Monday, 18 May 2015


Binadamu tunaye adui mkubwa kabisa ambaye tunaishi naye, tunatembea naye na tunalala naye na kushauriana naye kila kukicha. Adui huyo si mwingine ila Nafsi iliyojaa uadui, uwovu na majivuno yakiambatana na kiburi na kutafuta kukomoana, pasipo sababu za maana. Hakuna tabia mbaya katika tabia za binadamu na yenye kuchukiwa kama tabia hii.

Tabia hizi kama zikimea kwenye nafsi zetu basi uondoa mfungamano wa kirafiki na kindugu na hata majadiliano yetu hukosa busara na hikma kiasi cha kupelekea kwenye utengano na uhasama.

Naweza kuuhita ugonjwa huu kwa jina la maradhi ya kimaadili yanayompata mtu, maradhi haya ya chuki na uadui ni miongoni mwa maafa makubwa ya ufanisi na utulivu wa nafsi, yanaotokana na tabia mbaya ya hasira ya kushindwa katika medani ya kutafuta maisha au kushindwa kwako katika kile unachokitafuta katika kuboresha maisha yako, kiasi ya kuvuruga mtiririko wa fikra chanya na kupelekea kuvuruga uthabiti wa kiroho wa mtu.

Huenda ni kutokana na sababu Fulani fulani za kukosea hapa na pale au kujaribu hiki na kile. Kushindwa uku umfanya muhusika kupata hamaki na kujichukia na kupelekea kuwachukia wale waliofanikiwa kimaisha, kiasi ya kwamba kwa wale wasio na uvumilivu uamua kuwasingizia mambo haya na yale wale wanao waona kuwa ni maadui zao. Kiasi ya kusahau kuwa kufanikiwa au kuto fanikia ni mipango yako tu kutokuwa mizuri au kwa kutaka kutumia njia ambazo si za kimaadili, kama vile wizi au utapeli.

Hamaki hizi ni ile chuki iliyojengeka muda mrefu kiasi cha kusababisha moto uliofunikwa chini ya majivu ambao unaweza kutoa cheche za chuki na uadui zitakazounguza na kuteketeza mazao ya ufanisi na utulivu wa nafsi yako.

Uadui hauwezi kuondoa ubaya. Bali hulipanua na kulichimba zaidi donda. Kwa kawaida, uhasama humfanya hasimu ajitetee zaidi na alipize kisasi zaidi, akitegemea kupata utulivu wa nafsi, kumbe ndio anajirimbikizia machungu ambayo umletea maradhi ya saratani ya akili na kupelekea kuwa na maamuzi yasiofaa na yaliojaa visasi na chuki.

Kutotumia akili na kutofikiria matokeo mabaya ya kufanya ugomvi, akifikiria kwamba anamkomoa mtu kumbe anajikomoa mwenyewe. Maana kila binadamu ana kamusi ya maisha yake na kuna baadhi ya watu, hawana maneno kama vile 'samehe au upendo' kabisa, bali kuna maneno kama vile 'uadui, ugomvi, nitamkomoa, atajuta katika maisha, ataipatapata fresh' na mishabaha na minyambuliko yake ndiyo iliyojaa humo.

Watu wengi wanashindwa kuelewa kwamba kushikwa na hasira sana ni dalili ya kutopevuka kiakili. Hata hivyo, tusikereke na watu kama hao, bali tuwafunike kwa shuka ya amani na upendo na kwa nasaha njema.

Moyo wa kuweka kisasi na kukomoana ni dalili ya unyonge wa nafsi. Na ni ishara ya maudhi na maonevu aliyoyapata mtu udogoni mwake aidha shuleni au madrasa au mtaani kwake alipokuwa akiishi au aliyo yaona katika familia au wazazi wake.

Mambo haya huweka athari mbaya na kinyongo katika moyo wake kwa kadiri kwamba nafsi yake husumbuliwa na aina moja ya chuki iliyotia fora. Kwa ufupi, kukomoana na kulipiza kisasi ni njia mojawapo wanayoitumia wenye kujihisi duni ili kufidia kushindwa kwao.

Hutumia visingizio mbalimbali kuwakera wengine na utenda uhalifu wa hatari kulipiza kisasi kwa yale yaliomsibu alipokuwa mdogo, akitafuta kujifariji ukubwani kwa masahibu ya utotoni.

Watu wa aina hii mara nyingi wanakuwa wamelelewa katika koo duni na wakapata vyeo au kusafiri nchi za mbali na kujiona kuwa wao ni bora, hivyo kupelekea kuwa wajeuri. Kwa njia hii hutaka kufidia uduni waliolelewa nao katika koo hizo. Na ujiona ni watu bora kuliko wengine, na hutaka kutumia uhasidi na ubinafsi wao kujitangazia ubora wao. Wengi wetu tunaweza kuwatambua watu wa aina hii miongoni mwetu.

Baadhi ya watu huvaa ngozi za urafiki au uswahiba au kujionesha kuwa ni mpenda dini na haswa hizi zama za utumiaji wa mitandao, watu uweza kukuomba urafiki na kuwaongeza kwenye orodha ya watu utakaokuwa ukiwasiliana nao, kumbe ni wanafiki kwa njia hii wanaweza kuwakomoa au kuwaangamiza wengine katika jamii kuonekana kama ni wasaliti.

Siku zote moyo wa mwenye wivu, husda na roho mbaya, daima uona uchungu na uwa hauna raha wakati wowote. Mtu anayejifunga katika kuta nne za majivuno na nafsi yake ikatawaliwa na chuki, hatajali kamwe kuwaaribia wengine isipokuwa atazingatia matakwa yake tu. Kwa hivyo, atajaribu kwa nguvu zote kuwaudhi na kuwakera wengine na kujifanya mashuhuri na msifiwa, na kuilazimisha jamii imuone yeye ni bora.


Basi nadiriki kusema kwamba, kumdharau mtu mshari na kujiepusha na marumbano yasio na tija ni fimbo tosha kabisa, kwa sababu ukiingia wenye marumbano na mtu mshari atakushusha hadi ufikie upeo wake wa kufikiri kijinga na kipumbavu, na kisha atataka kukugaragaza kwa upumbavu wake, na kwa sababu hana hoja, mwishoni utashindwa kuendelea naye.

Lakini ukiingia kwenye marumbano ya hoja dhidi ya wasomi, ukiwashinda au wakikushinda basi utafaidika kwa elimu yao, kwa sababu wana upeo unao lingana na wewe, na hapo lazima utaondoka na faida japo mbili au tatu.

Siri moja kubwa sana ya kumuumiza mtu mshari kisaikolojia ni kumdharau na kumfanya kama hayupo, yeye mwenyewe ndio atakuwa akiangaika, maana hajui umeuchukuliaje upumbavu wake.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!