Monday 5 December 2016


Je Kila Dhehebu Lina Jannah na Jahanamu Yake?

Wengi wanaweza kushanga kwa anuani ya kichwa cha makala hii ndogo hapo juu, na hapa narudia tena kuuliza, hii pepo tunayosifiwa na MwenyeziMungu kuwa hakuna jicho hata moja lililowahi kuiona au hata mwenye kufikiri akaifikiria na kupatia jinsi yake ilivyo ni nani atakayeishi humo!?

Tunafahamishwa kuwa Ikiwa mtu ataingia Peponi, basi ataishi maisha ya furaha pasi na kuugua, maumivu, huzuni au kifo. Mwenyezi Mungu atakuwa radhi nae, na ataishi humo milele.

Pepo ni makazi aliyo waandalia MwenyeziMungu waja wake wema; Ndani yake kuna neema ambazo macho hayajawahi kuziona wala masikio hayajawahi kuzisikia na wala haijawahi kufikiriwa na yeyote akapatia katika fikra zake hizo.

Miongoni mwa neema hizo ni mito ya maziwa na asali. Huko watu wataishi maisha ya milele, hakuna kufariki wala hakuna kuzeeka. Watu wote watakuwa katika umri mmoja wa ujana. Neema yeyote utakayo ihitaji utaletewa.

Sifa na neema za peponi ni nyingi kiasi hatuwezi kuzihadithia na kuzimaliza hata tukiishi miaka elfu na zaidi hapa duniani.

Lakini licha ya sifa zote hizo zinazohusu pepo, na tukijiangalia sisi Waislamu napata mashaka kiasi cha kujiuliza, hivi hii pepo na sifa zake zote hizo ni Muislamu yupi haswa ambaye ameandaliwa hayo yanayopatikana kwenye hizo pepo!? 

Sababu kubwa ni kwamba wengi wetu tumekamatika kwenye ushabiki wa kimadhehebu zaidi na kuacha misingi ya Uislamu wetu na kutetea madhehebu na itikadi.

JE HAYA MADEHEBU NA HIZI ITIKADI ZETU NDIO ZITAKAZO TUPELEKA PEPONI!?

Je Waislam sisi wa zama hizi, tunajuwa zaidi ya wale waliotutangulia mbele ya haki? Kiasi leo hii yoyote yule ambaye hakubaliani na madhehebu au itikadi tunazo zikubali sisi basi huyo ni wa kutiwa motoni na peponi tunawapeleka wale tuwapendao na kuwatupa motoni tunaotofautiana nao kifikra!?

Hii yote inasababishwa na nini kama si kudumaa au kuto baleghe Kiakili na Kiroho, na ilo ndilo linako pelekea wengi wetu kukosa kuhishimiana katika majadiliano yetu na haswa tunapotumia mitandao ya kijamii.

Mwenyezi Mungu Anasema katika Qur'an: "Na wabashirie walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo mito kati yake." Qur'an, Surat BAQARA 2:25

Je hao walioamini na wakatenda mema ni kina nani na wanatoka kwenye madhehebu yepi na itikadi gani/zipi katika hizi itikadi na madhdhebu tulizonazo leo hii!?

Mwenyezi Mungu Anasema tena ndani ya Qur'an: "Na wale walioamini na wakatenda mema tutawaingiza katika Pepo zipitazo mito kati yake kwa kudumu humo milele..." Qur'an, Surat AL I'MRAN 4:57

Swali linajirudia tena... Je hao walioamini na wakatenda mema ni kina nani na wanatoka kwenye madhehebu ipi na itikadi gani/zipi katika hizi itikadi na madhdhebu tulizonazo leo hii!?

Kwa kweli Waislamu sisi wa sasa tuna tabia ambayo ni mbaya kabisa, tabia iliyo ondoa mafungamano ya Kindugu na kirafiki na umoja katika jamii kiasi tumekuwa hatusikilizani tena, tumekalia kubezana, kutukanana kukebeihana, ugomvi ndio umekuwa dini yetu na kuacha dini tuliopewa na MwenyeziMungu na kukumbatia tulioibuni wenyewe.

Ni muda sasa wa kuzibadilisha nafsi zetu na kurejea kwenye Uislamu alotuachia Mtume Muhammad (salla Allahu 'alayhi wa-sallam).

Kwa kweli kunahitaji juhudi na jitihada za makusudi kabisa, kama juhudi aliyoifanya Mtume (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) katika kubadilisha ada za kijahiliya na itikadi zao.

Mtume (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) anasema hivi: "Uislamu ulianza katika hali ya ugeni, na utarudi katika hali ya ugeni kama ulivyoanza."

Kwa hiyo, hatuwezi kuepukana na ugeni wake kwani Uislam ni mpana sana na tunatakiwa kufanya jitahada za makusudi kabisa kuambatana nao, ni wajibu wetu sisi wenyewe kuamua kwa dhati kabisa kuifanya Qur'an, ndio Mwongozo wetu na si kimaneno tu, hata tabia zetu ziendane kama tunavyo fundishwa kwenye Qur'an na Sunna.

"Na hakika wanaomcha MwenyeziMungu watakuwa katika mabustani na chem chem, Wataambiwa ingieni salama usalimini" Qur'an SURATUL HIJR15:45-46.

"Hao ndio kundi la Mwenyezi Mungu. Sikilizeni hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo linaloshinda (linalofaulu)". Qur'an SURAT AL-MUJAADALAH 58:22.

Twamuomba Allah na atuepushe na fitna za kimadhdhebu na kiitikadi na atujaalie tuwe ni miongoni mwa watu wa peponi na si pepo hizi za kimadhehebu na kiitikadi ambazo wenyewe wamesha chaguana tayari. Tuingize kwenye pepo uliyo tuandalia Waislamu, kwa maana Mwenye kuingia peponi hatoki daima dawamu. Aaminyn.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!