Friday, 18 November 2016

Maovu yote yametoka Bara, ili nalo Je?

Utafiti uliofanyika mwaka 2014 uko Zanzibar kuhusu Hali ya Liwati na Ushoga imeelezwa kuwa asilimia 25 ya wanawake wanafanya mapenzi kinyume cha maumbile ama na waume zao au na wanaume wengine kama njia ya kukimbia kupata ujauzito na mambo mengine.

Takwimu hizo zilitolewa na Katibu wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar kutoka wilaya ya magharibi, Sheikh Nassor Hamad Omar, wakati akiwasilisha ripoti ya awali ya utafiti wa kamati ya kupambana na vitendo vya liwati katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Tunguu, kwenye kongamano la vijana kuhusu udhalilishaji wa kijinsia na mimba za mapema.

Alisema takwimu hizo zimekusanywa kutokana na utafiti uliofanywa na Jumuiya ya Maimamu (JUMAZA) katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

Na sababu ya kufanya hivyo, ama wanawake hao wanaogopa kupata ujauzito hasa wale ambao bado hawajaolewa lakini wako kwenye mahusiano yasio rasmi (Ndoa) na hata wale walioko kwenye ndoa.

Aidha utafiti huo umegundua watoto wengi wenye umri wa kuanzia miaka 9 hadi 20, wanaingizwa katika vitendo viovu ikiwemo liwati na usagaji.

Leo ni miaka miwili (2) tangia ripoti hiyo itolewe adharani mwaka 2014, japokuwa swala ili limekuwa likijulikana sana na kila mtu akiulizwa anajuwa kuwa miji ya Zanzibar maswala ya Liwati yapo, japo yanafungiwa macho.

Kama ilivyo kawaida ya Wazanzibar wengi, hata ili laweza kuwa limeletwa na Wabara, maana Zanzibar kila ovu limekuwa ni jambo ambalo asili yake ni Bara. Wizi umetoka Bara, Ulevi umetoka Bara, Ushoga na Usagaji janga ili nalo asili yake itakuwa bara tu!

Hii tabia ya kurembea kila ovu kuwa asili yake Bara, imekuwa ni jambo la kawaida sana, siku ukisikia askari amepiga mtu au nyumba fulani imeingiliwa na mapolisi basi utasikia maneno tu... "Mijitu ya Bara hiyo".

Zanzibar si Pepo kiasi kusiwe na mambo yote hayo, ulevi, umalaya, wizi, ushoga na maovu mengine yote yalikuwepo tangia zama za Sultani na yanaendelea mpaka leo.

Hii tabia ya kukana na kuona kuwa mabinti, vijana na wazee wa Kizanzibar ni Malaika hawawezi kujiingiza kwenye maovu, matokeo yake ndio haya, kwa sababu wazazi wameshindwa wenyewe kuwalea watoto wao kwenye maadili mema kwa visingizo tulivyo vitaja, na matokeo yake ndio haya...!

Zanzibar imepoteza mwelekeo wake baada ya kukumbatia siasa tena si kukumbatia tu, kiasi wameibeba siasa kiasi cha kusahau udugu baina yao, leo utawasikia huyu Mpemba na huyu Muunguja, nayo sijui yameletwa na Wabara, wanajisahau kuwa hakuna kisiwa kimeumbwa kikawa na watu ndani, wote asili yao ni nje ya Zanzibar, sasa hii tabia ya kurembea kila kitu kuwa kimekuwa import kutoka Bara, haita wafikisha popote.

Kwa kweli wananchi na viongozi wa SMZ inabidi wabadirike sasa kwani itakapofika adhabu ya MwenyeziMungu Basi wajue kiama chao kitaanzia hapa hapa duniani, Ahera zitaenda hesabu tu...

Zanzibar ilikuwa ni chemchem ya dini. Kama ilivyokuwa miji iliyokuwa na Waislamu wengi na dini kuwa na nguvu zaidi, kama Zanzibar, Waislamu wakafikia hatua ya kufuata sharia chache katika Uislamu, zinazohusu ndoa na mirathi na watawala wakiwateua makadhi kushughulikia hayo. Unguja Makadhi wa Kisunni ndio waliokuwa wengi na Pemba Makadhi wa Kiibadhi ndio waliokuwa wengi.

Walimu wa dini walikuja kutoka nchi za Kiarabu, hasa Masheikh wa Kisunni kutoka nchi za kusini ya Bara Arabu, baadhi yao wakiwa ni wafanyabiashara.

Maarufu katika hao ni Sheikh Muhammad Abdulwahab (1703 – 1792 AD). Kadhalika huu ulikuwa wakati wa kuanza kwa biashara na nchi za Ulaya ambayo baadaye mfalme Said bin Sultan aliiendeleza. 

Karne ya 19 AD elimu za maarifa ya Uislamu ziliendelea. Watawala wa kifalme kutoka Oman ambao walikuwa wa madhehebu ya Ibadhi walishughulikia dola na biashara hawakuingilia itikadi za Kisunni na Masunni hawakuingilia watu walioitakidi Ushia.

Zanzibar ilikuwa sana kiuchumi na kisiasa ilidhibiti karibu mwambao wote na kufanywa kituo kikuu cha biashara yote ya nje hasa mali kutoka bara.

Wanazuoni wa miji ya Mwambao walitembeleana kubadilishana elimu na kufanya biashara, walitunga vitabu na kufungua madrasa kubwa kubwa za kufundisha elimu ya dini, wengine walikwenda nje kusomesha kama vile Uganda na kwingineko.

Kwa vile Uislamu ushamiri sana Zanzibar, Wamisheni pia walifurahia fursa ya kuanza harakati zao Zanzibar kuendeza Ukristo, kwa matumaini kuwa wakifanikiwa kubadilisha imani ya Kiislamu Zanzibar itakuwa ni rahisi kuifanya jamii nzima ya Mwambao kuwa ya Wakristo.

La muhimu ni kuwa Wazungu hatimaye walichukua hatamu za dola (ukoloni ukaanza) wakashika kisu mpini, ikawa Waislamu wameshika kwenye makali. Khatima ya jamii ya Waislamu Zanzibar ikawa katika mikono ya Waingereza.

Hali ilikuja kubadilika pale Zanzibar walipoichukulia siasa kuwa ndio mkombozi wao kiasi cha kuona vyama vya siasa ndivyo vitakavyoweza kuondoa matatizo yao na kusahau Uislamu wao, chuki na husda zikaanza kidogo kidogo kujitokeza miongoni mwao, kiasi wafuasi wa vyama kuanza kuchukiana.

Hali  nzima ikabadilika. Hadi kufikia karne ya 20 elimu ya Kiislamu pamoja na utamaduni wa Kiislamu ukafifia, Zanzibar kidogo kidogo ikaanza kupoteza mwelekeo.

Kabla ya mapinduzi kulikuwa na vyama vya Afro-Shirazi Party (ASP) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP). Washirazi na Waafrika wengi walikuwa wana-ASP. Waarabu wengi walikuwa wana-ZNP.

Pia, chama cha ASP kilikuwa chama cha watu wa Ng'ambo na wale walioishi mashambani na chama cha ZNP kilikuwa chama cha watu walioishi mjini.

Vyama viwili hivi vilipigania uhuru na walishinda. Waingereza waliondoka na wananchi walipiga kura. ASP, chama cha watu wengi, kilipata viti vichache ingawa ZNP, chama cha watu wachache, kilipata viti vingi.

Baadaye, Washirazi wengi waliondoka ASP na waliunda chama cha ZPPP na waliunguana na ZNP kwa kufanya serikali. Mwezi wa Januari mwaka 1964 kulikuwa na mapinduzi.

Nyerere na watu wa TANU waliwasaidia ASP ambayo ilikuwa ikiongozwa na Karume. Walifanya mapinduzi yaliyopelekea kumwagika kwa damu nyingi zisizo na hatia damu za Waislam. Sultani alifukuzwa na kukimbilia Uingereza. Watu wengi wenye asili wa Oman walirudi kwao Oman.

Baada ya hapo kila mtu anajua kilichojili, hakuna haja ya kukumbushana vidonda vilivyokwisha kauka na kubakia makovu, lakini la muhimu ni kwa Wazanzibar wenywe kukaa chini na kuondoa tofauti zao za kisiasa kwa sababu ndizo zinazowafanya wasahau kuwa wao kinacho waunganisha ni La ilaha 'illa-llah, Muhammadur-rasulu-llah.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!