Wednesday 28 October 2015


Tatizo la uchaguzi wa nchi ya Bongo imekuwa kama mchezo wa mpira wa watoto uko mitaani, kila mtu amekuwa referee, katikati ya mchezo firimbi nyiingi kiasi watazamaji wanachanganyikiwa kama ni faulo au kona au mpira wa kurushwa au ni frii kiki.

Tatizo la mpira wa kitoto mitaani mkijifanya kumpiga sana chenga aliyeleta mpira usishangae akautia kwapani mpira wake, mara huyooo anayoyoma na mpira wake.

Wahenga walisema kuwa wakati ni ukuta, na ukiamua kupigana nao utaumia, na pengine kusababisha maumivu kwa wengine, na si ajabu hatimaye ukaleta maafa mabaya zaidi.

Nchi ya Bongoland kuna amani. Amani hii haikutengenezwa na yeyote kutokea kwenye jukwaa la siasa. Wala haitokani na mikopo ya IMF au ruzuku ya 'kutoka nchi wahisani'. Ni amani ya asili iliyojengwa na kudumishwa na mabibi na mababu wa nchi hii. Kama ulikuwepo uhasama baina ya wananchi wa makabila mbalimbali, mabibi na mababu hao walikwisha umaliza na kuwapatanisha wahusika ambao leo ni watani tu; wakutaniana katika misiba na sherehe.

Juhudi na mbinu za wakoloni za kutaka kutumia dini na makabila ili waendelee kutawala nazo zilishindikana. Wananchi waliungana kwa dini na makabila yao, wakawang'oa wakoloni.

Ninasema hayo kwasababu hivi sasa nchi yetu imo katika mfumo wa siasa za kidemokrasia, mfumo unaotoa haki kwa kila mwananchi kuamua kujiunga na kupigia kura chama akitakacho.

Ikiwa kama tumekubaliana kuwa na demokrasia ya mfumo wa vyama vingi basi, demokrasia hiyo iachiwe ifanye kazi yake. Na si kuwa kama watoto wanaocheza cha ndimu mitaani.

Vilevile vyombo vya dola vinapaswa kujuwa kuwa, wananchi ndio mabosi wao, kwa sababu kodi za wananchi ndio utumika kulipia mishahara yao, hizi video tunazo ziona watu wakipigwa marungu ni unyanyasaji na ni kinyume cha haki za binadamu.

Mamlaka na vyombo hivyo vitambue kuwa hakuna kikundi chochote cha wananchi kilichosusiwa uongozi wa nchi, ndio maana wananchi wote wameamua kushiriki katika kupiga kura ili kuchagua mtawala wanaye muona kuwa anafaa.

Naamini kuwa mamlaka za nchi na vyombo vya dola vinatambua majukumu yake ya kuwatumikia wananchi katika wakati huu tuliomo kwenye Uchaguzi Mkuu. Lakini ni jambo la kusikitisha kuona mambo yaliyo kinyume kabisa na matarajio ya mwananchi.

Ndio maana nauliza, mfumo wa siasa wa vyama vingi uliporudishwa nchini mwaka 1992 na kuifanya nchi hii kurejea tena kwenye mfumo wa vyama vingi, lakini mbona tunaona hali ni kinyume na mazingira ya kujenga demokrasia yakipindishwa, sasa kama hiyo demokrasia wanaifanya hivi mnataka nini badili yake?

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!