Monday, 5 December 2016

Mfumo wa maisha ya Muislamu umetawaliwa na sheria maalum ambapo ili mtu aishi kama Muislamu wa kweli inambidi awe na elimu.

Kuujua Uislamu ni kuwa na elimu na kila Muislamu anatakiwa aujue Uislamu wake. Kwa kweli muumini mjinga asiyejua dini anakuwa sawa na bendera inayofuata upepo

Elimu huanza tangu utotoni, ni utaratibu uliopo tangu kutangaza kwa Uislamu kwa watoto wa Kiislamu kupelekwa katika madrasa kufundishwa mambo mbalimbali ya dini ya Kiislamu.

Uislamu haubagui elimu na haswa elimu itakayomletea manufaa binadamu katika dunia na akhera yake, hivyo Uislamu haukuhimiza elimu ya aina moja tu, aidha hiwe iliyopewa jina la elimu akhera au elimu dunia.

Kama wasemavyo wahenga kuwa elimu haina mwisho binadamu hujifunza kila siku hivyo Muislamu hujifunza elimu katika utoto na utu uzima kwa kadiri na kwa kiwango atakachoweza au kutosheka nacho.

Hata hivyo kiwango ambacho Muislamu anatakiwa afikirie ni kuijua misingi ya Uislamu wake kama vile nguzo za Uislamu na imani na lengo la kuumbwa kwake.

Jambo ambalo kwa kweli hivi sasa linasikitisha ni kwamba wazazi wengi wamesahau ule wajibu wao wa kuwapa elimu ya dini watoto wao, wakidhani kuwa watoto wanaweza kujifunza kupitia google.

Na wale ambao Kwa sababu moja au nyingine wameweza kuwapeleka watoto zao Madrasa, wamekumbwa na jinamizi la kutowathamini walimu wa madrasa kiasi cha kuona kuwa madrasa ni sehemu tu ya kuwapeleka watoto ili wao wapate nafasi za kupumzika majumbani na kufanya shughuli zingine bila kubughudhiwa na kero za watoto.

Hali hii ndio imepelekea mpaka walimu wa madrasa kuonekana kuwa awana thamani yoyote kwa jamii.

Binafsi nakumbuka mpaka kufikia miaka ya 1980 kulikuwa na madrasa nyingi za kufundishia watoto, na zilikuwa zikifundisha kwelikweli na wakati mwingine nakumbuka kulikuwa na hata na mashindano mbalimbali kama vile usomaji wa tajwid, Kaswida n.k.

Siku hizi madrasa zimekuwa chache sana na baadhi ya madrasa hizo kufa kwa kukosa watoto au kwa walimu kukosa kulipwa mishahara, kwa kuwa wazazi wanaona kuwa elimu ya dini haistahiri kulipiwa.

Wanasahau kuwa hao walimu wa madrasa nao ni binadamu na wana maisha yao na familia zinazo wategemea kimaisha.

Moyo ule wa kuwasaidia kihali na mali walimu wa watoto zetu umekufa na badala yake watu wenye watoto zao wamekuwa wakithamini sana elimu ya sekula na huku walimu wa madrasa wakiwa hawana msaada wowote. Wakati umefika kwa wazazi kufufua moyo wa kuwasaidia walimu wa madrasa ili kuinua hali zao za maisha.

Masheikh na Maimau misikitini wana wajibu mkubwa wa kuwaelimisha Waislamu kwamba elimu ni faradhi kwa Waislamu hivyo ni lazima watoto wa Kiislamu wahimizwe kusoma elimu za Madrasa na elimu zingine zenye manufaa na wakati huo huo wasiwache kuwathamini walimu hao wa Madrasa, kama wanavyo wathamini walimu wa shule za kawaida ili nao wajione kuwa wana wajibu mkubwa kwa jamii kuwafundisha na kuwaelimusha watoto ambao nao watakuja kuwarithisha watoto zao siku za mbele.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!