Sunday 22 May 2016

Ni Nani Mwanaadamu? Nani Wewe Na Nani Mimi? Kwa Nini Tupo Hapa Katika Ardhi?

Haya ni maswali muhimu sana, Kumzungumzia Mwanaadamu kwa kumuhusisha na Allah (s.w.) ni eneo jingine linalohitaji kufahamika vyema ili kuifanya midahalo kati ya Waislamu na wasio Waislamu, hasa Wakristo, iwe yenye maana.

Qur’an inatufahamisha kwamba sisi Wanaadamu tumeumbwa kwa vitu vitatu.  Kwanza, tumetokana na udongo ambao unawakilisha umbile la mwili. Pili, tumetunukiwa akili na kipawa cha kufikiri (intellectual) ambacho hakina budi kutumiwa na Mwanaadamu.

Akili inaweza kuwa si toshelevu lakini vile vile si kikwazo cha imani. Na tatu, tumepuliziwa roho inayotokana na Allah:
Ambaye ametengeneza umbo la kitu, na akaanzisha umbo la mwanaadamu kwa udongo.
Q32:7

Katika aya nyingine Allah analiweka wazi zaidi hili kwa kutufahamisha:-

Na (kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika, "Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo mkavu unaotoa sauti, wenye kutokana na matope meusi yaliyovunda. Basi nitakapomkamilisha na kumpulizia roho inayotokana na Mimi, basi mumwangukie kwa kumtii.
Q15:28-29

Kwa hiyo, Muislamu hayaoni maisha ya Mwanaadamu hapa ardhini kama ni adhabu iliyotokana na wazazi wetu wawili Adamu na Hawa kula tunda la mti uliokatazwa. Bali tukio hilo kihistoria linaitakidiwa kuwa ni fundisho kwa Adamu na Hawa kabla ya kuletwa hapa duniani. Hili ni eneo jengine lenye ukinzani.

Qur’an inafundisha kwamba hata kabla kumuumba mtu wa kwanza, Allah (s.w.) alikusudia kuanzisha maisha na ustaarabu wa kiumbe huyu hapa ardhini. 

"(Wakumbushe watu khabari hii) wakati Mola wako alipowaambia Malaika:  "Mimi nitaleta khalifa katika ardhi."
Q2:30

Hii ina maana kwamba Muislamu haikubali dhana ya dhambi ya asili iliyorithiwa kutoka kwa wazazi wao kwa kuasi amri ya Mwenyezi Mungu ya kutokula tunda la mti uliokatazwa.

Allah amemuumba mtu ili aje kuwa Khalifa; mdhamini au mwakilishi wa Allah katika ardhi. Dhamana aliyobeba Mwanaadamu na jukumu lake kwa Muumba (Allah) ni kumuabudu. Ibada kwa Muislamu haikomei katika kutekeleza kaida fulani fulani (rituals).

Ibada katika Uislamu ina tafsiri pana; ni kuiendea shughuli yoyote yenye manufaa kwa mtu binafsi au jamii kwa ujumla kwa mujibu wa maelekezo ya Allah (s.w.)

Kwa maana hii, Muislamu anaitazama ardhi, mazingira na rasilimali zake kama ni neema kutoka kwa Allah kwa Mwanaadamu ambayo anapaswa kuitumia ili kufikia utimilifu wa amana (lengo) atakayowajibika kwayo mbele ya Muumba.

Hii ndiyo sababu kubwa Qur’an kusisitiza kusoma, kama inavyojitokeza katika Wahyi wa kwanza:

"Soma kwa jina la Mola wako Aliyeumba. Soma na Mola wako ni karimu sana. Ambaye amemfundisha (Binaadamu) kwa wasitu wa kalamu. Amemfundisha Mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui"
Q96:1-5

Hivyo, kwa kuwa Waislamu huko nyuma walikuwa na yakini juu ya imani yao, na juu ya maamrisho ya Qur’an kuhusu kusoma, walianzisha na kusimamia ustaarabu na taaluma za sayansi zilizopea. Walirithishana na kuziboresha hazina hizo ambazo baadaye zikaja kuwa cheche za mwamko wa Ulaya.  
Tungependa kusisitiza hapa kwamba iwapo Waislamu wa zama hizi watakuwa wakweli katika imani yao, historia ile itajirudia.

Wale wote woga hawako tayari kulipokea dai hili na kwa hiyo wanaogopa mdahalo na hilo linathibitisha utukufu wa Uislamu. Bila shaka ndilo umbile aliloumbiwa kwalo Mwanaadamu:

Basi uelekeze uso wako katika dini iliyo sawa sawa - ndilo umbile Mwenyezi Mungu alilowambia watu. Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe vya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo dini iliyo ya khaki lakini watu wengi hawajui.
Q30:30

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!