Sunday 8 March 2020

SIKU YA MWANAMKE DUNIANI.

JE, Jamii na Uislamu Unasemaje Kuhusiana na Ukombozi na Kumtukuza Mwanamke!?
Siku hii ya tarehe 8, kwenye baadhi ya ma group ya tovuti baraza, haswa WhatsApp, nilituma meseji mbili, moja ilikuwa ya maneno kuhusiana na wababa, kuwapatia simu zao wake zao kama sehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani. Meseji ya pili, ilikuwa ni video ikionyesha moja ya familia akiwemo baba, mama na watoto, uku Mwanamke/mama akionekana amebeba mzigo kichwani na mtoto mgongoni hali akiwa ni mja mzito, hali ya kuwa /mwanammebaba akiwa anafata kwa nyuma uku amekamata bakora mkononi. Wengi waliochangia, waliangukia kwenye kujadili meseji ya kuwaachia simu zetu wake zetu kama njia moja wapo ya kuadhimisha siku hii.
Lakini pia walijitokeza wanaharakati wa aina mbili, kuna wale ambao wamelichukulia siku hii kama siku ambayo haifai kuadhimishwa kwa kuwa tu si katika sikukuu ya imani ya dini na haswa Uislamu. Na kuna waliochukulia tu kuwa ni swala la mzaha tu na si jambo la kutiliwa maanani.
Kitu ambacho nilikiona cha ajabu kidogo ni kwamba ni watu wawili au watatu tu kwenye group mbili tofauti, ndio kidogo waliweza kuchangia kuhusiana na ile video, ambayo ilionyesha dhairi kumkandamiza na kumtweza nguvu mwanamke. Nami nilituma meseji zile kwa makusudi kabisa, ili kuona kuna mwamko gani katika jamii zetu haswa linapokuja swala la haki za mwanamke katika jamii zetu. Kiuhalisia unaweza kuona kwamba, wengi wetu, tumekuwa watu wa kuchangia mada bila kutafakali kwa kina au tunachangia tu, kwa kuwa tunaona kuwa kilichoko hakiendani na aidha imani au mila au baadhi ya tamaduni au mazoea tu, tuliokuwa nayo. Kabla ya kuelezea kile ninacho ninachokitaka kukielezea kwanza kabisa tuangalie historia ya hii siku kwa ufupi kidogo. Siku ya Kimataifa ya Wanawake au International Women's Day (IWD) ni siku inayodhimishwa tarehe 8 Machi kila mwaka kote ulimwenguni. Ni sehemu katika harakati za haki za wanawake ulimwenguni. Historia yake ilianza muda kidogo, miaka ya mwanzoni mwa karne ya 20, yaani mwaka 1909. Baada ya wanawake wa kiharakati uko Urusi kupata vipingamizi vingi nchini mwao, ndipo mnamo 1917, Machi 8 ikawa siku ya kitaifa ya wanawake nchini Urusi. Baadae, Chama cha Kijamaa cha Amerika kilipanga Siku ya Wanawake huko jijini New York mnamo Februari 28, 1909, kulihamasisha wanaharakati wengine haswa wajumbe kutoka Ujerumani kama Bi. Clara Zetkin, Käte Duncker na wenginewe walipendekeza katika Mkutano mwingine wa mwaka 1910 wa nchi za Kijamaa wa Jamii wa Wanawake kwamba "Siku maalum ya Wanawake" iandaliwe kila mwaka. Siku hiyo ilisherehekewa sana na wanaharakati wa siasa za kijamaa na nchi za kikomunisti hadi ilipopitishwa na wanaharakati wa wanawake mnamo mwaka 1967.
Umoja wa Mataifa ulianza kusherehekea siku hiyo mnamo 1977.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake leo, kwa baadhi ya nchi ni siku ya mapumziko ya umma, katika nchi zingine ni siku ya kawaida tu kama siku zingine za juma. Katika sehemu zingine, ni siku ya maandamano, makongamano, semina na mikutano ya kumudhimisha mwanawake. Kama ilivyo kwa baadhi ya walimwengu walivyojipangia kuwa tarehe 8 mwezi wa tatu wa kila mwaka ni siku ya mwanamke, duniani. Je Uislamu Unasemaje Kuhusiana na Ukombozi na kumtukuza Mwanamke!?

JE NI SWALA LA HAKI NA USAWA WA KUFANANA AU NI SWALA LA WAJIBU?

Hoja hii imejengwa juu ya msingi kwamba kwa vile heshima ya binaadamu ni sawa kwa mwanaume na mwanamke, hivyo lazima wote wapate haki zinazofanana bila kujali majukumu yao katika maisha. Hapana shaka, utu na heshima yao ni sawa kwao wao wote; wote wanapaswa kuwa na haki sawa. Lakini vipi kuhusu kufanana kwa haki zao? Kwa muktadha huo, hakuna yeyote kati ya mwanamke na mwanaume mwenye nguvu na uwezo wa ‘kuwepo’ bila ya kumuhitajia mwenzake. Badala ya kufuata kibubusa, tunapaswa kuamua kwa makusudi kabisa kutumia akili zetu kufikiria sisi wenyewe, na kujiuliza maswali yanayokuja akilini mwetu, iwapo ni kweli haki sawa zinamaanisha haki zinazofanana? Kwa kweli hayo ni mambo mawili tofauti. Usawa ni haki ya kuwa na daraja sawa kithamani na hadhi ambapo kufanana maana yake ni kulandana. Inawezekana baba akagawa mali zake kwa watoto wake watatu kwa usawa lakini sio kwa kulingana. Jaalia mali yake inajumuisha vitu mbali mbali kama vile maduka, mashamba na badhi ya mali zilizokodishwa. Baba kwa kuzingatia vipaji vyao na mambo ambayo kila mmoja anapenda, anaamua kumpa mmoja duka, mwingine shamba na wa tatu mali zilizokodishwa. Anazingatia kuwa thamani ya mali aliyopewa kila mmoja wao ni sawa na wengine na kila mmoja amepewa kutokana na kipaji chake. Hivyo aligawa mali yake kwa usawa lakini sio kwa kulingana. Uwingi ni tofauti na ubora, na usawa ni tofauti na kufanana. Uislamu hauamini juu ya kulingana (uniformity) kwa mwanaume na mwanamke. Lakini wakati huo huo hauwapendelei wanaume katika maswala ya haki. Umezingatia kanuni ya usawa kati ya mwanamke na mwanaume lakini haukubaliani na kufanana kwa haki zao. Usawa ni neno linalifurahisha, kwa sababu linaashiria hali ya kutobagua. Lina utukufu maalum. Linaamsha na kuleta heshima, hasa linapohusiana na haki. Ni neno zuri lilioje 'Usawa na Haki.' Mtu yeyote mwema atafurahishwa na uzuri wake. Hapa hakuna ubishi wowote kuwa mwanaume na mwanamke ni sawa kama binadamu na haki zao za kifamilia zinapaswa kuwa sawa kithamani. Kwa mtazamo wa Uislamu wao wote ni binadamu na hivyo wana haki sawa. Kitu kinachopaswa kuangaliwa hapa ni kuwa mwanaume na mwanamke, kwa sababu ya tofauti zao za kijinsia, wanatofautiana katika mambo mengi. Asili yao haitaki wafanane. Nafasi hii inataka wasifanane katika haki nyingi, majukumu, wajibu na adhabu. Katika nchi za Magharibi jitihada zinafanyika sasa kuzifanya haki na majukumu yao kufanana, na kupuuza tofauti zao za asili na za ndani. Hapa ndio kuna tofauti kati ya mtazamo wa Kiislamu na mfumo wa Kimagharibi, nukta inayobishaniwa ni suala la kufanana kwa haki sio usawa wa haki kati ya mwanamke na mwanaume. Usawa wa haki ni nembo tu ambayo imewekwa kwa makosa katika zawadi hii ya Kimagharibi. Ukichungulia kwenye historia za nchi za Ulaya ya kabla ya karne ya 20 ni mfano dhahiri wa dhulma kwa mwanamke. Mpaka mwanzoni mwa karne ya 20 mwanamke wa Ulaya alinyimwa haki za kibinadamu katika maisha ya kila siku na kisheria. Hakuwa na haki sawa wala zinazofanana na mwanaume. Machafuko yaliyosababishwa na maendeleo ya kuboreka kwa viwanda katika karne ya 19 na 20, na hali mbaya ya wafanyakazi iliyofuatia, hasa kwa wafanyakazi wa kike, yalisababisha macho yaelekezwe kwenye masaibu ya mwanamke na ndio maana suala la haki zao lilizingatiwa sana.
Hali hii ndio ikapelekea kuwepo na wanaharakati wengi wa haki za binadamu na haswa haki za wanawake.
Katika fikra hizo hizo wanaharakati wasio ufahamu Uislamu, wanafikiria pia Uislamu haumpi uhuru na haki mwanamke, lakini wasichojua kuwa Uislamu umemkomboa mwanamke kutokana na udhalilishaji wa Kimagharibi ambao umemfanya mwanamke kuwa ni bidhaa itembezwayo. Katika Uislamu, familia yoyote duniani inajengeka kupitia mwanamke na mwanaume. Katika mpango alioamua kutuwekea Mola wetu Muumba.
Na ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Kutafuta elimu ni faradhi juu ya kila Muislamu mwanamme na mwanamke.
Hali hii ndio ikapelekea kuwepo na wanaharakati wengi wa haki za binadamu na haswa haki za wanawake.
Katika Uislamu, familia yoyote duniani inajengeka kupitia mwanamke na mwanaume. Katika mpango alioamua kutuwekea Mola wetu Muumba.
Ni wajibu wa Muislamu (Mwanaume na Mwanamke) kuelewa kwamba kutafuta elimu ndani ni faradhi kama ilivyo faradhi ya Swalah.
Mwanamke katika familia ana majina mengi na hakuna familia inayoweza kuwepo bila ya mwanamke. Tuangalie tulipotoka Kwa muktadha huo, jamii zilizopita kabla ya Uislamu zilimdhalilisha mwanamke kwa sababu tu ya jinsi yake. •Mwanamke alinyimwa mirathi ya mali ya wazazi wake na badala yale walirithi wanaume tu. •Mwanamke alirithiwa yeye mwenyewe kwa nguvu (baada ya kifo cha aliyekuwa mumewe), mwanamke alilazimishwa kurithiwa na mmoja wa wanafamilia wa aliyekuwa mumewe bila ya ridhaa yake. •Mwanamke aliuawa baada ya kuzaliwa tu kwa kuogopa aibu ya mtu kumpata mtoto wa kike wakati alitarajia apate mtoto wa kiume. •Mwanamke aliuzwa kama ‘bidhaa’, na kadhalika. Uislamu umemkomboa mwanamke na umemrejeshea yale yote ambayo jamii na mila potofu zilimnyang’anya mwanamke ikiwemo haki zake alizopewa na Mola wake Muumba. Lakini kuja kwa Uislamu ukamtambua mwanamke, ukamthamini na ukamuahidi malipo mema kama alivyoahidiwa mwanaume. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'an Tukufu Sura ya 4 (An-nisaai) aya ya 124: "Na anaye fanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini - basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya tundu ya kokwa ya tende." Mwenyezi Mungu akasema tena katika Sura ya 16 (An-nahli) aya ya 97: "Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda." Akasema tena Mwenyezi Mungu katika Sura ya 40 (Ghaafir) aya ya 40 (nanukuu): "Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo uwovu wake, na anaye tenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu." Aya zote hizo tatu zinaonyesha namna Uislamu ulivyomtambua na kumthamini mwanamke na kuonyesha iwapo atajibidiisha kutenda matendo yanayomridhisha Mola wake Muumba, basi afahamu kwamba malipo ya mema yake ni sawa na malipo atakayolipwa mwanaume ambaye anatenda mema mfano wake. Pili, Uislamu ukakemea vikali ile tabia ya kijinga ya kumuua mtoto wa kike pasina hatia kwa sababu tu ya jinsi yake. Mwenyezi Mungu anasema katika Sura ya 16 (An-nahli) aya 58 – 59: "Na mmoja wao akibashiriwa kwa msichana, uso wake unasawijika, naye kajaa chuki. Anajificha asionekane na watu kwa ubaya wa aliyo bashiriwa! Je,akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? Tazama uovu wa wanavyo hukumu!" Aya hii inaonyesha namna Uislamu ulivyochukizwa na kukemea kosa la kumuua mtoto wa kike kwa sababu tu ya jinsi yake. Pia Uislamu umemtukuza mwanamke kwa kumpa mirathi badala ya kurithiwa yeye mwenyewe. Katika Uislamu mwanamke ni mrithi kama ambavyo mwanaume ni mrithi. Aidha, Uislamu umemtukuza mwanamke kwa kumpa mambo maalum, makubwa na mazuri ambayo mwanaume hakupewa. Mfano wa mambo hayo ni: • Mosi, Uislamu umempa mwanamke nasabu na haki za mtoto aliyemzaa bila hata ya kuangalia na kuzingatia iwapo amemzaa kwa ndoa au bila ndoa. Mwanamke anapomzaa mtoto, mtoto huyo atakuwa wake tu na watarithiana. Lakini mwanaume akimzaa mtoto ili mtoto huyo ahusiane naye kisheria kwa mfano kumuozesha akiwa ni binti au kurithiana ikiwa mtoto wa kike au wa kiume, ni lazima amzae ndani ya ndoa.
• Pili, Uislamu umempa mwanamke cheo cha kupewa mahari kwa ajili ya kuolewa kisha baadaye mume abebeshwe majukumu yote ya ulezi wa mke. Kitendo cha mume kubebeshwa majukumu ya kumlea mke kingetosha kuwa ni kigezo cha mwanamke kutoa yeye mahari, kwani kwa kawaida ilivyo yule anayepewa huduma ndiye alitakiwa kuinunua au kuichangia huduma hiyo.
• Tatu, Uislamu umempa mwanamke utukufu wa juu. Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: "Hawatukuzi wanawake ila mtu mtukufu na hawadharau wanawake ila mtu duni" Yaani utukufu (ubora) wa mwanaume na uduni wake unapimwa kwa namna anavyowatukuza au kuwadharau wanawake.
• Nne, Uislamu umempa mwanamke haki ya kuitikiwa kwanza. Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: "Watakapokuita baba yako na mama yako, muitikie mama yako."

• Tano, Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: "Pepo iko chini ya nyayo za kinamama."
Kwa muktadha huo, Uislamu umemkomboa mwanamke na umemtukuza sana. Hivyo basi kampeni yoyote ‘chafu’ ya kumdhalilisha mwanamke ni wajibu wa jamii yote kushirikiana kuipiga vita kampeni hiyo. Wale wasanii, wanamuziki na watangazaji wa matangazo katika magari ya wazi ambao huwavisha wanawake ‘nusu uchi’ kisha wao wakavaa suti tena zenye stara, tunapaswa tuwakemee wasiwadhalilishe wanawake. Mashindano ya ulimbwende, ambayo wasichana wakipitishwa mbele za watu uku wakiwa wamevalia vichupi tu, si kumkomboani bali uko ni kumdhalilisha mwanamke. Pia hata matangazo ya biashara katika mabango, Luninga na kwenye mitandao, yazingatie maadili yasimdhalilishe mwanamke kwa kumpiga picha ya ‘nusu uchi’ eti ‘kuvutia’ biashara. Uku wakiwavika viremba vya ukoka eti wao ni super woman, waliokombolewa kifikra, kumbe ni kuwaridhisha wapenda kuangalia nyuchi za wanawake tu. Basi namalizia kwa Ayah hii: Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari. Qur'an Surat Al-Hujurat 49:13

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!