Thursday, 26 May 2016

WAISLAMU kwa ujumla wanaingia kutimiza nguzo ya nne ya Uislamu ya Funga katika Mwezi  Mtukufu wa Ramadhan.

Kuna faida za mwenye kufunga kiimani na kiafya, kwa sababu wapo baadhi ya watu hufikiria kufunga ni mateso au manyanyaso kwa mfungaji.

Faida za kufunga zipo nyingi, miongoni mwao ni kutekeleza mojawapo ya amri za MwenyeziMungu alizotuteremshia na faida ya utekelezaji huu ni kuingia peponi siku ya mwisho.

MwenyeziMungu anatuamrisha kupitia Qur'an kwa kusema:
Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu. Surat Baqara [2]:183

Faida ya pili ya mfungaji wa swaumu ni kujizoesha kuwa na subira, yaani katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan, mtu anajifunza jinsi ya kuwa mvumilivu na kustahamili njaa, kiu na matamanio ya kimwili.

Mtume Mohammad (SAW) anausifia mwezi huu kwa kusema, “Huo mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kusubiri na hakika subira malipo yake ni pepo.

Faida ya tatu kwa mfungaji ni kuwa muadilifu na kujifundisha usawa baina ya tajiri na maskini.

Kwa hali ya kawaida tajiri ni nadra kushinda njaa, hivyo basi pindi anapokuwa katika swaumu anajua machungu ya njaa hata anapotembelewa na maskini akiombwa msaada na mtu huyo mwenye njaa aweze kumsaidia kirahisi akiwa anafahamu namna njaa inavyouma.

Inakuwa vigumu kwa tajiri ambaye hajawahi kushinda njaa kusikia uchungu na kuwa mwepesi kumsaidia mwenye njaa kwa sababu anachukulia kama njaa ni jambo la kawaida.

Kuhusu hilo la kufunga, Hakika si jingine, MwenyeziMungu amefaradhisha kufunga ili tajiri na maskini wapate kulingana (katika shida ya njaa na kiu), basi 

akapenda viumbe vyake wawe sawa na amuonjeshe tajiri maumivu ya kushikwa na njaa ili apate kumhurumia mnyonge na apate kumsikitikia mwenye njaa.”

Faida ya nne na ambayo ni muhimu zaidi wanayoitegemea ni kusamehewa dhambi yote ya mwaka ikiwa mwenye kufunga amefuata masharti yote na kufunga kwa ajili ya MwenyeziMungu kama alivyosema Mtume Muhammad (S.A.W).

Anasema, “Enyi watu! Hakika umewaelekeeni nyinyi Mwezi wa Ramadhani kwa baraka, rehema na msamaha, mwezi ambao ni bora mbele ya MwenyeziMungu kuliko miezi yote, siku zake ni bora kuliko siku zote, masiku yake ni bora kuliko masiku mengine yote na saa yake ni bora na muhimu kuliko saa zote.”

Hivyo kutokana na maneno hayo Mtume Muhammad (S.A.W), anaonyesha kufunga kwa Muislam katika mwezi huu ni bora na heri kwake.

KWANINI SWAUMU INA THAWABU KUBWA?

Hii inatokana na kuwa muumini anapokuwa anaswali, lazima wanadamu watakuona, ukienda kuhiji Makka lazima utaonekana na ukitoa Zakah muhusika uliyempa atajua, lakini ukifunga ni MwenyeziMungu pekee ndiye anayejua kama kweli utakuwa umefunga au lah.

Qur'an inasema kwamba kwa aliyefunga hastahili kujionyesha kwa vitendo vya kuonyesha unyonge, hali ya kukasirika mithili ya mtu aliyeudhiana na watu na isitoshe awe mkarimu kwa watumishi wake hadi watu wengine wa nje.

Vilevile mwenye kufunga swaumu anakuwa katika ibada, hata kama atakuwa amelala, anapata thawabu ya ibada ikiwa hakumsema mtu.

Mwenye kuificha swaumu asijitangaze kwa wengine kuwa amefunga, basi MwenyeziMungu atawahubiri malaika hivi “Kiumbe wangu ametakiwa alindwe na adhabu yangu, basi mlindeni na malaika watakulinda.”

Faida ya tano ya Swaumu inahusu upande wa afya zetu, kwa kawaida chochote kifanyacho kazi sharti kipumzike kwa muda, hii inajumuisha hata kwa upande wa mitambo.

Kwa mfano, mitambo ambayo imeundwa kwa vyuma imara tena vyenye nguvu hufika wakati ambao hulazimika kusimamishwaa kwa marekebisho ili kuiendesha kwa ubora.

Swali hapa linakuja, kwa nini sisi ambao tumeumbwa dhaifu tusivipumzishe viungo vyetu, hasa tumbo ambalo huendelea na kazi mfululizo kwa miezi 11? Hapo utauona ulazima wa kupumzisha matumbo yetu ili kuhifadhi afya zetu.

Kuhusu hilo la kusaidia kiafya hata madaktari wakubwa duniani wamewahi kulizungumzia hilo la kufunga.

Baadhi ya madaktari wakuu ulimwenguni, wamekaririwa wakithibitisha kuwa kufunga kuna faida kwa mfungaji na hata Mtume Mohammad (S.A.W.) anathibitisha hilo pale anaposema, “Fungeni ili mpate afya nzuri.”

Kila kitu kina utakaso, kitakaso cha mwili ni kufunga (Swaumu).”

Kwa mujibu wa daktari mmoja mkubwa kutoka Marekani, Dk. Car, amewahi kusema, “Ni wajibu juu ya kila mgonjwa ajizuie kula japokuwa kwa muda wa siku moja katika kila mwaka.”

Dk. Car katika maelezo yake aliongeza, “Vijidudu viambukizavyo maradhi huendelea na kunawiri pale mwenye mwili anapoendelea kula na kuvilisha, hivyo basi vitaendelea kukua.’’

Baadhi ya madaktari Waislamu na wasio Waislamu wameafiki shauri hili.

Naye Dk. Abdul Aziz bin Ismail anadai kwamba kufunga siku moja ni kinga ya maradhi kwa mwaka.

Isitoshe kwa siku za hivi karibuni, kuna hospitali mbalimbali zinazohimiza na kusisitiza umuhimu huu, kadhalika mara nyingi tunashuhudia wagonjwa wengi ambao huzuiwa kula kwa manufaa ya afya zao.

Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Cairo, Dk. Muhammad Dhawahir, anasema: “Ugonjwa wa kuzidi maji mwilini, unene, moyo, ini, pafu na mengineyo huzuiwa kwa mtu kufunga Swaumu.”

Basi ni matumaini yangu makubwa kwa kila mwenye kujaaliwa atakuwa ni mwenye Kufunga Ramadhani ili tufaidike na kuhimarisha Iymaan zetu pamoja na Siha zetu.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!