Tuesday 27 September 2016

JE, UMEWAHI KUTAFAKARI THAMANI YA WAKATI?

Je, umewahi kufikiri sekunde, dakika, saa, siku, mwezi na mwaka vipitavyo?

Wakati mwengine tunapokuwa tumetulia tunahisi kama muda nao umetulia. Tahamaki baada ya saa au siku kupita mtu anatambua kuwa wakati umekwenda haraka sana.

Kila mtu hivi sasa analamika namna muda unavyokwenda mbio, kiasi hata marafiki wanafikia kusema, "Wiki ilopita tu tulikuwa pamoja, ajabu imekuwa kama jana!" "Nilikosha gari yangu wiki iliyopita, ajabu namna ilivyochafuka kwa muda mfupi tu!" Basi vipi tunatumia kitu hichi cha thamani tulichotunukiwa kinachopita kwa kasi?

WAKATI UNAKWENDA MBIO:

Kama tutatafakari kidogo, tutaona kuwa muda tulioubakisha katika ulimwengu huu unamalizika harakaharaka. Binaadamu anapitia mambo mengi baina ya utoto na makuzi yake ikiwa ni pamoja na, kusomeshwa, maisha ya kujitegemea na taaluma mbalimbali za kazi, ndio kusema maisha ya kila siku ya kila mtu yanazunguka hapohapo. Mambo kama mitihani ya darasani, tafrani za kazini na majukumu ya ndani vinapokutana pamoja mtu hujikuta tayari amezongeka. Hali hiyo humsahaulisha madhumuni halisi ya maisha au kwa maneno mengine husahau hata sababu ya kuwepo kwake hapa duniani.

Katika hali isiyoepukika, kila siku utakutana na taarifa za vifo unaposoma magazeti ua kusikiliza vyombo vya habari. Watu wengi hupata mshtuko wa ghafla unaowazindua na baadae huguswa na aliyekufa. Kama marehemu alikuwa kijana, watu huona amekufa mapema na ameyakosa mambo ya msingi kama kazi na ndoa. Ukweli wa jambo hili ni kwamba, kifo kinamfika mtu yeyote wakati wowote. Hakijali mtoto, kijana au mzee, kinaweza kuja katika sura ya maradhi ya moyo au ajali ya barabarani. 
Ingawa watu wanatafakari juu ya mambo haya, baada ya muda mfupi mawazo yao yanafutika na wanarudi kuendelea na shughuli zao na kupanga mipango mengine kama vile halikupita jambo lolote.

Lakini umewahi kujiuliza kuhusu mipango uliyojiwekea imekuwa kama ulivyopanga?
Basi tutambue kuwa, sisi si wapangaji. Kila mara mambo huja kinyume.

Kwa kawaida tunapanga kwa ajili ya baadaye, lakini ni lazima muda wote tufahamu kuwa mambo yetu yapo chini ya udhibiti wake Allah. Mambo yote Alikwisha yapanga, na tunaonyeshwa kila siku. MwenyeziMungu ametufanyia siri kubwa sana. Siri inayohusisha utulivu wa maisha yetu na mwisho mwema. Sababu ya kusema haya ni pale Allah anapotuonyesha ukweli huu ndani ya Qur'an kama inavyofuata:

"...Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
Surat al-Baqara [2] 216

Mawazo na kujiliwaza kwa kupoteza muda na mambo ya pumbao ni katika uovu uliopangwa na shetani. Kupoteza muda, au 'kutupa wakati, kama inavyochukuliwa na wengi ni jambo la kawaida katika jamii zisizoishi katika misingi ya dini. Kwa hali yeyote, muda wote waumini wanatakiwa kutumia muda wao waliopewa na Allah kujikurubisha kwake na kutafakari namna ya kuutumikia Uislamu, Waislamu na jamii kwa ujumla wake.

MwenyeziMungu kwenye Surat Al-A's'r [103] 1-3 anatufahamisha mambo makubwa sana yenye kupaswa kuzingatiwa kwenye maisha yetu.

Naapa kwa Zama!
Hakika binaadamu bila ya shaka yumo katika khasara,
Ila wale walio amini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri
Surat Al-A's'r [103] 1-3

MwenyeziMungu anaapa kwa zama zote zilizopita, zilizopo na zijazo kuwa kwa sababu kila jambo lina mazingatio ndani yake.

Sababu yake haswa, sisi binadamu tupo katika namna fulani ya kukhasiri, yaani tumeghilibiwa na pumbao na matamanio ya kidunia. Kiasi ya kupelekea mioyo yetu kutokuwa na amani hata kidogo, kila siku twenda mbio kifikra na kimatendo.

Kila kukicha tunafikiria ni kwa nmna gani tunaweza kumkomoa fulani, kumsema fulani, kumkejeli au hata kumtukana, kwa kuwa tu aidha yeye ni sunni, Ibaadh, Sarafi au kwa kuwa tu hakubaliani na harakati zetu tunazo ziona kuwa ndio mwafaka kabisa katika harakati za kiulimwengu.

Watu wanakesha mitandaoni, ili kusoma habari za wale ambao hawakubaliani nao, ili kuona nini ameandika, ili ajitengenezee uadui, akikosoe kile kilicho andikwa hata kama ni kweli au atukane tu, kwa kufanya hivyo anafikiria kuwa anamkomoa hasimu wake huyo kumbe ndio anazidi kujiangamiza katika kaburi la kisaikolojia, kiasi mtu huyu hukosa raha nafsini mwake, japokuwa mbele za watu hujifanya ni mwenye furaha na mafanikio tele, kumbe moyoni yu ateketea kwa chuki na hasadi zake.

Tunapoteza kweli muda kwa mambo ambayo hayana faida kwetu wala kwa jamii yetu wala Uislamu wetu, zaidi ya kutudumaza kiakili.

Lakini hata hivyo, bado MwenyeziMungu anatuhasa na kwa kutufahamisha kuwa ni wale tu walio muamini MwenyeziMungu na wakatenda mema, na wakadumu juu ya ut'iifu, na wakasemezana na kuusiana kwa kushikamana na Haki, kwa itikadi, na maneno, na vitendo. Na wakausiana wasubiri na wavumilie mashaka yanayo wapata wenye kushikamana na Dini. Basi hao ndio wenye kusalimika na hiyo khasara, wenye kufanikiwa duniani na Akhera.

Hakika wakati ni kitu muhimu chenye thamani kubwa kuliko dhahabu. Lazima mtu awe na matumizi bora ya wakati. Badala ya kuangalia tamthilia kwa masaa manne au matano, Muislamu atumie muda huo kujifunza utamaduni wa uislamu wake, ajiongezee elimu ya dini yake, asaidie watu, aweke mazingira yake safi na ajipange vizuri katika asili yake na maendeleo.

Wakati ndio jambo lililokuwa muhimu sana kwa Mtume wetu Muhammad (Rehma na Amani ziwe Juu yake). Kwa hakika alitumia kwa makini kila sekunde na dakika kwa manufaa ya Umma wa kiislamu na jamii kwa ujumla. Hii ndio sababu Mtume Muhammad (Rehma na Amani ziwe Juu yake) akikerwa sana na watu wanaochezea wakati.

Ni muhimu sana kuwa na matumizi bora ya wakati. Moja ya matatizo yanayo wakabili  watu wengi leo ni kupiga soga na kutumia muda mwingi bila kuthamini umuhimu wake maishani. Huwa tunakosea sana katika hili.

KILA KITU DUNIANI KITAFIKIA MWISHO

Watu, wanyama, maua, matunda na vyakula hata kama vimehifadhiwa kwenye baridi vyote vitaangamia. Maisha ya milele yapo peponi pekee. Huko hakuna mwisho, ujana wenye kuendelea, ni sehemu pekee ambayo watu daima watabaki vijana.

Ukiisha chuma tunda peponi, jipya linatokea muda uleule. Kinyume na hapa duniani inapotubidi tusubiri kila tunda na msimu wake. Peponi hakuna tatizo la msimu wa matunda. Unatumia muda kwa uwapendao. Utafanya unachopenda wakati unaopenda.

Utajipamba upendavyo, hakuna maradhi, uchovu wala kuhangaika. Kuna raha zisizokatika wala kwisha. Kinyume kabisa na maisha haya ya duniani. Daima tunahangaikia. Kamwe hatutosheki na kile tukitakacho, na tukikipata hatutosheki, mfano simu mpya, inatushughulisha muda mfupi, likitolewa toleo jipya sote tunataka tuipate badala ya lile toleo la mwanzo.

Kila mtu atatumia muda uleule alopangiwa na Allah. Hivyo upotezaji muda unapunguza manufaa ya muda wako wa kuishi hapa duniani na wala hutoupata tena ukisha kupita.

ALLAH NI MUUMBA WA KILA KITU:

Allah ameahidi kutulipa pepo yenye uzuri usiokwisha. Matarajio ya kuipata pepo yatazidi tutakapo ilinganisha na maisha haya ya ulimwenguni. Kwa mfano hapo ulipo unapofumba macho na kuleta taswira ya mambo mazuri mazuri na ukatamani yatokee, Allah atakufanyia mambo mazuri milele huku ukiyaona waziwazi hata akili haijapa kufikiri.

Tumekwisha ahidiwa kupata hatima njema pindi tutakapofuata maelekezo yake Allah hali tumeondoa shaka, wala hatujiweki roho juu kwa jambo lisilo na maana. Tunapaswa kutafakari neema nyingi tulizopewa bila ya kusahau dhumuni la kuwepo kwetu hapa duniani na kubadilisha mfumo wa maisha yetu uende sambamba na maelekezo ya dini.

Kila sekunde, dakika na saa inayotupitia ni hatua moja kuelekea kaburini. Muda mfupi tuliopewa hapa ulimwenguni daima ndio utakaoamua makazi yetu ya  milele huko Akhera. Hivyo, kuwa na matumizi sahihi ya wakati ndio jambo bora la kuazimia. Ndani ya Qur'an, Allah anatufahamisha kuwa maisha haya ya dunia ni maisha ya muda mfupi,

"Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka?
Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanao weka hisabu.
Atasema: Nyinyi hamkukaa huko duniani ila kidogo, laiti ingeli kuwa mnajua."
Surat al-Mu'minun [23]112-114)

Muumini wa kweli lazima ajichunge kukaa bure ili shetani asije akampambia  dunia. Kwa njia hiyo pekee ndipo mtu anaweza kusalimika. Qur'an inatufahamisha kuwa waumini hawakai bure:

"Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi..."
Surat al-Mu'minun [23] 3

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!