Wednesday 31 October 2018

CHIMBUKO LA SHEREHE ZA HALLOWEEN
Je Wangapi Wanasheherekea Siku Hii?
Miaka hii ya karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watu kusheherekea siku hii ya Halloween (Watakatifu, Mizimu au wafu), wengi wanao sheherekea halloween hawajui kuwa hii ni moja ya sherehe za Kipagani. kwa ufupi ni kwamba watu wengi husherehekea sikukuu ya Halloween bila kujua chanzo chake.

ASILI YA HALLOWEEN
Asili ya sherehe zenyewe haswa ni tamasha la dini ya kiuchawi inayoitwa Wiccan, ambao hufuata desturi za Waseltiki wa kale (Celtic uko Ireland) na wao bado huita Halloween kwa jina lake la kale, yaani, Samhain (tamka Sawin), nao husema kwamba huo ndio usiku mtakatifu zaidi katika mwaka.

Sherehe hii ni hitimisho la kipindi cha mavuno na kuanza kwa majira ya baridi na kuanza kwa mwaka mpya wa Kiseltiki. Kipindi hicho cha baridi kilikuwa kinaitwa kipindi cha mwaka kisicho na nuru (Darker Half of the year) kulingana na kalenda ya Waseltiki, kipindi ichi ndio mwanzo wa mwaka mpya wao.

Sherehe hizi kwa sasa ufanyika kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi 1 Novemba ya kila mwaka.

Kipindi hiki cha mwisho wa mavuno, kiliaminika kwamba usiku huo kabla ya mwaka mpya mpaka au kizuhizi kinacho watenganisha walio hai na wafu huwa kinatoweka hivyo mizimu ya wafu huja duniani tena. Na wafu au Mizimu hiyo wanaweza kutembea katikati ya watu walio hai na kuwasababishia madhara na majanga mengi ikiwemo kuharibu mavuno yao.

Lakini pia waliamini kuwa mizimu hiyo au wafu hao wanapokuja duniani wanaweza huwasaidia watabiri kutabiri mambo yao katika mwaka huo wa baridi na giza.

Waliamini wanapofanya kafara (sherehe) na kuacha vyakula nje ya nyumba zao au kutoa vyakula na wanyama kwa ajili ya kafara. Mizimu yenye roho nzuri itawasaidia kukivuka kipindi cha badiri kwa salama.

Katika kuadhimisha hii siku, makuhani wao wakishirikiana na raia wengine, walitengeneza moto mkubwa (Bonfire). Moto ambao ulitumika kuchoma mazao ya nafaka na wanyama kama matambiko kwa mizimu (wafu) ya Waseltiki. Walipokuwa wakifanya hivi, walivaa mavazi rasmi ya kutambikia miuzimu yao.

Walivaa mavazi ya aina mbalimbali kama vile, Vinyago (Cenhadon) vichwa na ngozi za wanyama, wengine walivaa mavazi ya kutisha kwa lengo la kuwachanganya mizimu wadhani na wao ni mizimu wenzao hivyo wasiwadhuru kwa namna yoyote ile wanapokuwa nje usiku wa samhain. Wengine waliwapa hii vitu vitamu kama vile peremende ili kuituliza isiwadhuru.

MUUNGANIKO WA IMANI
Kwenye Karne ya 7 Papa Boniface wa Nne alianzisha sherehe ya kila mwaka ya Siku ya Watakatifu Wote ili kuwakumbuka wafia-imani. Lengo haswa la sherehe hii ilikuwa ni kuifunika sherehe hii ya halloween, na baadaye ikahusisha pia watakatifu pamoja na mashahidi wa imani na ikaondolewa toka May 13 na kuwa Nov 1.

Baadae ikaja kuwa sikukuu ya makanisa kadhaa duniani kama vile Kanisa Katoliki la Kirumi (RC ndio wahasisi), Ushirika wa Anglican, Kanisa la Methodist, Kanisa la Kilutheri, Kanisa la Mabadiriko (the reformed Church), na makanisa mengine ya Kiprotestanti. 

Vilevile Kanisa la Orthodox ya Mashariki na Makanisa ya Kikatoliki ya Mashariki na Makanisa ya Kilutheli ya Uturuki (Byzantian Lutheran), pia usherehekea siku ya Jumapili ya kwanza baada ya Pentekoste. Makanisa ya Orthodox ya Mashariki ya Wakaldayo na makanisa ya Katoliki ya Mashariki.

Kufikia karne ya 18, ukristo ulienea zaidi kwenye jamii ya Waseltiki na kufanya Waseltiki waunganishe baadhi ya mila zao na mila ngeni kwao za ukristo.

Kanisa lilikuwa linajaribu kuiua Samhain ya kipagani kwa kuwapatia shereehe au maadhimisho yenye mrengo wa kitakatifu zaidi. kwa mfano All Souls day, Siku za Roho Zote ni tamasha katika baadhi ya Makanisa ya Kikristo, ufanya sala kuwaombea roho za wafu, ambayo ufanyika mwezi Novemba kila mwaka.

Kwenye sherehe hii watu walivaa kama kuwaiga watakatifu wa Kikristo au mfano wa malaika wakawasha moto. Sikuhii ya watakatifu ilikuwa inaitwa Siku ya Watakatifu Wote (All hallows au All hallowsmas  ikiwa na maana All Saints).

Wafia utamaduni hawakutaka kuiwacha sherehe yao, japo walikuwa tayari wameshakuwa Wakristo wa Kikatoliki na Kiprostetanti. Baadae ule utamaduni wa usiku wa Samhain katika eneo la Waseltiki nao ukaanza kuitwa Usiku wa Watakatifu (All-hallow Evening au Eve) na hatimaye likaja neno Halloween.

Waseltiki walijitahidi kuukubali ukristo hapa na pale lakini walishindwa kuacha imani zao za kipagani na hivyo wakaamua kuzichanganya changanya na Ukristo kukidhi mahitaji yao. Na ndio Samhain yao ilivyogeuka kuwa Halloween. Hivyo wapagani walioletewa ukristo walilichukua neno All hallows lenye maana ya Watakatifu Wote neno ambalo lilitumika siku ya watakatifu ya wakatoliki, wakaliweka katika sikukuu yao ya kipagani na hatimaye wakapata jina lao la Halloween.

HALLOWEEN YAHAMIA NCHINI AMERIKA KARNE YA 19

Mwanzoni mwa karne ya 19 maelfu ya wahamihaji kutoka nchini mbalimbali walihamia nchini Marekani Wahamiaji hawa ambao wengi walitoka Ireland ambao walikuwa wanakimbia janga la ukame na njaa mwaka 1845 mpaka mwaka 1852, inasemekana njaa ile iliuwa watu zaidi ya milioni moja. Waairishi walipo hamia Marekani walikuja na desturi na mila zao za kusheherekea siku ya Halloween, na baada ya muda, desturi hizo zinachanganywa na zile za wahamiaji wengine kutoka Uingereza, Ujerumani, Afrika, na sehemu nyingine za ulimwengu.

Mpaka kufikia Karne ya 20 Halloween ikaja kuwa sikukuu maarufu kotekote nchini Marekani. Mpaka leo hii Wamarekani wanaadhimisha sherehe hii ya Halloween, na ni moja kat ya sikukuu kubwa kabisa.

Siku hii si kwamba ilianza kwa kishindo la hasha, ilipoingia Amerika, Halloween ilibadilika kidogo kidogo. Vionjo na manjonjo kadhaa viliongezewa, mfano ndugu na hata majirani walikutana na kusimuliana visa na ngano (hadithi za wafu) na simulizi za kutisha. 
Wengine wakiwafata watabiri kusikiliza maajaliwa yao, vilevile waliburudika kwa kuimba na kucheza. 

Waamerika nao wakaanza kuvaa mavazi ya Halloween wakipita nyumba hadi nyumba kuomba chakula na pesa kama sehemu ya kusherehekea Halloween. Kumbuka utaratibu huu ulitoka kwa waseltiki ambao walipita nyumba hadi nyumba wakiomba mazao na wanyama ili wakatoe kafara zao kipindi kile cha mwanzo.

Utaratibu huu ndio ukaja kuwa "Trick or treat" ya leo inayofanyika Halloween. Trick or treat ni kwamba watoto wanapita nyumba hadi nyumba wakikusanya peremende (pipi), biskuti wengine wanatoa pesa. Trick ni kitisho tu kuwa usipotoa watakufanyia mazingaombwe. Treat ndiyo hiyo unawapa ili wasikufanyie mazingaombwe.

MAPAMBO NA ZAWADI
PEREMENDE: Waselti wa kale walijaribu kuwatuliza roho waovu kwa kuwapa peremende. Baadaye, kanisa liliwatia watu moyo waende nyumba kwa nyumba Mkesha wa Siku ya Watakatifu Wote ili kuwaombea waliokufa na kupewa chakula kama malipo. 
Mwishowe hiyo ikaja kuwa desturi ya Halloween, watu walienda nyumba kwa nyumba wakiomba peremende na kuwatisha watu wasiowapa peremende.

MAVAZI: Waselti walivaa vinyago (Cenhadon) ili roho waovu wadhani kwamba wao ni roho na hivyo wasiwadhuru. Kanisa liliingiza desturi za kipagani katika sherehe za Siku ya Wafu na Siku ya Watakatifu Wote. Baadaye, waadhimishaji walienda nyumba kwa nyumba wakiwa wamevalia kama watakatifu, malaika, na mashetani.

MABOGA: Aina fulani ya boga linaloitwa tanipu lilichongwa na kutiwa mshumaa ili kufukuza roho waovu. Watu fulani walisema kwamba mshumaa huo uliwakilisha nafsi zilizokuwa zimezuiliwa toharani. Baadaye, watu walianza kutumia maboga ya kawaida.

SHEREHE ZA HALLOWEEN SIKU HIZI
Ingawa Halloween huonwa kuwa sikukuu tu ya kujifurahisha na haswa watoto, na kila mwaka idadi ya watu wanaoisherehekea katika nchi mbalimbali inazidi kuongezeka. Hata hivyo, watu wengi ambao wameanza kuisherehekea hivi karibuni hawajui kwamba ishara, mavazi na hata mapambo, na desturi za Halloween, ambazo nyingi zinahusianishwa na viumbe wa roho wenye nguvu zisizo za kawaida na uchawi, zilitoka kwa wapagani.

Nchi za Ulaya ya Kaskazini ikiwamo Uingereza walikuwa wakisheherekea siku hiyo ambapo wahamiaji kutoka Scotland na Ireland walioingia Marekani waliingia na utaratibu huo wa maisha.

Sherehe hii nchini Marekani ilianza kupata nguvu mwanzoni mwa karne ya18 mwanzoni wa mwaka 1900, ambako watu walikuwa wakipelekeana kadi za pongezi, karatasi zenye maua na urembo wa aina mbalimbali.

Hata hiyo mavazi ya kuvaa siku hiyo hususani majira ya jioni maarufu 'trick-or-treat' yalianza kuonekana miaka ya 1930 na mengine miaka 1950 Halloween ilianza kuingia hadi mashuleni.

Siku hii ya Halloween watoto mashuleni huruhusiwa kuvalishwa mavazi ya ajabu ajabu, wengine wakiigiza watu maarufu, wengine wakivaa kama wanyama na kadhalika, na ndio wakati huu trick or treat upamba moto.

Na kuanzia hapa sasa Halloween ikawa utamaduni mpya wa Wakazi wa Ireland (Waairishii) na Waamerika. Wamerikani ndio wanaongoza kwa kusherehekea Halloween, na ndio kipindi cha michezo ya Kuigiza na sinema za kutisha zikiambatana na maudhui ya mauwaji na kichawi.

Baadae mahitaji ya vitu kwa ajili ya siku hii yalizidi kuwa makubwa kadiri sherehe hizo zilivyokuwa zikipata uungwaji mkono na jamii mbalimbali.

Kwa sasa siku hii imeonekana kuwa ya kiuchumi (Kibiashara) zaidi kutokana na utengenezaji wa vitu mbalimbali muhimu kwa ajili ya siku hii. Halloween imekuwa biashara kubwa inayowaletea wafanyabiashara mabilioni ya pesa ulimwenguni pote.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!