Monday 16 December 2019

Kuna Uwezekano Mkubwa wa
Wafungwa Wengi Kurudi Magerezani

Hivi karibuni, kwa maana ya Tarehe 9 Desemba Mwaka 2019, katika maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Tanzania) Rais John Joseph Pombe Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 5,533 nchi nzima ikiwa pia sehemu ya kupunguza msongamano wa wafungwa Magerezani.

Idadi hiyo ni kubwa kuwahi kutokea nchini, huku ikikadiriwa kuwa idadi hiyo ni sawa na asilimia 15% ya wafungwa wote nchini Tanzania.

Rais alisema kuwa wapo baadhi watashangaa kwa uamuzi wake wa kuwaachia wafungwa wengi kiasi hicho lakini alidai kuwa 'aliguswa moyoni' kufanya hivyo.

Walionufaika na msamaha wa Rais Magufuli ni pamoja na wale waliokuwa wakitumikia kifungo kisichozidi mwaka mmoja na wale ambao wamekuwa wakitumikia vifungo vya muda mrefu lakini wamebakiza muda usiozidi mwaka mmoja kumaliza vifungo vyao.

SWALI la kujiuliza, je hao wafungwa, wametayarishwa kuja kukabiliana na hali halisi ya kimaisha uku uraiani?

Kama vile  askari wanaotoka vitani, kabla ya kuja uraiani kwanza upitia kwenye vipimo vya kisaikolojia ili kuondokana na ile hali ya Post-traumatic stress disorder, ili kuwawezesha waweze kuishi vyema na raia na kuondoa ile hali ya woga, dhiki na mashaka na miemko ya kiakili na kuwaondolea zile kumbukumbu mbaya walizopitia vitani.

Matayarisho hayo uwaweza wanajeshi, kukabiliana na maisha ya uraiani kwa amani na kuepuka kufanya uhalifu au hata kuwadhuru raia kutokana na matatizo ya kiakili walioyapata vitani.

Hata kwa wafungwa haswa wale wa muda mrefu na wale ambao uhalifu wao ulitokana na kudhuru watu wengine kama vile mauwaji na ubakaji na jinai zingine. Hao wote baada ya kutumikia kifungo kwa muda mrefu, ujikuta wanakuwa wageni na maisha ya uraiani.

Ukizingatia kwamba jela nyingi za kiafrika, zimejaa uonevu na kuoneana haswa miongoni mwa wafungwa wenyewe kwa wenyewe na kesi zingie zinaripotiwa kuwa baadhi ya wafungwa wananyanyaswa kingono, mapigano baina ya wafungwa, na vitendo vingine vya ukatili ni kawaida katika magereza mengi.

Lakini hali hii sio tu kwa wafungwa hata walinzi wao (askari Magereza) hufanya kazi katika mazingira yenye dhiki kubwa ambayo inapelekea kuongeza uwezekano wa wafungwa kuteswa bila ya sababu za msingi.

Na haswa wafungwa wa kike wako katika hatari kubwa ya kushambuliwa kingono na walinzi wa Magereza.

Wengi wao (wafungwa) hata kutembelewa na ndugu, jamaa na marafiki ni kwa nadra sana, kiufupi wafungwa wengi wanakuwa wametengwa na jamii kwa asilimia kubwa sana. Kutengwa uku kunaweza kuongeza hatari ya mfungwa kukosa afya ya akili kama vile unyogovu na wasiwasi (depression and anxiety).

Hali hii upelekea wafungwa wengi kuathirika kisaikolojia (kimwili na kiakili) na kujikuta wanabadilika kitabia. Na kupelekea wengi wao kuona kuwa wametengwa na jamii kutokana na makosa waliyo yafanya uko nyuma, na hii uwapelekea wengi wao kukosa subra na hata kuwapelekea kutumia nguvu kupata kile wanacho kitaka na hata kurudia tena kufanya jinai (makosa waliyo yafanya kabla ya kwenda jela) kwao uona ni jambo la kawaida.

Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya wafungwa waliotoka jela, ukamatwa tena ndani ya miaka mitatu, kama si miezi michache tu.

Ushauri unaotakiwa kufuatwa ni kuwatumia Wataalam wa afya ya akili (A mental health professional) kuwasaidia wale wote waliotoka jela. Mtaalam anaweza kusaidia wafungwa kurudi tena katika jamii (Uraiani) na kurejesha tena uhusiano mzuri kati ya na ndugu, jamii, marafiki pamoja na familia husika.

Bila ya kuwaandaa hao wafungwa, tusishangae kusikia wengi wao wamerejea kufanya jinai na uhalifu ule ule au zaidi ya ule na kurejeshwa tena Magerezani (Jela).

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!