzu katika somo la kusema uongo.

Miaka inapita hatimaye anafikia wakati anahitaji kuwa na mwenza, mvulana anajua kabisa ukweli haulipi na msichana hali kadhalika. Kibongobongo huwezi ukaenda kwa msichana mrembo ukamwambia nakupenda lakini sina hela na hata kazi sina, hapo unatafuta matusi. Ni muhimu kutangaza kuwa unatoka katika familia tajiri, tena baba yako mdogo ni Igweee kule Iringa au Songea, wengi wa ndugu zako wanaishi kwa Obama we uko Bongo kuangalia mali zao na huwa unaenda kwa Obama mara nne kwa mwaka.

Garantii utapata mpenzi hapo. Na binti naye hawezi kufanya kosa na kukwambia ukweli kuwa ana watoto watatu wa baba mbalimbali, ila atakwambia yuko chuo. Uzuri wake Wabongo malezi yanamfanya Mbongo awe anapenda kudanganywa. Toka akiwa mdogo, akililia kitu mama yake anamwambia, "Tema tumpige", kweli anatemea mama'ake anapiga hewa basi kitoto cha Kibongo kinanyamaza kimeridhika.

Rafiki yako Mbongo akijenga bondeni, usikosee ukamwambia ukweli kuwa iko siku maji yatakuja kumzingira, ujue urafiki utaisha, we mdanganye mwambie "Maji yanaogopa binadamu" hapo atakusifu kuwa wewe ni rafiki wa ukweli na una akili kwelikweli kama mchwa.

Sasa ngoma iko wakati Wabongo wanapotaka kutafuta viongozi wao,  hapo ndipo utamsikia mtu anayetembelea gari la shilingi milioni 100 anajisifu kuwa anaishi maisha ya Mbongo wa kawaida, pamoja na kuwa wote wanajua kuwa jamaa muongo, huyo ndiye watambeba na kumshangilia.

Ole wake aseme ukweli kuwa yeye na familia yake wanaishi maisha ya kifahari, wala hazijui shida za wananchi zaidi ya kusoma kwenye magazeti, atatukanwa huyo mpaka ajisahau kuwa yeye ndio mwomba kula kama si kura.

Ukitaka uongozi hapa we anza na  uongo kuwa umekuwa unakosa usingizi kila ukifikiria maendeleo duni ya wananchi, hivyo umeamua kujitolea maisha yako kuwatetea ili kuwaletea maendeleo. Usije ukamalizia na ukweli kuwa unazimezea mate milioni mia mbili ukimaliza ubunge.

Itakuwa imekula kwako na ubunge utausikia redioni...!

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!