Monday, 5 December 2022

 NILIKWENDA KUNUNUA MWENYEWE DUKANI

Hivi Siku Hizi Bado Kuna Wanao Tafuna Tambuu!?

Nipo Zangu Likizo, Ndani ya Jijila la Dar, Nakatiza Mitaa ya 'Uhindini' Karibu na Palipokuwa na Jumba la Sinema la Cameo, Lengo ni Kuelekea Walipokuwa Wakiishi Wakwe Zangu, Mtaa ya Kisutu.

Nikaikumbuka hii mitaa enzi hizo nikiishi mtaa wa Livingstone, walikuwa wakiuza sana Tambuu, ila ni ayami sasa sijaona 'Wahindi' wala 'Waswahili' wakitafuna Tambuu.

Zamani ukipita hii mitaa unakuta watu wanatafuna tu. Sasa usiombe jamaa awe anatafuna akiwa ghorofani halafu 'aipunguze' mdomoni wakati wewe unapita chini. Utasimulia.

Nikakumbuka kisa kilichonipata, miaka kadhaa nyuma. Nipo zangu nyumbani, mtaa wa Livingstone, Kariakoo. Miaka ile ya 80, bado kinda hata ubwabwa wa shingo bado kunitoka, sina hili wala lile. Hata sijui lile wazo lilikuja vipi, ila mpaka leo naamini kabisa, yaani haki ya Mungu tena, ndani ya mtima wangu kuwa; siku ile nilitembelewa na ibilisi wa Kibaniyani.

Tena atakuwa ni Mgujarati tu afiriti yule ayari, maana si kwa ushawishi ule ulionikamata, kiasi cha kushindwa kufikiria vizuri. Wala sikuwa na uraibu wa kula Tambuu, ila siku ile nilikamatika, nikajikuta nipo kiguu na njia kuelekea maeneo ya Kisutu, Uhindini.

Nikakatiza zangu Mnazi Mmoja, huyoo kiguu na njia, nikapita Mtaa wa Libya, mpaka makutano ya mtaa wa Libya na Zanaki, kisha nikachepuka kidogo kuingia mtaa wa Mtendeni, kisha nikaingia mtaa wa Mlima, kabla ya kukanyaga mtaa niliokusudia, mtaa wa Kisutu, dukani kwa Muhindi, Makaputura.

Ni baba wa Makamu, mnene haswa, kakaa dukani kwake, akipenda kuvaa kaputura akiishikiza kwa anjali, na ndio ikawa rakabu yake, Mzee/Babu Makaputura. 

Duka limesheheni vitu kadhaa wa kadha, vimewekwa bila mpangilio maalum. Harufu ya Agarbatti inachomeka iliyowashwa mbele ya Ganesha na Lakshmiina, ina hanikiza kiasi cha kukera kwenye pua, harufu badala ya kuanisi ikawa inakera kiasi.

Akanitazama, bila ya kutabasamu, anafungua kinywa chake kunisemesha, huku nikishuhudia meno yake, yaliyobadirika rangi na kupata rangi ya Kahawia, iliyochanganyika na Chanikiwiti na mdomo wake uliojaa mate Mekundu kama damu kwa kula tambuu.

Kisha anatema mate mekundu yasiyopendeza, "Nini nataka veve", akaniuliza kwa rafidhi yake ya Kihindi, nami nikajikuta namjibu bila kufikiria, nataka tambuu, akanitazama kisha akaniuliza, "Nani Natuma veve tambuu" Kaka, nikamjibu, "Nambari gani iko nataka" nikamjibu, namba kumi na tatu, "Nambari Kumi na tatu, Taveja yeye" ndio babu, we nipe tu, ataiweza, nikamjibu. "Nataka gapi, bili, tatu inne" Moja tu inatosha.

"Haya subiri kidogo nategeza wewe, ile spesho kabisa, Tikee" uku akitingisha kichwa chake... Nikaitikia Tikee. Kulikuwa na majani ya Tambuu mezani, akachukua jani moja akalipangusa kidogo, kisha akaweka Popoo pamoja na chokaa kidogo juu ya jani la mtambuu, akaongeza na Tumbaku, Kungu Manga kidogo, Jagir gur na vikorokoro vingine wala sivikumbuki tena.

Akachana gazeti na kunifungia, "haya lete shiligi bili", nikampatia, kisha huyoo nikaongoza kurudi zangu, nyumbani. Nikapita mtaa wa Mrima, nikafungua kifurushi changu cha tambuu, nikabugia yote kinywani.

Sikumbuki kutema mate, kila yakijaa kinywani, nayameza kwa ule utamu wa ile sukari guru... Dakika si nyingi, nikaanza kuhisi Andasa ikipanda kidogo kidogo.

Afanaleki! Nikaanza kuhisi ubongo wangu haujatulia, harabu ya ile tambuu, yaani chugachugia, nilitia akili siku hiyo, dunia yote niliona kama inakwenda upande upande, nami nikaifatisha.

Kumbe walio niona siku ile wakastaajabu, wakapatwa na mpagao, mtu mfupi mie kwa jinsi nilivyokuwa nikitembea, kama mtu mwenye milonjo, maana si kwa miondoko ile ya mikogo.

Wakaja kuniuliza, siku ya pili yake, kumbe nilivyokuwa naangaika na andasi kichwani, na mwendo nikabadirisha, nikihisi barabara zimeinamia upande mmoja wa kushoto, nami ili nisidondoke nikajikuta natembea kuinamia upande wa kuume, natembea kama mtu aliyepigwa dafurao na lori la Jay Fong la mwaka 74.

Nilikuwa natembea kama Kaa au Ngadu, yaani nikitembea upande upande, siku hiyo niliongea lugha zote za Kihindi, Kibengali, Kigujarati, Kitelugu, Kiurdu, mpaka Kibanyani nilikijua siku hiyo... Kudadeki.

Hata nyumbani sikumbuki nilifikaje, nilijikuta tu nimepitiliza mpaka uwani, huku nimeshika kibatari nilichokiwasha, tena ni saa kumi jioni, mie naona giza.

Siku hiyo nilitapika mpaka nyongo... Nikanyororeka kama Kinyonga aliyelishwa ugoro... 

Kuanzia siku hiyo nilikoma, sikutia mdomoni si Tambuu wala Kubeli au nduguye Pariki...

Friday, 2 December 2022

NILISHIKWA KWA TUHUMA ZA KUSAFIRISHA MADAWA YA KULEVYA.

Nilipo Ruhusiwa tu, Breki ya Kwanza Ilikuwa Maliwatoni...

Nipo Ndani ya Ndege, Aina ya Airbus, Tumehabiri Watu Wengi Sana, Hii ni Moja Kati ya Ndege Kubwa Sana za Abiria, Ndege Inamilikiwa na Shirika la Ndege la Falme za Kiarabu la Imarati (Emirates).

Nikitokea zangu ughaibuni moja kati ya nchi za Ulaya, naelekea zangu Afrika Mashariki kwa likizo fupi.

Nitakaa Dubai kwa siku kama tatu hivi, kisha baada ya hapo nitaunganisha ndege kuelekea kwenye nchi ambayo ndio kuna kitovu changu.

Ndio kwanza nimemaliza kuweka mzigo wangu kwenye Saraka (Dambra) ya kwenye ndege.

Kitu ambacho binafsi sikipendi sana na hii ni kwa sababu ya kimo changu, maana mimi si mrefu wa sifa wala si mfupi wa kuchusha.

Ghafla nikashikwa bega la kushoto, mshiko ule uliandamana na sauti kavu kidogo, ya mwanamke wa Kiafrika, mtu mzima, amekonga kiasi chake, kwa haraka haraka, nikakadiria umri wake, anapata miaka 60 au 65 hivi. Na kwa ile rafudhi yake, nikahisi kuwa anatokea Afrika Magharibi, na kama sikosei atakuwa tu ni Mpopo na kama si Mnaijeria basi ni Mghana.

Akaniomba nimsaidie kuweka begi lake kwenye saraka, yaani sehemu ya juu ya kuhifadhia mizigo.

Lakini ghafla kabla sijainama kuchukua mzigo wa yule bibi, mtu mmoja mrefu kiasi aliyekaa karibu nasi akajitokeza na kumsaidia yule mama mtu mzima.

Kila mtu akakaa kwenye kiti chake, wakati tupo angani, yule bibi akaanzisha mazungumzo. Alikuwa ni mzungumzaji mzuri, mwenye kujua mengi.

Nami kama kawaida yangu, napenda mazungumzo na haswa ninapogundua ninaweza kuelimika kwa namna moja au nyingine.

Tuliongea wakati wote, kiasi cha kuifanya safari ya saa tisa ya kwenda Dubai kuhisi imekuwa fupi sana.

Mara, sauti ya rubani ikasikikia kupitia kipaza sauti akitangaza kwamba tumeingia kwenye anga ya Dubai na muda si mrefu ndege itatua kwenye kiwanja cha ndege cha Dubai.

Ghafla yule bibi ambaye amefanya urafiki nami akanza kulalamika maumivu ya tumbo.

Nami kwa uungwana niliokua nao nikiongozwa na moyo wangu uliojaa huruma kwa yule ajuza, nilibonyeza kitufe cha msaada, na muhudumu wa kwenye ndege akaja kutusikiliza, akataka kujua shida ni nini.

Nikamwambia kuwa jirani yangu hakuwa anajisikia vizuri.

Lakini cha ajabu yule bibi, ghafla alianza kuniita mimi kuwa ni kijana wake (My son, my son...), na uku akiwa amenikamata mkono, hakutaka kuniachia.

Msimamizi akaniambia kuwa hakuna kitu wangeweza kufanya zaidi ya kumpa dawa za kupunguza maumivu na tusubiri hadi tutakapotua.

Yule muhudumu akamtaarifu rubani, naye rubani akatangaza kwamba tumepatwa na dharura ya mgonwa ndani ya ndege na akatushauri sote tutulie na tusiwe na wasiwasi kwani yule mgonjwa atahudumiwa.

Yule bibi alikuwa akilia na kutokwa na jasho kama vile aliyemwagiwa ndoo nzima ya maji.

Nikajaribu kuuachanisha mkono wake na wangu, lakini yule bibi alikataa kuniachia mkono wangu... Kila mtu alidhani kuwa mimi na yule bibi wa Kipopo ni mtu na mwanae.

Ndege ilipokwisha tua na kusimama, yule kijana aliyesaidia kuweka mzigo wa yule bibi kwenye Saraka, aliondoa mzigo wake, kisha akasaidia tena kushusha sanduku la Bibi Mpopo na kuliweka kwenye kiti.

Yule jamaa kabla ya kuondoka alininong’oneza kwa kunishauri nijitenge mbali na huyu bibi na niwaambie wahudumu wa ndani ya ndege kuwa mimi na yule bibi hatukusafiri pamoja.

Wafanyikazi wa kwenye ndege waliniuliza kama tuna uhusiano na bibi yule, niliwaambia kuwa tumekutana kwenye ndege. Sikumjua kabisa kabla...

Wakati naondoka nikamuaga na kumtakia kila la kheri, lakini yule bibi aliniomba nimsaidie kumbebea mkoba wake.

Lakini yule jamaa aliyemsaidia kuuweka mzigo kwenye saraka ya kwenye ndege aliniangalia, tukatazamana machoni, nikamuona akitikisa kichwa kwa msisitizo. Nikamuelewa!

Tukawaachia wahudumu wamsaidie.

Basi mimi na abiria wengine tukatoka ndani ya ndege na kumwacha bibi wa Kipopo anasubiri kiti cha magurudumu.

Nashuru niliweza kujikongoa kutoka kwa yule bibi, baada ya waudumu kufika na kumsaidia mizigo yake na yeye akawekwa kwenye kiti cha matairi.

Tulipokuwa tukingoja mizigo yetu, tukasikia sauti kali ikiamuru "... Stop, Stop! You are Under Arrest...!"

Nageuka kuangalia kumbe anayeambiwa asimame na kuwa amewekwa chini ya ulinzi ni yule bibi wa Kipopo alikuwa akikimbia, akijaribu kuwatoroka Askari na wafanyakazi wa kwenye ndege.

Kumbe walipo mshusha tu, tumbo lilipona ghafla na mara moja na akasimama na kuanza kukimbia uku akimuachia mkoba mmoja wa wafanyakazi wa kwenye ndege, na kukimbia kuelekea nje...!

Kwa bahati nzuri polisi wa uwanja wa ndege walikuwa na kasi kuliko yeye. Walimshika na kumrudisha uku wamemvisha pingu za mikono.

Bibi wa Kipopo bila haya wala soni usoni akaanza kuniita tena... "My son... My son, ooh! How could you do this to me, ooh...!"

Mwanangu ... Mwanangu! Unawezaje kunifanyia hivi...!

Ndio sasa nikaelewa na fahamu kunirudia uzuri, kumbe bibi alikuwa amebeba dawa za kulevya na alikuwa akijaribu kunihusisha na mimi, ili yeye apate upenyo wa kutoroka!

Kwa bahati nzuri, yule bwana ambaye alikuwa amemsaidia kushusha mzigo wake toka kwenye saraka, alijitokeza na kuwaambia polisi wa uwanja wa ndege kuwa mimi na yeye (Bibi wa Kipopo) tumekutana tu kwenye ndege.

Polisi walichukua pasipoti yangu na kumwuliza yule bibi ataje majina yangu kamili ikiwa ni kweli mimi ni mwanae na tulikuwa tukisafiri pamoja.

Kwa neema ya Mungu, sikuwa nimemwambia hata jina langu la kwanza, bibi wa Kipopo akabakia tu anag’aa ng’aa macho! Uku akiendelea tu kusema "...he is my son, ...he is my son, ooh!"

Hata hivyo Polisi wakanitaka nifuatane nao kwenye chumba kidogo ambapo nilihojiwa sana.

"Nilikutana naye wapi? ...Nilipanda wapi...? Huyo bibi alipanda wapi...!?" Na maswali mengine mengi ya kimtego.

Na mizigo yangu yote ilipekuliwa na kuchambuliwa sana, wakachukua alama za vidole vyangu ili wakaangalie kama nilisha wahi kukamatwa...!

Taarifa za kipolisi zilipokuja, alama zangu za vidole hazikupatikana popote, si kwenye mizigo ya yule bibi wala kwenye kazidata za Kipolisi!

Niliruhusiwa kuondoa baada ya takribani saa tatu za mahojiano, maana hata mwenyeji wangu alisha anza kukata tamaa.

Hakuna siku nilijawa na hofu kama hii siku, na haswa kama ujazoea maswala ya kukamatwa na polisi, tena basi nikiwa nchi ngeni, nchi ambayo kesi za dawa za kulevya hukumu yake ni kifungo cha muda mrefu kama si cha maisha, kwa kweli nilichanganyikiwa...

Nilipo ruhusiwa tu, breki ya kwanza ilikuwa ni maliwatoni, uko niliharisha kweli kweli, nadhani ni ule woga na fikra zilizonizonga kuwa sasa ndio basi tena, naiwacha dunia kizembe...!

Tangia siku ile nikajifunza jambo moja, la kutogusa mzigo wa mtu yoyote yule. Labda mzigo uwe wa familia yangu na nimeupakia na kuufunga mwenyewe... 

Zaidi ya hapo hata sijali, tena nimeapa kabisa, Haki ya Mungu tena, sikusaidii, nimekukuta uwanja wa ndege na mizigo yako hata ikiwa unayo mizigo iliyo kuelemea au umekongeka ukakongoroka utaibeba na kuishughulikia wewe mwenyewe.

Sitakupa hata toroli ya kuweka mzigo wako!

Mizigo yako... shida yako... Hiyo ndio sera yangu mpya safarini.

Na kama ni ndani ya ndege na ikiwa huwezi kuifikia sehemu ya kuwekea mizigo, kwenye saraka, na ikatokea kuwa mimi ndiye mtu wa karibu zaidi, nitakachoweza kukusaidia ni kukuambia umwite muhudumu wa kwenye ndege akusaidie...!

Maana Nazi Mbovu Harabu ya Nzima.

Nawatakia Wasafiri, Safari Njema...!

Tuesday, 29 November 2022

NILIKESHA NIKIMTAFUTA
Tukio Linalo Fanana na Ukweli!

Alhamdulillah Ndio Neno Nitakalo Lirudisha Kwa Mola Wangu Siku Zote Katika Uhai Wangu Ila Sintoweza Kumsahau Binaadamu Kwa Ukatili Wake...!

Siku ya Jumanne majira ya saa mbili na nusu usiku nikiwa msikitini nikimalizia swala ya isha simu yangu ikiwa katika kimemeshi iliita mara nyingi sana, huwa sina kawaida ya kupaparika ninapokuwa mbele ya Mola wangu...!

Alhamdulillah baada ya swala nilitazama simu nakuona nimekosa miito kadhaa kutoka kwa dereva wa madrassa anae mchukua mtoto wangu na kumrudisha nyumbani siku za masomo... ilikuwa yapata saa tatu hivi usiku...!

Nilishtuka kidogo nakuhisi labda kuna tatizo barabarani nikampigia kwa haraka... Swali la kwanza alilo niuliza... Leo umekuja mwenyewe kumchukua mtoto wako madrassa...!?

Nikiwa katika mshituko nilimwambia siwezi kufanya hivyo bila kutoa taarifa... Basi sheikh tupo hapa karibu saa nzima mwanao hatumuoni, na hivi sasa ni saa tatu usiku...! (Kwa kawaida huwa wanatoka saa Mbili Usiku baada ya Swala ya Isha)

Niliharakisha kwenda nyumbani na kuchukua usafiri kwa haraka na kuelekea madrassa kwake maeneo ya karibu na Vijana Mwananyamala... Kufika nakuta waalimu na walezi wote katika taharuki na kusikitika...!

Nikiwa ni mzazi nilipiga moyo konde na kutaka kujua kulikoni, maelezo yalionyesha kuwa kuna magari binafsi yanayo kuja kuwafuata watoto na yale ya madrassa walio ingia mkataba. Hisia zikaja pengine kwa utoto atakuwa amepanda gari inayokwenda njia tofauti na nyumbani...!

Basi ikawa ni kutafuta namba za simu za wazazi kuwauliza watoto wao kama walikuwa na mwanangu kwenye magari yao na majibu yalirudi yale yale kuwa hapana hatukuwa nae...!

Hapo ilikuwa yapata saa nne na nusu usiku nikiwa katika kuomba dua na kumdhukuru Allah kila wasi wasi unapo itawala nafsi yangu...!

Baada ya hapo tukapata hisia pengine wakati wa kuruhusiwa yeye hakupanda gari yoyote badala yake amefuatana na watoto wanaoishi karibu, wale wanao kwenda kwa kutembea makwao hivyo akapoteza mwelekeo asijue anapo kwenda kwa udogo wake...!

Mimi na mwalimu wake tukaamua kuongozana pamoja na tulitembea mpaka kituo kidogo cha polisi Garden pale Mkwajuni na kuulizia kama wamepata taarifa yoyote ya mtoto aliyepotea jibu lilikuwa hapana. Na askari aliyepo zamu akatuambia kuwa taarifa ya kupotelea kwa mtoto inapaswa itolewe baada saa 24 tangia kupotea.

Subhanallah mtoto mwenyewe ndio kwanza ana miaka minne, nikiwa katika mawazo masaa 24 kwa mtoto wa miaka minne, nikachoka kabisa. Nilicho amua kufanya ni kumwachia nambari zangu za simu askari wa zamu, ili kama kutakuja taarifa yoyote apate kunifahamisha.

Tukarudi madrassa na kuchukua usafiri na kuelekea kituo kingine kidogo cha polisi maeneo ya Mwinjuma ili kuwapa namba zangu kwa taarifa yoyote itakayo patikana.

Baada ya kutoka Mwinjuma, tukaamua kupita njia za ndani ndani huku nikitazama huku na kule, kila mtoto niliemuona, nilihisi anafanana na mwanangu, nasimama kuangalia kama ndie au lah.

Hatimae tukafika sehemu tukakuta mkusanyiko wa watu, nikiwa na ghamu nikawauliza nikiwa sina uhakika wa jibu nitakalopata.

Ajabu wakanambia kuna mtoto katangazwa kapotea yupo msikitni, kwa Makunganya...!

Tukatoka mbio mbio huku nimekunja kanzu yangu, makubazi mkononi kuelekea uko msikitini, uku nikiomba dua za kila aina nilizozikumbuka. Kufika tukafanikiwa kumuona kiongozi wa Msikiti, mtu wa makamu hivi, anafika miaka 50 kwa uchache, huku nikiwa na shauku ya taarifa ya mtoto wangu. Nikamuuliza kuhusiana na huyo mtoto alopotea.

Kiongozi yule akanijibu kuwa ni kweli kuna mtoto wa kike darasani la pili kapotea, umri wake unakadiriwa miaka nane mpaka kumi hivi.

Niliishiwa nguvu nakulazimika kuendelea na safari ya kurudi Mwinjuma...!

Tulipofika kituoni majibu niliyoyapata hapo ni yale yale tu, kuwa tusubiri saa 24 ndio tutoe taarifa rasmi ya kupotelewa na mtoto. Hivyo na hapo kituoni nikaacha namba zangu na kuelekea kituo kingine kidogo cha polisi pale Mtambani.

Baadaa ya kuzunguka vituo kadhaa vidogo vya polisi, vilivyo jirani nikakata shauri kwenda kituo kikubwa cha Oysterbay kutoa taarifa na kujua kama wana habari yoyote ya mtoto alopotea. Baada ya kumaliza maelezo yangu, askari alokuwa zamu akachukua Simu ya Upepo (Radio Call) ili kuwapa taarifa askari waliopo katika doria, kama watapata kumuona mtoto mwenye umri wa miaka minne akitangatanga mitaani wapate kumchukua na kumuifadhi.

Majibishano ya radio ya kituo na walioko doria yakanifahamisha kuwa, kuna operesheni maalum ilikuwa inafanyika usiku ule, na ili tatizo langu lishughulikiwe na askari walioko nje, itabidi kwanza wamalize operation zao kisha ndio watashughulika na tatizo langu.

Kwa kweli nilikuwa nimechanganyikiwa haswa, nikashindwa hata namna ya kufikiri. Ukizingatia kuwa muda umekwenda, kiasi ni saa tisa kasoro usiku.

Ghafla simu yangu ikawa inaita namba ilikuwa ngeni, baada ya kuipokea nikawa naiangalia kama vile kitu cha ajabu. Nataka kuipokea tu, ikakata.

Naangalia vizuri, betri ya simu inakaribia kumalizika, kiasi imebakiza asilimia 10% tu...!

Mara simu ikaita tena, nikaipokea kwa haraka sana na kuelekeza sikioni, kiasi nikajipiga na simu sikioni, na simu kuniponyoka, nikaiokota kwa haraka na kuilekeza sikioni tena, na kuita kwa sauti ya kitetemeshi.

Haloo, baba fulani hapa naongea, nikajitambulisha, sauti ya upande wa pili ikanitaka niende kituo cha Mwinjuma kuna taarifa muhimu inanihusu.

Moyo ukaongeza kasi mara dufu, kiasi cha pumzi kunipaa nikahisi kizunguzungu kwa mbaaali. Nikajikaza kiume nikamfahamisha askari wa pale Oyterbay kuwa nakwenda kituo kidogo pale Mwinjuma.

Baada ya kumwachia nambari zangu za simu, nilitoka mbio nikamsahau hata niliye enda naye pale kituoni, mbio mbio mpaka kituoni, Mwinjuma...!

Nimefika nikihema pumzi juu juu, kama Wibari alokoswakoswa na mbwa wa msasi , Alhamdulillah nilimkuta tayari mkuu wa madrassa na waalimu wengine nao wapo pale, baada ya kungojea kidogo askari wa zamu, aliniita na kuniambia niende upande wa pili. Nikakuta watu kama wa familia moja wanaume wawili na wanawake wawili mmoja kampakata mtoto, kumwangalia vizuri nakumuona mwanangu pembeni...!

Allah Akbar, hakika moyo wangu ulikuwa katika furaha na michirizi ya machozi katika mashavu yangu nikamnyakuwa mwanangu na kumkumbatia kwa furaha, uku namuuliza kwa upole.

Ulikuwa umeenda wapi Arhaan wangu...? Akanijibu kuwa alienda kutembea na rafiki yake...!

Nilitoa shukran zangu nyingi kwa hao wasamaria wema na kisha nikawauliza ni wapi walikompatia mtoto wangu?

Wakanambia wamemkuta sehemu inaitwa Mchangani mbali sana na madrassa kwake na walijaribu kupita nae katika madrassa nyingine kuuliza kama wanamjua walipo kosa ndio wakaamua kumleta kituoni hapo...!

Nikatoa pesa kiasi cha elfu kumi kumi mbili, ili niwape kama ahsante yangu kwao, uku nikiwaambia kuwa japo si hela nyingi, lakini niliomba wazipokee kama shukran na usumbufu walioupata.

Mmoja kati yao akanikatalia kata kata, na kunambia walicho kifanya ni wajibu wao kama wazazi, na tatizo halina mmoja, leo mimi kesho hata wao wanaweza kupata tatizo na wanatarajia wema kutoka kwa yeyote yule.

Uku machozi yakinilenga lenga, nikawashukuru sana watu wale, kisha nilimchukua binti yangu ili kurudi nae nyumbani.

Baada ya kupeana pole na waalimu wake waliohangaika kutembea mtaani usiku ule huku na kule kumtafuta hatimae tumefika nyumbani yapata saa kumi alfajiri, hoi bin taaban.

Baada ya kumuuogesha na kumpa chai tukiwa katika kumuhoji taratibu mimi na mama yake alisema kuwa alikuwa na rafiki yake anaitwa Mwajuma walitoka pamoja ni marika sawa ila huyo anaishi karibu sana na huwa anarudi kwao kwa kutembea tu.

Akaendelea kutufahamisha kuwa walipo fika kwa kina Mwajuma, waliingia ndani ila babake na Mwajuma akamwambia atoke arudi uko Madrassa.

Hebu fikiria ndugu yangu ni wazazi wa aina gani hao... Walioshindwa hata kumuuliza mtoto jina la mzazi au hata nambari za simu!?

Mbaya zaidi walipigiwa simu mwanzo kabisa, tulimpigia mama yake na Mwajuma, akawa hapokei simu, ikawa inaita tu, kisha tukampigia mumewe alipo pokea alisema kuwa hana taarifa yoyote ile kuhusu mtoto wangu.

Hakika binaadamu ni viumbe wa ajabu na katili waso na huruma, binafsi nimesamehe ila sinto sahau somo walilo nipatia usku ule...!

Nikiwa natafakari hali ya usiku ule, nikawa najiwazia tu, vipi kama angelikwenda kwenye barabara kubwa yenye magari mengi na ahadi ikatimia, si wangekuja kujuta au mioyo yao ishaingia kutu, kiasi hawana tena huruma kwa watoto wa wenzao?

Nikaamua tu kumshukuru MwenyeziMungu, mtoto wangu kapatikana salama usalmini...! Nikakatizwa na sauti ya Mwazini ikitukumbusha kuwa muda wa sala ya alfajir umetimu.

Nikanyanyuka zangu taratibu, kuelekea msikitini kutimiza wajibu wangu kwa Mola wangu...!

Alhamdulillah... Ndio neno langu la leo na mpaka kesho kwa Mola wangu...!

Friday, 11 November 2022

 BIRIKA BATI, KIKOMBE BATI,
NA HATUKUKOMA.

Hivi wakulaumiwa walikuwa watengenezaji au wanunuaji au watumiaji!?

Yaani hata sielewi, vikombe gani vinaunguza namna ile? Au walikuwa wanatukomesha tukivunja vikombe vya udongo!?

Halafu kikombe cha chai, ila kinapicha ya nyanya. Sikuvipenda, sivipendi, sitavipenda.

Na kwa nini nivipende, uwenda hivi vikombe ndio vimetukomaza midomo tukiwa bado makinda.

Nahisi ndio maana Watanzania tumekuwa watu wa kupiga sana stori... Sasa wewe fikiria chai ya moto, kuiwacha huwezi, hapo sasa ni stori tu, kumbe janja yako unavizia ipowe, hapo ni stori plus umbea na mikingamo.

Basi nikwambie, siku hiyo nikamtembelea binamu yangu wa kike maeneo ya Magomeni, nikitokea zangu maeneo ya Gerezani, Kariakoo, chini nimevalia viatu vyangu vya Kung Fu shuzi, medini Chaina. Shati langu la Juliana, picha ya ndege, kubwa kiasi na chini nimevalia suruali yangu ya kodrai.

Mtu mimi na ufupi huu, ukiniona kwa mbali, utafikiria nguo zatembea zenyewe. Huyoo kiguu na njia, nikakatiza zangu Jangwani, na jua lile la saa tisa alasili. Kufika home kwake, kanikaribisha uwani, nyumba nzima yupo peke yake, wapangaji wapo mitaani, awajarudi bado.

Kanikaribisha kwenye Kigoda, baada ya salamu na kujuliana hali akanikaribisha chai ya mkandaa, akanitilia kwenye kombe la bati, chai imekolea viungo, inawasha kwa karafuu na tangawizi, ikakolezwa na pilipili mtama, chai kama uji wa mgonjwa na mie ujanja ikawa ni kupiga stori za kupoza chai, fu fu fuuu, nyiingi!

Japo tupo uwani, lakini joto la saa tisa, jiji Dar nalo halikuniwacha, utafikiri nimemwagiwa maji, mara akanyanyuka na kuniita niende chumbani kwake...!

"Binamu njoo chumbani nikuonyeshe mambo, ila nakuonya usimwambie mtu..."

Ghafla nikajikuta nameza mate machungu, nahisi nilitaka kutema nyongo, ikaishia kohoni, chai kidogo inipalie, nilajikuta naimeza bila kujua kuwa naunguza kolomeo.

Nami bila ajizi nikajikuta nipo chumbani, hata sijui nimefikaje, maana fahamu zikikuwa zinaingia na kutoka...

Hakuna pa kukaa ila kwenye kitanda, mwenyewe katandika mashuka yake ya kufuma kwa mkono, maua ya rozi (mawaridi), kafanya seti kamili, mapazia ya dirishani na mlangoni. Vingine kafunikia radio yake, kaseti aina ya National na kitambaa kingine kakitandika kwenye meza.

Pembeni ya chumba kuna mtungi wa maji, umefunikwa na sahani ya bati na kata yake imewekwa pembeni kidogo, picha za wanamuziki wa Boney M na ABBA group zilizokatwa kutoka kwenye magazeti ya Sunday News zimebandikwa ukutani, pamoja na picha ya Buraku, kafanana na mwanamke wa Kihindi.

Kwenye meza kuna viboksi viwili vitupu vya sabauni ya Lux na lifebuoy pamoja na kibox cha dawa ya kusugulia meno ya Colgate. Pembeni kidogo, kuna kabati la vyombo lenye wavu, na kabati la nguo lenye kioo.

"Kaa basi hapo we nawe wima wima tu, kama mgambo wa site" sauti yake ikakatiza mawazo yangu yaliokwenda mbali ya hapo, maana mawazo yalikuwa mbingu ya sabaaa nacheka na kufurahi na malaika wa peponi.

Nikakaa kitandani, moyo unakwenda kasi kama wa Mbayuwayu... Akanitazama kisha akanambia, huku kaweka umakini usoni, yaani yupo siriasi kabisa... "binamu hii iwe siri yetu, ukimwambia mtu, mi na wewe basi tena sitakushirikisha kwenye mambo mazuri haya."

Nikahisi masikio ghafla yamenisimama wima kama mbwa wa msasi kaona windo, nikanyoosha na shingo kama Njiwa Manga...

 Nikahitikia kwa kutingisha kichwa, akanambia "Apiya binamu, kuwa hutotoa siri, sema Hakiyamngu..." nikajikuta natamka, kwa kigugumizi, kilicho nikamata, hata kilipotokea sijui...

"Ha-ki ya M-ngu tttena, si-si-mwambii m-mtu mi mi-ye, Waalaahi Nakuapia, mmmh na mchanga huu naramba." Huku nikiinama na kwa kutumia kidole cha shahada, nikapangusa sakafu na kuramba...

Moyo ukaongeza kasi kama garimoshi la Mjerumani kwenye vita kuu ya kwanza ya dunia sanjari na tumbo likapata kusema, gruuuh.

Akanitazama kisha akanambia: "Haya mie nakuamini voo binamu yangu, najuwa we mambo yako ya kizungu, ndio mana nakupendaga..." Akatamka huku anaelekea kabatini kwake na kufungua kabati...

Hamadi, katoa doti tatu za vitenge vya wax na kuvirembea pale nilipo kaa, kitandani. Enzi hizo tukuvihita vitenge vya Burundi.

"Nimeletewa jana na shemejio..." Sauti yake ikaanikiza pale chumbani.

Nikamuuliza, Mmm! Shemeji yupi huyo...!? Yule mjeshi wa Ngerengere!?

Akanijibu: "Uwachi na wewe, wa Ngerengere wapi!? Yule nishamtosa siku nyingi... Huyu humjuhi wewe, mwenyewe anafanyakazi bandarini, hivyo vitenge vya Magamu (Magendo), vilikuwa vinapelekwa Burundi kontena nzima, yeye ndio kavinyakua hivi vitatu, kaniletea nimuuzie."

"Kimoja shilingi 25, ila kwa wewe binamu yangu, nitakuuzia kwa shilingi 22, na wewe ukauze upate faida japo kidogo."

Nikamtazama, kisha nikapiga fundo moja la chai ya moto, yaani hata sikuhisi kuunguzwa, hiyo midomo na koromeo nilikuja kuhisi nimebabuka, usiku wake nisharudi nyumbani.

Ghafla nikajihisi kama biskuti ndani ya chai ya moto au kiowevu, nikawaza mfukoni nina shilingi Moja ya Mwenge na sumni tu ile ya sungura...

Enewi, yalikuwa tu maisha yenye changamoto zake, furaha, uzuni, vicheko vyote vilikamilisha uhalisia wa maisha yetu, hatukuacha kutembeleana, japo bidhaa muhimu zilikuwa adimu... kula kwa kaya...


😉🤭🤣

Tuesday, 8 November 2022

LIKIZO YANGU, JIJINI DSM (DIZIM)

Na Kumbukumbu Iliyopotea

Nilipokuwa likizo jijini Dar es salaam, nikajikuta tu nimepata hamu ya katembelea kwa miguu, mitaa ya Gerezani, Kariakoo. Nikapitapita mitaa iliyosongamana watu wa kila aina, nikakumbuka kufuchama Rununu yangu, kwa kuchelea wivi, wasijeichukua bila ruhusa yangu, huku sauti za wabeba mizigo wakiyosayosa maneno ya kutiana nguvu, nikapishana na wenyeji wachache sana, wakihisabika kwa vidole vya mkono, wengi wao ni wageni.

Huyo nikayoyomeka zangu, nikajikuta natokea mtaa wa Nkrumah, taratibu nikashuka zangu mwelekeo wa Mnara wa saa, nikatupa macho upande wa kushoto nikasoma kibao, kilichofubaa kwa rangi baada ya kutelekezwa miaka dahari, neno NEW CHOX bado likisomeka, kumbukumbu ikarejea miaka mingi nyuma, nikatabasamu sanjari na kusikitika, maana umuhimu wa jengo hilo kwa sasa haupo tena, nani anakwenda sinema siku hizi!?

Hata ile hoteli ya Continental sina uhakika kama bado inatoa huduma, nakumbuka tulikuwa tukienda kucheza Disco na vijana wenzangu.

Nikakumbuka hata wale wakaazi wa vitongojini, nao hawakuachwa nyuma, serikali iliwafungulia vituo vya burudani vya kijamii, kwa wakazi wa jiji la Dar, watakuwa wanakumbuka majumba ya DDC, kama vile Amana Social Hall, DDC Kariakoo, Keko na pale Magomeni.

Pale Ilala awali ilikuwa pia ni mahali ambapo wengi wakienda kungalia sinema siku za mwisho wa wiki na siku za sikukuu. Kiufupi majumba haya ya jamii, yalikuwa nchi nzima.

Nikakumbuka kuna jumba moja lilikuja mwishoni, katika miaka ya 80, jumba ambalo ndio lilikuwa jumba lenye uwezo wa kuingiza watu wengi sana, likijulikana kwa jina la Star Light Cinema.

Kiukweli hii ni kumbukumbu nzuri na ya kuuzunisha, maana enzi hizo kweli ilikuwa jambo la tunu sana kwa mtoto au hata mtu mzima kupelekwa sinema.

Kwanza halikuwa jambo rahisi kwa mtu tu asiye na ubavu kupata tiketi, haswa filamu ikiwa ni mpya na waigizaji wakiwa ni maarufu.

Nakumbuka walanguzi wa tikiti za sinema, vijana kwa watu wazima, wenye nguvu zao, wengi wao weshatangulia mbele za haki, walikuwa wakimaliza kulangua pale New Chox sinema, walikuwa wakikimbilia Avalon sinema, alafu sasa pale kidirishani, tikiti zilikuwa zikiuzwa nusu, kisha zilizobakia wale Wahindi wakiwapa watu wao na kuziuza kwa bei ya juu.

Nikajikuta natabasamu, kumbukumbu iliyokuja baada ya hapo, nikatamani kucheka, maana siku hiyo pale Chox niliwahi kidirishani kabla ya dirisha la kununulia tikiti halijafunguliwa, nikajuwa leo napata tikiti tena zile siti za nyuma kabisa, kama si mstari A basi D.

Ghafla lango likafunguliwa kuruhusu watu waingie kununua tikikiti, sanjari na dirisha la kuuzia tikiti, hamadi nikajikuta hewani kama Sapatu, nimepigwa kibega kimoja tu, nikajikuta nimetupwa huko karibia na vyoo, chali kama mtoto wa Komba kaanguka mtini.

Nikajizoazoa zangu, nikabakia nimetumbua zangu macho kama mtu aliyekabwa na nguto, kumeza siwezi wala kutema ziwezi. 

Enewei, pale jumba la sinema la Empire nako wakimaliza kuuza, walikuwa wakienda zao Empress, Ila jumba ambalo vijana wengi wakilipenda ni jumba la Empire kwa sababu walikuwa wakionyesha sinema nyingi za hollywood, na waendeshaji walikuwa na tabia ya kuongeza sauti haswa wakati wa mapigano, ili kuwakoleza watizamaji.

Majumba ya Cameo (Mtaa wa Jamhuri,) na Odeon (Mtaa wa Zaramo na Jamhuri) haswa yalikuwa maarufu kwa sinema za Kihindi, wakifuatiwa na New Chox Cinema (Mtaa wa Nkuruma) na Avalon (Mtaa wa Zanaki) na Empress (Mtaa wa Samora) alafu ndio Empire (Mtaa wa Azikiwe). 

Kule Msasani, kulikuwa na jumba la sinema, likitwa Drive-Inn, wakiingia na magari yao, ila wakazi wa Msasani wengi walikuwa wakijazana nje ya ukuta na kutazama sinema, japokuwa hawakuweza kusikia sauti lakini wengi wakiridhika na hiyo hali.

Drive-Inn-Cinema
Drive-Inn Cinema

Nakumbuka kumtembelea Marehemu, ndugu yake na baba, mitaa ya Msasani, sasa ndugu yangu mmoja (yeye ni mkubwa kuliko mimi, naye pia ni marehemu), akanipa ofa bubu ya kwenda kutazama sinema, ah ah ah ah, akanipeleka Drive inn, kufika tukakaa nje ya ukuta na kununu zetu karanga na maji ya sharubati, tukatafuta tofali na box chakavu kisha tukaa kuangalia movie, tukisumbuliwa na mbu hapa na pale.

Sikumwambia kitu maana nilikuwa nikimuheshimu, mwenyewe nilishazoe kwenye majumba yetu ya kawaida, kama ukishindwa kununua tikiti basi unafanya kila njia kupenya au unampa pesa kidogo mwangalizi wa tikiti na kukuingiza ndani, ila kama jumba limejaa, basi unakaa kwenye ngazi za kutokea nje... Ah ah ah ah, ama kweli siku hazigandi.

Vijana wa leo wanaweza kushangaa wakisikia kuwa hata wimbo wa Taifa ulikuwa ukipigwa kabla ya onyesho, ila baadae sana ikaja kuondolewa kwa sababu ilisemekana kuwa hakukuwa na heshima, sababu wengine walikuwa ni walevi na hawakuwa wakisimama wima pale wimbo wa Taifa unapopigwa.

Hii biashara ya sinema ilikuja kuanza kudorora vilipoanza vituo vya Runinga na kushamili kwa biashara ya kuazimana kanda za video, na maktaba za kukodisha kanda za video, hizo zilikuwa enzi za Mzee Ruhsa. 

Wengi walikuja kupendelea kukodisha kanda za video kuliko kwenda kwenye majumba ya sinema kwa sababu kwanza ilikuwa ghali kwa mtu mwenye familia, kugharamia watu zaidi ya wanne, pili filamu zenyewe nyingi zilikuwa baadae zikirudiwa rudiwa, nadhani shirika la filamu Tanzania lilikuja kufirisika na kushindwa tena kuagiza filamu mpya.

Haya majumba ya sinema, siku za mwisho mwisho walikuwa wakionyesha filamu mbili mpaka tatu kwa malipo ya kutazama filam moja, yaani ilikuwa ni kukesha, maana zilikuwa zikianza usiku.

Nakumbuka filam moja ya kihindi ilitamba sana katikati ya miaka ya 70 na mwanzoni mwa miaka ya 80, filam yenyewe ilitoka mwaka 1975. Ilitwa Sholay, hii filam Wahindi wa bongo walichapisha mpaka fulana zake na kuziuza!

Monday, 7 November 2022

WANAWAKE NA DAWA YA MAPENZI

Visa na Vituko Mitaani.

Nakumbuka Mwishoni Mwishoni Mwa Miaka ile ya 1980, Nilibahatika Kutembelea Mkoa wa Tabora, Mara tu Nilipopata Likizo Yangu ya Mwaka.

Baada ya safari ya siku mbili kwa Garimoshi kutokea Dar es Salaam, hatimae tukawasili mjini Tabora mida ya jioni na nikapokelewa na mwenyeji wangu na kuelekea nyumbani kwake, maeneo ya Igurubi wilayani Igunga.

Nyumba ilikuwa kubwa na mmoja wa Wapangaji alikuwa ni Mjombaake na Mwenyeji wangu, ambaye alikuwa ni Mganga wa Kienyeji aliyekuwa amepanga uwani, na alikuwa kiasi maarufu sana haswa kwa kina mama wanaotafuta dawa za mapenzi na mazindiko mbalimbali.

Nakumbuka kuna kipindi alipata mteja, mama mmoja wa Kinyamwezi. Huyo mwanamke inavyo onyesha alikua akiangaika sana kwa waganga wa kienyeji kutafuta dawa ya mapenzi ili kumtuliza mume wake.

Mwenyewe anadai kuwa mume wake alikua ni mtu wa kubadilisha vimada (siu hizi mnaita michepuko) kila siku.

Siku moja shoga yake alimwambia kuwa kuna mganga mmoja uko maeneo ya Igurubi wilayani Igunga, aende uwenda akafanikiwa shida yake. Huyo mama alikuwa anaishi maeneo ya Kaloleli uko Sikonge.

Siku ikafika akaamua kwenda kwa huyo mganga, maana huyo mganga kama nilivyo eleza tukiishi nae nyumba moja.

Kama ilivyo ada kwa mganga ukosi neno wala ukosi dawa, mganga alimpa yule mama madawa ya kila aina bila mafanikio yoyote yale.

Siku zikapita mganga nae akaona sasa hii ni shida, akimwambia yule mwanamke kuwa ameshindwa ni kujidhalilisha na wateja wanaweza kumkimbia.

Mganga akawa anafikiria amwambie masharti yepi ili bibie ashindwe na asimsumbue tena kumtafutia madawa.

Siku alipokuja tena yule mganga akamwambia amletee Nyoka aina ya Koboko ili amtengenezee dawa. Kama mnavyojua Tabora nyoka ndio kwao na haswa hao Koboko ni hatari sana kwa sumu yao.

Yule mganga akiwa na hakika kabisa yule mwanamama hawezi kumkamata huyo nyoka mwenye sifa ya ukali wa sumu na wepesi wa kugonga watu.

Basi yule bibie akakubali sharti lile akaondoka zake na kuanza kuzungukia mashimo ya nyoka uko porini.

Shimo moja baada ya jingine, kichaka kwa kichaka na mwishowe alifanikiwa kumkamata Koboko kwa kumweka unga katika chungu. Na Koboko alipoingia tu ndani ya chungu alikifunika haraka sana, kisha huyoo na baskeli yake kumpelekea mganga yule nyoka.

Kufika kwa mganga, mganga hakuamini macho yake aliposikia kuwa kaletewa nyoka, alipofunua chungu tu, nyoka katoka kwa hasira, na mganga nae kuona nyoka anamfuata uku kavimbisha shingo yake kwa shari aliyokuwa nayo akageuka akatimka mbio uku akimtukana yule mama, akisema...!

"...kama umeweza kukamata Koboko, mumeo anakushindwaje...!?"

Sisi wengine mashahidi macho tukaanguka kwa vicheko, maana zile mbio ni hatari... Yule Mganga alirudi baada ya siku tatu...Wednesday, 5 October 2022

JIJI LA DAR US SALAAMA
DAR ES SALAAM TANZANIA

Kabla ya mwaka 1868, Jiji linalofahamika kwa jina la Dar es Salaam, halikuwepo kabisa. Badala yake kulikuwa na mji ulioundwa na miji mitatu maarufu, ambayo ni Kunduchi, Mbwamaji na Tindwa. Kila mji ulijitegemea, huku idadi ya wakazi wake wote kwa jumla haikuzidi watu 2,000.

Kati ya miji hiyo mitatu, miji miwili ya Kunduchi na Mbwamaji bado ipo hadi leo huku mji wa Tindwa, uliokuwa na eneo kubwa zaidi, ulimezwa na nguvu za matukio ya kihistoria yaliyosababishwa na mabadiliko na mpangilio mji mzima wa jiji.

Tukio kubwa la kihistoria lililobadili mpangilio wa miji hiyo mitatu na kuzaliwa kwa Jiji ambalo leo hii linalofahamika kama Dar es Salaam lilitokea mwaka 1865 pale Sultani Majid, aliyekuwa mtawala wa Zanzibar, kununua eneo kubwa la ardhi ya mji wa Tindwa, iliyomilikiwa na Sharif Attas na Jumbe Tambaza (machifu wa Kimashomvi), eneo hilo lilianzia Bustani ya Mnazi Mmoja karibu na Mnara wa Saa (Clock Tower) mpaka Magogoni (Ferri) mpaka kuelekea Daraja la Selender kutokezea Upanga lilikuwa ni Shamba la Jumbe Tambaza.

Lengo la Sultani huyo la kununua ardhi hiyo inayoanzia eneo la Magogoni hadi eneo la Hospitali ya Osheni Rodi (Ocean Road), eneo ambalo lilikuwa pori linalotazama Bahari ya Hindi na ambalo lilikuwa na ukimya, kiasi cha wakazi wa eneo la Tindwa kulipa jina la Mzizima, kwa sababu kila aliyepita eneo hilo alihisi mwili wake kusisimka na kuzizima kwa hofu ya kuwaogopa Wanyama pori.

Alinunua hilo eneo na kujenga majengo makubwa kwa ajili ya kufungua chuo/shule ya kufundisha dini ya Kiislamu kwa lengo la kueneza Uislamu kutokea hapo kuelekea maeneo mengine ya Mrima, Pwani na Bara hadi Kongo na Burundi na kwa watu wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika ya Kusini na Afrika ya Kati.

Baada ya kununua eneo hilo, mwaka 1865 Sultani Majid aliingiza manuari kubwa za mizigo, zinazokadiriwa kuwa kati ya tatu hadi saba, zikiwa zimesheheni vifaa vya ujenzi na wataalamu wa ujenzi wa majengo ya chokaa na mawe, toka nchi za Bara Hindi na Uajemi. Na ndipo ujenzi wa majengo hayo ulipoanza kwenye eneo hilo la Mzizima mkabala na pwani ya Magogoni, huku majengo mengi yakijengwa eneo la Ocean Road.

Pamoja na Ikulu ile ya Magogoni, Seyyid Majid pia alijenga lile jumba la ‘Ocean Road Cancer Institute’ (ORCI) kwa sasa, ambalo mwanzoni lilikuwa ni Msikiti Mkubwa wa Ijumaa.

Ujenzi wa majengo hayo ulichukua takribani miaka mitatu na kukamilika mwaka 1868 na Sultani Majid mwenyewe alilipa jengo moja kubwa lilipo Magogoni hadi leo, jina la Dar us Salaama (tamka Daru Salaam), maneno ya Kiarabu yenye maana ya Nyumba ya Utulivu au Nyumba ya Amani. Na katika lango kuu pameandikwa maneno kutoka kwenye Qur’an Suuratul Hijr Ayah ya 46 isemayo (ٱدْخُلُوهَا بِسَلَـٰمٍ ءَامِنِينَ) Udkhuluuhaa Bisalaamin Aaminiin (Ingieni kwa salama na amani).

Wakoloni wa Kizungu walipokuja Tanganyika, mahala hapo ambapo palikuwa ni Msikiti Mkubwa wa Ijumaa, pakafanywa hospitali iliyojulikana kama ‘Ocean Road European Hospital’, iliyokuwa ikiwatibia Wazungu peke yao.

Na ndio utaona vijana wengi jiji la Dar es Salaam waliozaliwa baada ya uhuru kati ya miaka ya 60 - 70, wamezaliwa kwenye hospitali ya Ocean Road, ambayo sasa ni maalum wa kutibu saratani (Ocean Road Cancer Hospital), na kabla ya hapo yalikuwa ni majengo ya msikiti na mabweni ya vijana na wazee waliokuja kusoma Dar Us Salaam na bado mpaka leo muonekano wake ni ule ule.

Ikulu ile ya Magogoni wakati huo, ilikuwa imezungukwa na misikiti kadhaa ambayo yote, katika Utawala wa Kijarumani, ilibadilishwa matumizi na kufanywa taasisi nyengine.

Misikiti mingine iliyobaki ikasambaratishwa na kutumiwa kwa shughuli nyengine, ukiwamo Msikiti mkubwa uliokuwa baharini pale Forodhani, jijini Dar es Salaam, ulipogeuzwa kutoka msikiti na kuwa Kanisa la Mtakatifu Joseph mpaka hivi leo.

Kuanzia hapo, wakazi wote wa miji mitatu ya Kunduchi, Mbwamaji na Tindwa, wakabadili jina la Mji wa Tindwa na kuubatiza jina la jumba hilo kubwa kuwa Dar us Salaama, jina ambalo baadae lilimeza hata majina ya miji ya Kunduchi na Mbwamaji na kuifanya iwe vitongoji tu katika mji wa Dar us Salaam.

Kwa takribani miaka kumi tangu kufunguliwa kwa jengo hilo, raia toka nchi mbalimbali kuanzia Tanganyika, Msumbiji, Zaire, Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda, walimiminika katika jumba hilo na kupata elimu ya Uislamu iliyotolewa na masheikh wakubwa toka nchi za Uarabuni, Lamu na Mombasa Kenya na Zanzibar.

Kati ya mwaka 1875 na 1878, Wajerumani walivamia Tanganyika na kuiweka katika himaya ya utawala wao, na jengo hilo lilibadilishwa matumizi yake toka kuwa kitivo cha elimu ya Kiislamu na kuwa makao makuu ya serikali ya Kijerumani na baadae kuwa makazi ya Mtawala wa Kiingereza na leo hii ni Ikulu ya Taifa.

Mbali ya kubadilishwa jina kwa jengo hilo, toka Dar ul Salaam na kuwa Ikulu, hata jina lilipewa mji wake kutokana na jengo hilo pia limebadilishwa toka Dar us Salaama (Nyumba ya Utulivu/Amani) na kuwa Dar es Salaam (Bandari ya Amani) ambayo wajuzi wa lugha ya Kiarabu wanakata kuwa neno hilo Dar es Salaam halina maana ya Bandari ya Salama.

Tuesday, 27 September 2022

 FAIDA YA KUNYONYESHA

KATIKA miaka ya sitini na sabini, serikali mbali mbali duniani ziliwahamasisha kina mama kuacha kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama. Na badala yake watumie maziwa ya kopo.

Juhudi hizo zilizaa matunda yaliyokusudiwa. Yaani kina mama wengi waliacha kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama, na badala yake waliwanyonyesha maziwa ya kopo (bottle feeding).

Hata hivyo teknolojia hiyo mpya ilileta maafa ya maelfu ya watoto wadogo katika nchi mbali mbali. Hii ni kwa sababu, maziwa ya kopo hayana kinga, yanagharama kubwa, yanahitaji muda wa kuyaanda na usafi wa hali ya juu. Pia maziwa ya kopo hayana virutubisho vyote anavyovihitaji mtoto mchanga.

Baada ya maafa hayo, katika miaka ya hivi karibuni serikali kadhaa duniani zimeanza kuwahimiza kinama kuirudia teknolojia asilia. Yaani kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama.

Hata hivyo, maisha yetu ya kila siku yanatuonyesha kwamba, kuna kinamama kadhaa hasa katika mji ambao hawajawa tayari kuirejea teknolojia hiyo ya asili, licha ya faida zake nyingi kama zinavyowekwa wazi sasa na elimu ya sayansi.

Baadhi ya kina mama hao wasiotaka kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama wanaona jambo hilo ni kero na lina wanyima muda na uhuru wa ‘kustarehe’ (kwenda Bar, ufukweni, kwenye kumbi za muziki, kwenye makasino, kwenye pati, n.k.

Pia wapo wale wanao ona kwamba ‘kero’ ya kunyonyesha maziwa ya mama itawazeesha mapema na pia wataonekana kuwa hawaendi na wakati!

Kwa kuzingatia kasoro hiyo, iko haja kwa vyombo vya habari kuongeza juhudi za kuwahamasisha kina mama na jamii kwa jumla ili kuirejea teknolojia ya kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama. Makala hii inalenga katika azma hiyo. Kwa kuielimisha jamii faida zinazopatikana katika maziwa ya mama yanapotumika kwa unyonyeshaji watoto wadogo.

Awali ya yote maziwa ya mama ni mlo kamili wenye mchanganyiko wa virutubisho vyote inavyoweza kumpa mtoto afya kwa kipindi cha miezi minne ya kwanza bila ya kuihitaji nyongeza ya chakula kingine.

Maziwa ya mama pia ni chakula na kinywaji kilicho safi na salama. Vilevile maziwa ya mama yanakinga kwa mtoto na vilevile tayari muda wote.

Pamoja na faida hizo, maziwa ya mama yana gharama nafuu yakilinganishwa na yale ya kopo. Vilevile maziwa ya mama hayachafui mazingira. Kwa maneneo mengine maziwa ya kopo (makopo na mifuko iliyowekwa maziwa) yanachafua mazingira.

Zaidi ya hayo, teknolojia ya kumnyonyesha mtoto maizwa ya mama inaongeza mapenzi baina ya mtoto na mama. Pia utafiti wa kisayansi ulioripotiwa hivi karibuni na jarida la American Academy of Pediatrics", umeonyesha kwamba unyonyeshaji wa maziwa ya mama hasa kwa muda mrefu unaongeza uwezo wa utambuzi kwa mtoto.

HAYATI ZA UJANA WETU
SIKU YA IDD

Baada ya Mfungo Na Vile Vigoma vya Kula Daku, Jioni Tulielekea Viwanjani

Nimejikuta tu, Naandika, Kumbukumbu Chache Zilizobakia Miaka ya 70 Mpaka 80.

Nakumbuka Nilipokuwa Bado Kinda, Mwezi Kama Huu Ulioisha, Mwezi wa Ramadhani, Ilikuwa Baada tu ya Kumaliza Kufuturu, Basi Wale Matineja, Walikuwa Wakipitapita Majumbani Usiku Wakiimba na Wengine Hata Kucheza, Wakitumbuiza kwa Kupiga Vigoma vya Kula Daku.

Kwa Sie Tulikulia Dizim, yaani Dar Es Salaam Ilikuwa Jambo la Kawaida sana Kuwaona Vijana Wadogo Mida ya Saa Mbili Mpaka Nne Usiku, Wakipita Majumbani na Vigoma Vyao. Wakiwaimbia Watu Mitaani, "Kula Daku, Kula".

Wakati Mwingine Hata Vijana wa Makamo Pia Walitutumbuiza, Ila Hawa Ilikuwa ni Tofauti Kidogo, Wao Walikuwa Wakipita Kuanzia Mida ya Saa Nne Usiku

Hizo ni enzi ambayo Waislamu walikuwa na Imani, ilikuwa ikifika muda wa kufuturu, basi utaona wakitandika Mikeka na Majamvi, nje ya majumba yao. Kiufupi Wanaume Walikuwa Wakifuturu barazani, na kila mpita njia ukaribishwa, japo anywe nusu kikombe cha uji, uji uliokolezwa pilipili Manga (Pilipili Mtama). Na wanawake waliokuwa wakifuturu uwani. Kama ilikuwa ni nyumba yakupanga, basi wote wakaazi wa hiyo nyumba ujumuika na kupata futari kwa pamoja, kila mmoja akileta futari yake aliyopika siku hiyo.

Nimekumbuka baadhi ya maneno ya nyimbo zilizokuwa zikiimbwa.

Muulizeni mzungu alietoka angani bwana x2.

Babu kaungua ndevu kwa uji wa ramazani bwanaa...

Kula daku maneno yangu, kula eeh daku wee, daku kulaaa...

Huyu na huyu kama mtu na nduguye bwana...

Nasema huyu na huyu kama mtu na nduguye bwanaaa...

Ukiwaangalia sana mapua kama nguruwe bwana...

Kula daku maneno yangu, kula eeh daku eeh, daku kulaaa...

Kwa wale tineja, wakimaliza kuburudisha aidha wapewe pesa kidogo, Kuanzia senti 10, 20 au senti Hamsini, (Sumni), nyumba nyingine wakitoa Makoko na Matandu ya wali na maisha yaliendelea kwa furaha na amani tele.

Utoto ule waliweza kuaminiana, senti kidogo zilizokusanywa, masiku ya Ramadhani, waligawana siku ya sikukuu ya Idd Fitri, hazikuwa pesa nyingi, kiasi cha shilingi 10 au 15 au 20 kama mna bahati.

Ilikuwa ikifika jioni kila mmoja alielekea kwenye viwanja vya sikukuu. Na wachache wetu tulibahatika kununuliwa nguo mpya na viatu kwa ajili ya sikukuu.

Haikuwa ajabu ukanunuliwa shati na suruali, ukakosa viatu, au ukanunuliwa viatu ukakosa aidha suluwali au shati.

Tuliobahatika tulipewa na pesa kidogo, nadra sana ukapewa shilingi tano, ni mwendo wa shilingi kuja chini.

Sie tuliolelewa kwenye vitongoji vya Kariakoo na Gerezani, Kisutu, Upanga, Ilala, Magomeni na Buguruni kiwanja chetu Maarufu cha kushehereka, kilikuwa pale Kidongo Chekundu (sasa ni Jakaya M. Kikwete Youth Park - JMK), kiwanja kilicho kati ya mitaa ya Livingstone, Kiungani, Kisarawe na Lumumba, mbele ya shule ya msingi Gerezani.

Hapo Kidongo Chekundu, kulikuwa na Mabanda kadhaa wa kadha ya muda, yaliozungushiwa magunia, mabanda maarufu yalikuwa yale ya vikaragosi, ngoma ya Nachi, (mfano wa chakacha), mieleka na kadha wa kadha.

Nje kulikuwa na uchezeshaji wa korokoro (Kamari) na michezo mingine ya kubahatisha.

Kulikuwa na wachuuzi wa bidhaa wa kila aina, mihogo ya kukaanga na kuchoma, viazi vitamu na mbatata vilivyopondwa na kuwekwa pilipili ya unga kwa juu, vikiliwa na machicha ya nazi, mbwimbwi, ubuyu, juice za ukwaji, togwa, embe za kuchepa, karanga shikirimu za vijiti na kadharika.

Sherehe zilikuwa za siku tatu mfululizo, mabanda yakifunguliwa saa 10 jioni mpaka usiku wa saa nne.

Sie tulikuwa tukikaa karibu na viwanja, ilikuwa burudani tosha, kuona watu wa rika mbalimbali, wakitoka vitongoji vya mbali wakijumuika pamoja wakubwa kwa wadogo, kusheherekea sikukuu ya iddi.

Wengine wetu tulikwenda kutazama sinema kwenye majumba ya kuonyeshea filamu.

Kwa Dar es Salaam Kulikuwa New Chox, Odeon, Cameo, Avalon, Empress, Empire na Drive-inn Cinema kule Msasani, ambayo unaingia na gari lako.

Enzi hizo tulikuwa tukitumiana salamu kwa njia ya Redio, kulikuwa na watu maarufu wa kutuma salamu, yaani karibia vipindi vyote hawakosi hao watu na mwisho wa salamu unaandika ujumbe maalum, kama vile Salamu ni nusu ya kuonana n.k.

Ukibahatika, basi waweza kukutana na gari la RTD, likipita mitaani, na kuwapa watu nafasi za kutuma salamu zao za sikukuu, hapo utatakiwa utume salamu kwa watu watatu na kisha utatakiwa uchaguwe wimbo wa kusindikiza salamu zako.

Kule maeneo ya Posta ya zamani, pembeni ya jiji la Dizim, mkabala na shule ya Forodhani, kulikuwa na eneo ambalo sasa nahisi kumegeuzwa kituo cha feri, tukipaita Bombei. Hapo paliuzwa vitu vya Ubuge ubuge na ilikuwa kila Jumapili utawakuta watu ufukwemi, wakipunga upepo uku wakiangalia Meli na Majahazi yaliyotia nanga.

Kiza kikiingia, wale vijana wadogo wadogo waliokwenda kwenye viwanja vya michezo, wanajikusanya na kurudi majumbani mwao, kuanzia saa moja jioni.

Wale wa nje ya mji, wanasogelea vituo vya mabasi ya UDA hapo utakutana na foleni ndefu ya wasafi wakiwa kwenye foleni za kupanda mabasi. Hakukuwa na fujo za kugombea mabasi kama hivi sasa, watu wakieshimiana na uku pembeni kuna mgambo akichunga usalama wa abiria.

Ndani ya basi hata kama umewahi kukalia kiti, kama kulikuwa na mzee au mama mjamzito, basi alipishwa ili akalie siti ya basi. Ilikuwa kawaida kusikia mtu au watu wakisema, "...Jama Hakuna Muislamu wa Kumpisha Huyo Mama Mjamzito siti!"

DUNIA INA MAMBO!

Miwezi kadhaa iliopita, nilipata likizo yangu ya mwaka, nikafunga safari kwenda zangu Bongo, Tanzania. Kwenye pirikapirika zangu nikamtembelea mmoja wa marafiki zangu, rafiki yangu huyu tulisoma wote shule ya sekondari, kati ya miaka ya 80. 

Rafiki yangu amepanga maeneo ya Banana, amepanga chumba kimoja (yeye mpaka leo bado mseja), vyumba vingine kuna wapangaji wengine. Kwenye maongezi akanisimulia vituko vinavyo msumbua hapo nyumbani kwake. Akasema ni siku 3 hajalala usiku kwa sababu anasikia nyayo za watu asiowaona wakitembea ndani ya chumba chake na nje ya dirisha.

Siku ya kwanza usiku wa saa nane, alihisi watu ndani ya chumba, alipovuta shuka na kudhani ni hisia tu! Akasikia nyayo za watu ndani, ndipo alipopiga kelele zilizoamsha wapangaji. Na kuamua kuingia kwenye dua na maombi, lakini hakurudi kulala kwa hofu na kukesha mpaka muda wa alfajiri wa kujiandaa kazini.

Kwa kitete siku iliyofuata akanywa dawa ya usingizi ili hasisikie chochote. Asalale! Haikuwa dawa ya kudumu, kwani aliamshwa kwa kuguswa kiunoni tena na mtu asiyemuona. Baada ya hapo akaanza kusikia kama mtu anamwaga michanga juu ya bati. Vibweka, vikahamia ndani sasa, kwa kusikia nyayo za watu wakizidi kutembea kama wanamiliki chumba.

Hivi karibuni alinipigia simu kuwa kakimbia nyumba.

Kisa hicho kikanikumbusha mambo yaliyompata mmoja wa marafiki zangu wa mtandaoni, miaka ya nyuma alipokuwa anasoma Mtwara-Masasi girls alikuwa akisikia nyayo za watu ndani ya bweni lao, wakitembea usiku wa manane ilhali kila mwanafunzi alikuwa amelala.

Siku ya kwanza alisikia sauti ya viatu vilivyotoa sauti ya 'Ko ko ko' akaamua kusoma dua na maombi. Ile anamaliza tu kufanya maombi (kusoma dua) akasikia vicheko, alipiga ukunga na kuhamia kitanda cha juu kwa mwezake. (Vitanda vya bweni nadhani mnavijua)

Vibweka havikuishia hapo, akawa anaogopa kabisa kulala peke yake. Akawa analala na rafiki yake.

Sasa siku moja alipolala na rafiki yake kulipopambazuka alfajiri, rafiki yake alimwamsha akaoge. Lakini, yeye akuamka na kumwambia kuwa hataamka muda huo, amwache mpaka baadae kidogo.

Yule Rafiki yake akaenda kuoga na kumuacha akiendelea kulala. Aliporudi akamwamsha na kusema, "Lily umeoga na kurudi kulala tena?"

Lily akashtuka lakini akahisi amesikia vibaya.

Akamjibu, "Mimi sijaoga bwana. Umenibakishia maji?"

Yule Rafiki yake akazidi kusisitiza, "Lily utachelewa, amka ujiandae. Umeshaoga then urudi kulala kweli?" Ebu acha uvivu!

Pale sasa ndio mawenge ya usingizi yalipokata kabisa. Wakabishana huku Lily akizidi kusisitiza kukataa kwamba ajaoga.

Rafiki yake akasema, "Lilian nilikuomba mpaka sabuni lakini hukunijibu wala kunitazama."

Lily kufikia hapo akwa hana budi kwenda kuoga huku akitetemeka kwa hofu. Alipokuwa anarudi kutoka kuoga kuna mwanafunzi mwezake akamuuliza, "Lily una maji mengi enhee..."

Kipindi kile maji yalikuwa yanapatikana kwa shida, na walikuwa wanayachota kwenye kisima kwa ugumu sana. Hivyo  basi, ndoo moja ya lita kumi unaweza kuoga siku 2 au 3: sasa Lily akawa anajiuliza angewenzaje kuoga mara mbili?

Alipomuliza kwa nini anasema vile, yule mwanafunzi mwenzake akasema kwa sababu amemuona ameoga mara ya pili. Kidogo amwamini rafiki yake, kwa sababu walikuwa wanaoga nje wakiwa wamejipanga kwa mstari hivyo ilikuwa ni rahisi kuonana nani kaoga nani hajaoga.

Lily alianza kushikwa na hofu kupita kipimo baada ya wote kuungana na kusisitza alioga na walimuona.

Yule rafiki yake naye alipoona vituko vikimfuata naye akamkimbia kwa hofu na kwenda kulala bweni lingine. Akabaki peke yake.

Akabaki akijiuliza maswali ambayo hata wewe utakuwa unajiuliza. Huenda utakuwa na majibu nayo, lakini upande wake mpaka leo ajawahi kupata majibu.

 

Na siku aliporudi likizo, ndio hakurudi tena kwenye ile shule! 

Tuesday, 20 September 2022

MPANGO KINA WA MIAKA 5 YA KUREKEBISHA VIJANA - Panya Road

An Extensive 5 Year Reforms Program for The Youth - Panya Road

  • Hata Wafungwa Wanaweza Kufaidika Kwenye Programu Hii.
  • Tuwatumie Panya Road, Kuimarisha Uchumi kwa Kutoa Mafunzo ya Uzalishaji, Ufundi na Kazi za Amali, Mila na Utamaduni na Uzalendo.

Haya Matukio ya Panya Road, yananikumbusha tukio moja lililonitokea miaka mingi nyuma, zaidi ya miaka 40 hivi. Nakumbuka kushuhudia jamaa ninaye mfahamu, akikimbizwa na umati watu, wakimtuhumu kukwapua pochi ya mama mmoja, huku wakipiga kelele za mwizi.

Yule kijana alinipita mbio na huku akivua shati lake na kuingia kwenye jalala la taka, na kujifanya kichaa huku akigaagalika kwenye taka. Halafu aliniambia, “wakija waambie mwizi amepita.” Anamaliza kusema tu, waliokuwa wakimfukuza walifika pale, wakitweta.

Kuna waliokuwa na mawe na vipande vya tofali, wengine mapanga, marungu na silaha nyingine. Nilijua yule kijana alikuwa ni mwizi na miaka ile kulikuwa na vikundi vya vijana wahalifu wakisumbua sana watu kwa tabia zao za kukwapua kwapua watu.

Kidogo niwaambia wale watu, mwizi wao ndiye huyo hapo jaani. Lakini kitu fulani kiliniambia niache, sikumbuki kama ni woga au huruma tu iliyonijia, sikuwapenda wezi na pia sikupenda kuona wakiadhibiwa kwa kupigwa mawe au kuchomwa moto.

Walipo niuliza nikawaongopea huku nimejawa na hofu kwa mbali “Karuka huo ukuta, kadondokea upande wapili, kaacha shati lake hapa.”

Lile kundi hata sijui ilikuwaje, waliniamini, japo walikuwa na wasiwasi kidogo kwa yule kijana aliyepo jaani, lakini walinisikiza na kuamua kuondoka.

Yule kibaka, alinishukuru sana huku akinitaja kwa jina langu, kumwangalia vizuri kumbe tunafahamina, tukiishi mtaa mmoja, japo yeye alinizidi umri na hatukuwa marafiki, lakini kwa kule kutomchongea kwa wale watu, kulimfanya anione kuwa mimi ni jirani mwema.

Yule kijana alikuja kuhama, sijui walihamia wapi, ila ninachojuwa baba yake alikuwa ni mtumishi wa serikali, nadhani mzee wake alipata uhamisho mkoani.

Baada ya miaka isiyopungu ishrini, nilikuja kukutana na yule jamaa, mkoani Kigoma, keshakuwa mtu mzima, mwenye familia yake na uzuri zaidi ni mfanyabiashara mkubwa tu, akimiliki duka la spea za magari na boti za uvuvi.

Alinikumbuka nami nikamkumbuka, akanikaribisha nyumbani kwake, tukaongea mengi, akanambia kuwa hasingeweza kunisahau kwa sababu niliokoa maisha yake, na tangia siku ile aliyokimbizwa nami nikamsaidia ilikuwa kama ndio dawa, maana aliacha wizi, akajishughulisha na biashara na sasa anajitegemea na ana familia ya watoto wawili.

Lengo hapa si kuwahadithia tukio la kibaka mmoja aliyepata bahati ya kuokolewa miaka 40 nyuma, lahasha, ila nimekuwa najiuliza hivi awa vijana tunao waita Panya Road, ni kweli hatuna suluhisho la kudumu? Maana wengi wao ni vijana walio kati ya umri wa miaka 12 na 20 au 25 tu.

 

MPANGO WA KUWAWEZESHA PANYA ROAD

Binafsi natamani badala ya kuwafunga jela, tuwe na mipango maalum ya kuwarejesha Panya Road kutoka kwenye maisha ya kudhuru watu, uraibu wa dawa za kulevya na wizi na kuwageuza kuelekea kwenye maisha ya kawaida kupitia mafunzo maalum.

Kuwafundisha Panya Road kulihudumia Taifa lao na kuwatumia vijana hao katika kuwapatia mafunzo ya msingi ya kujiendeleza katika shughuli za kilimo, viwanda, uvuvi, ufundi na kazi za amali. Kuwafunza elimu ya uraia, Kuwafunza na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kijamii na utamaduni.

Mpango huu uwe wa miaka mitano (5), huu mpango utaratibu, kusimamia na kuendesha mafunzo endelevu hivyo basi kupitia mpango huu vijana hawa watajengeka kiuzalendo, wataweza kujitegemea na kujiamini.

Nakumbuka miaka ile kuanzia 1964 mpaka katikati ya miaka ya 70, serikali ya Tanzania ilikuwa mikakati ya kuwapeleka watu kwenye vijiji vya ujamaa.

Najua kuwa kulikuwa na matatizo ya kiutendaji, ndio maana jambo lile halikufanikiwa kama lilivyotarajiwa, lakini tunaweza kuchukua lile wazo kisha tukawashirikisha wasomi na wanaharakati wakalikarabati na kuliwasilisha tena, kisasa zaidi.

Kama vile serikali ilivyoanzisha JKT na baadae JKU kuwa ni vyombo vya kuelimisha na kuandaa vijana wa Kitanzania kiuzalendo, kimaadili, kinidhamu na kuwafanya raia wema wanaopenda kutumikia na kulinda nchi yao. Basi kwa nia ileile na uthubutu uleule, tunaweza kuanzisha "MPANGO KINA WA MIAKA 5 YA KUREKEBISHA VIJANA - PANYA ROAD" (AN EXTENSIVE 5 YEAR REFORMS PROGRAM FOR THE YOUTH - PANYA ROAD), kiufupi MKKV-Panya Road

 

WIZARA ZA SERIKALI ZITOE WATAALAMU.

Mpango huu wa miaka mitano, MKKV-Panya Road, unaweza kusimamiwa na wizara kadhaa, wakiongozwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo n.k.

Kwenye hizo kambi za kudumu, vijana wapewe mafuzo ya Stadi za Maisha ya kujitegemea kinadharia na kivitendo, Kusoma, Kuandika, Kuhesabu na utoaji wa elimu ya Msingi na Sekondari kwa ujumla wake.

Programu hii ya MKKV-Panya Road, pia ijumlishe kuwaandaa awa vijana Kisaikolojia, Kuwapatia Elimu za Mafunzo ya Kilimo, Viwanda, Uvuvi, Mapishi, Elimu ya Uraia na Uzalendo, Ufugaji, Ujenzi, Ufundi wa aina mbalimbali kama vile Uashi, Useremala na Ukarabati wa magari, elimu za dini, utamaduni na michezo.

Vilevile kuwepo wataalamu wa saikolojia na ushauri nasaha watakao weza kuwashauri na kuwasaidia awa vijana katika masuala ambayo yamewafanya wawe na tabia mbaya, ili kuwasaidia kuepukana na kurejea tena kwenye maisha ya uhalifu. Na kuwabadirisha kuwa raia wema, wanaojiamini, wanaojituma, wenye uzalendo na kuipenda nchi yao.

Kwa kushiriki katika programu hii ya MKKV-Panya Road, vijana watapata fursa ya kupata ujuzi unaohitajika katika maisha yao na kuwa na ujasiri na ushindani kwa taaluma yao baada ya kuhitimu.

Mbali na ujuzi wa kujifunza ili kuwa na nguvu kitaaluma, vijana watajengeka kiuwezo na kujiamini na kuweza kuanzisha miradi yao wenyewe.

Vilevile itasaidia kuwabadirisha na kuwa raia wema, wanaojiamini, wanaojituma, wenye uzalendo na kuipenda nchi yao.


NB:

Kama kutakuwa na kesi ya mauwaji kwenye uhalifu wa hao vijana, basi Sheria ichukuwe mkondo wake.
Hili wazo ni kwa wale tu ambao hawana kesi za mauwaji.

Tuesday, 13 September 2022

RAIS WA KENYA AMEAPISHWA

  • Vituo vya Ndani vya Runinga Vyanyimwa Nafasi ya Kurusha Matangazo.
  • Hofu ya Bw. William Ruto Kulipa Kisasi Yaanza Kujionyesha

Rais, William Kipchirchir Samoei Arap Ruto ameapishwa kuwa rais wa tano wa Kenya siku ya Jumanne tarehe 13 Sept 2022, katika hafla iliyohudhuriwa na makumi ya viongozi na wanadiplomasia wa kimataifa.

Angani mwonzi wa jua ulikuwa umefichwa na Mavunde yakisindikizwa na mawaga na kusababisha kibaridi cha mzizimo.

Chini ya mawingu kulikuwa na tukio adhimu, Mubashara kwenye Kituo cha Michezo cha Kimataifa cha Moi, Kasarani. Mpaka kufikia saa tano asubuhi, Uwanja ulikuwa umejaa watu pomoni zaidi ya waudhuriaji 60,000 walihudhuria wakipeperusha bendera ya Kenya na kucheza kwa furaha huku wakiburudishwa na nyimbo kadhaa wa kadha.

Ulinzi ulikuwa mkali kuzunguka eneo hilo, huku vikosi vya usalama vikijaribu kuwazuia mamia ya watu waliojaa lango la uwanja huo. Takriban dazeni ya watu walijeruhiwa walipokuwa wakigombania kuingia kupitia moja ya lango la dharura.

Katika hali hisiyo ya kawaida na iliyozusha maswali mengi kwa wamiliki wa vituo vya Runinga nchini Kenya, ni pale walipozuiwa kurusha Mubashara hafla ya kuapishwa kwa rais mpya, hali iliyotafasiriwa kuwa ni kutishia kwa uhuru wa vyombo vya habari.

Timu ya mawasiliano ya Rais mteule wa Kenya William Ruto ilivizuia vyombo vya habari vya nchini humo kuripoti habari za kuapishwa kwa rais, na kutoa haki za kipekee za utangazaji kwa kampuni ya Multichoice Kenya Ltd, mshirika wa kikundi cha Runinga cha kulipia cha Afrika Kusini.

Waandishi wa habari kutoka magazeti ya ndani na vituo vya redio waliruhusiwa kuripoti mubashara.

Wakati wa kampeni, Bw Ruto aliwahi kuvishutumu mara kadhaa vyombo vya habari vya Kenya kuwa vinaupendeleo dhidi yake, na baadhi ya wachanganuzi wa siasa za Kenya wanasema kuwa uamuzi wake huo wa kupiga marufuku vituo vya Runinga vya ndani kurusha hafla hiyo ni kulipa kisasi kwa yale yaliyotokea wakati wa kampeni.

Mutuma Mathiu, mhariri mkuu wa Nation Media Group, ambayo anamiliki vyombo vya habari vya magazeti na Runinga, alisema katika mahojiano kwamba walikuwa na jukumu la kitaifa kuwatangazia Wakenya na kuhabarisha dunia kile kinachojiri, lakini wakajikuta wanapigwa dafrao na amri ya rais mpya.

Hata hivyo, alisema, “Sidhani kama tunataka kuanzisha vita vya kupakana matope kwenye arusi na kisha kuchafua vazi la bibi-arusi.”

Bw William Ruto alishinda katika kura ya Agosti 9 kwa tofauti ya kura chache sana dhidi ya mpinzani wake, Raila Odinga, ambaye alikataa matokeo na kuyapinga katika Mahakama ya Juu. Lakini mahakama iliidhinisha ushindi wa Bw Ruto katika uamuzi uliotolewa kwa kauli moja wiki moja iliyopita.

Bw. William Ruto, mwenye umri wa miaka 55, aliwahi kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo kwa miaka 10 iliyopita, alizaliwa katika familia ya Kikristo katika kijiji kidogo cha Bonde la Ufa nchini Kenya, ambako alisaidia kazi ya ukulima ya kupanda mahindi na kwenda shuleni bila viatu. 

Alionyesha nia yake ya awali katika siasa katika miaka ya 1990, na kuwa mshirika mkubwa wa mtawala wa muda mrefu wa Kenya, Daniel arap Moi, alishinda nafasi katika Bunge na baadaye kuhudumu kama waziri wa kilimo na elimu ya juu.

Ongezeko la utajiri wa William Ruto ndani ya muongo mmoja umewastaajabisha watu wengi sana, Bw. William Ruto aliwahi kushtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilipomshtaki kwa uhalifu dhidi ya binadamu, ikimtuhumu kwa kusaidia kupanga ghasia zilizofuatia uchaguzi wa 2007. Lakini Mahakama ilitupilia mbali kesi dhidi yake mwaka wa 2016, kwa vile serikali aliyohudumu kama makamu wa rais ilizuia ukusanyaji wa ushahidi na mashahidi wakaghairi.

Licha ya ukwasi wake wa kutatanisha, akiwa na himaya ya biashara inayojumuisha hoteli za kifahari , ranchi na kiwanda kikubwa cha kusindika kuku, Bw. Ruto alianzisha kampeni yake mwaka huu kwa wachuuzi wa Kenya, umati wa vijana na wanaojitahidi kujipatia riziki. Wakati wa kampeni, Bw. Ruto alizozana na Rais wake, Uhuru Kenyatta, ambaye alimuunga mokono mpinzani wa Bw. Ruto, Bw. Odinga, waziri mkuu wa zamani na kiongozi wa upinzani .

Bw. Kenyatta hakumpongeza Bw. Ruto hadi Jumatatu jioni, alipomkaribisha katika afisi ya rais, Bw Kenyatta alikuhudhuria hafla ya kumuapisha rais mpya na kushikana mikono, lakini Bw Odinga alisema kwenye ujumbe wake wa Twitter kwamba hatahudhuria.

Dennis Itumbi, msemaji wa Bw. Ruto, alihalalisha hatua hiyo kwa kusema Multichoice Kenya sio tu mwanakandarasi pekee wa kibinafsi bali KBC ni mmiliki wa hisa ndani ya kampuni ya Multichoice Kenya. Wanjohi Githae, kutoka kwenye timu ya mawasiliano ya Bw. Ruto, alisema katika ujumbe mfupi wa simu kwamba ingawa vyombo vya habari vya ndani ya nchi vinaweza kuleta magari yao ya utangazaji, ila hakuta kuwa na nafasi ya kuegesha magari yao mahali popote karibu na uwanja.

Siku ya Jumanne asubuhi, Bw. Mathiu wa Nation Media alisema kuwa baada ya mazungumzo na timu ya Bw. Ruto, waliruhusiwa kuwa na magari yao ya kurushia matangazo, lakini matukio yote yatachukuliwa na kituo cha MultiChoice na wao watarusha matangazo yatakayorushwa na kampuni ya MultiChoice.

Mkataba na kampuni hiyo haujawekwa wazi lakini Bw. Mathiu alisema alitarajia MultiChoice haitafanya hiyana dhidi ya vyombo vingine vya ndani, kurusha matangazo watakayorusha wao.

Wachanganuzi wa vyombo vya habari wanatumai hatua hiyo haitaanzisha enzi ambayo vyombo vya habari vitakwazikwa zaidi. 

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!