Tuesday 27 September 2016

Tabiya njema ndiyo ishara na ndiyo matunda ya imani. Imani bila tabiya njema ni ibada isiyo na maana yoyote. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kalielezeya hili katika Hadith zake mbali mbali. Aliulizwa “DINI NI NINI?” Akajibu “DINI NI TABIYA NJEMA.” Na alipoulizwa, “hizaya ni nini?” Akajibu “HIZAYA NI UTOVU WA TABIYA NJEMA”.

Siku ya hukumu, tabiya njema itakuwa na mizani nzito zaidi kuliko kitu kingine chochote kile. Wale ambao tabiya zao ni pungufu na amali ni nyepesi, watahukumiwa hivyo hivyo.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema,” Hakuna kitu kitakachowekwa mizanini siku ya Hukumu ambacho kitakuwa na uzito zaidi kuliko tabiya njema.
Abu Da’ud na Tirmidhi

Katika mafundisho ya uislamu, tabiya njema ndiyo mtima wa ibada. Bila tabiya njema, ibada haina maana yoyote na itakuwa kama mila tu isiyo na umuhimu wowote na ni mazoezi tu ya viungo vya mwili. Kuhusiyana na Swala, Mwenyezi Mungu anasema:
“Bila shaka Sala (ikisaliwa vilivyo) humzuiliya (mwenye kusali) mambo machafu na maovu.” 
Qur'an Surat Al A'Nkabut 29:45

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “mtu asiyeacha matendo maovu na ya kidhalimu baada ya kusali, sala yake inajitenga mbali na Allah.
imesimuliwa na Tabrani.

Kuhusiyana na Swiyamu (swawmu), Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: Yoyote kati yenu asitamke maneno machafu au kumwendeya Mkewe au kugombana anapofunga swaumu, na mtu anapomuudhi au kumshambuliya, basi amwambiye: “Mimi nimefunga.”
Bukhari na Muslim.

Kuhusiyana na Hija, MewnyeziMungu anasema:

"Hija ni miezi maalumu. Na anayekusudiya kufanya hija katika (miezi) hiyo,
basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika hiyo Hija. Na kheri yoyote mnayoifanya, MwenyeziMungu Huijuwa."
Qur'an Surat Baqara 2:197

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

"Yeyote anayefanya Hija na kujizuwiya na maneno machafu na matendo yaliyoharamishwa atarejeya akiwa kama siku aliyozaliwa."
Bukhari na Muslim.

TABIYA YA MUISLAMU IPAMBIKE KWA KUEPUKANA NA MAMBO YAFUWATAYO:

HISIYA POTOFU:
Muislamu siyo tu ajiepushe na mambo yaliyoharamishwa bali awe makini kuepuka hata jambo lenye shaka. Tabiya hii inaainishwa na neno la Qur’an, wara ambalo lina maana mbili; Taqwa na hadhari. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

Kilichohalalishwa kimepambanuliwa na kilichoharamishwa kimepambanuliwa na baina ya hivyo viwili ni shaka ambazo wengi hawazijuwi. Hivyo, yeyote anayeepukana na shaka anashikamana na upambanuzi na hakika ya mambo katika kuitekeleza dini na kulinda heshima yake; lakini yeyote yule anayejitumbukiza katika shaka hutumbukiya katika haramu kama mchungaji anayelisha mifugo yake katika himaya (mipaka) na kuiachiya ile lakini siyo ndani kabisa. Kwa hakika kila mfalme ana himaya (mipaka) yake na kwa hakika himaya (Mipaka) ya Allah ni makatazo Yake. Kwa hakika ndani ya mwili mnakipande cha nyama, kikitengemaa hiki, mwili mzima hutengemaa na kikikumbwa na maradhi basi mwili mzima hudhurika, na huo, kwa hakika, ni moyo.
Bukhari na Muslim

Kiwango cha juu kabisa cha Taqwa kinabainishwa katika Hadith ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mtu hatafikiya asilani daraja la muttaqin (daraja la wachaMungu) mpaka aepuke hata kile kinachoonekana kuwa si dhambi kwani anacheleya kutumbukiya katika mambo yaliyoharamishwa.”
Tirmidhi

SITARA, KUYAKINGA MACHO NA MATAMANIYO:
Muislamu lazima ajiepushe kutazama sababu za dhambi kama vile kumtazama mwanamke aliyevaa hovyo kwa sababu kumtazama huko kwaweza kuamsha matamaniyo yanayoweza kumpelekeya mtu kutenda dhambi. MwenyeziMungu anasema:

"Waambiye Waislamu wanaume wainamishe macho yao (wasitazame yaliyokatazwa), na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao; bila shaka MwenyeziMungu Anazo habari za (yote) wanayoyafanya." 
Qur'an Surat An- Nur 24:30

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
Chungeni macho yenu na lindeni heshima yenu au la MwenyeziMungu atazigubika hizaya nyuso zenu.
Tabrani.

HIKIMA YA KUCHUNGA ULIMI NA MATUSI:
Mtu aepuke maneno yasiyokuwa ya kiungwana, maongezi ya kipuuzi, ufatani na usengenyi (utesi). Imam Nawawi kasema: “mjuwe kuwa mtu hapaswi kuzungumza isipokuwa lile lenye manufaa. Wakati mtu anashindwa kuamuwa kusema au kukaa kimya, kwa mujibu wa Sunna, ni kheri anyamaze ikiwa jambo halali la kusema lina uelekeo wa kupelekeya katika haramu au shaka.”

Hadith nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinasema kuwa ulimi unaweza kuleta janga au msiba. Baadhi ya Hadith ni hizi:

Uchafu wa ndimi zao wasababisha watupwe Motoni kifudifudi. Muumini hatuhumu-tuhumu, halaani-laani na hatumii lugha chafu. 
Tirmidhi

Mtu yeyote anayesema-sema sana ana makosa mengi na wale wanaotenda makosa mengi watakuwa na dhambi nyingi na wale wenye dhambi nyingi watakuwa motoni.
Baihaiqi

KUONA HAYA
Muislamu wakati wote awe mtu mwenye haya, lakini hii isimzuwiye kusema ukweli. Haya humzuwiya mtu kuingiliya mambo ya watu na kupayukapayuka. Haya huzaa Infaq ( yaani tabiya ya kutowa zaidi kuliko kupokeya) na huleta ile hali ya mtu kutosheka (kuridhika) na kile akipatacho baada ya kufanya jitihada. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

Imani ina matawi zaidi ya sitini au sabini, zito zaidi kati ya hayo ni Kalima, hakuna mungu isipokuwa Allah na la chini kabisa ni kuondosha kitu njiyani, haya ni mojawapo ya matawi hayo.
bukhari na Muslim

Mtu mwenye haya mara zote huepuka maovu na huchunga haki za wengine.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!