Thursday 7 January 2016

KWANINI NISIJIUNGE NAO!

Assalamu Alaiykum wa rRahmatullah wa Barakatuh

Hivi karibuni nilipata mwaliko kutoka kwa ndugu yangu katika Iymaan, wa kunitaka kujiunga na harakati za chama cha kisiasa cha Hizb ut-tahrir.

Ni kweli mimi nakubaliana jambo moja la kuwa Waislamu tunapaswa tuwe na kiongozi mmoja (Khalifa) ambaye ndio atakuwa msimamizi wa Waislam kwenye dola ya Kiislam (Khilafa).

Lakini sasa baada ya tafakari ya kina na kwa shukran zangu za dhati kabisa kwa yeye kuchukuwa muda wake na kuniandikia waraka mfupi wa mwaliko wake kwangu na kwa dhana yake njema kuhusiana na mimi, sina budi kushukuru kwa ilo na MwenyeziMungu atuwafikishe tuwe wenye dhanna njema kwa ndugu zetu wengine.

Binafsi kuhusiana na mimi kujiunga na harakati ya hizb ut-tahrir kwa sasa na kwa ukweli wa nafsi yangu na jinsi harakati zinavyo endeshwa sijakinaishwa na harakati nzima za chama cha hizb ut-tahrir.

Kwa nini ninasema hivyo, nasema hivyo si kwa sababu ya mabandiko ambayo tayari yamekwisha zungumzwa ambayo yanakosoa harakati nzima za chama cha hizb ut-tahrir, lahasha. Ni kwa sababu ambazo mimi binafsi ninaziona kuwa haziwezi kusogeza mbele kile ambacho kinatafutwa kwa kupitia chama cha hizb ut-tahrir.

chama cha hizb ut-tahrir kwa ujumla wamekuwa ni mahodari sana katika kupinga kila jambo linalofanywa na serikali za kisekula, hapa sina maana ya kutetea mfumo mzima wa kisekula hapana. Bali ninacho kiangalia katika kila hoja inayotolewa au kuandikwa kwenye makala mbalimbali za chama cha hizb ut-tahrir ni ukosoaji na kutoa suruhisho rahisi la utatuzi wa tatizo husika.

Mfano tunaweza kusema kuwa mfumo mzima wa jambo Fulani utatuliwa na Khilafa, sawa khilafa inaweza kutatua tatizo ilo, lakini ni kwa namna gani, je kuna uwezekano wa kuelezea vile Khilafa hiyo inayo tetewa na hizb ut-tahrir itatatua vipi tatizo husika?

Sikatahi kuwa uongozi wa Khilafa ndio ndoto ya kila Muislamu, lakini ni wangapi wanaelewa ilo? Je vipi mnaweza kuwashibisha au kuwauzia sera za chama cha hizb ut-tahrir Waislam ili waone kuwa chama cha hizb ut-tahrir ndio mkombozi wao?

Hizb ut-tahrir wapo sana kwenye dhanna nyepesi ya kinadharia, bila ya kuyafanyia kazi yale wanayo yaeleza. Kwanini nasema hivyo, tukiangalia mfano mmoja tunapozungumzia swala zima la kuondoa umasikini, tunajuwa kabisa kuwa Uislam tayari umeshaweka msingi wa kuondoa umasikini kwenye jamii. Hapa tunapaswa kuelezea ni jinsi gani kunahitajika ukusanyaji wa zakkah kwa kuweka misingi thabiti ya ukusanyaji wa hizo zakkah. Kwa maana ya kuwa na chombo imara ambacho kitakuwa kikihamasisha na kutoa elimu ya utoaji na ukusanyaji wa hizo zakkah.

Vilevile kuwe na utaratibu ambao masikini na mafukara wenye haki na hizo mali waweze kupatiwa haki zao, aidha ziwe ni fedha, nafaka au mifugo.

Kwa mfano huo mmoja tu, nilitegemea chama cha hizb ut-tahrir wawe na chombo cha wazi ambacho kitakuwa kikishughurikia jambo ilo, kama vile tunavyo ona vyombo vingine vya Kiislam ambavyo vinajitahidi kwa uwezo wao mdogo kukusanya zakkah na kuwatafuta wahitaji na kuwagawia. Sioni kwa nini tusubiri Khilafa ilihali jambo kama ilo linaweza kufanyiwa kazi na matokeo yake kuonekana wazi mbele ya umma mzima wa Kuislam.

Binafsi uku nilipo tupo Tukijishughulisha na Dawah kwa wale ambao si Waislam, na Alhamdulillah wengi wanaelimika na wengi wanarejea kwenye haki. Kama tungefuata utaratibu wa hizb ut-tahrir, basi tungeishia kuadika maelfu ya nakala kwenye mitandao. Lakini umeonekana kuwa wakipatikana watu wakaingia mitaani, wakajumuika kwenye harakati mbalimbali za kijamii kumewezesha kuleta athari nzuri kuhusiana na Uislam.

Nisikuchoshe na maelezo mengi, ila kwa ufupi ninacho kiona kwenye chama cha hizb ut-tahrir ni kukosekana kwa harakati halisi za kiutendaji ambazo zitaleta athari ya moja kwa moja kwenye jamii.

Mfano mdogo tu, yanapotokea majanga ya kiasili kama vile mafuriko, matetemeko ya ardhi na hata matatizo ya kutengenezwa na binadamu kama vile vita. nilitegemea chama cha hizb ut-tahrir kuwa mstari wa mbele kwenda kusaidia jamii iliyo athirika na majanga hayo.

Vilevile nilitegemea chama cha hizb ut-tahrir kiwe na taasisi mbalimbali ambazo zitaweza kuwasaidia waislam na wasio waislam, kama vile shule, zahanati, taasisi za fedha, udhamini wa masomo (scholarship) n.k.

Wakiweza kufanikiwa katika hayo, basi itapatikana athari kubwa sana na kukiwezesha chama cha hizb ut-tahrir kuonekana kweli ndio mkombozi wa Waislam. Lakini kwa jinsi hii ya sasa, ni sawa na kupigapiga miguu chini "Mark Time, March!" au 'Marking Time' yaani kama wanajeshi wanavyopiga miguu chini "shoto kulia shoto kulia" bila ya kusogea mbele wa nyuma. Na iki ndicho ninacho kiona mimi kwenye chama cha hizb ut-tahrir. Miaka inakwenda wapo hapo hapo walipo bila kusogea mbele.

Kama chama cha hizb ut-tahrir, kitasubiri mpaka ipatikane khilafa, kisha khalifa ndio aweze au awe ndio mwenye amri ya kukusanya Zakkah na kusimamia mambo mengine, basi matokeo yake ndio yatakuwa kama hayo ya wanajeshi kufanya Marking Time. (Miguu inasikika kwa sauti kama watu wanatembea kumbe hawasogei mbele wala nyma wapo tu hapo hapo), na ili ndio tatizo kubwa kwenye chama cha hizb ut-tahrir.

Zama za Mtume (saw) jinsi alivyofikisha Dawah yake kwa jamii, mpaka akafanikiwa kushika dola, inaweza kuwa tofauti na sasa kwa sababu, hivi sasa hizb ut-tahrir, hawawalinganii wasio waislamu, bali wanawalingania Waislam, tofauti na Mtume (saw), yeye alikuwa akiwalingania Makafiri, ndipo walipokuwa wengi na wa kutosha akasimamisha dola ya Kiislam.

Kipindi iki tulicho nacho, chama cha hizb ut-tahrir wanapaswa kuangalia mustakabari wa Waislam na kuyafanyia kazi matatizo yao kivitendo na si kuwalisha nadharia tu, uku wakikosoa kila linalofanya na serikali za kisekula bila wao kuonyesha kwa vitendo kwa yale machache wanayoyaweza kuyafanya.

Kitu kingine kama chama cha hizb ut-tahrir, lengo lao ni kufika uko kwenye Khilafa na ilihali wanawaacha wanachama wao kwenye maswala mazima ya kiroho ("...lengo la chama sio kuwalea watu kiroho") basi wajue hawatafika popote. Kwa sababu kama watu awapati chakula cha roho ina maana imani zao hazitakuwa kwa chama cha hizb ut-tahrir, zitakamatika kwenye vyama au kubakia kwenye madhehebu yao walio yazoea.

Kuhusiana na maswala ya kiroho hapa naweza kuelewa kuwa, chama cha hizb ut-tahrir, kinatega kuwapata wafuasi kutka kwenye madhehebu yote ya Kiislam. Na kwa wao kujiingiza kwenye maswala mazima ya Kiroho kunaweza kuwapoteza baadhi ya wanachama ambao wanaweza kutokubaliana na baadhi ya mafundisho kwa sababu yanakwenda kinyume na iymani zao za kimadhehebu.

Lakni hizb ut-tahrir wanajue kuwa maisha ya binadamu yanapokosa moja katika hao, yaani kushibishwa kiroho na kuyafanyia kazi yale wanayo shibishwa basi ujuwe naisha hayo hayatakuwa maisha mazuri.

Hitimisho langu na maoni yangu kwa chama cha hizb ut-tahrir, ni kwamba siku ambayo watatelemka chini kuja kwenye jamii na kuwa nao sambamba kwenye matatizo yao, ndio siku ambayo wataona zile "Marking Time" zimekuwa mwendo wa kusogea mbele, kinyume na hapo ni sawasawa na mtu aliye na kiu jangwani akahadaika na magazigazi akafikiria kuwa ni maji yaliotuama, akayakimbilia na kutofanikiwa kuyapata, mwishowe akajikuta anakufa kwa kiu.

Shukran.

2 comments:

  1. KICHWA CHA BLOG NI "TUPEANE NASAHA KWA MUJIBU WA DINI YETU" BILASHKA NI DINI YA UISLAM.

    KWANINI ALIYETUMA POST HATUMII JINA LAKE SAHIHI, KWANINI HATOI DALILI YA HOJA ZAKE KWAMBA MUISLAM HIZB KAKOSEA KWA DALILI KADHAA ZA KISHERIA NA USAHIHI WAKE NI HUU. IWAPO WANALINGANIA MAKAFIRI WASILIMU BASI NIAWLA ZAIDI KUWALINGANIA NDUGU ZAKE WAISLAM WAFUATE VIZURI MSTARI ALIOUCHORA MTUME SAW.

    MEDIA NIMUHIMU SANA KATIKA KULINGANIA NA MUHIMU ZAIDI NI MLINGANIZI KUWA NA IKHLAS.

    JE YEYE KATIKA DA'AWAH ANAYOFANYA LENGO MSINGI NININI NA KWADALILI ZIPI, NA LINATOFAUTIGANI NA HIZB.

    HAKIKA TUNAMPENDA MTUME SAW LAKINI NAONA NIWACHACHE SANA WANAOJUA KWAMBA KUMFUATA NIKATIKA IBADATI, FARADHI KISHERIA.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Tunashukuru sana kwa kutembelea blog yetu na pia tunashukuru tena kwa wewe kuweza kutoa mawazo na nasaha zako.

      Hii inaonyesha kuwa wamiliki wa blog wanatoa uhuru kamili kwa wachangiaji wa makala zao bila kificho au upendeleo wowote ule.

      Pili kutumia lakab si jambo lenye kukatazwa kwenye Uislamu na kila mtu anao uhuru wa kutumia lakab aipendao mradi tu, isiwe nje ya mipaka ya Uislam.

      Tatu, Ulipaswa wewe ukiwa kama mtetezi wa chama cha kisiasa cha Hizb ut-tahrir, kujibu huja juu ya huja kwa kila huja iliyoko kwenye makala hii, lakini kwa sababu zako binafsi ukuweza kujibu huja hata moja zaidi ya kulalamika.

      Basi ni bora ukawa na huja kulingana na makala hii ili wasomaji wengine wapate kufaidika.

      Shukra, ndugu zenu katika Uislam

      Delete

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!