Tuesday 6 September 2016

SIKU MOYO UTAKAPO SIMAMA

Hivi karibuni nilikuwa kwa daktari ili kupima afya yangu, uku uwa kuna utaratibu wa kupima afya za watu kila baada ya miezi kadhaa, ili kujuwa kama kuna tatizo basi waweze kulitafutia ufumbuzi na wakati mwingine kupata ushauri tu kuhusu hali uliokuwa nayo.

Katika vipimo kuna vya aina nyingi kuna kupima damu ili kujuwa kama kuna tatizo na kipimo kingine ambacho ni maarufu ni kile cha kupima presha yaani mapigo ya moyo yaani blood pressure monitor (Sphygmomanometer) na kile kifaa kingine madaktari wengi utawaona wanacho wamekining'iniza kwenye shingo zao kinaitwa stethoscope, ambacho wanakitumia kusikiliza sauti kwenye mapafu.

Baadae nikamuuliza daktari wangu, wastani wa mapigo ya moyo wa binadamu wa kawaida ni kiasi gani kwa dakika moja. Naye akanifahamisha kuwa kwa wastani moyo wa binadamu kwa dakika unapiga mara sabini (70). Hii ni sawa na kusema kwa dakika 1mn = 70bpm

Ukizidisha mapigo hayo ya moyo kwa saa moja yaani 70 x 60 unapata 4200, kwa siku yaa saa 24 unapata mapigo 100,800. Namba hii ukizidisha kwa siku 365 ambazo ni wastani wa mwaka mmoja, moyo wa binadamu utakuwa umepiga mara hizi 36, 792,000.
Baadae mawazoni nikawa najiwazia hii ina maana kuwa Wastani huu nikizidisha kwa umri wangu kamili naweza kukisia idadi ya mapigo yangu ya moyo.

Mfano wa mtu mwenye umri wa miaka 60 wastani wa mapigo yake ni 60 x 36, 792,000 = 2,207,520,000 mara milioni elfu mbili mia mbili na saba laki tano na elfu ishirini.

Sasa kama umri wako ni miaka thalathini ina maana ushakula nusu ya mapigo yalobaki basi utambue kuwa ushatweta mara 1,103,760,000 mara milioni elfu moja mia moja na statu laki saba na elfu sitini.

Kwa kuwa hatujui umri wetu na siku mioyo yetu lini itasimama kama tumebakisha nusu saa pengine robo saa au siku pengine miezi au mwaka.

Nikakumbuka kisa kimoja kiichotokea uko China, miaka 3,600 ilopita Mfalme katika mji mmoja wa Kichina alimuuliza Daktari wake Bwana Chi Po amueleze vipi Mauti yatamkuta.

Daktari yule, akaandika kumueleza hivi:
'Ukikurubia utu uzima mifupa yako itakua mikavu, na inangan'ganaa na kuuma (Osteoporosis), na matatizo ya tumbo yanaongezeka. Kila mara unapata maumivu (Chronic indigestion), na pia matatizo ya Moyo kila mara kama vile Moyo kuuma, kuhema pumzi juu juu, ukitembea lazima usimame kusubiri maumivu yapotee (Angina, au Chronic rrhytthmia). Mara kwa mara utakua unapata homa kutokana na (urinary-tract infections), na mifupa yako itavuliwa nyama (loss of lean muscle mass), macho yako yataingia ndani, na pia utakua unapoteza uweza wako wa kuona (cataracts), halafu hapo tena ile mashine itoayo sauti itasimama ghafla (heart failure) na hapo mboni yako ya jicho itakua haiwezi tena ku-kufanya kazi - sasa hapo itakua Mauti yashakuchukua'.
Akamalizia Dr. Chi kwa kusema;
“Mauti yanawasili pale mwili wa mwanaadamu unaposhindwa kupigana na maradhi”.
Kwenye Qur'an Tukufu Surat Yasin [36]: 68 MwenyeziMungu anatueleza…
'Na tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii?'
Maelezo:
Na tunaye mfanyia umri wake ukawa mrefu, tunamrudisha, kutoka nguvu akawa dhaifu. Basi je hawayazingatii haya wakayatia akilini ya uweza wetu kuyafanya haya, na wao wakajua kuwa dunia ni nyumba ya kupita ina mwisho wake, na kuwa Akhera ndiyo nyumba ya kubaki na kudumu?
----

Hapo kumrejesha nyuma kusudio lake ni kupunguzwa kidogo kidogo uwezo  wa ile nidhamu nzima ya kurudisha tena, kwani unapokua mdogo jino likitoka linaota jengine, lakini baada ya kufikia umri fulani linakua halioti tena, na hapo ile nidhamu inakua tayari imeshaanza pasi na mwanaadamu kujua.

Yaani baada ya kuwa na nguvu anakuwa dhaifu. Hayo ni kwa kuwa maisha ya mwanaadamu yanapitia vipindi vitatu, kukua, kutimia kukua; na ukongwe unaanza kwa kunywea kwa mafigo, ini, Ghudda Ddarqiya au Thyroid gland, na Pancreas, yaani Dongoronya. Na haya huleta athari katika kudhoofika mwili wote.

Mishipa ya damu nayo huanza kukacha na kunywea, na kwa hivyo hupunguka damu inayo kwenda katika viungo vyote vya mwili, basi ndio huzidi udhaifu juu ya udhaifu.

Na katika sababu za kukonga ni kuzidi nguvu za kubomoka kuliko kujengeka katika mwili, yaani Metabolism. Na hayo ni kwa kuwa Khalaya au Cells, za mwili zote zimo katika hali ya kugeuka, na pia Khalaya za damu, isipo kuwa Khalaya za ubongo wa kichwani na wa katika mifupa. Hizo hazigeuki muda wote wa uhai.

Ikiwa kiasi ya kuundika upya ni sawa ya kiasi cha kuharibika, basi hapana madhara yanayo tokea. Lakini ikiwa kuharibika ni kukubwa kuliko kujengeka katika kiungo chochote basi hapo hudhihiri madhara kwenye kiungo hicho.

Na kwa hivyo kila umri ukiwa mkubwa kiasi cha kujengeka kinapungua na kinazidi kiasi cha kubomoka kwa Khalaya,  na kunadhihiri kunywea, na kupungua nguvu kote. Na hukhitalifiana kiasi cha kujengeka kwa mnasaba wa kubomoka kwa kukhitalifiana namna ya mfumo (Nasiij, Texture). Katika hayo yanayo dhihiri kama ngozi iliyo funika mwili, na zilio funika paipu za kusaga chakula, na paipu za Ghudad, Glands, zinachakaa kwa upesi zaidi kila miaka ya binaadamu ikipita. Na hii ni sababu ya kuonekana upesi alama za kuzeeka.

Basi tujiulize siku tutakapo ondoka duniani ni hathari gani ambayo tumeiwacha nyuma, ni matendo yepi mazuri ya kukumbukwa kiasi watu waone kuwa wameondokewa na mtu ambaye alikuwa ni muhimu katika jamii?

Ewe Mola wetu tujaze Imani utujaalie sisi nguvu za kukuabudu wewe peke yako. 
Aamiyn

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!