Sunday, 17 April 2016

Ukipita pita mitandaoni na kupitia magazeti ya kila siku, si ajabu kukuta habari za kiongozi fulani au mfanyakazi wa idara kasimamishwa kazi au kafukuzwa kazi.

Hii ikanikumbusha enzi hizo wakati bado ningali mtoto, kila mtaa ulikuwa na kiwanja cha kuchezea, tena kikubwa maana unaweza ukakuta michezo mitatu ya soka na michezo miwili ya netiboli inaendelea kwa wakati mmoja.

Achana na wale waliokuwa wakicheza mdako, kombolela, gololi na hata kufukuzana tu. Kwenye soka enzi zile, tulikuwa na sheria zetu za kuongoza mchezo huo.

Sheria zetu hazikuwa zinafwata za FIFA, kwanza wakati huo hata hilo neno FIFA tulikuwa hatulijui. 

Wenyewe tulijitengenezea amri ambazo hazikuandikwa popote lakini kila mtu alikuwa anazijua kimoyomoyo.

Kwanza wakati huo mipira yenyewe ilikuwa tabu kupatikana hivyo wengi tulikuwa tunatengeneza wenyewe kwa kufunga manailoni na makaratasi na kuanza mechi ambazo kupumzika ni uamuzi tu, inawezekana mtu kishafungwa 20 kwa kumi na mbili, basi mnaamua kupumzika.

Lakini ilikuwa ikitokea mwenzenu mmoja wazazi wake wako vizuri wakamnunulia mpira wa kweli, hapo basi kidogo kulikuwa na taratibu mpya katika kuchezea mpira ule.

Tulijitengenezea amri kama kumi hivi. Amri ya kwanza ilikuwa mwenye mpira ndie anaeamua nani atacheza, hivyo kama uliwahi kumnyima kashata au andazi au peremende au bazooka au hata ashikirimu ya kijiti au kipakti ni wazi huchezi.

Amri ya pili ilikuwa mtoto bonge ndie golikipa, hilo lilikuwa halina ubishi. 

Tatu ni kuwa wachezaji wazuri ndio wanaochaguliwa kwanza na mwenye mpira kuwa watakuwa timu yake.

Amri ya nne ilikuwa kukiwa na penati ruksa kubadilisha kipa kama kipa wenu hamumuamini.

Amri ya tano ya mpira enzi zetu ni kuwa ukipiga mpira kwa nguvu au kwa mandochi yaani kwa vidole, kumbuka tulikuwa hatuvai viatu, basi mwenye mpira ana ruksa ya kukuonya au kukukataza usicheze. Amri hii inaendena na ile ya usicheze na viatu.

Amri ya sita ya mpira enzi zetu ni kuwa usipochagia hela ya kujaza upepo mpira utapigwa marufuku kucheza.

Amri ya saba ilikuwa hakuna marefa wala washika vibendera, na mpira unachezwa mpaka kuzunguka goli, ila mwenye mpira anaweza akageuka refa wakati wowote na atakachosema lazima kiwe.

Kati ya amri muhimu ilikuwa ni ile ya nane, si ruhusa kabisa kumkaba mwenye mpira, hiyo ni faulo. Tisa ni kuwa ukitoboa mpira unalipa. 

Mwisho ni kuwa mwenye mpira akikasirika au akiumia au akiitwa na mama yake ndio mwisho wa mechi.

Hayo yote enzi za utoto tuliweza kuyavumilia, basi na haya ya utu uzimani nayo tuyavumilie maana mwenye mpira ndio mwenye amri.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!