Sunday 14 February 2016

VISA NA MIKASA MITAANI

Luninga aka TV aka a.k.a KIOO a.k.a KIDEO, kidanganyawatu ni kitu moja hatari sana. Siku hizi TV ndio kimekuwa shule ya kila kitu. Kuvaa, kuongea, kuimba, kucheza, na siku hizi mpaka kulea.

Wasanii wanatengeneza video za singo zao kwa kukopi na kupest zile walizoona kwenye Luninga, hata muvi zinatengenezwa baada ya wajanja wetu kuangalia muvi kwenye Luninga, kisha kukopi na kupesti za kwao. Ila kali sasa ni wale jamaa zangu wanakopi na kupesti namna ya kulea watoto wao kwa kujifunza kwenye luninga.

Juzijuzi nilimtembelea rafiki yangu ambaye anajitahidi kuishi kama wale anaowaona kwenye Luninga, sasa yeye ana kavulana kake kako nasari, nako anakalea kama vile vitoto vya kwenye Luninga, mwenyewe anakaita Gunia sijui junia ndio hivyo hivyo, na kwa vile kule nasari kamejifunza kutamka Dadi and Mami badala ya baba na mama, jamaa yangu anajiona mjaaaanja, basi Kabwamdogo hako hakakaripiwi wala kukatazwa chochote.

Nilipata taarifa kuna siku kalimvua baba yake taulo alipokuwa katoka bafuni tena mbele za watu, jamaa akaishia kusema tu, "No Junia no...! is bad!” Na kucheka cheka huku akisifu, "Tatizo la huyu mtoto ni ana akili za kikubwa” Ene wei siku hiyo jamaa akanikaribisha kwake, basi kwa kweli ilikuwa kero, mara Junia kaleta mpira anaupiga mbele yetu anaangusha vitu, anatupiga usoni na mpira anaangaliwa tu, "Junia no!", anapanda meza mara kabati, jamaa yangu na mke wake utadhani wamelogwa, wanakenua tu meno, "No Junia no" Mara mbili hivi kakaniparamia na kutaka kunivua miwani yangu, 'Kwa ustaarabu wa nyumba ile na mie nikatoa ya kinafiki, 'No Junia no'. 

Bahati nzuri mama Junia akaingia jikoni, Baba Junia akaenda chumbani kidogo, sebuleni tukabaki mimi na hiki kidude kisichokuwa na chembe ya adabu. Si kikaanza vimaswali vya maudhi...! "Leo umekuja kula kwetu?" "Kwenu mna TV? Babako anakuleteaga chokoleti?" Kikawa mara kivunje kikombe mara glasi, mama yake anapiga kelele toka jikoni, "Junia yu a veri bed". Sasa chenyewe si kikakosea kikanipanda kichwani na kuanza kunivuta nywele nikaona sasa hii zereu.

Basi nilikishika mkono nikakitolea macho na kukifinya vizuri mgogongoni. Kwanza kilitoa macho kama kinataka kufa, kikaniangalia hakiamini akili yake kuwa kimefinywa na binadamu aliye hai, na mie nikakiambia kwa sauti ya chinichin... "We Junya ukinisogelea tena nakukata masikio kabisa".

Eeh bwana we kilitimka mle sebuleni mkojo unakitirirka kikaelekea jikoni. Kufika huko nilitegemea kianze kulia kwa nguvu, kikawa kimya. Mama yake anakiuliza "Junia umefanya nini tena baba?" kimya "Junia what has happened?" kimya, mama yake akaja huku chenyewe kimejificha nyuma ya gauni la mamake, "Huyu kafanya nini?" Nikajibu kwa sauti ya mtu asiye na dhambi kabisa... "Wala sijui nimeona tu katimka hapa kaja huko".

Baada ya hapo kukawa na displin mle ndani tukala na kuzungumza bila fujo. Baba Junia kila mara akimwangalia mwanae na kumuuliza, "Junia a yu sik? Unaumwa?" Junia akinitupia jicho mwenyewe alikuwa ananyamaza anajua kuna kukatwa masikio. 

Wengine hatuangaliagi Luninga ohooo!

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!