Thursday, 8 September 2016

Wengi wetu tunawaona vijana wengi mitaani wakijinasibisha na utamaduni wa ufugaji wa nywele zilizosokotwa na kuonekana kama mikia ya pweza (dreadlocks). Wengi wetu mtindo wa hizo nywele tunazijuwa kwa jina la Rasta au nywele za rasta.

Vijana hawa utawaona wakipendelea sana kusikiliza miziki kutoka Jamaika au ile yenye mirindimo ya Reggae ambayo asili yake ni uko uko Jamaika.

Mitindo ya ufugaji huu wa nywele si mgeni katika jamii za Kiafrika, kama vile wamasai na makabila mengine ya Kiafrika. Wapiganaji wa vita vya kuikomboa Kenya Mau Mau, waliopigana dhidi ya wakoloni wa Kiingereza kati ya 1952 hadi 1956, wakiongozwa na Dedan Kimathi, walikuwa na nywele hizi za rasta.

Vijana na watu wengi hawakuwaiga wala awakuwa na habari na ufugaji huu wa nywele, ni pale tu wanamuziki wa Kijamaika kupitia mtindo wa Reggae walipoonekana kufuga nywele kwa mtindo wa Misokoto na kupelekea kuwa maarufu kupitia bendi zao za muziki.

Ndipo kina sie nao tukajikuta tukiwaiga uvugaji huu wa nywele na hata uvutaji wa bangi ukahusishwa kama alama ya mapenzi ya urastafari, bila ya kujuwa kuwa Rastafari ni dini, iliyotokana na mchanganyiko wa Kikristo, harakati za kisiasa na mila za Kijamaika.

Rastafari ni imani iliyochimbuka uko Jamaika na inatokana na dini ya Kikristo katika miaka ya 1930, kufuatia kuvikwa taji la kifalme kwa aliyekuwa rais wa Ethiopia Haile Selassie I mwaka 1930.

Haile Selassie I

Wafuasi wake wamwabudu katika njia nyingi sawa kama vile baadhi ya Wakristo wanavyo muabudu Yesu, kuwa ni mungu au mwana wa mungu.

Wafuas wa imani hii ya Rastafari wanaamini kuwa Rastafaria ni njia ya maisha kufikia ukombozi kamili wa binadamu na haswa mtu mweusi.

Jina Rastafari ni limetokana na maneno mawili Ras pamoja na neno Tafari. Neno Ras ni cheo na jina la Tafari (Tafari Makonnen) ni jina la kwanza la Haile Selassie I kabla ya kuvikwa taji la ufalme.

Kwa lugha ya Kimhariki (Amharic), neno Ras, lina maana ya "kichwa" au Kiongozi na haswa uko Uhabeshi (Ethiopia) lina maanisha mtu anaye stahiwa kama vile “Mtoto wa Mfalme” (Prince) au Chifu.

Neno lingine ambalo limetokana na neno la Kiebrania Yah (יה) ni jina la Mungu katika Biblia, na linatokana ufupisho wa neno Jahweh au Yahuah (angalia Zaburi 68: 4 King James Version).

Wafuasi wengi wa dini hii ya Rastafari umuona Haile Selassie I kama Mungu (Jah) au Jah Rastafari (Mungu wa Rastafari) yaani ujio wa Pili wa Yesu Kristo "Mpakwa mafuta", yaani kuja mara ya pili kwa Yesu Kristo Mfalme na Dunia ambaye ndio huyo Haile Selassie I, Mungu katika utambulisho mpya katika mwili wa binadamu.

Theolojia na Imani ya Rastafari ni mwendelezo na mawazo kutoka kwa Marcus Mosiah Garvey Jr, mwanaharakati wa kisiasa ambaye alitaka kuboresha hali ya watu weusi uko Jamaika na ni wa aina tatu Nyahbinghi Order, Bobo Ashanti, na Kabila kumi na mbili za Israeli. 

Marcus Mosiah Garvey, amezaliwa Mwezi August 17 kwenye mji wa Saint Ann's Bay, nchini Jamaika mwaka 1897.

Marcus, alikuwa Kiongozi wa Kisiasa, mwandishi wa habari, mchapishaji, mwekezaji mfanya biashara na mzungumzaji mzuri wa lile analolisimamia.

Marcus Mosiah Garvey

Alianzisha chama cha kuwateta na kuwarejesha watu weusi Afrika kwa meli aliyoiita Black Star. Alikuwa ni mtu jasiri mjamaa mwanamapinduzi aliyekuwa na ushawishi mkubwa kiasi cha kuweza kupelekea msisimko na mwamko wa kimapinduzi kwa viongozi kadhaa wa Kiafrika na nje ya Afrika, kama vile, Kwame Nkrumah, Nelson Mandela, Jomo Kenyatta na wengine wengi.

Baadae alihamia London na kufarikia uko uko Uingereza akiwa na umri wa miaka 52. Athari ya kazi ya harakati zake za kumteta Mwafrika haswa mtu mweusi. Ndipo ikapelekea baadhi ya Wajamaika walioipenda Afrika haswa nchi ya Ethiopia kuanzisha harakati za kiimani na baade kuja kujulikana kuwa dini ya Rastafari miaka ya 1930.

Fikra za Marcus Garvey na Urastafari zimepelekea baadhi ya madhehebu kwenye dini hii ya Rastafari kumchukulia Garvey kuwa ni nabii na harakati zake zilikuja kupewa uzito haswa uko Jamaika kupitia muziki wa Reggae.

Bendi nyingi zilikuwa zikipiga muziki huu wa Reggae kwa mirindimo ya Kijamaika na bendi maarufu ambayo ilipelekea muziki huu wa Reggae kuwa maarufu ni bendi iliyojulikana kwa majina kadhaa kama vile The Teenagers (Vijana), The Wailing Rudeboys (Wavulana Jeuri Waombolezaji), The Wailers (Waombolezaji) na kadharika.

Bendi ya The Wailers, iliasisiwa mwaka 1963 na wanamuziki marafiki watatu, Hubert Winston McIntosh (Peter Tosh aliyefariki 1987), Neville Livingston (Bunny Wailer) na Robert Nesta Marley (Bob Marley aliyefariki 1981).

Reggae ilichanganya imani ya Rastafari (kutukuza Uafrika), mafundisho ya Marcus Gavey na harakati za walala hoi kisiasa.

Bob Marley & the Wailers

Mahadhi ya Reggae na Rasta yalitukuzwa na masharti rasmi mfano kutokula nyama, kusoma Biblia kama mwongozo wao, kufuga nywele, uvuta kasumba, bhang (Bangi) au Ganja.

Kiufupi tunaweza kusema kuwa uwekaji au ufugaji wa rasta ni katika imani ya dini ya Rastafari na si katika mila zetu za Kiislam. Uislamu unachunga nadhafa na usafi na pia mienendo yote kama tulivyofundishwa na Mtume wetu (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salam). Na yeye ndiye aliyetukataza tusijifananishe au kuwaiga wasiokuwa Waislam.

Kuhusu kujifananisha na makafiri Mtume (Swala Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salam) amesema:

Atakayejifananisha na watu, basi yeye ni miongoni mwao.
Abu Daawuud na Ahmad.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!