Sunday, 2 September 2018

• Ni Demokrasia ya asilimia ishirini (20%)
• Inashangaza Lakini Ndio Ukweli Wenyewe Huo.
• Ilikuwa ni ajabu kwelikweli, maana yule aliyejigamba kupenda demokrasia, akabatilisha maoni na uamuzi wa walio wengi!
• Na ile asilimia themanini (80%) wala hawakulalamika, badala yake uwamuzi ule ulishangiliwa na wote.

Mwaka 1992, mwaka ambao utakumbukwa sana na wale wanaofuatilia siasa za vyama kisiasa, kwa sababu ndio mwaka ambao vyama vya siasa viliruhusiwa rasmi nchini Tanzania. Ni baada ya kukusanywa kwa maoni ya wanachini nchi nzima (?) na kutakiwa kuchagua aidha vyama vya siasa viruhusiwe (virejeshwe) au visiruhusiwe. Na matokeo yake yalikuwa asilimia themanini (80%) ya wananchi ndio walitaka mfumo wa chama kimoja na iliyobaki asilimia ishirini (20%) ndiyo iliyokuwa ikitaka vyama vingi.

Hivi sasa nchi yetu imo katika mfumo wa siasa za kidemokrasia, mfumo unaotoa haki kwa kila mwananchi kuamua kujiunga na kupigia kura chama akitakacho.

Ingawa mfumo huu unakubalika na wengi katika nchi mbalimbali, kwa bahati mbaya, mfumo huu pia ulijengewa hoja na vyombo vya fedha duniani pamoja na mataifa makubwa ya nchi za Magharibi kama moja ya masharti ya nchi kukubalika kupata mikopo toka kwenye vyombo hivyo na misaada kutoka nchi za Magharibi.

Ndipo hapo tukaona maamuzi ya asilimia 20 (20%) wanakubaliwa na wale wa asilimia 80 (80%) mawazo yao yakatupwa pembeni.

Ndipo hapo aliyekuwa rais wa kwanza wa Tanganyika na baadae Tanzania JK Nyerere akiunga mkono uanzishwa au kurejeshwa upya kwa vyama vya kisiasa baada ya yeye kuvipiga marufuku baada ya uhuru mwaka 1961.

Wakati wa utawala wake hakukubali kabisa uwepo wa upinzani aidha ndani ya chama au nje ya chama, ilikuwa ni kosa la uhaini na baadhi ya waliojaribu walikiona cha moto.

Wale wote waliomuona kuwa alikuwa ni dikteta, akataka kuwadhihirishia kuwa yeye ni mpenzi wa demokrasia na anapendelea sasa kuwepo kwa vyama vingi vya kisiasa, japokuwa demokrasia hiyo hakuitaka kipindi cha utawala wake.

Matokeo yake tukajikuta tunapata vyama vilivyo anzishwa na watumishi ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa au waliwahi kuwa (?) waajiriwa wa usalama wa taifa kama vile kina Mabere Marando, Augustine Mrema n.k

Wengi wetu tukadhani kuwa uamuzi ule utakwenda sambamba na uanzishwaji wa vyama ambavyo vitafaidika kwa kupata mgao kutoka serikalini kupitia chama tawala, kwa maana ya kugawa mali za chama (CCM) aidha kurejeshwa serikalini au mali zile zigawanywae kwa vyama vilivyo anzishwa.

Nasema hivyo kwa sababu chama kilichoshika hatamu kiliweza kuchukuwa mali za umma bila ya idhini wa umma, na mali walizojichukulia ni pamoja na: Majengo ya serikali kwa ajili ya kuyafanyia shughuli mbali mbali za kichama; chama pia kilichukuwa viwanja, na mashamba kwa kutumia kigezo cha kwamba serikali na chama ni kitu kimoja na chama kimeshika hatamu, hivyo chama kikichukuwa ni sawa na serikali yenyewe imechukua; chama pia kilichukuwa magari ya serikali na kuyapeleka kwenye chama au hata wakati mwingine walichukuwa pesa hazina na kununua magari mapya kwa ajili ya chama cha mapinduzi!

Chama kilichukuwa kiwanda cha uchapishaji cha KIUTA na kukifanya mali yake, kiwanda hicho ndicho kilichokuwa kinamiliki magazeti ya UHURU na MZALENDO; chama kikitumia kigezo cha kwamba ndicho kilichoshika hatamu kiliweza kujinyakulia mali nyingi za kila aina, katika sehemu mbali mbali za hapa nchini; na kulingana utaratibu tuliokuwa tumejiwekea kwamba pesa au mali ya chama haikaguliwi basi wasimamizi walikuwa wakiendeleza vitendo vya ufisadi...!

Licha ya aliyekuwa rais wa kwanza kuunga mkono uwamuzi wa kuingia kwenye siasa za vyama vingi, lakini hakukubali mali za chama kurejeshwa serikali (Hazina) ili baadae ziweze kugawanywa kwa vyama vingine vya siasa, kwa sababu hata hivyo vyama wanachama wake kwa njia moja au nyingine wamechangia chama tawala.

Mali za CCM zingerudishwa, kisha katiba ingebadilishwa kabisa. Katiba ile ya chama kimoja, katiba ambayo ilimpa madaraka makubwa sana rais, madaraka ambayo ayaendani na siasa ya vyama vingi, kwa sababu katiba hii iliyozibwa viraka ni katiba ambayo Nyerere aliiweka ili kujilinda yeye binafsi na siasa zake, katiba ambayo haikuruhusu upinzani wowote katika utawala wake!

Katiba ingebadilishwa ili iendane na siasa za vyama vingi ndipo hapo sasa wanasiasa na wana harakati wange ruhusiwa kuunda mfumo wa vyama vingi, ili vyama vyote viwe na nguvu sawa na viwe na uwezo wa kutetea haki za wananchi na maslahi ya taifa kwa ujumla.

Siku serikali tawala ikiamua kuwa hakuna ruzuku kwa vyama vya kisisasa hapo sasa tutegemee vifo vya hivi vyama vya kisiasa, maana hata hizo ruzuku zenyewe hazipo sawa, utolewa kulingana na idadi ya wawakilishi bungeni.

Jambo lingine waanzilishi takribani wote walioanzisha vyama vya siasa kipindi kile walikuwa nao ndio wale wale waliotoka kwenye serikali ileile iliyokuwa inaongozwa na chama kimoja kushika hatamu, matokeo yake nao wamejikuta wamefata mfumo ule ule wa uongozi, ukiwa mwanzilishi hakuna wa kukupinga, kila changuzi ndani ya chama ni walewale tu na akitokea mwanachama anayetaka kugombea nafasi ya uongozi wanakuwa wakali na kumuona mwanachama huyo kuwa ni msaliti au ametumwa kuja kukivuruga chama.

Ninachosema ni kuwa ikiwa kama tumekubaliana kuwa na demokrasia ya mfumo wa vyama vingi basi, demokrasia hiyo iachiwe ifanye kazi yake, aidha ndani na nje ya vyama vya kisiasa.

Misingi ya uhuru na demokrasia inakataza wananchi kunyimwa haki hiyo. Misingi hiyo inataka mamlaka zote na vyombo vyote vikiwemo vyombo vya dola, kutambua na kudumisha demokrasia, uhuru na haki hizo za wananchi. Misingi hiyo inataka mamlaka na vyombo hivyo vitambue kuwa hakuna kikundi chochote cha wananchi kilichosusiwa uongozi aidha wa chama au wa nchi, ndio maana wananchi wote wana haki ya kujiunga na chama chochote kile na hata kugombea nafasi za uongozi ndani na nje ya chama.

0 comments:

Post a comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!