Thursday 16 June 2016

Tangia kutolewa tangazo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), tangazo la kuzima simu ‘feki’ za mkononi, watu wengi wameshikwa na taharuki na wengine kujawa na fazaa na wingi wa kizaazaa kwa kusikitika kuwa watakosa mawasiliano muhimu.

Wapo ambao wameamua kutafuta simu nyingine na kuna ambao wameamua kusubiri kuona kama kweli yatatimia.

Baadhi ya watu wanaichukulia hatua hiyo kwa mtazamo hasi, wakiangalia namna gani hasara watakayoipata baada ya simu zao kufungiwa mawasiliano. Na kuna wengine wameliona tamko ilo kama tamko halali litakalo waweka watumiaji wa simu kwenye nafasi ya kiusalama zaidi na kuepukika na wale wote wenye kutumia vibaya simu za mikoni.

Binafsi naliangalia swala ili kwa muono mwingine kabisa, tukisoma kwenye Qur'an tunakuta tamko la wazi kabisa, tamko ambalo kwa mwenye akili anaweza kulifananisha japo kidogo na tamko hilo na uwenda wengine nao wakalifanyia kazi na kujitayarisha nalo.

MwenyeziMungu anatuambia kwenye surat Al-'Imraan, [5]: 185 kuwa....

Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu. (Surat Al-'Imraan, 5: 185)

Swali la kujiuliza, ni wangapi ambao tumetaharuki na kujawa na fazaa na wingi wa kizaazaa kwa kusikitika kuwa ipo siku nafsi zetu zitaonja mauti na kufufuliwa ili kulipwa ujira wetu kwa namna tulivyoishi hapa duniani!?

Kikawaida, binadamu tunashambuliwa na maradhi chungu nzima kuanzia moyo, sijui Kisukari, sijui Presha, kuna Saratani na magonjwa mengi mengineyo ambayo sitayataja, lakini hiyo ni dalili ya kuanza kujitaarisha na ile safari ilotajwa katika Suratul Al-'Imraan na Surat Mulk kama tunavyosoma;

Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi... Surat Suratul Mulk [67]:02

Binadamu tunapaswa kujiandaa na safari yetu hii, ambayo kila mmoja wetu ataipitia. Tunapaswa Kumcha MwenyeziMungu, na tujijue kuwa siku itafika tutakufa na kukutana naye.

Kumbuka kuiogopa siku ambayo Malaika wa Mauti atakapokuja kuchukua Roho yako na kuzima mawasiliano yako na mtoto au watoto zako, ndugu zako, wazazi wako, marafiki zako na vipenzi vyako na si kuogopa na kutaharuki kwa TCRA kuzima mawasiliano ya simu yako.

Ewe Mwenye kujua ambalo halijawa, Mwenye kujua litakalokuwa na likiwa vipi litakuwa, na ambayo mengine hata hatujui kama yatakuwa. Tunamuomba Allah atufishe na kutufufua hali ya kuwa ni Waislamu na Kuturuzuku sisi mwisho Mwema.
Aamiyn.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!