Saturday 15 December 2018

KISWAHILI NA KIINGEREZA NI
LUGHA ZA TAIFA LA TANZANIA
Waweza Ona kuwa ni Ajabu Lakini Ndio Ukweli Wenyewe.

Unaweza kushangaa na kicha cha habari hapo juu, lakini huo ndio ukweli ambao wengi wetu hatu hujuwi.

Lugha ya Kiswahili ni lugha kongwe, ni lugha ambayo ikizungumzwa na wakaazi wa Afrika Mashariki na ya kati kabla ya kuja kwa Wakoloni wa KIjerumani na Waingereza.

Lugha ya Kiswahili ilitumika na wafanyabiashara wa pwani ya Afrika Mashariki, ikaendelea kutumika kipindi cha mkoloni (Mjerumani), wakoloni wa Kijerumani waliendelea kuwaachia Watz waongee lugha yao ya Kiswahili.

Alipokuja Waingereza hapo ndipo Kiingereza kikawekwa kwenye mitaala ya kufundishia, na ndio utaona wazee wengi waliosoma enzi ya Muingereza na hata Mjerumani, wanaongea na kuandika Kiingereza kizuri sana, tena kile fasaha  kile cha Oxford.

Tulipopata Uhuru na kujitawala rasmi, lugha ya Kiswahili ndio ikawa lugha rasmi ya kufundishia, kiingereza kikabakia kuwa lugha ya Kiutawala (Kiserikali) kwenye mambo ya sheria na biashara za Mabenki n.k.

Ilikuwa mtu akisikika anaongea Kiswahili aidha watamuona kuwa anajikwenza na kujiona Msomi au anajitia kimbelembele kwa kuzungumza lugha ya mkoloni, kiasi watamuona kuwa ni mtu mwenye majivuno.

Vijana wengi waliosoma baada ya uhuru ni aghalabu sana kuwasikia wakiongea Kiingereza vizuri, kwa sababu hakuna shuruti au ulazimisho wa wao kuona kuwa wanapaswa kuzungumza Kiingereza. Matokeo yake Majumbani, Maofisini na hata Seikalini asilimia 99.99 ni Kiswahili, ila kwenye yale mambo ambayo yanahitaji sheria kwenye makaratasi ndio uwa kwa Kiingereza.

Idadi ya watoto walipaswa kuanza shule ya msingi, haikuwa ya kuridhisha sana, kiasi kukapitishwa Azimio ndani ya Azimio la Arusha kuwa kuwepo na dhamira ya wazi ya kuwapatia watoto na kila ambae hakusoma elimu ya msingi ambayo kijana anapomaliza aweze kujitegemea.

Ndipo mwaka 1974 kukapitishwa Azimio la Musoma, 1974 "Elimu kwa wote" Universal Primary Education (UPE). Kwa kifupi ikaitwa elimu ya UPE na harakati zake zilikuwa kubwa kuanzia mwaka 1977.

Mikakati haswa ilikuwa kwa wananchi waishio vijijini ambao wengi wao walikuwa hawana mwamko wa kutaka kusoma, ndipo mipango ikafanywa ili kila mtu angalau ajue tu kusoma na kuandika. Kulikuwa pia na wazee ni wengi wasiojua kusoma na kuandika; kukaanzishwa "Elimu kwa watu wazima".

Vijana wengi waliingizwa shule za msingi, na haikuwa ajabu kwa wale walokuwa wamesoma miaka ya 70 mpaka 80, kusoma na vijana waliokwisha pea kiumri wa kuanza shule. Tulifikishwa mahali pazuri kitakwimu duniani kuhusu wasojua kusoma na kuandika.

Wakati huo huo, kulikuwa na matatizo ya kukosekana kwa walimu wa kutosha, ndipo hapo sasa, serikali kupitia wizara yake ya Elimu, ikaweka mikakati ya kuwapeleka kusomea ualimu vijana wengi waliomaliza darasa la saba waliopata maksi za wastani, wakaitwa walimu wa UPE.

Walimu awa walikuwa kama vile wasaidizi wa walimu, kwa sababu elimu yao hakuwa kubwa kiasi cha kupewa wanafunzi kusomesha, kwa sababu wao wenyewe waliishia shule za msingi (darasa la saba) na kisha kupelekwa kusomea ualimu na kurejeshwa kufundisha shule za msingi.

Kidogo kidogo, kutokana na upeo wao kuwa si mkubwa, pamoja na kudharauliwa, elimu ya msingi ikaanza kushuka, na angamizo ubwa lilikuja pale dunia ilipokuwa kwenye mgogoro wa kiuchumi, hali ambayo iliyakumba mashirika ya fedha ya duniani kama vile IMF, Benki ya Dunia (WB) n.k.

Kwa ufupi naweza kusema kuwa mambo yote hayo yamesababisha sekta ya elimu kuwa na upungufu mkubwa wa rasilimali zinazosababisha mabadiliko ya maendeleo kwenye elimu ya UPE, hali ile ikasababisha kushuka kwa kwa wingi ubora katika ngazi zote za elimu nchini Tanzania.

Walimu wasio na upeo na juzi wa kutosha, mishahara duni, mazingira magumu ya kazi pamoja na miundo mbinu afifu imepelekea walimu walio na upeo na ujuzi mzuri kukosa hali na hamasa ya kufundisha vizuri, wengi wao wakajikuta wakijishughulisha zaidi na biashara ndogo ndogo ili waweze kujikimu kimaisha.

Msumali wa mwisho wa kwenye jeneza la elimu, lilipigiliwa kati ya mwaka 1978–1979, pale tulipoingia kwenye vita na Uganda, mika miwili ile ilipelekea nchi kutumia mabilioni ya pesa kwenye vita na kusababisha wizara zingine kama wizara ya Elimu, kupunguziwa bajeti yake ya fedha. Na mzimu wa ufukara ukaendelea kutuandama mpaka leo, hatujaweza kunyanyuka tena, japokuwa tuliambiwa tufunge mikanda kwa miezi kumi na nane, lakini mpaka hivi sasa zaidi ya miaka 38 haijafunguliwa.

Mambo ni mengi sana kwa kweli, na hata sasa bado lile jinamizi la ukosefu wa elimu nzuri linatuandama, kwa sababu kizazi kile kilichopitia elimu ya mkoloni, wengi wao kama hawapo serialini basi washajipumzikia majumbani mwao na hawajishughulishi tena na harakati zozote za kuinua elimu au walisha tangulia mbele ya haki...

Kizazi kilichobakia ndio kile ambacho kilipitia kwenye elimu ya UPE na waliobakia ndio awa wa kizazi cha doti komu, sasa hivi mtoto anajifunza Kiingereza shule, akirudi nyumbani asilimia 100 Kiswahili, mtaani ndio kabisa, ni Kiswahili kilicochanganyika na lugha za misimu. 

Kizazi cha doti komu ndio vijana watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii ni vijana wasio penda kujifunza wala kukubali kuelekezwa. Hawapendi kusoma, bandiko lenye kurasa mbili kwao ni kubwa mno. Ndio hao wenye kuchanganya Kiswahili na Kiingereza na ilihali lugha zote hawazijui.

Uandishi wao umeathriwa na utumaji wa meseji kabla ya kuja kwa mitandao ya kijamii. Ilipoanza kuja kwa mitandao ya kijamii na tovuti balaza (Forums) ndio utaona wakiandika bila kuweka irabu, au kukatisha maneno, sababu ya yale mazoea ya kukata maneno.

Kuna haja ya makusudi kabisa, ya serikali na taasisi binafsi kuliangalia swala hili, kwa sababu tunapo elekea siko, maana si ajabu leo hii ukaona wahitimu wa vyuo vikuu wawe wanasheria au waandishi wa habari au wachumi, wengi wao awajui kuandika Lugha zote hizi aidha ya Kiswahili au ya Kiingereza, na kama ikitokea kwa bahati mbaya mtandao wa google kuzimwa, basi na wao watakuwa wamezimika kabisa kabisa.

Mapambano ya Makubwa ya Kielimu Yanahitajika Nchini Tanzania...

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!